Huu ni upotofu
TUNAYASEMA haya, kwanza ili kusahihisha upotofu. Pili, kujivua na upotofu huo. Na tatu kuweka rekodi kwamba upotofu huo ulisahihishwa.
Mufti na Sheikh Mkuu wa BAKWATA Sheikh Hemed bin Jumaa juzi usiku katika Maulidi huko Kigoma amechanganya mambo mawili: Kosa zito ambalo ni miongoni mwa madhambi makubwa - yaani kosa la kukiuka amri ya Allah. KOSA LA UZINZI. Kosa hilo amelichanganya na umuhimu wa kuleta sulhu baina ya watu waliofarikiana.
Kilichobainika katika mawaidha ya Mufti wa BAKWATA ni kwamba:
Kwanza yajuzu mume kumdanganya mkewe baada ya kumtuhumu uzinzi. Ilimradi urongo huo ameukusudia asigombane au kukosana na mkewe baada ya kufanya uchafu wake.
Pili, katika kuficha uovu huo waweza, pia hata kutunga 'Qur'an' ya urongo.
Tatu, Mtume aliwahi kuletewa urongo huo na akaufurahia.
Suala la sulhu alilokuwa akilisisitiza halina ubishi katika Uislamu. Lakini hiyo inahusu watu wawili waliokosana na anayeleta sulhu ni mtu wa tatu.
Ukifanya uchafu wa zinaa, suala haliwi sulhu baina yako na mkeo uliyekosa uaminifu kwake. Bali suala muhimu huwa kufanya dhambi kubwa ambayo hukumu yake hapa duniani ni kurujumiwa kwa mawe.
Haiyumkini Mtume wa Allah afurahie urongo wa mtu anayeongopa baada ya kutenda dhambi kubwa.
Mufti amedai kuwa yupo Sahaba mmoja 'aliyefumaniwa na mkewe akiwa na mfanyakazi wake wa ndani. Mke akaja juu. Yule Sahaba akabisha kuwa hajafanya tendo lolote na yule mfanyakazi.
Mke akamuambia soma Qur'an, kwa kujua kwamba kama anajanaba hatathubutu kusoma.
Mufti anadai kuwa yule Sahaba alishindwa kusoma Qur'an hali ya kuwa ana janaba. Lakini akatunga Qur'an yake ya urongo. Akasoma ugomvi ukaisha.
Hata hivyo, Mufti anadai yule Bwana baadae alikwenda kwa Mtume. "Nimeangamia", yule Bwana alimwambia Mtume.
Kisha akamhadithia yaliyomsibu na Qur'an yake
ya urongo. Mufti anadai Mtume alicheka huku akimuambia arudie tena kusoma
Qur'an ya urongo. Baadae Mtume akamweleza kuwa ipo rukhsa kuongopa kuleta
sulhu.
JAMBO LA KUZINGATIA:
Sheikh Mkuu hakuwa anafafanua sura ya (23:5-6). Muelekeo ungekuwa huo ingekuwa suala la kumuelimisha mkewe. Na wala pasingekuwa na sababu ya mkewe kukasirika na kumuapiza.
Lakini picha aliyoijenga Mufti ni ya mtu aliyefumaniwa, kisha kosa kuhalalishwa kwa urongo wa kuleta sulhu.
Sisi tunasema hii si sawa. Yawezekana Mufti kasoma kwenye vitabu, lakini ikumbukwe zipo Israiliyati nyingi zilizoingizwa kwenye vitabu. Ndio maana zikawepo hata kanuni za kupima hadithi ili kuzitambua za urongo, dhaifu na hadith sahihi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |