Aheri ya unyapara kuliko mizengwe

Na Ahmed Hussein

MARA kadhaa viongozi wetu wamekuwa wakisikika au kuripotiwa kusema kuwa wahisani wasitushurutishe kinyume na matakwa yetu.

Si hivyo tu, hata wapinzani nao wameonywa kuwa wasijipe matumaini ya kwenda Ikulu kwa mgongo wa wahisani.

Nao watazamaji kutoka nje pia wametahadharishwa kuwa wasijekuwa wanyapara.

Kwa ujumla, kauli zote hizo zinaficha fumbo fulani ambalo lahitaji tafakari ya wananchi. Wao kama wapiga kura, kimsingi ndio wenye haki ya kuamua nani wawe viongozi wao.

Hivyo, yabidi wajiulize, ni kwa namna gani wahisani hao wataweza kufanya khiyana ya kuwadhulumu haki yao hiyo ya kidemokrasia.

Je, hao wahisani pia watapiga kura, na je, watajiandikisha kwa idadi gani kuweza kupiku kura za wananchi washindwe kupitisha viongozi wanaowataka.

Ama kwa kufanya mikutano ya hadhara kuwashawishi wananchi kuchagua viongozi, au je watakwiba kura na kuwahonga wananchi.

Majibu ya maswali hayo ndiyo yatakayotuwezesha kuielewa mantiki ya kauli ya Rais, na kwa 'kuing'amua' mantiki hiyo ndipo tutakapoweza kufumbua fumbo la onyo la Rais kuwa tusichaguliwe viongozi kwa matakwa ya wahisani.

Sote tunakubali ukweli wa kidemokrasia kuwa wahisani au kwa jina lingine wafadhili hawana haki ya kupiga kura katika uchaguzi wetu. Kwa hiyo hawana hiyari wala uwezo wa kutuchagulia viongozi wanaowataka.

Isitoshe, wenye haki ya kulalamikia suala la kuchaguliwa viongozi ni wapiga kura. Wao ndio wanaostahiki kumkemea na kumchukulia hatua mtu yeyote yule mwenye azma ya kuhujumu maamuzi yao yanayowakilishwa na kura zao.

Ni muhimu ielezwe wazi ni kwa njia gani wahisani watatuwekea viongozi kinyume na ridhaa yetu. Na labda itakuwa jambo la busara zaidi tukipata ufafanuzi wa wazi juu ya mahusiano baina ya wahisani na wapinzani.

Hatudhani kama kweli yupo muhisani anayeweza kugeuza matokeo ya kura zetu mbele ya macho yetu na mbele ya Tume ya Uchaguzi.

Na kama wahisani ni "vibaka" wa kura ni vizuri tufahamishwe na wao pia wafahamishwe. Itangazwe bayana kwamba wahisani wana mpango wa "kutupachikia" viongozi tusiowataka kwa wizi wa kura. Vivyo hivyo kama wahisani wana njama za kuhujumu uchaguzi wetu kwa rushwa tuelezwe.

Kwa mtazamo wangu, wahisani hawana sifa zote hizo chafu zaidi ya hivyo serikali ina uwezo na nyenzo za kutosha kudhibiti kitendo chochote cha kuhujumu uchaguzi wetu.

Kwa hali hiyo hata "unyapara" sio tu hauna nafasi bali asilani hauwezi kuathiri matokeo ya uchaguzi. Kidemokrasia na hata kikatiba usimamizi wa wageni katika uchaguzi haukiuki utaratibu na mamlaka ya Tume ya Uchaguzi.

Wanachokifanya wasimamizi hao hakitofautiani na kile wanachokifanya wasimamizi katika vyumba ya mitihani.

Hawa wasimamizi huwa hawana mamlaka ya kuongeza wala kupunguza alama za watahiniwa na hawana uwezo wa kupinga matokeo ya mtihani. Kwa maana hiyo hawana nafasi ya "kumpasisha" mtahiniwa wamtakaye au kumkwamisha yule wasiyemtaka. Sasa kama kuna mtahiniwa asiyependezwa na msimamizi basi huyo bila shaka ana ajenda ya siri.

Halikadhalika, "unyapara" wa wageni watakaosimamia zoezi la upigaji kura hauwezi kuathiri kwa namna yoyote maamuzi ya wapiga kura. Kinyume chake utawasaidia wapiga kura hao kupata haki yao ya kuwapata viongozi watakaowapa kura zao.

Kama kufanya hivyo ndiyo tafsiri ya "unyapara" wenyewe usiotakiwa basi tunalazimika kuamini kuwa huenda wanaotoa shutuma hizo wana ajenda yao ya siri ambayo inahofiwa itatibuliwa na wasimamizi hao wa kimataifa.

Kwa mantiki hiyo, kelele za viongozi dhidi ya wahisani zinamaanisha kwamba wahisani hao wanataka kutusaidia kupata viongozi wasiotakiwa na chama hicho.

Hii ina maana kuwa uchaguzi huru na wa haki ni msiba kwa chama fulani. Ndio maana viongozi wa chama hicho wamekwishatamka kuwa demokrasia haina maana ya chama tawala kushindwa uchaguzi. Inavyofahamika ni kuwa demokrasia kama dhana, haichagui mtu wala chama fulani bali inaweka mazingira bora ya uchaguzi.

Kwa kuwa wahisani mara kwa mara wamekuwa wakihimiza demokrasia na kwa kuwa viongozi wanakiona kitendo hicho kinalenga kutupatia viongozi "wasiotakiwa", basi ni wazi nguvu za wahisani zinahitajika mno ili demokrasia iweze kuleta matunda yaliyokusudiwa.

Nguvu ya mvutano baina ya wahisani wanaotaka demokrasia na viongozi wanaotaka uchaguzi wa "mizengwe" inaonesha wazi kuwa bila usimamizi wa wageni viongozi "wasiotakiwa" hata wakipigiwa kura zote wanaweza kukwama!

Basi tu umekosekana uwezo, lakini huko nyuma ilikwishatangaza kuwa uchaguzi wa mwaka huu ungegharamiwa na serikali. Ilionekana kuwa kwa kufanya hivyo, yangepata mazingira bora ya "mizengwe" dhidi ya demokrasia.

Ni jambo la kheri kwa wapinzani, wapiga kura na wanademokrasia kwa ujumla kwamba serikali imekwishanyoosha mkono kwa wahisani kufanikisha uchaguzi huo.

Na kwa bahati njema, wahisani wamekwishachangia fedha kwa madhumuni hayo, hivyo watakuwa na haki ya kusimamia kuhakikisha kuwa mapesa yao hayapotei kwa uchaguzi hewa.

Kwa kuwa wasimamizi wa nje hawaji kupiga kura wala "kuiba kura" hatuna sababu ya kuchelea "unyapara" wao kwa kisingizio cha "uhuru" wa nchi yetu. Kwa maana hiyo, tusiwakaripie bali tuwakaribishe kwa wema.

Nadhani ni aheri ya unyapara kuliko mizengwe.


Sheikh Mbukuzi atembelea Dodoma na kusema:
Demokrasia haihitaji kutunisha misuli

Na Mwandishi Wetu

DEMOKRASIA haihitaji silaha wala kuvimbisha misuli, Sheikh Mbukuzi amesema.

Akiongea katika Msikiti wa Nunge amesema, kinachofanyika ni kunoa fikra na kuwatambua viongozi wanaofaa.

Amewataka wananchi wasizugwe na kauli za wanasiasa, bali wapime kauli zao na matendo yao.

Sheikh Mbukuzi amehoji uadilifu wa serikali ya CCM inayojinadi inao huku ikiwepo rekodi ya mauaji ya Mwembechai.

Akiwa katika Msikiti wa Al-Hudaa, Chamwino, Sheikh Mbukuzi aliwataka Waislamu waache woga. Alisema, woga ukikithiri utaendeleza dhuluma.

Amewataka Waislamu wautangaze uovu wanaofanyiwa na wajizatiti kuuondoa.

Sheikh Mbukuzi alitembelea mjini Dodoma hivi karibuni ambapo pia aliongea katika Msikiti wa Manyema.


Walokole wasaidia vyuo vya mihadhara


Na Mwandishi Wetu

TAKRIBAN watoto wote shule za msingi jijini wanagawiwa Biblia.

Biblia hizo hugawiwa kwa watoto Waisalmu na Wakristo.

Ustadh Hamza Shabaan amesema Biblia hizo zitatumika katika darasa za kuwasomesha akina "Mazinge na Magezi" wengi.

Amesema, darsa mbalimbali zitafunguliwa ili kuwasomesha watoto namna ya kuzichambua Biblia hizo.

Ustadh Hamza alikuwa akiwahutubia Waislamu Msikiti wa Mabibo Ijumaa iliyopita.

"Fungua Wagalatia, mpe huyo" itakapohamia mashuleni, wasilete tena yale ya Mwembechai, ameonya Ustadh Hamza.

Amesema, wanaozigawa Biblia hizo wasitaraji Waislamu watayakubali yaliyomoj bila uchambuzi.

Zitachambuliwa ili kugundua upotofu na yaliyo ya kweli ili kuyaweka wazi.

Inatarajiwa kuwa zoezi hili la kuzitumia Biblia za bure kuendesha darsa litaongeza idadi ya wahadhiri wa Biblia.

Katika kipindi cha wiki zilizopita, Biblia zilisambazwa katika shule za msingi jijini Dar es Salaam.

Biblia hizo wanapewa wanafunzi Waislamu na Wakristo.

Katika baadhi ya mashule ulizuka mtafaruku. Waalimu wa somo la Maarifa ya Uislamu walikusanya Biblia walizopewa watoto wa Kiislamu.

Waalimu 'walokole' walikuja juu na kulazimisha watoto Waislamu warudishiwe Biblia zao.


Dhulma tupu

Na Mwandishi Wetu
 

DHULMA imestawi nchini kinyume na serikali inavyodai kuwa ni ya uadilifu.

Hayo yamesemwa na Ustadh Hassan Mtihani juzi katika kumbukumbu ya mauaji ya Mwembechai.

Ustadh Hassan amesema, katika kadhia hiyo alipigwa risasi na akanyimwa matibabu kwa siku kadhaa.

Amesema, pamoja na jeraha kubwa la risasi alilokuwa nalo, alipigwa sana katika kituo cha polisi Magomeni.

Ustadh Hassan amesema, mateso aliyoyapata, hataacha kamwe kuzungumzia haki.

Pamoja naye, alipigwa risasi Chuki Athumani ambaye baada ya kukosa matibabu alipooza.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook