BARUA ZA WASOMAJI:


Mfa maji haishi kutapatapa

Ndugu Mhariri

NAPENDA kuwahabarisha viongozi wa nchi hii kuwa tumechoshwa na vitisho vyao juu ya wimbo wa kuchanganya dini na siasa. Wamekuwa wakiwashutumu Waislamu kwa madai kuwa wanahubiri siasa misitini.

Baadhi ya Maimamu wanafikishwa vituoni kuhojiwa juu ya suala hili. Lakini sijasikia Padri hata mmoja au shutuma dhidi ya Kanisa lolote, na sio kwamba hawachanganyi dini na siasa kama wanavyosema.

Hii ni kuonesha ni jinsi gani wamezidiwa na wasipoangalia watajishushia hadhi kama wanavyofikiria mpaka wananchi watawadharau.

Je, hawaoni kwamba siasa na dini havitengamani? Jambo la pili ni kwamba Misikiti ilikuwa nyumba za ibada pamoja nakuzungumza masuala yote yaliyowahusu Waislamu ikiwemo vita na mengineyo.

Iweje leo Waislamu watake kutatua matatizo yao waende majukwaani na kwenye viwanja vya siasa? Eti wasichanganye dini na siasa.

N.H.R. Kajuna,
Morogoro.


Bunge la udini

Ndugu Mhariri

NAOMBA unipe nafasi kwenye gazeti lako adhim, nitoe dukuduku langu. Nina imani kuwa udini, ni kumhusisha Mwenyezi Mungu na serikali. Hivyo hakuna ruksa serikalini.

Swali, sasa kwanini bunge linapoanza, linaanza kwa udini (dua). Cha ajabu zaidi ni kwamba wabunge Wakristo wako makini juu ya Ukristo wao, lakini wabunge Waislamu wanaiuza dini yao kwa thamani ndogo. Ninawausia wamuogope Mwenyezi Mungu.

Omar Kivurande,
Pongwe,
Tanga.


Serikali itueleweshe wananchi

Ndugu Mhariri

NAPENDA kuchukua fursa hii katika gazeti hili ili niweze kuuliza maswali yangu yanayo kereketa moyoni mwangu.

Sasa yapata miaka 38 tangu tupate uhuru, serikali yetu inakiri kwamba haina dini, sasa je, maneno haya ni hakika? Na kama ni hakika serikali haina dini kwanini hujiingiza katika maswala yahusuyo dini hasa yale ya ndoa zilizofungwa na dini. Kwa mfano ndoa imefungwa na Padri au Sheikh inakuwaje baada ya mfarakano kesi iende serikalini ikiwa tulifungishwa na Sheikh au Padri?

Jambo la pili, ni juu ya zoezi la serikali katika ulipaji madeni ya ndani na nje. Je, wale walioshikwa uhujumu wakataifishiwa mali zao watalipwa lini na nani?

Vile vile hao wa nchi za nje kama vile Uingereza na Ujerumani ambao sisi ni koloni lao, wametulipa nini? Ikiwa wao walichuma mali zetu kama vile madini, pembe za ndovu na kadhalika. Kila siku watujazia madeni tu, madeni hayo mpaka lini?

Khaifa Juma,
S.L.P. 1,T
Tunduma.


AN-NUUR litokea mara mbili

Ndugu Mhariri

NAOMBA unipe nafasi katika gazeti lako nitoe maoni yangu. Ingekuwa bora gazeti hili linatolewa mara mbili kwa wiki badala ya mara moja kama ilivyo sasa.

Kwani ndio chombo pekee ambacho tunakitegemea kuamsha fikra na kujua mambo mbalimbali yahusuyo Uislamu pamoja na matukio mbalimbali yahusuyo Uislamu na Waislamu pamoja na ulimwengu kwa ujumla.

Ni ukweli usiofichika kuwa limesaidia kwa kiasi kikubwa kuamsha fikra za Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Na watu wameanza kuuelewa ujumbe.

Hivyo kwa kuzingatia hayo mimi nadhani kuna haja ya AN-NUUR kuwa linatoka mara mbili kwa wiki.

A.H. Maaswabirina,
Mwanza.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook