VYAMA vyote vilivyoandikishwa kuwa vya kisiasa ni vya kisiasa na lengo lake kubwa ni kutwaa madaraka ya kuongoza nchi au kwa maneno mengine kupigania kuingia Ikulu kwa kutumia kura za wananchi.
Dhana hii haitazami chama kinaungwa mkono na kina nani, au wafuasi wake ni wa kabila gani, au dini gani, bali unaotizamwa ni sera zake na mwelekeo wake wa kisiasa katika kupigania maendeleo na maslahi ya wananchi.
Imetokea baadhi ya vyama kunasibishwa na ukabila kwa sababu tu vina viongozi wa kabila fulani au wafuasi wengi wa kabila fulani. Na baadhi ya vyama kunasibishwa na dini kwa vile viongozi au wafuasi wake wengi wanaonekana ni wa dini fulani.
Kutokana na mwelekeo wa CCM ambao umekuwa ukiwakatisha tamaa wananchi, vyama vingi viliibuka kwa nguvu kubwa ili kuiondoa CCM katika madaraka.
Jambo la ajabu, CCM imeshindwa kuendeleza ushindani wa kisiasa dhidi ya wapinzani wake bali tulichokishuhudia ni ushindani wa kuhujumu upinzani. Vyama kadhaa hivi sasa vipo kama havipo. Vile ambavyo vilikuwa na majina na vile ambavyo vilikuwa tegemeo kubwa kwa upande wa upinzani kuingia Ikulu vimesambaratishwa na kupoteza nguvu na mwelekeo.
Jambo ambalo liko wazi na haliwezi kupingwa na Mtanzania yeyote yule ni kuwa Chama Cha Wananchi (CUF) kimekuwa imara bara na visiwani.
Uimara huu umekifanya kiungwe mkono na wananchi wengi kwa kuonekana kuwa ni tegemeo la pekee la kuwakomboa wananchi chini ya Mwenyekiti wake na mgombea wa kiti cha Urais Prof. Ibrahim Lipumba.
Uimara na nguvu waliyonayo wana-CUF hivi sasa inaonekana kuwa tishio kubwa kwa CCM hasa wakati huu ambapo uchaguzi upo karibu.
Moja ya ushahidi kuwa CUF imekuwa ni tishio ni jinsi wananchi wanavyojitokeza kwa wingi katika ziara za Mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Lipumba.
Umati mkubwa umekuwa ukijikusanya kwenye mikutano yake ambapo wananchi wengi hurudisha kadi za CCM na kukata kadi za CUF.
Hali hiyo inaifanya CCM ijione kuwa imeshachokwa na kwamba wananchi walio wengi hivi sasa wanataka mabadiliko.
Kutokana na hali hiyo kile kinachoonekana kama hujuma dhidi ya CUF kimeanza kujitokeza. Lengo hasa ni kukidhoofisha chama hiki ili kuivunja kasi yake.
Moja ya mbinu ya mwanzo kutumika ili kisikubalike kwa wananchi ni madai yaliyotolewa kuwa CUF ikitwaa madaraka ya nchi itaua muungano, madai ambayo yamejibiwa mara kadhaa na viongozi wa CUF kuwa chama cha CUF hakipiganii kufufua na kuimarisha uchumi wa Tanzania tu bali pia kudumisha na kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuliko ulivyo sasa ambapo migogoro midogo midogo imekuwa haiishi.
Kama haitoshi, hivi sasa madai kuwa CUF ni chama chenye mwelekeo wa kidini hayatolewi tu na viongozi wetu bali hata baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikipiga mnada huo.
Gazeti moja linalochapishwa na Kanisa moja hapa nchini hivi majuzi liliandika katika ukurasa wake wa mbele kuwa CUF ni chama cha Waislamu bila kufafanua Uislamu wa CUF ni upi.
Imegundulika kuwa makusudio ya madai haya ni kuwavunja moyo wananchi wasikiunge mkono ili kukidhoofisha.
Kwa uchambuzi wa haraka haraka ni kuwa madai hayo hupandikizwa katika mtazamo kuwa kiongozi au viongozi wa juu wa chama hicho ni Waislamu, jambo ambalo halijengi hoja ya kweli kuwa ni chama cha Waislamu.
Na mtazamo unapandikizwa kufuatia yale mazoea ya kuwaona viongozi wa nchi hii na wanasiasa wengi ni Wakristo. Ndio sababu kujitokeza kwa chama hiki chenye kiongozi Muislamu kukaonekana ni kioja. Sasa je, hivi vyama vyenye viongozi Wakristo ni vya Kikristo?
Hivi sasa wananchi wameshakomaa kisiasa,wanajua safi na ghafi, wanajua chuya na pumba. Propaganda za ukabila na udini haziwezi kuwa na nafasi katika siasa ya leo wala katika harakati zao za kupigania haki, usawa na demokrasia zaidi.
Watanzania hivi sasa wanahitaji ushindani wa kweli wa kisiasa wenye lengo la kutukwamua kutoka katika kero mbalimbali zinazoikabili nchi hivi sasa. Hawakubali propaganda zenye lengo la kuwabakisha kwenye matatizo yanayoweza kutatulika.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |