Wakubwa waumbuana
MAJIRA, Jumatano, Julai 20, 1994
WABUNGE jana waliumbuana na mawaziri kila mmoja akitafuta nja ya kujitetea ili aeleweke kwa wananchi kuwa ndiye mkweli kuhusiana na mgao wa maeneo ya uwindaji wanyamapori nchini unaosemekana kuwa sio halali.
Akifunga hoja yake kuhusu mapendekezo ya matumizi ya wizara ya Maliasili, Utalii na Mazingira, Waziri Juma Hamad Omar aliliambia Bunge baada ya kuapa, kuwa, baadhi ya wabunge ambao wamemshambulia kuwa anahusika na uwindaji wa kampuni moja ya Royal Fontiers, nao pia wanaendesha miradi kwa kushirikiana na makampuni mengine ambayo yana kumbukumbu mbaya kiutendaji.
"Dawa ya neno ni neno", alisema Bw. Omari wakati anajibu hoja iliyotolewa jana na Mbunge wa Monduli, Bw. Ole Moloimet kuwa yeye pamoja na Mkurugenzi wa Wanyamapori, Bw. Muhidin Ndolanga wanahusika na kampuni mbili ambazo zimegawiwa kila moja maeneo mapya yasiyopungua matano kila moja, wajiuzulu ikibainika kuwa waliyagawa maeneo hayo kwa makampuni hayo isivyo halali.
Bw. Omar alikubali kuwa yeye anahusika na kampuni ya Royal Frontiers ambako yuko ndugu yake Bw. Rashid Omar na kwamba Mkurugenzi wake wa wanyamapori Bw. Ndolanga anahusika na kampuni ya Game Frontiers.
"Ndiyo ninakubali kuwa ninahusika na moja ya kampuni hizo na kwamba Mkurugenzi wa wanyamapori anahusika na kampuni nyingine", alisema kukafuatia ukimya wa kitambo kidogo, halafu akaendelea.
"Lakini hata hivyo ugomvi wangu na Bw. Moloimet ambaye ni rafiki yangu wa siku nyingi haupo hapo, upo katika masuala yake binafsi yanayohusu kampuni ya uwindaji inayomilikiwa na Mkurugenzi mmoja mwenye asili ya Kigiriki ambaye mbunge huyo anataka akapewe eneo la uwindaji katika jimbo lake", alitoboa siri hiyo ambayo hapo juzi ilikuwa imefunikwa.
Juzi, Bw. Moloimet alieleza bunge kuwa Waziri pamoja na Mkurugenzi wkae wa wanyamapori wametoa mgao isivyo halali kwa kampuni mbili wanazoshukiwa kuzimiliki.
Aidha, alidai mbunge huyo, Mkurugenzi huyo aligawa au kuongeza maeneo kutoka 109 hadi kufikia 149 katika kipindi kifupi sana kwa madhumuni ya kutaka kutoa migao hiyo isiyo halali.
Bw. Omar aliliambia Bunge mgogoro kati yake na mbunge wa Monduli, Bw. Leipilal Ole Moloimet unatokana na yeye kuinyima milki kampuni hiyo ya uwindaji ijulikanayo kama Bundu Safaris inayomilikiwa na mfanyabiashara mmoja mwenye hoteli maarufu hapa jijini inayoitwa Ettienes, Bw. George Alexious.
Bw. Omar aliliambia bunge kuwa Bw. Moloimet aliwakilisha kwake jina la kampuni hiyo akitaka ipewe eneo liitwalo Lolita lillopo katika jimbo analowakilisha mbunge huyo.
Waziri huyo alisema kuwa licha ya kwamba kampuni hiyo ilikuwa haikutimiza masharti yanayotakiwa kulikuwa na ugumu wa kuipa eneo hilo ambalo alisema limekuwa likimilikiwa na kampuni ya "wazalendo wa siku nyingi" wenye kampuni moja iitwayo Northern Enterprises ambayo mmoja wa wakurugenzi ni Bw. Said Kawawa.
"Kama ni kuumbuana haki ya Mungu naapa nitawaumbua", alisema Waziri huyo na kuongeza. "Sasa waheshimiwa wabunge wenzangu naomba mtuhukumu; nimnyime Northern Enterprises ili nimpe Bundu Safaris.. tume imeshaundwa wacha ifanye kazi yake", alisema Bw. Omar kwa kugugumia.
Akiwa amezungukwa na wabunge ambao walikuwa wamejaza sehemu karibu zote kuliko ilivyo siku za kawaida, Waziri Omar alisema kuwa wizara yake iliamua kuinyima kampuni hiyo eneo hilo kwa vile ilibanika kutoka kwa mkuu wa wilaya kuwa kampuni hiyo ilikuwa imetoa malipo kwa viongozi binafsi badala ya serikali na wanavijiji.
Aidha, alisema, kampuni hiyo ilidhamini vyama vya siasa kwenda katika kampuni fulani huko Dodoma na kwamba inadaiwa nyara na makampuni mengi ya nje ambazo haijapeleka huko toka mwaka 1989.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Bundu Safaris Ltd., Bw. Alexious amesema madai ya Waziri kwamba kampuni yake inadaiwa na idara ya wanyamapori siyo sahihi, na kwamba anazo nyaraka kuthibitisha kuwa hadaiwi kitu chochote na idara hiyo.
Akielezea madai yaliyotolewa na Bw. Omar Bungeni, Alexious alisema madai hayo yamekuja kwa sababu idara ya wanyamapori imempatia waziri huyo taarifa za uongo, ambazo zimetumika kulidanganya bunge.
Kuhusu uhusiano wa mwindaji huyo na mbunge wa Monduli, Bw. Alexious alisema Tanzania haina sheria yoyote inayokataza watu kujenga urafiki. Alisema haoni ubaya kuwa rafiki yake Bw. Moloimet, lakini alisema mbunge huyo hakai bure katika hoteli yake iliyoko Dar es Salaam. "Analipia malazi na chakula kama wateja wengine", alisema.
Hata hivyo alisema mbunge wa Monduli ni Mtanzania anayeipenda nchi yake sana na ana uchungu na maliasili ya nchi hii. Hapo ndipo wanapokutana kimawazo", Bw. Alexious alisema.
Aliongeza kuwa anachojua ni kuwa Bw. Moloimet alisomea mambo ya hifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na wanyama huko Ujerumani, labda ndiyo maana anaelewa mambo ya hifadhi wanyamapori kuliko watu wengine.
Kuhusu uwindaji katika eneo la Yaeda Chini ambalo mbunge wa Mbulu Bw. Philip Marmo aliliomba bunge mwaka jana kuwa libaki sehemu ya kuwinda nyama ya kitoweo kwa kabila la Wahadzabe, Waziri Omar alisema mbunge huyo ndiye aliyekiuka kanuni yeye mwenyewe.
Alisema ingawa alimhakikishia Waziri kuwa eneo hilo alitatumika kwa mawindo ya biashara, Bw. Marmo alimwandikia yeye Waziri kuwa amepokea kikundi kimoja chini ya Bw. Mousoud ambacho kilishawasili Arusha tayari kwa kutaka kuwinda huko.
Katika hali ambayo ilikuwa ni ya kutatanisha kati ya mbunge huyo na Bw. Omar, mbunge alitaka barua hiyo isomwe bungeni, kwani inawezekana kuwa Waziri alitumia nafasi hiyo kulidanganya bunge kwa kumchafulia jina lake.
Huku kukiwa na mvutano ambao ilibidi Naibu Spika wa Bunge, Bw. Kihaule aingilie kati mara mbili kusuluhisha, Bw. Omar alisisitiza kuwa kulikuwako na mawasilano kati ya yeye na Bw. Marmo kuhusiana na uwindaji huo, lakini hakuisoma barua hadi kupitishwa mapendekezo yake.
Katika hali ambayo ilielekea kuonyesha kuwa Bw. Marmo na Bw. Omar walishindwa kuelewana kwa jambo wanalolijua wenyewe ambalo wengine wote hawakuweza kulielewa kila mtu aliendelea na shughuli zake- mbunge alitoka nje wakati ambapo waziri aliendelea kujieleza.
Kuhusiana na suala la madege ya kijeshi ambayo yaliingia nchini mwishoni mwa mwezi uliopita na mwanzoni mwa mwezi huu, Bw. Omar alisema kuwa ndege hizo ni za Falme za Nchi za Kiarabu (UAE) ambazo ziliingia nchini kwa vibali maalum na masharti yote ya uhamiaji yalifuatwa.
Alisema kuwa wanyama waliowindwa na watu walioandamana na ndege hizo ni suala kutoka katika hifadhi ya Loliondo ambayo amepewa Brigedia Mohamed Ali wa UAE kupitia kampuni yake iitwayo Ortelo Business Tanzania Ltd.
Wakati bunge lilipokaa kama kamati ya matumizi
kupitia mapendekezo ya wizara hiyo, mashambulzi yalizidi huku wabunge wakitoa
shilingi katika mshahara wa waziri kutaka wapewe maelezo kuhusiana na hoja
mbalimbali walizozitoa wakati wa mjadala huko nyuma.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |