Katika kusherehekea Maulid, Waislamu waambiwa:
Oanisheni Sira na mazingira yenu

Katibu tawala mkoa wa Lindi bwana Musa Mdidi amewataka Waislamu kuichambua historia ya ujumbe wa Mtume Muhammad(s.a.w) kwa kuioanisha na mazingira yao.

Bwana Mdidi amesema katika kipindi cha utume Maka historia imeshuhudia jamii ya Mtume ikiwa katika kiza kinene cha ujahili.

Amesema, Mtume alitumia miaka 13 kuwaanda Waislamu kiimani kabla ya kuusimamisha Uislamu jamii katika kipindi kilichofuatia.

Katibu huyo Tawala alikuwa akiongea akiwa mgeni Rasmi katika Hafla ya Maulid ya Mtume(s.a.w) iliyofanyika juzi kimkoa katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi.

Bwana Mdidi aliwaambia waumini waliohudhuria madhimisho hayo kwamba hawanabudi kujiangalia wao kama Waislamu wakati huo huo wakiwa wanajamii wanaopaswa kuwajibika kidini na kijamii, waijue nafasi yao kama Waislamu halikadhalika nafasi yao kama raia waishio katika jamii mchanganyiko.

Kijamii, alisema Bwana Mdidi, hali ya Waislamu leo hii haitofautiana sana na ile ya wakati wa Mtume kipindi cha Makka ambapo yeye na masahaba zake waliendesha maisha yao wakiwa memba wa jamii hiyo.

"Tumuangalie Mtume na masahaba waliishi vipi katika kipindi hiki cha Makka wakiwa sehemu ya wanajamii waliotakiwa kuhusika katika mambo mbali mbali ya kijamii ", alisema na kuongeza kuwa, "Miaka 13 ya utume Makka ilishuhudia utawala wa kijahili ulioendeshwa kiukoo ambao mali au nasaba ya mtu ilikuwa kipimo cha thamani yake".

Aidha, alisema, jamii hiyo iligawanyika katika matabaka ya mabwana na watwana ikiongozwa na itikadi dhalimu ya kishirikina.

Waislamu hawanabudi kuzingatia namna Mtume(s.a.w) alivyoweza kutumia fursa mbali mbali kujiweka sawa kidini na kijamii akilenga kile kilichokuja kujitokeza miaka kadhaa baadaye" alisisitiza.

Akizungumzia wajibu unaowapasa Waislamu kidini, Sheikh Mdidi alisema kama ilivyokawaida kwao kuadhimisha uzawa wa Mtume kila ifikapo Rabiul Awwal ya kila mwaka wa kiislamu, basi maadhimisho hayo yaandamane na kumtii Mtume kwa kuiga Mwenendo wake.

Alisisitiza jambo hilo kwa kunukuu Qur'an aya ya 3, sura ya 31 inayomuamrisha Mtume(s.a.w) aseme, ikiwa Waislamu wanampenda(kikweli kikweli) Mtume basi wamfuate kwa anayowaamrisha, wakifanya hivyo Mwenyezi Mungu atawapenda na atawasamehe madhambi yao.

Alisema kumfuata mtume kutampelekea muumini kuwa na mwenendo wa mtu ambaye ulimwengu umemtaja ni nambari wani katika watu bora kabisa waliopata kutokea katika Historia.

Sheikh Mdidi alisema kitabu "the best Hundred" kimetaja baadhi ya sifa zinazomuweka Mtume Muhammad(s.a.w) katika nafasi hiyo kuwa ni pamoja na kuwa Kamanda mkuu wa jeshi aliyeshiriki vita kadhaa akiwa mstari wa mbele(military men) wakati huo huo akiwa kiongozi wa familia aliyetimiza kikamilifu majukumu ya kifamilia(family men).

Mtume(s.a.w) alitawafu Dunia akiwa ameshiriki vita visivyopungua 23 akiwa kamanda aliyeongoza mapambano katika medani ya vita.

Kuhusu mporomoko wa maadili katika jamii, Katibu huyo Tawala alilaumu vituo vya Televisheni kwa kusema kuwa vinachangia kwa kiasi kikubwa kuiharibu jamii ya watanzania hasa watoto na vijana.

Aliwataka Waislamu kuchukua tahadhari dhidi ya programu ambazo alisema wanaoziandaa hulenga kuipotosha jamii.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook