Na Kivuruga Nguzo
MUNGU hana choyo. Yeye amemjaalia kila mtu aliyekamilika, kuwa na uwezo na ujasiri wa kuyakabili magumu kwa uvumilivu na subira na mwishowe kuibuka akiwa mshindi.
Katika kupanda, kuotesha, kupalilia na kuwekeza mbegu ya harakati ya kujiweka huru, au kuondoa bendera ya uhuru wa wachache wanaowatia utumwani walio wengi, kutokata tamaa ndiyo moyo unaosukuma damu ya mafanikio.
Cha msingi ni kuweka nia pamoja na mikakati ya kujinasua bila kuzembea, iwekwe jitihada kunyanyua mguu, kukata mgororo, kuvunja wigo na kupiga hatua kuelekea kwenye ngome za wakandamizaji.
Kunahitaji moyo na ujasiri wa kuyaendeleza matokeo mazuri ya kutoka minyororo hadi kuwazingira makupe waliotuweka zizini wakatufanyisha kazi na kuwanenepesha kwa ujira wa kufa njaa, kukos na kikundi cha wakimbizi wanaoweza kuswagawa na kufanikiwa kuwadhibiti wasiwepo nchini. Wapo mamilioni, wanachotakiwa ni kujipanga safi na kusonga mbele kwa namna itakayowatatiza wasifanye uharibifu wananchi pale wanapozuia sahani ya mlo isiwaondoke.
Wakati wa kusonga mbele wimbo uwe, "Anayekubali kushindwa sio mshindani". Lengo kila mwananchi aelewe kuwa kukata tamaa ni sawa na kukaza kitanzi shingoni. Ni sumu inayoua akili na moyo vifanye jitihada za kujing'oa kwa makucha.
Kiasili muhimu katika mbolea ya kustawisha mmea wa kujikomboa ni ule moyo wa matumaini na yale mapigo yake ya kutokabali kushindwa.
Hili likizingatiwa husukuma mwendelezo wa jitihada za kukuza nguvu chipukizi ya wananchi kufikia kileleni ambapo kila mtu ataona, kutumia na kufurahia utamu wa matunda yake.
Ni nani hivi leo asiyejuwa kuwa utawala wakikoloni wa waliovamia ardhi yetu kutoka Ulaya ulistawi kwa kujichimbia chini mizizi yake kana kwamba haukupandikizwa.
Je, haukung'oka, ni nguvu ipi iliyowatoa kwenye makasiri na kuwafanya wafungashe virago bila ya kupenda? Leo hii tunawasoma kwenye mabuku ya historia.
Wananchi wana nguvu, wakiamua wanaweza kuitumia kujitia utumwani wakikata tamaa kwa kudhani kuwa ni Mungu aliyeshinikiza nguvu zao ziwatumikie na kuwanawirisha wakongwe wachache.
Ikidhaniwa Mungu ndiye anayewadumisha kwenye viti viongozi wa utawala usiojali wananchi itakuwa ni kumsingizia. Si Yeye anayewatia njaa, umaskini, maradhi na ujinga. Maana ameweka kanuni kuwa mwananchi hatovuna ila kile alichokitolea jasho na atayaona matunda yake.
Ni katika kanuni hii tunawakuta wazee wetu wameibuka na ushindi dhidi ya ukandamizaji wa watu weupe. Walifanya jitihada za kuamshana mpaka wote wakatambua dhuluma waliyotendewa haikupangwa na Mungu.
Wakawaambia mabwanyenye wa kikoloni kuwa mmetunyonya vya kutosha. Sasa tunataka jasho la kodi zetu lijenge na kuboresha afya za wananchi, nasi tupatiwe mlo kamili. Mapato ya utalii, madini, misitu, kilimo, uvuvi na viwanda yabadili vidungu tunavyoishi ziwe nyumba.
Ile hali ya kusema 'sawa Bwana mkubwa' na kuwatungia nyimbo, ngonjera na mashairi ya kuwasifia wanyonyaji wa kikoloni wakaikomesha.
Lakini tukijitathmini tulivyonufaika wananchi tangu wazungu waliposhusha bendera na kufunga virago vyao. Uhuru ule uliopatikana kwa jasho la babu zetu umetekwa nyara na 'wenzetu' wachache.
Ningependa kutoa ushahidi wa kuthibitisha hili. Wananchi wa mikoa ya Tabora, Kigoma, Mtwara, Rukwa, Pwani, Morogoro watakuwa miongoni mwa wawakilishi katika kulithibitisha.
Wale waliuza wananchi kwa kupewa ruzuku na kuvalishwa sare maalum nisingependa ushahidi wao. Hata huko awali, walikuwepo wasaliti waliowapiga bei wananchi na kuwa vipaza sauti kutetea ukoloni.
Wananchi wa sasa, Mungu katupendelea, ule msemo wa mwanzo mgumu hautugusi. Hatuanzi alifu kwa ujiti kama waliotutangulia.
Ni rahisi kuwaengua wenzetu walioimarisha ukoloni wao miaka arobaini sasa tangu aondoke Muingereza. Ipo njia ya kuwatoa kiungwana.
Kwa kuwa tuanwajuwa wao na kuyaonja yale wanayotufanyia, hatuhitaji wapoteze muda kutambua wamefanya nini. Itakuwa ni sawa na kumwuliza kibaka anayekusukumia makonde na kukusachi "eti unaniibia?".
Imekuwa bahati kuwa, kwa vitendo vyao wenyewe wanajua kuwa hawana cha kuwaeleza wananchi, wanatumia muda mwingi majukwaani kutoa vitisho eti kuna wananchi wasiopenda amani wanaotaka kuleta vurugu.
Na kama mafanikio ya utawala ni kufutiwa madeni, wananchi tuubane kwa maswali: Tangu Mjerumani ajenge reli ya kati ni lini wananchi wa Tabora, Kigoma, Shinyanga, Mwanza na Kagera walikopa pesa wakatengeneza barabara?
Je, wanaochangia maji ya msimu ya kuchangia na ng'ombe kwenye vidimbwi mtawaelezaje. Mtawaambia nini wanaopata maji ya mgao katika jiji.
Wapo wananchi wanaoponyeka kwa mwarobaini pindi washikwapo na maradhi. Bado haupatikani kila mahali na maradhi yote yanayoponyeshwa. Japo si kwenda nje ya nchi wangalipenda kupata matibabu hayo ndani ya nchi kwa kodi zao.
Hakuna uwezo wa kumpa mwananchi dawa na matibabu ya bure, anatakiwa kuchangia. Wale wanajisifu na kutangaza mafanikio ya kukusanya kodi hujipa ufadhili.
Cha kushangaza, upo uwezo wa kodi za wananchi kutumika kwa mamilioni nje ya nchi kugharamia matibabu vigogo au kujua (check) kama wanaumwa. Hakuna hospitali nchini?
Mungu hana choyo. Wananchi watapata na kuonja
matunda ya kile walichokifanyia jitihada.
Na Amri Ramadhani
TUKIWA tumebakiwa na miezi michache kufikia uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, tumeanza kushuhudia matumizi ya mbinu mbalimbali ya kujijenga kisiasa.
Mbinu hizi zinazotumiwa na wanasiasa zimekuwa zikishamiri kufuatana na dhiki au faraja inayopatikana dhidi ya nchi yetu. Kuna wakati nchi yetu ilipokumbwa na mafuriko ya mvua za El-Nino. Kipindi hiki tulishuhudia wanasiasa hao wakisifia utawala na kudai kuwa hawatafikia ahadi walizoahidi walipochaguliwa eti kwa sababu za mafuriko yale.
Ukame ulizikumba sehemu za wafugaji. Wafugaji hao wakaamua kuuza mifugo yao kwa wingi kwa sababu kwanza hawakuwa na malisho ya kulisha mifugo yao na pili hawkauwa na chakula, hivyo njia rahisi ilikuwa kuuza mifugo hiyo ili wanunue chakula. Wakati huo tulisikia serikali iliyoko madarakani ikijigamba eti imedhibiti mfumuko wa bei kwa nyama kushuka hadi kufikia shilingi 600 kwa kilo moja.
Sasa ukiangalia utagundua kwamba serikali yetu inangoja matukio ili ipate umaarufu. Nyama ile kama nilivyosema hapo juu ilishuka bei kwa sababu ya ukame uliozikumba sehemu za wafugaji na wala ukame ule haukusababishwa na chama tawala au serikali.
Hivi karibuni mashirika ya fedha za kimataifa na nchi wahisani kwa pamoja zilipitisha azimio la kuzipunguzia sehemu ya madeni nchi maskini sana duniani. Azimio lile halikuwa na sharti la kwamba asamehewe anayelipa tu. Lengo ni kuzisamehe nchi masikini bila kujali kasi ya uliopaji wa madeni ya nje.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosamehewa sehemu ya madeni yake. Katika mkumbo huo Tanzania imesamehewa shilingi trilioni 1.6 kati ya shilingi trilioni nyingi ilizokuwa ikidaiwa.
Kwa kuwa msamaha huu umekuja wakati serikali iliyoko madarakani inamaliza muda wake, hadithi inataka kuwa tofauti. Kuna baadhi ya watu wanataka kunasibisha msamaha huo na juhudi za Rais Mkapa za kulipa madeni ya nje hivyo kutaka jamii ya Watanzania waamini kwamba CCM ni chama kinachotoa viongozi makini wanaoweza kutufanya tusamehewe madeni.
Tunaweza kukubali hilo, lakini watujibu maswali haya: Je, hizo nchi zingine zilizosamehewa madeni nazo zina uongozi imara kama wa CCM ya Tanzania? Kama zina uongozi imara kama wa CCM mbona Senegal pamoja na kusamehewa madeni tayari chama tawala kilichoongoza "mafanikio" hayo wananchi wa nchi hiyo wamekikataa?
Msamaha huo uliotolewa kwa nchi maskini kabisa za Afrika, Pasifiki na Carribean (APC) hata hivyo unaelekea ni kiini macho tu na mbinu mpya za mashirika hayo ya fedha na nchi wahisani kuendelea kuzinyonya nchi changa.
Kwanza wametusamehe fedha ambayo ni ongezeko la riba tofauti na kiwango tulichokopeshwa na pili wanajua fika kwamba kiwango kilichobakia hakiwezi kulipika dahari.
Wananchi wachague viongozi ambao watatumia siasa kama chombo cha uzinduzi cha kuwatoa watu katika sera za umaskini, ufukara na udumavu wa mawazo na badala yake kuwaelekeza kwenye matumaini ya maisha bora, yenye neema, ubunifu na haraka ya maendeleo halali yenye tija.
Viongozi watakaowaongoza Watanzania kwa kuwapa uwezo wa kujiongezea taaluma na mbinu za kuishi pamoja katika jamii ya leo ya kimaendeleo, yenye utawala wa sheria na kujenga imani ya maamuzi ya kidemokrasia na maisha ya haki sawa kwa wote.
Siasa ndiyo inayotakiwa kuutumikia uchumi, kwa maana kwamba wanasiasa wapate sifa na kuchaguliwa tena kutokana na jinsi walivyotatua matatizo ya uchumi ya nchi zao na raia wao badala ya kungoja "neema" ya kusamehewa madeni. Tukisamehewa madeni tutawapongeza waliotusamehe, siyo viongozi wetu waliokopa.
Mazingira ya sasa ya Tanzania yanahitaji viongozi watakaosikia kilio cha watu wa chini kuliko kilio cha watu wa nje. Umefika wakati tuwe na viongozi wabunifu wa mambo ya uchumi ili rasilimali zetu zitumike ipasavyo kuinua maisha ya wananchi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |