Walazimishwa kukubali ufufuko wa Kristo
Na Mwandishi Wetu

ZIPO habari kuwa wanafunzi Waislamu shule ya Utete walilazimishwa kuchangia sherehe za Pasaka.

Kufuatia hatua hiyo, Mwalimu mlezi wa wanafunzi hao aliulalamikia uongozi wa shule.

Ifuatayo ni barua yake ya malalamiko kwa Mkuu wa shule:

Bismillahir Rahmani Rahim
Shule ya Sekondari Utete
S.L.P. 45
UTETE/RUFIJI

MKUU WA SHULE
SHULE YA SEKONDARI UTETE
S.L.P. 45
UTETE/RUFIJI

YAH: KUPINGA WANAFUNZI WA KIISLAMU KUCHANGISHWA FEDHA NA KUSHEREHEKEA SIKUKUU YA PASAKA 24/4/2000

Tafadhali husika na mada ya hapo juu.

Kwa masikitiko makubwa naomba kutumia fursa hii kupinga tukio hilo la aina yake katika historia ya Jumuiya yetu hapa shuleni.

Sherehe iliyokusanyiwa michango hiyo ni Pasaka ambayo msingi wake ni kufufuliwa kwa Nabii Issa (Yesu) a.s. Muislamu haruhusiwi kushiriki, kuchangia, au kuunga mkono kwa namna yoyote ile jambo linalopingana na itikadi ya Dini yake (Uislamu).

Pasaka ni sikukuu ya Kikristo ambayo msingi wake ni kinyume na itikadi za Kiislamu. Kwa mantiki hiyo kuwahamasisha na kuwachangisha fedha wanafunzi wa Kiislamu ni kusababisha kupingana na maadili yao kwa sababu Qur'an inakanusha kuwa Nabii Issa (a.s.) amekufa. Mwenyezi Mungu amesema:

"Na kwa (ajili ya) kusema kwao; "Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Mariamu, Mtume wa Mungu, "hali hawakumuua wala hawakumsulubu bali walibabaishiwa (mtu mwingine). Na kwa hakika wale waliohitilafiana katika (hakika) hiyo wamo katika shaka nalo. Wao (kabisa) hawana yakini juu ya hili (la kuwa kweli wamemuua Nabii Isa), isipokuwa wanafuata dhana tu. Na kwa yakini hawakumuua". (4:157)Q.

Pia kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, Waislamu hawaamini kuwa Nabii Issa (a.s.) amefufuliwa, imani ambayo ndiyo itikadi na kilele cha sikukuu ya Pasaka kwa Wakristo. Kwenye sura ya 3:55 Mwenyezi Mungu amesema:

"(Kumbukeni) Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa: Mimi nitakutimizia muda wako wa kuishi (hawatakuua hao maadui). Nitakuleta kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, (hawataweza kukudhuru) na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru".

Naomba pia urejee muhtasari mbalimbali wa vikao vya mahafali kwenye jumuiya yetu juu ya maazimio ya kupigwa marufuku kucheza 'Disco' hapa shuleni. Kwa mantiki ya kupigwa marufuku ni kuchelea athari zake zinazosababisha mmomonyoko wa maadili kwenye jamii. Lakini kwa mshangao mkubwa burudani ya Pasaka siku hiyo iliambatana na 'Disco'.

Uharamu wa 'Disco' kwenye Uislamu:

-. Huwasahaulisha wachezaji na watazami kumkumbuka na kumtukuza Allah (s.w.)
-. Huchezwa katika mchanganyiko wa wanawake na wanaume na huwa ni kichocheo kikubwa sana cha zinaa.

Hivyo basi, kitendo cha kuruhusu 'Disco' siku hiyo ni ukiukwaji wa azimio la upigwaji marufuku suala hilo.

Allah ametuharamishia kukaribia vishawishi vya zinaa kama ifuatavyo:

"Wala msikaribie zinaa. Hakika hiyo ni uchafu (mkubwa) na njia mbaya (kabisa) " (17:32)

Naomba hatua kali za kinidhamu zichukuliwe kwa wote waliohusika na mpango huo.

Natanguliza shukrani za dhati.

Wabillah Tawfiq
Mbonde A
MWALIMU MLEZI WA WANAFUNZI WA KIISLAMU

Nakala:
(1) Katibu Mkuu
UMAKURU
(2) Katibu Mtendaji
TAMSA.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook