Sakata la Banana

Na. Dkt. Abdallah J. Saffari
MHADHIRI MWANDAMIZI WA SHERIA NA WAKILI

HIVI karibuni nchi ya Zimbabwe imekumbwa na machafuko makubwa pengine kuliko wakati wowote tangu ijipatie uhuru kutoka ukoloni wa Kiingereza (kupitia mlowezi Ian Smith) mnamo 1980. Machafuko haya yameletwa na Waafrika ambao wameyatwaa mashamba mazuri ya Wazungu kwa vile wao hawana ardhi nzuri ya kulima. Lakini gumzo jingine kubwa ni kutupwa kwa rufani ya Canan Banana na Mahakama ya Rufani ya nchi hiyo. Canan Banana ambaye ni kiongozi wa kanisa, alikuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe kuanzia 1980-1985. Katika kipindi chake hicho ilidaiwa alimlawiti kwa nguvu au vitisho mpambe wake. Jambo hilo lilikuwa siri mpaka pale mpambe huyo alipomuua askari mwenzake ambaye 'alimdhihaki' kuwa alikuwa mke wa Banana. Ndipo upelelezi wa kina kuhusu kashfa hiyo ukaanzishwa na polisi na hatimaye Banana akapatikana na hatia ya kulawiti na kutumia vitisho katika kutekeleza ufuska wake huo. Akapewa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja. Pia akaamuriwa kumlipa fidia mpambe wake aliyemlawiti dola za Kimarekani 6,400. Banana hakuridhika na uamuzi wa Mahakama Kuu, ndipo akakata rufaa katika Mahakama ya Rufani, ambayo nayo yakaitupa nje rufani yake.

Nia ya makala haya fupi ni kulitazama sakata hili kwa mapana zaidi ili tupate mafunzo muhimu hususan katika mazingira ya hapa hapa Tanzania. Tutazingatia zaidi dhana ya utawala bora, itikadi, unafiki, ujasiri na uhuru wa mahakama.

2.0 Kitendawili

Wakati upelelezi wa kesi dhidi ya Banana ulipopamba moto, Banana alikimbilia Afrika Kusini. Watafiti wa masuala haya walihisi Banana alitaka kukwepa mkondo wa sheria. Itakumbukwa kwamba wakati huo Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, hakuwa katika mlahaka mzuri na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Kwa nini, hatuwezi kusimulia zaidi kwa sasa! Lakini ni dhahiri kuwa mambo mawili yalitokea mpaka Banana akarejea Zimbabwe kukabili mashtaka yake. Kwanza labda mwenyewe aliona ni bora asikwepe mkondo wa sheria. Au, pili, inawezekana kabisa Nelson Mandela hakukubali tofauti zilizokuwepo baina yake na Mugabe zimsaidie Banana kukwepa mkondo wa sheria.

Kwa vyovyote vile ilivyokuwa, matukio haya mawili yanaturejesha katika dhana ya utawala bora. Dhana hii inahusu mambo mawili makubwa. Mosi ni utekelezaji wa yale ambayo serikali imeahidi wananchi kwa uwazi kadiri inavyotakiwa. Lakini pili, na muhimu vile vile, ni uwajibikaji kwa kushindwa kutekeleza yaliyoahidiwa. Kiungo na mhimili mkuu katika utekelezaji wa mambo hayo mawili ni utawala wa sheria: wenzetu huita rule of law.

Kutokana na kidokezo hicho kidogo tu tunaweza kuona kuwa polisi wa Zimbabwe hawakuogopa kumchunguza Canan Banana kutokana na ulawiti wake. Na serikali nayo, hususan Rais Mugabe, hakuingilia kabisa upelelezi wa kesi dhidi ya Rais aliyemtangulia. Dhahiri dunia nzima na hasa madheha (mashoga ) wa Uingereza wanaelewa msimamo thabiti wa Rais Mugabe dhidi ya ufuska huo. Kwa hivyo hakuonyesha upendeleo. Akaacha sheria ichukue mkondo wake bila kujali madaraka, cheo cha dini wala umri wa Banana.

Na hapa tunapata funzo la namna ambavyo polisi wanavyotakiwa kupeleleza masuala kwa utaalamu na maadili ya kazi yao. Kwani hatua ya kwanza na muhimu kabisa katika kuendesha mashauri ya jinai ni upelelezi yakinifu. Huu unawezekana tu kwa kuzingatia utaalam na maadili bora ya kazi. Hivyo basi rushwa na vitisho vya aina yoyote ile kutoka kwa wakuu wa polisi au viongozi wa serikali ni adui mkubwa wa ufanisi katika hatua hii. Ni bure kufungua na kuendesha kesi ambayo haina ushahidi madhubuti kwani dhahiri mahakama yatamuachia mshtakiwa kwa kutokuwa na kesi ya kujibu.

Ustadi na uadilifu wa polisi wa Zimbabwe katika upelelezi wa shauri la Banana unastahili kuigwa na polisi wa hapa nchini ambao maarufu zaidi kwa unyanyasaji raia kuliko kuwalinda raia hao. Mauaji ya Kilombero na Mwembechai na udhalilishaji wa raia kule Zanzibar kwa hivi sasa ni mifano michache tu.

Zaidi ya hayo, wananchi wamekuwa wakiwatuhumu kuhusika na vitendo vinavyoashiria rushwa. Hukamata vijana na kuwabambikizia kesi za bandia eti wavuta bangi au wazururaji na hata kudai kuwa ni majambazi wa kutumia silaha. Nia yao ni 'kuvutiwa pochi'. Chambilecho Profesa Lipumba, "Humkamata mtu mchana na kumwambia 'mbona taa ya baiskeli yako haiwaki?" Ila la ajabu ni kuwa polisi hawa ni maarufu kuacha kupeleleza au kufuatilia mashauri mazito. Hapa tutatoa mifano miwili kutoka magazeti ya mwaka jana na mwaka huu. Gazeti moja lilitoa habari za kusikitisha kuhusu mwanaume mmoja pale Magomeni Mapipa alivyokuwa akimlawiti kijana wa kiume takriban miaka kumi na kumgeuza 'bibi' kabisa. Mlezi wa kijana huyo alipeleka malalamiko yake kituo cha polisi Magomeni. Lakini licha ya ushahidi mzito kuhusu suala hilo polisi hawakufanya lolote. Na hivi juzi tu gazeti moja limeelezea mfanya biashara wa Kipemba alivyomnajisi kigori wa miaka nane pale Buguruni. Mzazi wa binti huyo alikwenda polisi Buguruni kutoa taarifa ya kosa hilo. Lakini polisi walichukua siku mbili nzima bila kumkamata yule mhalifu licha ya ushahidi kamambe kabisa. Na walipomkamata baada ya shinikizo, wakamuachia siku ile ile. Lakini polisi hao hao ni mabingwa wa kuwakatalia dhamana vijana ambao wanadai wametukana tu au kunywa gongo au kuzurura! Huweza kuwasweka hata wiki nzima bila kuwafikisha mahakamani huku wakidai upelelezi haujakamilika.

3.0 Itikeli

Kwa muktadha wa makala haya itikeli ni murua yaani tabia ya uadilifu ambayo inamtenganisha binadamu na matendo maovu. Kulawiti ni miongoni mwa makosa makubwa mno ambayo dini zote zimeainisha pasi shaka yoyote. Na historia inaelezea jamii nzima nzima na kaumu zake zilivyohilikishwa kwa kushiriki lawiti. La ajabu ni kuwa kuna watu na mataifa yao ambao wamediriki, bila aibu, kuhalalisha lawiti. Na sio hapo tu, wamejaribu hata kupunguza umri wa kushiriki vitendo hivyo kutoka miaka kumi na nane hadi kumi na sita. Inadaiwa zaidi ya wabunge wa nchi yenye usongo na Robert Mugabe ni madheha!

Lakini chambilecho Mwalimu Nyerere: "Tamaa na heshima havitangamani". Tamaa inayowakumba viongozi na watu wengi ni ama ya pesa, vitu au kujitaanisi tu katika ufuska kama huu wa lawiti. Matokeo watu hao, hata wawe viongozi wakuu kiasi gani, huishia katika lindi la fedheha wakafa wanatemwa mate kwa kinyaa.

Banana alikuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe, ni kiongozi mkuu wa moja ya makanisa na alikuwa Mhadhiri wa Theolojia katika Chuo Kikuu Zimbabwe. Hivi leo amevuliwa vyeo vyote vile viwili kutokana na ufuska wake.

4.0 Unafiki

Jazaa ya mnafiki ni moto wa jahanam. Na mnafiki afaa aogopwe kuliko adui wa kawaida. Waama mnafiki ina maana pana, lakini yatosha hapa kutumia maana ya yule atendaye kinyume na anavyojifanya.

Unafiki ni mbaya kwa kila mtu lakini ni mbaya zaidi kwa viongozi hususan wa serikali na dini. Yafaa tutafakari hapa Tanzania kuna akina Banana wangapi serikalini, misikitini na makanisani!

5.0 Ujasiri

Kuna hadithi inaeleza kuwa Mtume Muhammad aliwaambia masahaba wake kwamba moja ya Jihad kubwa ni kuthubutu kumkosoa mtawala dhalimu. Hadithi hii inatufundisha na hakika kutusukuma kuwa wajasiri katika kutetea ukweli na haki zetu.

Kwa kufichua ukweli ndipo leo Banana analala gerezani kutumikia kifungo cha kulawiti. Inasikitisha mno kuwa kwa zaidi ya miaka minne Banana alimgeuza mlinzi wake kuwa 'mke' wake kwa kutumia vitisho. Wengi tungesema laiti kijana yule angemaizi na kufuata funzo la kukaidi uonevu, basi katu asingefikwa na hali ya kugeuzwa mke wa Banana. Kwa hakika ingekuwa aula zaidi angeielekeza bunduki yake dhidi ya Banana kuliko yule kijana aliyemtanabahisha ukweli kuwa alikuwa mke wa Banana. Pamoja na yote hayo, pia ni vizuri kutambua ujasiri wa kijana huyo kusema ukweli dhidi ya Banana licha ya kuchelewa na hakika, kuafiki, kufanyiwa vitendo hivyo.

Tujiulize basi Watanzania wangapi ambao ni jasiri wa kukataa kufanyiwa udhalimu na kunyang'anywa haki zao? Na wangapi watakubali kufichua, kwa kinywa kikuu, maovu yote ya viongozi wa serikali au wa kidini?

Kwa mustakabali huu huu basi, ni bora kuwapongeza wote pamoja na viongozi wa siasa na dini ambao wanapinga udhalimu wa kila aina bila kuogopa anayeufanya. Na ni bora kuwabeza wale wote wanaogeuka mabubu kugubika uovu kwa sababu za woga tu au tamaa. Kwa hakika watu wenye tamaa kama hawa ni akina Banana wa aina nyingine. Yafaa kuwaanika wazi kabisa na kujitanibu nao kama hawajirakibishi.

6.0 Uhuru wa Mahakama

Mahakama yana nafasi adhimu katika kuhakikisha utawala bora. Kwa sababu yeyote ambaye anaona haki zake zinadhulumiwa basi tegemeo lake ni mahakama. Lakini ni pale mahakama yanapokuwa yana uhuru wa kuamua kwa mujibu wa sheria sio vitisho au hofu ya watawala. Kadiri tunavyokumbuka utendaji wa mahakama za juu za Zimbabwe kuanzia 1980 umedhihirisha namna yalivyoweza kusimama kidete katika mashauri mazito. Kwa uchache wa muda bora kutoa mifano mitatu tu.

Kwanza ni kuwa mara baada ya uhuru 1980 wazungu kadhaa walishtakiwa kwa ujasusi dhidi ya serikali mpya. Lakini mahakama yaliwaachia washtakiwa hao kwa kukosa ushahidi wa kuwatia hatiani. Kitendo hicho kiliiudhi serikali. Tena basi wakati huo Rais wa Zimbabwe alikuwa huyu huyu Banana. Waziri Mkuu alikuwa Robert Mugabe ambaye ndiye Rais wa Zimbabwe kwa sasa. (Ama kweli historia hujirejea!). Bila ya aibu yoyote serikali ya wakati huo ilituma polisi na kuwatia hatiani washtakiwa wale tena ndani ya jengo la mahakama. Historia inatuonyesha tena kuwa wakati huo Jaji Mkuu wa Zimbabwe alikuwa Philip Telford Georges. Inasemekana Jaji Mkuu Georges aliajiriwa huko Zimbabwe baada ya sifa kem kem za utendaji bora hapa Tanzania kutoka kwa Mwalimu Nyerere. Kitendo cha kukamatwa washtakiwa ndani ya mahakama kilimkifu mno Georges. Baada ya mtafaruku kati yake na Serikali ya Zimbabwe kuhusu suala hilo Georges alijiuzulu.

Georges alijiuzulu kutokana na dhana na kanuni adhimu ya uhuru wa mahakama.

Kesi nyingine ilikuwa ile ya Edgar Tekere ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa ZANU-PF. Tekere alishtakiwa na wenzake kwa mauaji ya mzungu mmoja mara baada ya uhuru. Lakini mawakili wake walidai kuwa mashtaka dhidi yake ni batili kwa vile Sheria Dhidi ya Ugaidi iliyopitishwa na serikali ya walowezi wa wakati ule, ilikuwa inampa kinga. La muhimu hapa ni kuwa idadi kubwa ya majaji wa Zimbabwe wakati ule walikuwa wazungu. Itakumbukwa tena kuwa hali hiyo ilisababisha tena Jaji Mkuu wetu wa sasa Barnabas Samatta na mwenzake Jaji Rufani Mstaafu Lameck Mfalila kuazimwa na Serikali ya Zimbabwe. Bila ya kujali tofauti za itikadi baina yao na Edgar Tekere majaji wale, kwa uhuru kabisa, waliafiki kuwa Tekere na wenzake walikuwa na kinga dhidi ya mashtaka yanayowakabili.

Kesi ya tatu ndiyo hii ya Banana.

Mbali na uhuru wa mahakama sakata hili linadhihirisha namna ambavyo shauri hili limepelelezwa, kuandeshwa na kutolewa hukumu katika ngazi zote za utekelezaji wa sheria. Hivi leo Tanzania kuna watuhumiwa wa kesi za mauaji nchi nzima ambao wamegoma kula kutokana na kucheleweshewa kesi zao. Pale Keko miezi miwili tu iliyopita mahabusu wa aina hii zaidi ya kumi walikuwa manusura kufa kwa kugoma kula. Ikabidi wawekewe maji kwa njia za mpira na sindano. Sababu kuu ya ucheleweshaji wa mashauri yao ni nyingi lakini 'maarufu' ni kutokamilika kwa upelelezi, na siku hizi ukosefu wa karatasi.

Kuna baadhi wanaweza kudai kuwa kesi ya Banana imesikilizwa upesi kwa vile yeye alikuwa Rais wa zamani. Lakini hapa kwetu kuna kesi nzito za mawaziri wa zamani ambao kila uchao hupigwa kalenda. Ingekuwa vyema mno kama nazo zingesikilizwa upesi kama kesi ya Banana bila kujali matokeo: iwe kutiwa au kutotiwa hatiani kwa watu hao wakubwa! Vinginevyo dhana inayojengeka ni kuwa mashauri kama hayo ni kiini macho; chambilecho Wahindi: "Danganya toto, kula kunde bichi."

Na inatia shaka zaidi pale mtuhumiwa wa cheo anapovutwa karibu na mkuu wa nchi ilihali anakabiliwa na tuhuma nzito za rushwa! Wahindi pia wana msemo: Janja ya paka kwisha tambua, fika jikoni, piga piga makia!. Kwa kifupi watu hudhani hapa kuna mushkeli mkali.

Lakini sakata hili pia lina funzo jingine kubwa katika masuala ya dhamana. Mara baada ya kutiwa hatiani Banana alipewa dhamana wakati akisubiri matokeo ya rufani yake. Utaratibu huu pia ndiyo uliotumiwa na Mahakama Kuu ya Afrika Kusini katika kesi ya wizi dhidi ya Mchungaji Allen Boesak. Itakumbukwa pia kuwa wiki iliyopita tu ndipo Allen Boesak alipoanza kutumikia kifungo chake baada ya Mahakama ya Rufani ya Afrika Kusini kutupilia mbali rufani yake.

Kesi hii ya Banana na Mchungaji Boesak ni mafunzo makubwa kwa mahakama zetu za ngazi zote. Sheria ya dhamana ya Tanzania inaeleza waziwazi kuwa dhamana huweza kutolewa na polisi kabla hata shauri kupelekwa mahakamani. Na mahakama nayo yanaweza kutoa dhamana mara shauri linapofikishwa mbele yake. Lakini zaidi ya yote, sheria pia inaruhusu mtu kupewa dhamana kabla rufani yake kusikilizwa kwa masharti ambayo sheria imeyaweka. La ajabu ni kuwa mahakama yetu hayana utamaduni wa kutoa dhamana kabla ya kusikilizwa rufani. Mfano mzuri ni kuwa Mahakama Kuu ilikataa kumpa dhamana Mchungaji Christopher Mtikila wakati akisubiri matokeo ya rufani dhidi ya kesi yake.

Suala la masharti ya dhamana na athari zitokanazo na kukataa kutoa dhamana ninalizungumzia kwa kirefu katika kitabu changu kipya Mashtaka ya Jinai na Utetezi ambacho kilipata kutolewa na gazeti hili la Annur kwa awamu. Ninachotaka kusisitiza hapa ni kuwa utafiti hapa Tanzania unadhihirisha kuwa asilimia hamsini ya rufani zote hukubaliwa. Lakini kinyume na matamko ya kimataifa kuhusu haki za binadamu, serikali haitoi fidia kwa mtu ambaye ametumikia kifungo kabla ya rufani yake kusikilizwa na kushinda. Hatari kubwa zaidi ni kuwa kutokana na ucheleweshaji mkubwa wa mashauri ya jinai katika ngazi zote za mahakama, rufani nyingi husikilizwa na kutolewa hukumu baada ya watuhumiwa kutumikia kifungo.

7.0 Msamaha wa Rais

Karibu katiba za nchi zote, pamoja na Zimbabwe, zinampa Rais uwezo wa kumsamehe mtu ambaye ametiwa hatiani kwa kosa la aina yoyote ile. Hapa Tanzania kila mwaka Rais hutumia mamlaka yake hayo kuwasamehe anaoona wanastahili msamaha huo. Hivi sasa wachunguzi wanasubiri kuona iwapo Rais Mugabe atamsamehe Banana adhabu aliyoanza kuitumikia. Kwa kweli kama ilivyoelezwa hiki ni kitendawili kikubwa kutokana na msimamo mkali wa Mugabe dhidi ya mashoga. Je, atalegeza msimamo wake huo kumnusuru mkuu wake wa zamani?

8.0 Hatimisho

Kwa hiyo basi kesi ya Banana ina mafunzo makubwa kwa viongozi wa serikali ya Tanzania, viongozi wa dini na wananchi wote kwa jumla katika maeneo ya utawala wa sheria, utendaji bora wa polisi, ujasiri, unafiki, uhuru wa mahakama na tamaa kama ilivyoainishwa kwa muhtasari hapo juu. Yatosha tu kusisitiza tena kwamba utawala wa sheria ndiyo mhimili wa utawala bora. Sheria ni msumeno. Ni lazima itumike bila kujali itikadi wala cheo cha mtu kama ambavyo imejionyesha mara nyingi nchini Tanzania.

Hii leo magereza yamefurika vijana ambao yawezekana wamebambikiziwa makosa wakati sehemu kubwa ya viongozi wanaishi kwa vipato ambavyo dhahiri ni nje ya uwezo wao! Kesi za mahabusu zinachukua hata miaka kumi kusikilizwa. Magereza yamejaa idadi kubwa ya wafungwa na mahabusu karibu mara tatu zaidi ya uwezo wake. Chakula ni kichache hivyo kusababisha wafungwa na mahabusu wanyonge na watoto kugeuzwa 'wake' za wafungwa na mahabusu wakubwa. Magazeti ya nchi hii yamejaa simulizi za kutoa machozi za namna ambavyo vijana na watoto ambao wanastahiki kuwa shuleni, wanageuzwa wake katika magereza. Mahakama nayo hukazana kuwanyima dhamana washtakiwa bila ya kujadili matatizo ya polisi pamoja na mazingira mabaya mno magerezani. Dhamana kabla ya rufani ni kioja kutolewa na mahakama za nchi hii ingawa sheria iko wazi kuhusu jambo hilo.

Aidha, tunajifundisha kujitanibu na unafiki wa kila aina na kujikita katika kutetea haki kwa udi na uvumba. Na hatimaye tunajifunza pia kuwa tamaa mbele mauti nyuma.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook