Hivi kuna siri gani Bakwata na CCM
Naomba nimuulize, yeyote anayejua,
Ufasaha anijuze, nami nipate elewa,
Shaka isinitatize, ukweli nikiujua,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Bakwata ya waumini, CCM nayo vipi,
Chadema na Namba wani, asichague kwa vipi,
Mapenzi yake rohoni, tuyaingilia vipi,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Kila siku twasikia, matangazo redioni,
Viongozi wausia, siasa mbalimbali na dini,
Vipi wanakazania, Bakwata misikitini,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Omari katuambia, amani kuienzini,
Nani asiyetambua, umuhimu wa amani,
Nani alokuambia, wapinzani wahuni,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Hebu geuza Zambia, mzinduke akilini,
Chiluba ametulia, vita vimezuka lini?
Kwa debe kuwapigia, inatutoka imani,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Mfumo wa vyama vingi, umeenea dunia,
Wala haina msingi, kelele kutupigia,
Amani yake msingi, ni ya ukweli sikia,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Haisimami amani, bila haki wasikia,
Kama wataka amani, kazana kuwaambia,
CCM namba wani, usawa kutupatia,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Bakwata wamechelewa, ukweli twawaambia,
Ni budi kuondolewa, kiti walichokalia,
CCM namba wani, usawa kutupatia,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Fumbo fumbia mjinga, mwerevu atalijua,
Wananchi si wajinga, kweli wameshaijua,
Meshawafanya wajinga, na sasa wamekataa,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
Beti kumi nasimama, mbele sitoendelea,
Nawakumbusha Ulama, dini kusimamia,
Kwa haya mambo ya vyama, pabaya mtafikia,
Hivi kuna siri gani, Bakwata na CCM?
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |