Kilimo:
Ili Tanzania ijinasue katika dimbwi la umaskini ni lazima pawepo na mapinduzi ya kilimo. Sera zisizotabirika ikiwa ni pamoja na kuvunja vyama vya ushirika vya wakulima wenyewe, operesheni vijiji, operesheni maduka, mashamba ya mfumaki yameacha makovu sugu kwa wakulima na sekta ya kilimo.
Nchi yetu haina huduma bora za kilimo cha kisasa, hatutumii utafiti na mafunzo kwa wakulima kuongeza tija. Barabara na mawasiliano vijijini ni mabaya sana. Kuendeleza kilimo tunahitaji kuongeza motisha kwa wakulima wapate bei nzuri ya mazao yao.
Hatua za makusudi zahitajika kuboresha huduma za kilimo na kuweka usimamizi wa kuwalinda wakulima wasinyongwe na wafanyabiashara wanaoshirikiana kupunguza ushindani katika soko huria na kupanga bei ndogo kwa mazao ya wakulima.
Serikali ikishirikiana na taasisi za kimataifa iboreshe utafiti wa kilimo na mafunzo kwa wakulima, kodi na ushuru wa mazao ya kilimo hayawezi kutokea bila matumizi ya zana na pembejeo bora. Nikichaguliwa kuwa Rais, serikali itashirikiana na taasisi za fedha na vyombo vya wakulima kuweka utaratibu wa mikopo ya kununua zana na pembejeo za kilimo.
Elimu:
Kukua kwa uchumi wa kisasa wenye uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi unategemea wafanyakazi wenye ujuzi na maarifa. Hivi sasa dunia inashuhudia mapinduzi ya teknolojia ya mawasiliano ya habari (Communication and Information technology) ambayo yanaleta mageuzi makubwa ya uchumi na biashara ya kimataifa.
Uchumi wa kisasa unatumia kompyuta na mtandao wa Internet. Ili Tanzania ishirikiki kikamilifu na ifaidike na uchumi wa ulimwengu inatulazimu kuweka mkakati wa kuboresha na kupanua elimu toka elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu.
Serikali itachukua hatua za masukudi ikishirikiana na taasisi za kimataifa kusambaza matumizi ya kompyuta na mtandao (Internet) katika mashule yetu. Elimu bora ya msingi ni haki ya kila mtoto. Nikichaguliwa kuwa Rais, itakuwa marufuku kumfukuza mwanafunzi kwa kisingizio cha kukosa ada. Serikali itashirikiana na wazazi, mashirika ya dini, taasisi zisizokuwa za kiserikali na wahisani wa nje kuhakikisha kuwa kila mtoto wa Tanzania anapata fursa ya elimu ya msingi iliyo bora.
Serikali itashiriki katika kuongeza na kuboresha shule za sekondari na vyuo vikuu na kuongeza ufanisi ili sehemu kubwa ya matumizi yalenge katika kutoa elimu.
Waheshimiwa wajumbe, elimu na teknolojia inayoongezeka kila wakati ili tusiachwe nyuma inatubidi tujenge mazingira yatakayowezesha kushamiri utamaduni wa kujiendeleza kielimu katika maisha yetu.
Nikichaguliwa kuwa Rais, tutalenga kutumia asilimia 25 ya matumizi ya serikali katika sekta ya elimu.
Kupambana na Ukimwi
Ukimwi ni tishio la kuwepo kwa taifa letu. Inakadiriwa kuwa katika kila watu mia moja waishio mjini 25 wana virusi vya ukimwi. Vijijini kuna wananchi 10 katika kila 100 wenye virusi vya ukimwi. Wajumbe wa mkutano mkuu tukiendelea kuonea haya ukimwi utatumaliza. Mimi nikichaguliwa kuwa Rais nitatumia wadhifa na heshima ya Ofisi ya Rais kuweka msukumo maalum kwa Watanzania na hasa vijana waelewe vizuri athari za ukimwi na namna ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu. Kimaumbile ni rahisi zaidi kwa wanawake kuambukizwa virusi vya ukimwi kuliko wanaume.
Waheshimiwa wajumbe wanawake wanaathirika vibaya zaidi na ukimwi. Katika kila Watanzania watano wenye virusi vya ukimwi, watatu ni wanawake na wawili ni wanaume. Waheshimiwa wajumbe naomba tueleze vizuri kuwa wanawake wengi wanaoambukizwa ukimwi sio kwa sababu za uasherati bali wanaambukizwa na wanaume waliopata radhi hili nje ya ndoa. Uhuru wa ukombozi wa wanawake na kuongezeka kwa uwezo wao wa kupata ajira na kujiendesha kimaisha unasaidia kupunguza ongezeko la ugonjwa huu.
Nikichaguliwa kuwa Rais, tutaweka mkakati wa kitaifa kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa mtu ambaye hivi sasa hana virusi vya ukimwi, kuambikizwa ugonjwa huu.
Utafiti katika nchi nyingi umeonesha wazi kuwa vijana wanaofahamu vizuri athari na jinsi ukimwi unavyoenea. Wanajikinga na hawaambukizwi virusi vya ukimwi ukilinganisha na wale ambao hawana elimu ya ugonjwa huu. Kuwapa vijana wetu kuhusu ugonjwa huu ni kuwapa kinga ya radhi hili hatari.
Serikali ikishirikiana na taasisi za kimataifa, na shirika la Afya Ulimwenguni WHO kufungua vituo maalum vya kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu na kutoa tiba inayopunguza athari na kuongeza muda wa kuishi kwa wale wenye virusi vya ukimwi.
Barabara:
Mawasiliano mabovu ya barabara ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya uchumi yatakayopunguza umaskini. Nikiwa Rais nitasimama kwa karibu.
Uanishaji wa utaratibu wa kukarabati barabara zetu kuu na za vijijini. Rushwa imekithiri katika Wizara ya Ujenzi na inachangia kwa kiasi kikubwa ukarabati hafifu wa barabara zetu.
Kupunguza rushwa kwa kuweka utaratibu ulio wazi wa kutoa zabuni na kuwajibika kwa watendaji wa serikali na makampuni ya ujenzi kutasaidia kupunguza rushwa na kuimarisha matengenezo ya barabara ili mali asili ya nguvu kazi iliyoko mikoa ya kanda ya ziwa na mikoa ya kusini itumiwe kuinua maisha ya wananchi wa mikoa hii na Watanzania kwa ujumla. Barabara kuu ya Mwanza mpaka Dar es Salaam na barabara ya kusini inayounganisha mikoa ya Lindi na Mtwara na Dar es Salaam zitawekwa lami.
Waheshimiwa wajumbe mnaweza kujiuliza kuwa mambo yote yanahitaji fedha. Je, fedha zitapatikana wapi kuinua viwango vya elimu, kuongeza huduma za kilimo, kupambana na ukimwi, kujenga barabara, kuweka mazingira bora kwa wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazoongeza ajira.
Pamoja na majigambo ya serikali ya awamu ya tatu kuwa imeongeza ukusanyaji wa kodi, mfumo wetu wa kodi ni mbaya unawabana wafanyabiashara wadogo wadogo na wakati kulipa kodi na kusamehe makampuni makubwa kwa kisingizio kuwa wao ni wawekezaji.
Sehemu ya pato la taifa linalokusanywa kama kodi limepungua toka asilimia 13.4 mwaka 1996 mpaka kufikia asilimia 11.9 mwaka 1999. Tanzania inakusanya sehemu ndogo ya pato la taifa kama kodi ukilinganisha na wastani wa asilimia 15 wa nchi nyingine za Kiafrika. Kwa kuongeza uwajibikaji wa mamlaka ya kodi kuondoa misamaha ya kodi na kupunguza viwango vya kodi na kuongeza adhabu ya kukwepa kodi. Tanzania pia inaweza kukusanya alau asilimia 15 ya pato la taifa kama kodi. Serikali itabana matumizi kwa kuwa na wizara chache zisizozidi kumi na tano. Misaada toka nje ya kusaidia elimu, afya na ujenzi wa barabara haitanyofolewa na kutumiwa vibaya.
Nikichaguliwa kuwa Rais, serikali itaacha kutumia utaratibu wa sasa wa Cash Budget. Kwa miaka mitano iliyopita bajeti inayoidhinishwa na Bunge na Matumizi halisi katika Wizara na sekta mbalimbali ni vitu viwili tofauti kabisa. Bajeti ya serikali yangu itazingatia gharama halisi na makadirio ya mapato yaliyosahihi. Mapengo ya muda mfupi kati ya matumizi na mapato yatazibwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Waheshimiwa wajumbe wa mkutano mkuu ili tuweze
kujenga nchi yenye haki sawa kwa wote na tujenge uchumi imara utakaoleta
neema kwa wote ni lazima tuing'oe CCM. Watanzania wamechoka na CCM na wana
matumaini makubwa na CUF kuwa ndie atakayekuwa mkombozi wao. Mmeniteua
kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya CUF. Kazi yetu kubwa ni kujiandaa kwa
uchaguzi. Tuwahamasishe wananchi wote wa Tanzania wenye umri wa miaka 18
na kuendelea wajiandikishe kupiga kura. Siku ya uchaguzi sote tushiriki
na tulinde kura zetu.
HAKI SAWA
KWA WOTE
Hotuba ya Maalim Seif baada
ya kupitishwa kugombea Urais Z'bar- 2
NA hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliyelikemea hili, hata wale wanaodai kuwa wao hawapendezwi na haya na kwamba eti wakichaguliwa kuiongoza Zanzibar watawahakikishia Wazanzibari "usingizi bila khofu".
Dhana ya haki za binadamu ni dhana pana sana na inayoendelea kukua kila siku. Anayekusudia kuwa kiongozi wa nchi analazimika kulielewa hili na kulipa nafasi inayostahki katika uendeshaji wa serikali na uongozaji wa nchi. Mimi nikichaguliwa kuwa Rais nitalipa nafasi kubwa suala hili. Nitasimamia barabara utekelezaji wa Tamko la Haki za Binadamu (Bill of Rights) kama lilivyo katika Katiba ya Zanzibar na kuliimarisha zaidi.
Watu watakuwa huru kwa maana halisi ya neno UHURU. Uhuru wa kujiendeleza na haki ya maoni, uhuru wa kuandamana, uhuru wa kuanzisha au kujiunga na chama au jumuiya yoyote, uhuru wa mtu kwenda anakotaka na uhuru wa mtu kuabudu dini anayoitaka ni miongoni mwa haki za msingi za binadamu zitakazohakikishwa na kulindwa. Cha msingi ni kuwa anayetumia haki hizo havunji sheria au kuathiri haki na uhuru wa mtu mwingine.
Kupiga vita rushwa
Ni jambo linaloeleweka kuwa haki haiwezi kustawi pahala penye rushwa. Rushwa ni adui wa haki. Si ajabu kuwa sababu moja kubwa inayopelekea kukosekana kwa haki za msingi za raia katika Zanzibar hivi sasa ni kukithiri kwa tatizo la rushwa. Rushwa limekuwa ni jambo la kawaida kabisa . Wakuu wa serikali wanashindwa kupambana na watendaji serikalini wanaokula rushwa. Nchi haiendi mbele kutokana na kushamiri kwa rushwa. Na kama aliyekuwa Waziri Mkuu wa Singapore, Lee Kuna Kuan Yew alivyowahi kuwaambia viongozi wa nchi za Afrika kwamba penye rushwa hakuwezi kuwa na maendeleo.
Hivyo mimi nikiwa Rais, nitakuwa mkali sana kwa wale wote waanaotoa na kupokea rushwa. Vita hivi vya kupambana na rushwa vitasaidiwa sana na kuwepo kwa Baraza la Wawakilishi lenye uwezo na uhuru wa kuihoji na kuibana serikali pamoja na kuwepo kwa mahakama huru zitakazoweza kuwahukumu wale watakaobainika kuwa na hatia. Haya yatahakikishwa katika serikali nitakayoiongoza.
Kupiga vita umaskini
Yote haya niliyoyaeleza ni muhimu sana. Lakini ukweli mmoja ambao haukwepeki ni kuwa Wazanzibari wataweza kuyafaidi haya vizuri iwapo watahakikishiwa kuwepo kwa hali bora za maisha yao. Hali iliyopo sasa chini ya serikali ya CCM ya umaskini uliokithiri miongoni mwa Wazanzibari walio wengi ni ya hatari sana kwani imeanza hata kujenga chuki kati ya matabaka ya "walio nacho" na "wasio nacho". Umasikini huu kwa kiasi kikubwa umetokana na vijana kukosa ajira. Vijana wanapokosa ajira hushindwa kuzisaidia familia zao na kuzaa jamii yenye dhiki. Bidhaa hujaa madukani lakini wanunuzi wakakosekana. Mzunguko wa fedha huathirika na uchumi wa nchi kuzorota.
Kukabiliana na matatizo haya ni lazima kuwa na mpango kabambe wa kupambana na umaskini (Poverty Eradication Programme). Mimi nadhani hili ndilo suala la msingi kabisa kwa Wazanzibari baada ya kujenga umoja wa kitaifa.
Mwelekeo wa serikali itakayoongozwa nami utakuwa ni kuwafanya Wazanzibari washughulishwe zaidi na hamu ya kujiendeleza na kuleta maendeleo ya uchumi wao na wa nchi yao badala ya kushughulikia tofauti ndogo ndogo zisizo na msingi.
Katika kuwasaidia kunyanyua hali zao za maisha, serikali yangu itahakikisha tunajenga uchumi imara kwa kuweka mazingira mazuri yatakayopelekea nafasi za ajira kuongezeka - iwe za kujiajiri au kuajiriwa.
Biashara kustawishwa
Historia ni shahidi kuwa Zanzibar ilikuwa ndiyo kituo kikuu cha biashara katika eneo hili la ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Iliweza kuwa hivyo kutokana na nafasi yake ya kijiografia iliyopo ambayo ni muhimu sana kibiashara (strategic area). Ni imani yangu kuwa mpango wowote wa kuondoa umaskini na kujenga uchumi imara wa Zanzibar hauna budi kuzingatia ukweli huu. Biashara ndiyo ufunguo wa matatizo ya kiuchumi na ukosefu wa ajira visiwani Zanzibar.
Mimi nikiwa Rais, katika kipindi cha miaka mitano ya serikali yangu nitasimamia kuona kuwa Zanzibar inaitumia kikamilifu nafasi yake hii kwa kunyanyua uchumi na kuongeza ajira. Katika kufanya hivyo, Zanzibar ina mengi ya kujifunza kutoka nchi nyingine ulimwenguni zenye nafasi kama hii ambazo ni pamoja na Singapore, Hong Kong, Hawaii, Dubai na Mauritius.
Lengo la serikali yangu litakuwa ni kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikuu cha biashara na mawasiliano kati ya Afrika Mashariki na Kati na upande mmoja wa nchi za Ghuba, Bara Hindi na Mashariki ya Mbali kwa upande wa pili. Hili halitakuwa ndoto ya Alinacha kama lilivyokuwa katika serikali inayomaliza muda wake visiwani. Nitasimamia kwa dhati kuiona Zanzibar inageuka na kubadilika kuwa mlango wa kuingilia na kutokea Afrika (The Gateway to and out of Africa) kama ilivyokuwa katika siku zake za kung'ara huko nyuma. Nyota ya Zanzibar itang'ara tena katika serikali itakayoongozwa nami na wananchi watafaidi matunda yake.
Wakati jitihada za kutupeleka huko zinaendelea, mipango mingine ya muda mfupi ya kunyanyua uchumi wa Zanzibar itatekelezwa. Kama Rais, nitatumia madaraka yangu kusimamia vizuri matumizi ya kile tulicho nacho. Nitasimamia vyema Hazina ya Nchi kwa kuhakikisha kuwa mapato ya serikali yanakimu matumizi yake na kwamba kodi inayotozwa inafuatana na huduma safi zitakazotolewa kwa wananchi, wakaazi na hata wageni wanaotembelea Zanzibar.
Huduma muhimu za kijamii
Kumairika kwa uchumi kutatupa nafasi ya kutoa huduma za uhakika za jamii kunzia na Elimu, Afya, Maji, Umeme na Njia Kuu za Usafiri. Napenda kuchukua tena ahadi kwamba serikali itakayoongozwa nami itatoa umuhimu mkubwa katika kunyanyua kiwango cha elimu na huduma za afya Zanzibar. Naahidi kwamba Bajeti ya sekta hizi itakuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka hadi huduma hizi ziwe za kuridhisha na kuwafanya wananchi waache kukimbilia nje kwa ajili ya matibabu au selimu ya watoto wao.
Tatizo la muda mrefu la maji linaloendelea kumsumbua takriban kila Mzanzibari litamalizwa na kusahaulika kabisa. Tutatafuta njia mbadala za kutoa umeme utakaokuwa wa uhakika na wa bei nafuu ambao kila mwananchi awe wa mjini au mashambani ataweza kuumudu. Barabara zote za Unguja na Pemba zilizochakazwa na serikali ya CCM zitajengwa upya. Uwanja wa Ndege wa Zanzibar utapanuliwa na kuongezewa huduma ili uwe kweli ni Uwanja wa Kimataifa na Bandari ya mjini Zanzibar ambayo wakati wowote inaweza kuanguka kutokana na kuharibika kwa nguzo zinazoisimamia nayo itafanyiwa matengenezo haraka iwezekanavyo kwa kushirikiana na nchi wahisani ambazo ziko tayari kusaidia na ambazo tutaziomba zirejeshe misaada yake mara tu serikali ya CUF itakapoingia madarakani. Matengenezo haya yanakusudiwa yawe chachu ya kufungua milango ya maendeleo mengine ya Zanzibar.
Kupambana na madawa ya kulevya
La mwisho kabisa lakini muhimu sana kwa maendeleo ya Zanzibar litakalosimamiwa na mimi binafsi nikiwa Rais ni kupambana na biashara ya utumiaji wa madawa ya kulevya ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi visiwani. Cha kusikitisha ni kuwa wanaojishughulisha na biashara hii wanajulikana lakini wanaachwa huru kufanya shughuli zao huku polisi ikiwanyanyasa vijana ambao wengine wamelazimika kujiingiza katika utumiaji wa madawa haya kutokana na kukata tamaa ya maisha.
Mimi naamini kuwa wengi kati ya watumiaji wa madawa haya wataacha tabia hii pindi wakipata ajira na shughuli ya uhakika ya kufanya. Wanachohitaji ni kusaidiwa na siyo kunyanyaswa. Serikali itakayoongozwa nami italishughulikia hili kikamilifu na kuisafisha jamii na uchafu huu na wakati huo huo itapambana na waingizaji wa madawa ya kulevya kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria. Wawekezaji watakaobainika wanatumia nafasi zao kama vichaka vya kuficha uharamia wao watafutiwa leseni na mikataba yao na kuondoshwa nchini mara moja.
Hitimisho
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa wajumbe, inaweza kuonekana na baadhi ya yenu kuwa mambo haya ninayoahidi kuyasimamia na kuyashughulikia ni mengi na mengine yanahitaji fedha nyingi ambazo inaonekana hatuna. Hilo mimi halinishtui sana kwani naamini penye nia pana njia. Wengi wanaona haya hayawezekani kwani wanayatazama kwa kioo cha serikali ya CCM. Naam! Ni kweli kuwa unapoyatazama haya kwa kioo cha serikali ya CCM utaona hayawezekani tu.
Hata mimi naamini vivyo hivyo kuwa hakuna serikali itakayoundwa na CCM inayoweza kuyatekeleza haya. Wala hakuna mwana-CCM yeyote anayeweza kujigamba kuwa yeye ni tafauti. Wote ni sawa sawa -jora moja, mkasi mmoja. Tatizo siyo mtu, tatizo ni mfumo wanaousimamia.
Waliopita waliahidi mengi lakini wakashindwa kwani mfumo wanaousimamia ni wa CCM ambao katu haiwezi kuwa mfumo wa kutengeneza, CCM katu haiwezi kujenga. Ni wazi basi kuwa kinachotakiwa kubadilishwa ni mfumo wenyewe wa utawala na siyo mtu. Vinginevyo, tutakuwa tunabadilisha soji tu lakini punda atakuwa ni yule yule - mpunda mpiga mateke.
Wazanzibari tunapaswa kutahadhari sana - tusikubali kutafunwa na nyoka mara mbili kutoka pango moja. Tumeshayaona mengi katika miaka 36 ya utawala wao. Sasa umefika wakati wa kuwabadilisha. Ndio maana, natoa wito kupitia ukumbi huu wa Wazanzibari wenzangu wote kuungana nami na CUF kwa ujumla kuleta mabadiliko ya kweli kwa manufaa ya nchi yetu na vizazi vyetu.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |