Pamoja na dini yenu, AN-NUUR teteeni demokrasia
Ndugu Mhariri
POKEA pongezi nyingi kutoka kwangu mimi msomaji wa gazeti lako. Kwanza natanguliza shukrani nyingi kwa ujasiri wa hali ya juu unaooneshwa na gazeti lako katikati ya mbinyo wa serikali dhidi ya vyombo vya habari.
Mfano dhahiri ukiwa ni huu wa majuzi tu uliotokea baada ya Askofu Kakobe kuhojiwa na Masai Studio. Sasa hivi hakuna tena kipindi cha Kiti Moto, wala hakuna chombo chochote cha habari kilichoonesha msimamo wa kuilaumu serikali ili wananchi wapate uhuru wa kueleza mawazo yetu.
Mpaka sasa tumeshafahamu kuwa adui wa demokrasia katika nchi hii ni CCM na serikali yake. Serikali ya CCM imeachia uhuru wa magazeti kwa kuwa inajua kuwa wasomaji wa magazeti ni wachache sana tena wapo mijini tu na wakati mwingine siyo miji yote inayofikiwa na magazeti.
Pale ambapo CCM inajuwa kuwa ni kwa faida ya wananchi, na ni hasara kwa upande wake inazuia, na kuona kuwa ni heri kuendelea kuwaburuza wananchi katika ujinga kuliko waelewe waendako na kuhamasisha maendeleo yao.
Mpaka sasa hapa Tanzania hakuna maana yoyote ya kuwa na vyombo vya habari binafsi kama Redio na TV. Kama yanayotangazwa huko ni mpaka yapate kibali cha CCM na serikali yake.
Ebu fikiria kama vyombo vya habari vya Marekani vingemwomba Rais Clinton ruhusa ya kutangaza kashfa yake ya mapenzi dhidi ya Monica, habari zile tungezifahamu?
Vipi hawa CCM kitu kama Tume ya Jaji Kisanga imetoa mapendekezo yake baada ya kutumia mamilioni ya walipa kodi, badala ya taarifa hiyo moja kwa moja kuwaendea Wabunge ambao ni wawakilishi wa walioituma Tume kwa pesa zao mapendekezo hayo kwanza yanapelekwa NEC-CCM.
Hapo ndipo tunapojiuliza, kama NEC-CCM ndio walikuwa na uamuzi wa mwisho, pesa za wananchi zilitumika kwa sababu gani! Hapo ndipo tunapofahamu kuhusu sera ya CUF anayoihubiri Mwenyekiti Lipumba ya kuwa umaskini wa nchi hii umetokana na kitendo cha watawala kufanya uchumi utumikie siasa badala ya siasa kutumikia uchumi.
Ndugu Mhariri, ninakuomba gazeti lako liishutumu serikali ya CCM kwa kuua kwa makusudi demokrasia kwa kutumia Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).
Mifano miwili ya hivi karibuni imenikera sana, mmojawapo ukiwa ni siku CCM ilipomteua mgombea wake na kumchangia pesa ili akachukue fomu ya kugombea. Ilisikika sauti ya hotuba kupitia RTD ikiwashutumu wale wanaofanya mikutano na kuiita "ya ndani" eti wanavunja sheria kwa kuwa hairuhusiwi katika mikutano ya ndani kuweka vipasa sauti nje, sauti hiyo ikatoa mfano eti mfano halisi ni "huo waliokuwa wanahudhuria wao".
Jambo hilo lilinikera kwa sababu wakati wanauita mkutano wao, mkutano wa ndani usio na vipaza sauti, RTD inautangaza nchi nzima. Kwa hiyo kama walioendesha mkutano wa ndani walifunga vipaza sauti na wakavamiwa na polisi, wale waliotumia Redio kwa mkutano waliouita wa ndani walitakiwa nao wavamiwe na kufunguliwa mashitaka kama tungekuwa katika utawala unaojali sheria.
Jambo la pili lililonikera sana ni la hivi karibuni ambapo mikutano mikuu miwili ya vyama vya siasa ilikuwa na vikao kwa ajili ya kuwathibitisha na kuwachagua wawakilishi wao katika kinyang'anyiro cha kuwania Urais katika uchaguzi mkuu.
Chama cha CUF kilikuwa na kikao chake mjini Mwanza nani chama cha pili kwa wingi wa viti vya Ubunge. Chama kingine kilikuwa CCM ambacho kilikuwa na kikao chake mjini Dodoma na ndicho chama tawala na cha kwanza kwa wingi wa viti vya Wabunge.
Pamoja na kwamba vyama hivi ni vya wananchi walipa kodi na maskini wenye usongo na maendeleo ya nchi yao ni mkutano wa CCM uliosikika RTD tangu asubuhi mpaka jioni. RTD ilijifanya haijui lolote kuhusu mkutano mkuu wa CUF Mwanza kiasi kwamba hata taarifa yoyote kuhusu hotuba ya viongozi wakuu na wagombea wa viti vya Urais hatukuzisikia.
Hiyo ndiyo demokrasia na uhuru wa vyombo vya habari tena unaoitwa uhuru wa kutoa mawazo tunaohubiriwa na CCM kwamba wamejengea demokrasia ya kweli, demokrasia itakayotufanya tuwe sawa na haki sawa katika nchi yetu mkutano mkuu wa CCM na vyama vingine uwe na haki sawa katika vyombo vya habari vya serikali. Isipokuwa kama CCM wanayo Redio walioijenga basi wanaweza kuitumia kama wapendavyo, lakini si uvunjaji wa sheria na ukandamizaji wa demokrasia kutumia vyombo vya serikali vinavyoongozwa na kuendeshwa na wananchi wote kwa manufaa ya chama kimoja.
Rais Mkapa anazo kofia mbili za mamlaka, moja ni kiongozi wa serikali na pili ni mwenyekiti wa chama chake CCM. Katika kofia zake hizi ni muhimu sana RTD na TVT kufahamu kuwa Mkapa anaposafiri mikoani akiwa na shati la kijani yuko tayari kuhamasisha ukuaji wa chama chake na kupokea kadi za watu wanaorudi CCM.
Katika safari kama hizo Mkapa hana tofauti na Mrema na Lipumba au Cheyo na Makani (Bob) ambao hao ni wenyeviti wa vyama vyao. Nao wanapohutubia na kuhamasisha mpaka kupokea kadi za wale wanaojiunga na vyama vyao wanatakiwa watangazwe kama Mkapa anatangazwa. Ila Mkapa anapokuwa katika ziara za kiserikali anatakiwa kuwa tofauti maana hapo ni Rais wetu.
Kwa kifupi, RTD na TVT wanatakiwa wawe wanatuma waandishi wa habari na wapiga picha ili kufuatana na viongozi na kwa ustawi wa nchi yetu na demokrasia kwa ujumla.
Demokrasia ya kweli ni lazima ifuatane na utoaji wa habari bila upendeleo, maana ni kwa ajili ya Taifa na maendeleo ya wananchi wake. AN-NUUR lipigieni debe hili, sambamba na haki zenu, mauaji ya Mwembechai na haki za Waislamu kwa ujumla asili yake ni kukosekana uhuru wa kutumia vyombo vya habari vya Taifa.
Mwinjilisti Salvatory,
S.L.P. 72617,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
UJUMBE wa Mhe. Rais Mkapa kwa vijana juu ya suala la ukimwi hauwezi kuachwa upite hivi hivi.
Mimi nashauri serikali ifanye kazi kuwa kufuta ile dhana potofu ya "ngono salama". Msukumo wa kampeni hii uwe Hapana. Hakuna ngono salama nje ya mipaka ya uadilifu katika ndoa.
Pamoja na hayo serikali ichukue hatua kufuta madanguro na kuondoa vishawishi mbalimbali.
Salma Juma,
Kibaha.
Ndugu Mhariri
LICHA ya jitihada zinazofanywa na wanahabari kupitia taasisi zao kuwashauri wanahabari wa vyombo mbalimbali kutofanya upendeleo katika utendaji kazi wao na kujiingiza katika ushabiki wa vyama, bado RTD na TVT vinapendelea CCM waziwazi.
Ilitazamiwa kuwa vyombo hivi vya habari vya Taifa vingelikuwa mfano mwema wa kuigwa na vyombo vingine kwa kutoa habari bila upendeleo wala ushabiki. Lakini kinyume chake, vyombo vinavyojitegemea ndio kidogo vyenye kuzingatia wito wa kutopendelea au kubagua upande wowote.
Hivi majuzi imefanyika mikutano mikuu maalum ya vyama vya CUF na CCM. Vyama vyote hivyo vilifanya mikutano hiyo kupitisha wagombea wao viti vya Urais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
Jambo la kusikitisha na kushangaza ni kuwa wakati mkutano wa CCM ulitangazwa moja kwa mjoa na RTD kutoka kule ulikofanyika, mkutano wa chama cha CUF sio tu hakutangazwa bali haukuweza kuripotiwa hata kwa sentensi mbili. Badala yake vyombo vya habari vya nje hasa hasa Sauti ya Ujerumani ndio iliyotangaza mkutano huo.
Kitendo hicho si tu kinaonesha picha mbaya duniani, bali kimewanyima wananchi haki yao ya kupata habari mbalimbali nchini.
Vyovyote iwavyo, wananchi wamegawanyika katika mitazamo mbalimbali ya kisiasa lakini wao kama raia na wapiga kura wana haki ya kupata habari za pande zote. RTD haina haki ya kuwabagua wananchi hawa kwa sababu ya itikadi zao.
Tukitazama vyombo vya habari vya wenzetu kule nje hasa Marekani na Ulaya, twaona jinsi vinavyofanyakazi kwa ajili ya wananchi wote wawe wapenzi au wapinzani wa serikali. Katika kampeni za uchaguzi wowote wa nchi hizo vyama vyote na wagombea wote hupewa nafasi sawa katika vyombo vya habari, ili wananchi waamue wenyewe nani anayefaa kupigiwa kura.
Jambo hilo linafanya uchaguzi uwe na ladha ya kusisimua hata kwa watu wa nchi nyingine. Lakini uchaguzi wetu leo hii hauna ladha. Tunaipongeza sana Sauti ya Ujerumani kwa kazi ya ziada wanavyotufanyia. Radio hiyo ndiyo iliyotupatia habari za kusisimua kuhusu uchaguzi mkuu ujao wa nchi yetu. Inavitangaza kwa usawa kabisa vyama ambavyo, mwaka huu ndivyo vitakavyochuana vikali Bara na visiwani yaani CUF na CCM.
Kwa bahati nzuri Sauti ya Ujerumani inasikika vizuri zaidi na inawafikia wananchi wa pembe zote za nchi kuliko hata Radio yetu ya Taifa ambayo haisikiki kabisa katika maeneo kadhaa ya nchi.
Kwa kweli watu wengi hupendelea zaidi kusikiliza Taarifa za habari za sauti ya Ujerumani kutokana na uchambuzi wake wa habari mbalimbali za ulimwengu zikiwemo za nchi yetu. Ili kupata habari za uchaguzi mkuu, imekuwa kawaida sasa kuwakuta watu wakijumuika jirani na Radio zao kusikiliza sauti ya Ujerumani nyakati za adhuhuri na jioni.
Tunaiomba Radio yetu ya Taifa iige mfano huo wa sauti ya Ujerumani.
Ni busara wale wanaofanya juhudi ya kuvihimiza vyombo vya habari kuwa vizingatie mizani sawa wakati wa kampeni za uchaguzi, waiase zaidi RTD ambayo kama itajirekebisha itaonesha mfano kwa vyombo vingine vya habari.
Vinginevyo jitihada za wasamaria hao hazitazaa matunda kwani wengine nao hawatovumilia kuona kuwa upande fulani unapendelewa.
Batuli Hussein,
Morogoro.
Ndugu Mhariri
HAIWEZI kuwa tumedhamiria kuimarisha umoja wetu na muungano wetu halafu Zanzibar kuew na mgogoro tuseme: Zanzibar ina katiba yake na Rais wake.
Hoja ikiwa hiyo, mbona ikitaka kujiunga na OIC tunakuja juu. Mbona ikitaka kubadili katiba haisemwi - wana uhuru wao.
Kama tunathamini muungano, matatizo ya Zanzibar yatugusa pia.
Vinginevyo basi tutakuwa tunafurahia ikipatwa na janga na kuchukia ikipata Ne'ma.
Alhaj Othman Khalil,
Tanga.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi niwaase wananchi wenzangu wa Zanzibar kuwa katika nchi yetu tatizo letu ni chama tawala. Kwa hivyo tusijidanganye kuwa eti mtu fulani atatusaidia eti kwa sababu msimamo wake ni mzuri japo yumo katika chama cha CCM.
Ndugu zanguni, hata hao tunaowaona wabaya hivi leo pia hapo mwanzo walikuwa wazuri, lakini chama kimewaharibu.
Ukiwa na kapu la samaki waliooza, hata ukiweka samaki mzima naye pia ataoza.
Hivyo, tusimtazame mtu tutazame chama. Sera za chama hicho zitabaki pale pale japo kiongozi ni mwingine. Kiongozi huyo hawezi kwenda kinyume na sera za chama chake. Vinginevyo chama kitamwajibisha kama kina Jumbe na kina Seif Sharif.
Tukumbuke Dk. Salmin alipotaka kujiunga na OIC, jinsi alivyoandamwa na chama chake. Kijumla matatizo yetu Wazanzibari hayatotatuliwa na mtu yoyote yule kupitia CCM.
Tujihadhari.
Thunei Idrisa,
Zanzibar.
Ndugu Mhariri
NAOMBA niseme machache. Gazeti moja la kila wiki Juni 15, mwaka huu limeandika habari kubwa ukurasa wa mbele kuwa "mgogoro sasa watokota CUF".
Mgogoro wenyewe ni mjumbe wa mkutano mkuu wa CUF kutumia kanuni iliyowekwa na Chama chake ya kumuuliza mgombea Urais maswali.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, swali aliloulizwa mgombea wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF lilikuwa uwezo wake katika kudhibiti matumizi ya Chama.
Mimi sikuona mantiki ya kuuita utaratibu huu kuwa ni mgogoro.
Kwa maoni yangu hii ni demokrasia ambayo hata katika mkutano wa CCM haikutokea.
Hakuna mwana CCM aliyethubutu kumuuliza Mkapa maswali.
Mimi naamini swali aliloulizwa Mhe. Seif Shariff ni kutokana na utaratibu mzuri uliowekwa na chama unaopelekea wanachama kujiamini. Kutokuhoji kama ilivyotokea katika mkutano wa CCM ni ububusa.
Hassan Raphael,
Mabibo,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |