Mipasho ya khanga iwe ya kufunza

ILIKUWA ni siku ya Jumatano majira ya saa 2.00 asubuhi huko Kinondoni B, mtaa wa Isere, katika nyumba ya Mzee Alisa, akinamama wawili (wote wapangaji), mama Saleh na mama Maimuna, walitwangana makonde hadi mmoja wao kupoteza jino moja. Majirani walipotokea kuamua na kuuliza kulikoni - jibu lilikuwa chanzo ni khanga aliyovaa mama Saleh iliyoandikwa "Kama unaweza panda juu ukazibe".

Khanga ni kipande cha kitambaa kilichorembwa na maua, rangi mbalimbali na kuchapishwa maneno yenye kutoa tafsiri kulingana na watumiaji (wavaaji). Kipande hicho cha kitambaa aghalabu huwa na upana usiozidi mita mbili na urefu usiozidi mita moja.

Vazi la Khanga ni maarufu sana kwa Waswahili wa maeneo ya Mwambao wa pwani ya Afrika Mashariki.

Uvaaji wa Khanga katika maeneo hayo kulingana na historia, ulianza tokea karne ya 19.

Kutokana na kuenea kwa uvaaji wa khanga kutoka sehemu za mwambao hadi bara, pia kumepelekea kwa kiasi fulani wageni wengi wanaoingia nchini kuvutiwa na vazi hilo, mfano Wazungu, Wachina na kadhalika.

Uvaaji wa khanga hutoa tafsiri tofauti kulingana na haja ya wavaaji wenyewe. Kuna wale wanaoona kuwa khanga ni vazi la ziada kwa mwanamke - yaani baada ya kuvaa nguo, juu hujitanda khanga kama ni sitara ya ziada. Wengine husema kuwa ni vazi maalum la siku ya harusi kwa wanawake , yaani Bi harusi. Tafsiri ya wengi husema kuwa khanga ni nguo au vazi la kwanza kwa mtoto mchanga siku anayokuja duniani.

Hata hivyo matumizi ya khanga ni mengi mno kama vile wakati wa sala kwa wanawake wa Kiislamu, joto linapokithiri baadhi ya watu huvaa khanga ili wapate hewa, khanga pia hutumika kama kifutia maji baada ya kukoga.

Vile vile, khanga hutumika kama sare maalum ya harusi ambapo humaanisha umoja au muungano baina ya pande mbili husika.

Kwa upande wa bei, khanga huuzwa kati ya shilingi 1100 hadi 1500 (kwa zile zinazotoka India) na shilingi 3000 (kwa zinazotoka Kenya).

Kabla ya kuangalia ujumbe ulionao katika khanga kwanza na tuone wavaaji wa khanga wanavyosema: "Kwa kweli mimi napenda sana kuvaa khanga, lakini huwa navutiwa zaidi maua na rangi ya khanga yenyewe bila ya kujali jina la khanga", anasema Bi Aisha Abdulla.

Maneno hayo ya Bi Aisha yanatofautiana na akina mama wengi ambao husema wanapenda na kuvutiwa zaidi na majina ya khanga iwe ya mapenzi au mafunzo lakini hasa ya mipasho.

Majina katika khanga hubeba kazi ya kuwa mdomo wa mvaaji au hata mtu anayemtunukia mlengwa zawadi ya khanga.

Ujumbe ulionao katika khanga mara nyingine huwa dhahiri na wakati wengine huwa umejificha, hivyo huhitaji uchambuzi wa kina kulingana na kila mtu na mtazamo wake.

Kwa kutumia mifano michache ya majina ya khanga na tuangalie majina yafuatayo na ujumbe uliomo ndani yake:

"Titi la mama tamu".

Jina hili linakusudia kutoa msisitizo juu umuhimu wa akinamama kuwanyonyesha watoto wao kwani mbali ya kuwa maziwa hayo yana ladha pekee kwa watoto bali pia ni bora kwa afya ya watoto.

"Nani kama mama".

Huu ni ujumbe mzito unaosisitiza haja ya watoto kuwathamini wazazi wao (hasa mama) kwani ni mtu ambaye alichukua tabu nyingi na ustahamilivu wa kipekee wa kulea mimba, kukuzaa, kukulea hadi ukafikia hapo ulipo. Hivyo watoto ni lazima waelewe kuwa mama hawezi kulinganishwa na mtu yeyote hata mtu huyo awe amekufanyia mema gani.

"Si mzizi si hirizi bali moyo umeridhi".

Hapa ni jibu tosha kwa wale ambao hupenda kushutumu au kutia fitina hasa katika masuala ya mapenzi ya watu wawili katika ndoa. Mara nyingi katika jamii, inapotokea mume kumpenda sana mkewe kupita kiasi, basi nong'ono za pembeni zitaanza kuwa eti si bure lazima atakuwa amerogwa na mkewe. Sasa jina hili linawaeleza watu wa aina hiyo kuwa mapenzi shina lake ni moyoni halihitaji dawa za aina yoyote.

"Nipende nijisikie wambea waumie".

Ni ujumbe anaotuma mwanamke kwa mumewe azidishe mapenzi ili wale wanaochunguza na kutoyatakia mema mapenzi yao basi, watahayuri na wasijue la kufanya hali ya kuwa watakuwa wanaugulia nyoyoni.

"Mpenzi wangu habibi yuko wapi simuoni".

Ni tamko linalomlenga mtu ambaye kwa sababu moja au nyingine amemtenga mwenzake bila sababu inayoeleweka na mtoaji ujumbe huo. Hivyo huyo mpenzi aliyemtenga mwenzake anapaswa ajue kuwa mwenzake anateseka bila ya kuwa na yeye karibu. Ujumbe huu huweza hata kufikishwa na watu waliokaribu na malalamikaji.

"Kila ulionalo wasema na hili pia kaseme".

Ni salamu anazopewa/anazoelezwa mtu mbea ambaye hukaa na kuchunguza undani wa mtu na baadaye kupeleka umbea kwa mtu mwingine iwe mambo ya mume na mke, ya mke kwa mume, jirani na jirani au katika mazingira yoyote yale yatakayohusisha pande mbili.

Mbali ya yote hayo, ujumbe katika khanga huweza ukaleta athari mbaya au nzuri kwa wahusika.

Ushahidi wa hayo ni kuwa athari mbaya mara nyingi hupatikana katika majina ya mipasho ambapo watu hufikia kufarakana na kupigana hadi kuwekana kilema.

Na kwa upande wa athari nzuri ni pale majina ya mafunzo mema yanapoweza kubadili tabia za watu au watu kutekeleza ujumbe mzito uliomo katika khanga hasa masuala ya jamii. Na kwa upande wa mapenzi huweza yakamea au yakavutia watu wengi zaidi.

Hata hivyo, uvaaji wa khanga kikawaida una namna zake si vizuri kuvaa khanga moja tu (mwanamke) na kutembea nje ya nyumba yako au kuvaa khanga moja kutoka nje ya chumba chako katika nyumba yenye zaidi ya familia moja. Pia jambo la msingi na la kuzingatia ni kuwa uvaaji wa khanga usiwe ndio chanzo cha migongano katika jamii, bali na zivaliwe kwa nia njema tu.


Mila mbaya ziachwe

HISTORIA inatuonesha kuwa kila jamii ina mila na utamaduni wake na jamii hiyo hufuata na kuendeleza mila na utamaduni wake kutoka kizazi hadi kizazi.

Wanajamii hulazimika kuzifuata na kuziendeleza mila na tamaduni zake kwa kupenda au kutopenda.

Miongoni mwa mila na tamaduni hizo kuna zilizo nzuri ambazo huleta maelewano na maendeleo katika jamii na nyingine si nzuri kwani huleta mifarakano, unyanyasaji na kurudisha nyuma maendeleo.

Mila na tamaduni zilizo nzuri ni bora zikaendelezwa hasa zile zilizokwishaanza kufifia.

Katika jamii nyingi karibu zote hapa Tanzania na Afrika kwa ujumla walikuwa wakiheshimu sana wazee, na wazee walikuwa ndio washauri wakuu katika jamii. Walikuwa wakisuluhisha matatizo mbalimbali katika jamii kama ugomvi wa hapa na pale hasa kwa vijana wanandoa.

Heshima hiyo kubwa waliyokuwa wakipewa wazee imeanza kufifia na katika baadhi ya jamii imetoweka kabisa. Sehemu kadhaa wazee wanaonekana wachawi na wanauliwa hasa mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Hapo zamani huwezi kumuona mzee amebeba mzigo uwe mkubwa au mdogo, ni lazima tu kijana anayemfahamu au asiyemfahamu atamsaidia tu. Lakini sasa inasikitisha kuona kijana anampita mzee mwenye mzigo bila kumsaidia au hata kumsabahi wanapigana vikumbo kama wanyama porini.

Zamani watu walikuwa wakishirikiana na kusaidiana katika shida na raha, wakifanya kazi kwa pamoja na hii ilisaidia kuleta maendeleo na mshikamano na kipato cha watu kilikuwa hakitofautiani sana. Leo kila mtu na lake na matokeo yake masikini wamekuwa wengi na ombaomba kuzidi kuongezeka kwani walio nacho wamekuwa wabinafsi wa roho zao.

Ni bora watu wakabadili mwenendo wa sasa na kurudia hali ya zamani ya kushirikiana na kusaidiana ili kuondoa tofauti ya hali ya maisha iliyoko sasa.

Kuna baadhi ya mila na tamaduni za jamii fulani fulani zimekuwa zikiendelezwa ambazo zinamnyanyasa, kugandamiza, zinaleta mifarakano na kurudisha nyuma maendeleo kwa ujumla.

Mila hizo ni kama kuwatumikisha wanawake katika shughuli za kilimo na ufugaji na kutowapa mapenzi yanayotakiwa.

Mila hii ni mbaya na inamnyanyasa mwanamke kwa kumfanya kama mtumwa.

Uislamu umempa nafasi kubwa ya upendo mwanamke na kumfanya kama malkia wa nyumbani kwani huwa pambo la nyumba na hatakiwi kufanya kazi yoyote zaidi ya kuzaa na ni wajibu wa mume kuweka mtumishi wa kufanya kazi.

Kwa hakika kati ya mila na tamaduni zilizombaya nyingi hunyanyasa na kumgandamiza zaidi mwanamke. Kwa mfano kuna baadhi ya makabila huamini mwanamke mjamzito hatakiwi kula baadhi ya vyakula ati vitamharibu au kumuua mtoto tumboni, vyakula hivyo kama mayai kwa madai mtoto atakosa nywele, ukiangalia kwa undani mila hii inamkosesha mama na mtoto virutubisho vyenye faida mwilini.

"Mwanamke kwetu mwiko kula mafirigisi na akila tu atapigwa na wanaume wa familia hiyo", anasema Grace Hoka ambaye kabila lake ni Muha.

Mila nyingine mbaya na ya hatari ambayo bado inaendelezwa ni baadhi ya makabila kurithi mke wa kaka yake au mjomba wake.

Mila hii inamfanya mwanamke aolewe na mtu asiye na mapenzi nae na asipewe uhuru wa kuchagua. Uislamu unakataza hivyo na ndio maana mwanamke anaozeshwa baada ya kuulizwa kama amekubali kuolewa.

Katika mila hizi potofu, nyingine husababisha kuongezeka vitendo vya ukahaba. Mfano katika kabila moja nchini mwanamke aliyeolewa kama atazaa mtoto ambaye amekufa basi atawajibika kutengwa na jamii na atapelekwa porini akaishi peke yake lakini hapati mtu wa kuongea nae au kuishi naye, hatakubalika kurudi nyumbani mpaka apate mimba nyingine sio ya mume wake bali wa kabila jingine kutokana na hali hiyo wanawake wengi huenda mjini kufanya ukahaba.

Ili tuishi maisha mazuri na ya raha ni vema tukaendeleza mila na tamaduni zenye manufaa kwetu na tukaacha mila zenye kutuharibia maisha yetu na kila mila tuiangalie upande wa Uislamu unasemaje kama inakubaliana nayo basi tusiiache.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook