KABLA ya mkutano hapa nilikuwa nazungumza
na Mwenyekiti wetu wa Dodoma mjini akinikumbusha harakati za wafanyakazi
wa Reli kabla ya kupata uhuru.
Wakati ule mzee Christopher Kassanga Tumbo akiwa Katibu Mkuu wa Wafanyakazi wa Reli wa Tanganyika, wafanyakazi wa Reli walifanya mgomo ulioitikisa Serikali ya wakoloni.
Na kwa kweli uti wa mgongo wa chama cha TANU ulikuwa wafanyakazi hawa wa Reli, ndiyo waliokipa chama cha TANU nguvu katika mapambano yake na mkoloni ili nchi hii ipate uhuru.
Kwa hiyo wananchi wakati huu, leo ikiwa mwaka wa 2000, ni wakati muafaka kabisa wa kufanya tathmini ya miaka 40 ya uhuru wa Tanganyika na Tanzania.
Wazee waliokuwa vijana miaka ya 50 na 60 nadhani wanakumbukumbu, serikali ya mtanganyika ilimsuta mkoloni ikamueleza, ikawaeleza wakoloni tupeni miaka 10 ya uhuru, ikiwa Tanganyika itajitawala kwa miaka 10 itafanya mambo mengi zaidi katika miaka 10 kuliko mkoloni wa kiingereza na mkoloni wa kijerumani waliyoyafanya kwa muda wa miaka 75.
Wazee nadhani mnakumbuka ahadi hii na msuto huu tuliowasuta wakoloni kwamba tukipewa miaka 10 ya kujitawala, serikali ya watanganyika itafanya mambo mengi zaidi katika miaka 10 kuliko mambo waliyoyafanya wakoloni kwa muda wa miaka 75.
Sasa ni miaka 40 si miaka 10, miaka 40 ya utawala wa chama kimoja, Serikali ya chama hicho hicho ndiyo iliyoendelea kutawala tangu mwaka 61 mpaka hivi leo. Vile vile tulipokuwa tunatafuta uhuru sababu za kutafuta uhuru tulizokuwa tukizitoa ilikuwa ni kuboresha maisha ya mtu wa kawaida.
Tulipokuwa tunatafuta uhuru, tulisema tuna maadui watatu; ujinga, maradhi na umasikini, kwamba serikali yetu itapambana na maadui watatu. Sasa tuna miaka 40 ni nini hali ya maadui hawa watatu; ni nini hali ya umasikini wa Tanzania, ni nini hali ya umasikini wa wananchi wa Dodoma.
Wananchi wa Dodoma katika ulimwengu huu wa leo, karne hii ya 21, ukiorodhesha nchi za ulimwengu ambazo hazina vita vy ndani kama vile Ethiopia,Eritrea, Siera Leon, Liberia, Congo. Ukiorodhesha nchi ambazo hazina vita vya ndani, nchi zinazoongoza kwa umasikini, nchi ambazo ni nambari wani kwa umasikini ni Tanzania. (Makofi).
Kama CCM ni nambari wani, basi ni nambari wani kwa kuwaletea watanzania umasikini wakawa ni nambari wani kwa umasikini. (Makofi).
Wananchi, hali ya umasikini wa Watanzania inatisha. Miaka 40 baada ya uhuru ukiwachukua watanzania 100, uwachukue bila ya kuchagua, 50 watakuwa ni masikini wa kutupa, wako hoi taabani.(Makofi). Hawana uhakika wa mlo wao wa siku.(Makofi).
Wananchi miaka 40 baada ya uhuru, katika kila watanzania mia moja, hamsini ni masikini, na Tanzania kwa mali asili ina bahati kubwa. Tanzania in ardhi, ina maeneo yenye hali ya hewa mbali mbali bali mazao yanayokubali Tanzania ni mazao ya aina mbali mbali.
Ukitazama katika nchi za kiafrika katika takwimu ya mazao yetu tuliyokuwa tukiuza nchi za nje, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi ambayo zilikuwa na mazao ya aina mbali mbali yanayouzwa nchi za nje. Kulikuwa na katani, pamba, kahawa, korosho, chai, karanga, ufuta, ngozi, nyonyo, asali, nta.
Katika nchi ambazo zina mazao ya aina mbali mbali ya kilimo ambayo yanaweza kuuzwa nchi za nje, Tanzania ilikuwa na mazao ya kila namna, na Tanzania ina mabembe, mito na maziwa. Tanzania ina bandari sio kama Uganda ambayo gharama zake za usafiri ukiagiza kitu toka nchi za nje, gharama za usafiri zinakuwa kubwa mno, kwa hiyo nafasi ya kuweza kuiendeleza nchi ni ngumu zaidi. Sisi tuna bahati, tuna bandari nne. Kwa hiyo kwa mali asili, Tanzania ina bahati kubwa.
Madini, tuna almasi, tuna dhahabu na hivi sasa uvumbuzi yakinifu uliofanyika wa dhahabu katika Afrika madini ya dhahabu, Tanzania ni ya pili baada ya Afrika kusini.(Makofi). Tuna makaa ya mawe, tuna madini ya aina mbali mbali, kwa hiyo Tanzani haiwezi kulaumu kwamba haikujaaliwa madini, haikujaaliwa ardhi. Umasikini wetu sio laana ya Mwenyezi Mungu, ni laana ya CCM (Makofi).
Wananchi wa Dodoma tuelewe kwamba, matokeo ya umsikini wa Tanzania ni sera, sera mbovu na tutazizungumzia hizi Sera. Miaka 40 baada ya uhuru hali ya umasikini wa Tanzania inatisha. Na kwa kweli hatuna sababu ya kuwa na umasikini. Hakuna ajira, vijana 700,000 kila mwaka wanaingia kutafuta kazi, kazi rasmi zinazoanzishwa nchi nzima hazizidi 20,000 na Wananchi serikali yetu haina Sera ya kukuza ajira ina sera ya kupunguza ajira.
Na wananchi ikiwa Serikali itafanya mipango, viwanda vikaanzishwa hapa, vikaongeza ajira ya watu waliostaafu, kila mmoja akawa anapata wastani wa mshahara wa shilingi 50,000 kwa mwezi watu 5000 ni kwamba mwisho wa mwezi Dodoma patakuwa na ongezeko la shilingi 250,000,000.
Kama patakuwa na wafanyakazi 5000 wameongezeka wakawa wanapata mshahara wa wastani wa shilingi 50,000 kutakuwa na ongezeko la kipato cha shilingi milioni 250,000,000. Sasa hawa wafanya kazi watahitaji kununua vitanda, watahitaji kununua viti, seremala naye atapata ajira. Akiuza viti atapata ajira, atahitaji vijana wengine wa kumsaidia kusudi atengeneze viti vya kutosha aviuze. Fundi cherahani kuna watu wanataka kushona suruali au shati au gauni au anataka kupunguza mtumba kama suruali kubwa anataka kupunguza, fundi cherahani naye atapata ajira. Hata muuza mchicha, muuza nyama kama kuna shilingi milioni 250,000,000 zimeingia mjini huyu naye atapata soko
Watu 5000 wangepata ajira wenye kipato chenye hakika kila mwezi, watasababisha watu wengine 10,000 waweze kufanya biashara, waweze kupata ajira. Na kama utapunguza watu 5000, ukapunguza milioni 250 seremala aliokuwa mchapa kazi kweli kweli, anatengeneza viti vizuri, anatengeneza makochi mazuri, makochi hayo hayatauzikana. Pamoja na ustadi wake wa kutengeneza makochi, pamoja na juhudi zake za kufanya kazi, kama hakuna mzunguko wa fedha katika uchumi, seremala atakosa kazi, pamoja na kwamba ni mjuzi, fundi muashi naye atakosa kazi, pamoja na kwamba ni mjuzi wa kujenga nyumba, watu watapoteza ajira. Ukipunguza kazi watu 5000 una sababisha 10000 wengine wakose kazi.
Kwa hiyo ni muhimu kabisa katika sera, serikali iwe na sera za makusudi za kuongeza ajira. Kama serikali haina sera za makusudi za kuongeza ajira, haiwezi ikapunguza umasikini.
Ndugu wananchi serikali yetu na hasa katika kipindi hiki imekuwa haina sera ya kujaribu kuongeza ajira katika nchi, matokeo yake "ukapa" umetapakaa.
Nyie wenyewe mnaweza mkajitazama, tazama zile senti ulizokuwa nazo 1995, jipapase mifukoni mwako jiulize leo mtu uliyekuwa unamuomba akukopeshe 500 anakupa 2000, leo mueleze akupe 100 hana! Leo Mtu akikupa 2000 unamshukuru utadhani umefunguliwa milango ya pepo, pamoja na kwamba hii 2000 haifiki popote, hali ilivyokuwa ngumu.
Hali ya umeme wa Tanzania inatisha. Sera ya elimu ya Tanzania ya makusudi ilikuwa kwamba, elimu anayostahiki kijana wa Tanzania, ndoto na njozi ya kijana wa Tanzania ilikuwa ni elimu ya darasa la saba, asome mpaka darasa la saba arudi kijijini akajiunge na kijiji alime kwa jembe la mkono. Kwamba kijana wa Kitanzania hastahiki elimu ya sekondari, matokeo yake wananchi wa Dodoma ni ya hatari. Katika Dunia ya leo ukichukua uwiano wa vijana wenye umri wa kwenda Sekondari miaka 14, miaka 18, vijana wenye umri wa kuwa shule za sekondari na wale vijana walioko shule za sekondari Tanzania ni ya mwisho.
Katika kila vijana 100 wenye umri wa kuwa sekondari, vijana saba, vijana saba tu ndio wako sekondari.
Mkoa wa Dodoma nadhani una shule za sekondari kama 22 miaka 40 baada ya uhuru na kwa Dodoma vijana wenye umri wa kuwa shule sekondari ukilinganisha na wale vijana walioko shule za sekondari, nadhani kuna vijana wanne katika kila vijana 100 ndio wako shule za sekondari na wengi wa vijana hawa ni wageni wageni watoto wa watumishi wa serikali.
Hata elimu ya msingi, elimu hiyo ya darasa la saba tuliowahakikishia, hivi sasa kuna vijana wa kitanzania wenye umri wa kuwa shule, vijana zaidi ya 2, 500,000 hawako shule za msingi. Kuna vijana hapa mkoa wa Dodoma wanaofukuzwa shule za msingi kwa sababu hawana ada. Na maendeleo shule za msingi yanazidi kuporomoka, katika kila vijana 100 wanaopaswa kuwa shule za msingi hapa Dodoma ni vijana 55 tu walioko shuleni, vijana 45 hawataenda shuleni. Na hawa 55 wanaoenda shuleni elimu yao imeporomoka. Muulize kijana yeyote wa darasa la saba 9 x 7 ngapi, hali ya elimu inatisha.
Mimi nilipokuwa shule ya msingi, mwalimu katika kijiji chetu alikuwa mtu wa juu sana mtu anayeheshimika sana, wanafunzi tunafikiri tujitahidi kusoma ili tuwe kama mwalimu fulani, tuwe kama mwalimu John, tuwe kama mwalimu Juma, mwalimu alikuwa nadhifu. Jana tulipokuwa tumetokea Gairo kwenda Mpwapwa tunapita njiani asubuhi, unapotegemea watoto akili yao bado nzuri watakuwa darasani, tunaona msururu wa watoto wanaenda shamba, asubuhi kipindi cha kwanza ni kwenda shamba. Kusoma ni kudogo waalimu wako hoi. Mwalimu hivi sasa sio kielelezo, mtoto anaweza kusema nataka niwe kama mwalimu huyu. Mwalimu anaonekana kama ni balaa, waalimu wako hoi. Unaingia darasani Mwalimu kandambili kafunga waya(makofi).
Mwalimu unamtazama, unamueleza kijana jitahidi uwe kama mwalimu huyu kijana anaona unamtakia nini hasa yeye.
Itaendelea Ijumaa
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |