Alipokaribia umri wa miaka 40, Muhammad (s.a.w.) alizidisha kukaa katika pango la Hira kwa muda mrefu zaidi kuliko hapo awali na kila alipoita, ndoto zake zilitokea kweli. Siku moja katika mwezi wa Ramadhani, 610 A.D., Muhammad (s.a.w.) alipokuwa katika fikra na mazingatio ya undani juu ya Allah (s.w.), ghafla alitokea mkuu wa Malaika, Jibril (a.s.), mle pangoni na akamuamrisha kusoma. Muhammad (s.a.w.) alikuwa Ummy asiyejua kusoma wala kuandika. Hivyo akiwa katika hali ya kutetemeka kwa msituko, alimjibu Jibril; "Sijui kusoma". Jibril alimkumbatia Mtume kwa nguvu mpaka akahisi taabu, kisha akamwachia na kumuamuru tena kwa mara ya pili: Soma". Jibu la Mtume likawa lile lile la mara ya kwanza, "Sijui kusoma". Jibril alimkumbatia tena Mtume kwa nguvu kama alivyofanya katika mara ile ya kwanza. Jibril alirudia tena amri yake na jibu la Mtume likawa lile lile. Kisha Jibril alimsomea Muhammad (s.a.w.) aya tano za mwanzo za Surat, 'Alaq (96:1-5). Historia ya kushuka wahayi huu wa kwanza imeelezwa vema katika hadithi ifuatayo:-
Bibi 'Aysha (r.a.) amesema: Kilichoanza katika wahayi wa Mtume (s.a.w.) ni ndoto za kweli.Alikuwa Mtume (s.a.w.) haoti, isipokuwa kilidhihri kile alichoota. Kisha akaona ni bora kujitenga.Akawa anakwenda Jabal Hira kujilinda na maovu. Basi alikuwa akichukua masurufu kwa ajili hiyo. Masurufu haya kila yalipoisha alirudi tena kwa Bibi Khadija aliyemtayarishia masurufu kama yale (ya kwanza) mpaka ikambainikia haki akiwa pangoni Hira. Basi akamjia malaika (Jibril) humo pangoni akamuamrisha kusoma. Mtume (s.a.w.) alijibu "Sijui kusoma". Mtume aliendeleakuhadithia: akaimba na kwa nguvu mpaka nikahisi taabu na akaniambia soma, nilijibu:"Sijui kusoma". Kisha alinibana tena kwa kwa nguvu kwa mara ya pili mpaka nikahisi taabu.Kisha aliniachia tena na kuniamrisha tena kusoma.Nikajibu tena:"Sijui kusoma". Akanikumbatia tena kwa nguvu kwa mara tatu mpaka nikahisi mashaka, kisha akaniachia akasema:
"Soma kwa jina la mola wako aliyeumba.Ameumba mwanadamu kwa pande la damu. Soma na Mola wako ni karimu sana. Ambaye amemfundisha (mwanadamu) kwa msaada wa kalamu.Amemfundisha mwanadamu mambo aliyokuwa hayajui. (96:1-5).
Mtume wa Allah alirejea na wahayi huu huku moyo wake ukidunda kwa khofu aliyokuwa nayo.Alikwenda kwa mkewe, Khadijah na kumwambia: "Nifunike!" Walimfunika khofu ile ikatoweka na baada ya hapo alimuhadithia Bibi Khadijah yale yote yaliyomtokea kisha akasema: "Hapana! Naapa kwa jina la Allah, Allah hatakufedhehesha. Unakaa vizuri na kuwafanyia wema ndugu na jamaa zako, unawasaidia masikini, fukara unawakirimu wageni na unawasaidia waliokabiliwa na matatizo". (Sahihi Bukhari).
Huu ndio Wahayi wa kwanza uliomtawadhisha Muhammad (s.a.w.) kuwa Mtume wa mwisho wa Allah (s.w.) na hivi ndivyo alivyopokea. Katika hadithi ili ambayo tunafahamishwa kwa refu namna Mtume (s.a.w.) alivyopokea wahayi wa kwanza, tunajifunza yafuatayo:
Kwanza: Kazi ya kuongoza dini ya Allah si kazi nyepesi, bali ni kazi nzito inayohitajia maandalizi makubwa. Pamoja na kuwa Mtume (s.a.w.), kama Mitume wengine, aliandaliwa kuwa Mtume tangu utotoni mwake, bado alipewa makubwa zaidi alipokaribia kukabidhiwa utume, pale alipohamia pangoni ili kupata wasaa wa kujikurubisha kwa mola wake kwa kina kirefu zaidi. Maandalizi haya ya mwisho yaliambatana na kufahamishwa uhakika wa mambo mbalimbali kwa njia ya ndoto.
Pili: Kiongozi wa jamii ya Kiislamu awe mwenye Elimu.
Tatu: Suala la kuwepo Allah ni la kielimu. Tunajifunza kuwa kusoma (kujielimisha) juu ya mazingira na juu ya habari mbalimbali ni miongoni mwa mambo ya msingi katika kumuandaa mja kwa ajili ya kuhuisha na kusimamisha dini ya Allah (s.w.) katika jamii. Pamoja na kwamba Mtume (s.a.w.) alikuwa Ummy (asiyejua kusoma na kuandika) bado aliamrishwa kusoma na Jibril (a.s.) kama kielelezo kuwa kusoma ni jambo la msingi mno katika kazi ya kuhuisha na kusimamisha dini ya Allah (s.w.).
Nne: Mapinduzi ya kweli yataletwa kwa kuelimisha watu. Elimu ndio chombo cha kuleta Mapinduzi ya kweli hivyo watu waelimishwe.
Tano: Mitume wa Allah (s.w.) japo wanazaliwa mitume, hawajifahamu kuwa ni mitume mpaka pale wanapopewa utume na kuamriwa kuwa wajitangaze kwa watu kuwa wao ni mitume wa Allah. Hali kadhalika Mtume Muhammad (s.w.) hakujijua kuwa yeye ni Mtume wa Allah (s.a.w.) wala hakutarajia kuwa atakuwa Mtume siku moja ndio maana alikhofu sana alipojiwa na Malaika Jibril kwa mara ya kwanza.
Baada ya tukio hili ule moyo wa Mtume (s.a.w.) wa kutaka kuondoa udhalimu ulizidi, akawa hana hakika lipo afanye na lipi asifanye na akifanya aanzie wapi. Wakati yupo katika mawazo mazito haya siku moja alipokuwa anatoka Hira kuja nyumbani kwake alisikia sauti ikimwita alipoinua uso aliona kititi baina yha mbingu na ardhi kilichokaliwa na Jibril, malaika yule yule aliyemtokea Hira mtume alishikwa tena na khofu akaenda tena kwa Bibi Khadijah na kumuambia nifuke nifunike. Bibi Khadija akamfunika. Ni katika hali hii ndipo akateremshiwa wahayi wa pili na watatu kama ifuatavyo:-
Ewe uliyojifunika nguo gubigubi, simama uonye, Mola wako mtukuze. Na nguo zako uzisafishe, na mabaya yapuuzwe, wala usiwafanyie ihsani viumbe ili upate kujidhihirishia, kwa ajili ya Mola wako fanya subira, (74:1-7).
Wahayi mwingine ulioshuka katika mazingira kama hayo ni huu ufuatao:
Ewe uliyejifunika maguo simama usiku ila muda mdogo, Nusu yake au ipunguze kidogo. Au izidishe na soma Qur'an vilivyo. Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito. Hakika kuamka usiku kunawafikiana zaidi na moyo na maneno yanatua zaidi.Hakikamchana unashughuli nyingi. Na litaje jina la Mola wako na ujitupe kwake kwa kweli, (73:1-8).
Sura hizi tatu ndizo za kwanza kushushiwa Mtume Muhammad (s.a.w.) na ndizo zenye misingi ya awali ya kusimamisha Uislamu. Kwa hiyo ingawa ni kweli Mtume ameendelea kuwa katika uangalizi wa moja kwa moja wa Mwenyezi Mungu akiwa kama Mtume, aya hizi ndizo zilizoweka misingi ya kusimamisha Uislamu. Hivyo maandalizi ya Mtume (s.a.w.) kielimu tutayafungia katika aya za sura tatu hizi. Elimu ndio msingi wa kwanza anaopewa Mtume (s.a.w.) katika kazi yake ya Utume. Hapa anatakiwa Mtume (s.a.w.) afanye kazi yake ya Utume, kazi ya kusimamisha Uislamu, kitaalamu, kwa ujuzi, na kimipango.
Elimu imetangulia vyote kwa sababu nyingi.Elimu ndio inayomtofautisha mwanadamu na viumbe vingine na ndio msingi wa utukufu wa mwanadamu anapolinganishwa na viumbe vingine. Elimuj ndio chombo cha kutegemea cha kuleta mapindujzi ya kweli yanayotokana na badiliko la mwenendo na muelekeo wa mja. Vile vile mwanadamu amejaaliwa awe ndiye anaendesha Dunia, na elimu ni nyezo ya lazima katika utawala huu. Kwa kuwa elimu ni msingi wa kwanza wa kusimamisha Uislamu, kujielimisha ni faradhi kwa Waislamu wake kwa waume, ni amri na faradhi ya kwanza kabisa na ni Ibada. Kujielimisha huku ni katika upeo wa kuelimika katika maana halisi ya neno lenyewe. Isiwe elimu ya upande mmoja tu, kama ilivyozoeleka kuwa elimu ya Dini tu au Elimu ya Dunia tu, kitu kama hiki hakimo ndani ya Uislamu, lililo la lazima elimu hiyo iwe ni kwa ajili ya Allah. Hii ndio maana ya aya ifuatayo:
"Soma kwa jina la Mola wako ambae amemfundisha mwanadamu kwa msaada kalamu. Amemfundisha mambo aliyokuwa hayajui". (96:2-5).
Kanuni hii ya kusimamisha Uislamu kielimu, kimipango, kisayansi (n.k.) ilitumika wakati wote wa Mtume (s.a.w.) pamoja na njia nyingine zilipelekea kusimama kwa Dola ya Kiislamu. Katika aya ya 1 ya sura ya 73 na aya ya 1 ya sura ya 74 Muhammad akiwa keshapewa utume bado Mwenyezi Mungu anamwita, Ewe uliojifunika nguo, gubigubi, sio kwa kuwa tu amejifunika nguo, lakini ni kumuambia kuwa kazi ya utume uliyopewa si ya kubweteka au kulala, au kuogopa, ni kazi ya kuwaita watu kwenye njia ya Mwenyezi Mungu ndio maana mara tu baada ya aya ya kwanza ya 74:1 aya ya pili anaamriwa 'Simama uonye'. Kanuni hii imetumika wakati wote wa utume na inatumika hadi leo katika kujenga Uislamu. Kutilia mkazo kuwa kazi hii ni nzito aya ya tano ya 73 inakokoteza kuwa Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito (73:5). Baada ya hapo ndipo Allah (s.w.) anampa Mtume wake maelekezo ya namna ya kufanikiwa kwa kazi hiyo, "kwanza ni kuswali usiku".
Ewe simama usiku (kucha kufanya ibada) ila muda mdogo (tu hivi) Nusu yake au ipunguze kidogo (73:23).
Kuswali kuna ashiria kumtakasa Mtume (s.a.w.) sisitizo la kuswali usiku ni kutokana na ukweli kuwa usiku kuna ukimya, moyo hutua hivyo unyenyekevu mkubwa hupatikana na mja huwa karibu na Mola wake. Maandalizi haya yalikuwa ya lazima kwa Mtume kwani kazi ya kusimamisha Uislamu ni ngumu na inahitaji kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kiasi ambacho moyo wake hauna nafasi ya vitu vingine ila kumtumikia Allah (s.w.), si hivyo tu bali kuwa karibu na Allah (s.w.) humjengea mja kujiamini kunakotokana na kumtegemea Allah katika kila jambo afanyalo.
Hali hii hujenga ujasiri mkubwa unaotoka ndani ya imani na kukupa msukumo na nguvu na kutokuogopa chochote zaidi ya Allah (s.w.) kuwa karibu na Allah. Kwa kupitia njia ya kuswali usiku kunambadili mtu kutoka katika kuwa mtu anaendeshwa na silika za kinyama akawa mtu anaendeshwa na silika ya UTU Ubinaadamu, kutoka kuwa mtu wa shetani akawa mtu wa Mungu. Kujitakasa kunajenga matumaini ya kudumu ya mafanikio ya duniani na akhera na kunavunja silika ya kukata tamaa na kuchanganyikiwa ambazo ni sifa za asiyemtegemea Mwenyezi Mungu. Inakokotezwa katika aya ya sita ya Suratul Muzzamil:
Na litaje jina la Mola wako na jitupe kwake kwa kweli (75:6).
Hivyo ni dhahiri kwa Waislamu wa leo kusimamisha Uislamu kunahitaji maandalizi, maandalizi ndio jambo la kwanza kwa hiyo fursa zitumike na ziundwe kwa mpango ili kuwaandaa viongozi vijana na watu wazima ili kusimamisha Uislamu. Maandalizi ya kwanza ni kuwaelimisha kwa kila fani na pili tujiandae kuwa wema, wacha mungu, kwani bila ya watu wenyewe kubadilika Uislamu hautosimama kama tutavyoona katika hatua ya pili.
Kanuni ya tatu ya kusimamisha Uislamu aliyopewa Mtume ni kumtukuza Mwenyezi Mungu. Kanuni hii pia ilikuwa ya msingi kabisa kwani utume wa mitume wote ulikuwa na kazi hii ya kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa vitendo ambako ni kufanya jitihada ya mwisho ya kuanzisha na kudumisha ufalme wa Mwenyezi Mungu hapa Duniani, kuanzisha serikali inayoendeshwa na sheria za Mwenyezi Mungu. Kazi hii Mtume aliikamilisha katika muda wa miaka 14 baada ya kufanya jitihada kubwa ya kufanyakazi kwa mfululizo na kuvishinda vipangamizi vyote. Lakini maana ya pili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu ni kuwa sheria za Allah peke yake ndio ziwe za kufuatwa kwa nyakati zote na mahali popote. Huu ndio ujumbe wa Mtume Muhammad, maisha yake yote amechunga na kuhakikisha kuwa sheria za Allah ndizo zinazofuatwa katika jamii. Basi nasi Waislamu wa leo ndivyo tunavyopaswa kufanya tusipumzike tufanye kila tuwezalo ili kusimamisha ufalme wa Allah hapa duniani na kutokomeza tawala zote ambazo ni zao la akili ya mwanadamu. Ni hivyo hivyo kwa sheria. Sheria zetu ziwe za Allah (s.w.) na tuondokane na sheria nyingine zozote ambazo ni zao la akili ya mwanadamu. Vile vile tunawajibu wa kuondoa maovu katika jamii kwa jitihada zote. Ili kazi hii ifanikiwe Mtume anaagizwa 'Na nguo zako zisafishe" kanuni hii inaingiza vitu vingi, inaingiza afya na saikolojia ya kuonekana mbele ya watu (Public appearance) na utakaso.
Ingawa aya hii inataja usafi wa nguo lakini inaashiria usafi wa roho, (nia) ukweli na kivazi. Katika kufanya kazi hii ya kusimamisha ufalme wa Allah (s.w.) hapa duniani, nia iwe safi, nia ikiwa safi na kwa hiyo ili upokelewe na watu wakusikilize lazima uwe nadhifu (msafi).
Kanuni hii inaungana na kanuni ya kupuuza mabaya. Aya hii imesaidia sana katika kusimamisha Uislamu. Mtume alifanyiwa mabaya mengi sana; pasingekuwepo na kanuni hii asingeweza kukamilisha kazi yake, kupuuza mabaya kumempa fursa ya kutokupoteza muda wa kushughulika na waliyomfanyia ya ubaya na upuuzi.Vile vile kumewaadhiri wafanyaji ubaya kwa kutokupata nafasi ya kugombana na Mtume. Yote haya Mtume anatakiwa ayafanye kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu si kwa kupata lolote kutoka kwa wanadamu. Na kwa sababu hiyo anapewa kanuni ya kufanya subira katika yote yatayomkuta wakati wa kufanya kazi hii.Kwa yote haya Mtume anatakiwa amtegemee Mwenyezi Mungu kikweli kweli na aisome Qur'ani.
Kusoma Qur'ani kutampelekea Mtume kukumbuka maelekezo
ya muumba wake hivyo kufuata maelekezo hayo na kuwa karibu na Allah (s.a.w.)
jambo ambalo linapanua eneo la kumtegemea kikweli kweli na kufanya kila
kitu kwa ajili yake. Hatua hizi zote, na mafunzo haya yote nasi leo tunapaswa
kuyapokea kama yalivyo na kufuata hatua zote kama alivyofanya Mtume katika
kusimamisha Uislamu.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |