Maulidi bora sana
Salam zangu za dhati, nawapa muuminina,
Pamoja na muuminati, na kila musilimina,
Na wote musilimati, atukidhi Maulana,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Tunasoma Maulidi, twazingatia maana,
Kuzaliwa Muhammadi, daima twajulishana,
Mtume wetu jadidi, katwachia Subuhana,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Kazaliwa bila hofu, na mama mwana Amina,
Kamzaa mtukufu, watu waka-ambizana,
Pongezi wakamsifu, wakazidi kujuwana,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Kazaliwa nchi ya Maka, kaishi hadi Madina,
Ukoo wa kusifika, Kuraishi nabiyina,
Twakumbuka kila mwaka, mwezi tunapo uona,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Mwezi wa mfungo sita, kazaliwa Sayidina,
Mtume alieleta, Uislamu wa dhamana,
Yote tunayafuata, kwa Mola ni bora sana,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Kapokea Kur-ani, toka kwa Mola Rabana,
Ukamilifu wa dini, kaitangaza bayana,
Ndiye Mtume yakini, Muhammadi Sayidina,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Mashehe dunia nzima, wote wakubaliana,
Ndipo twasimama wima, kumkumbuka bayana,
Heshima na taadhima, swalalau Sayidina,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Wakatabau ni basi, yatosha niliyonena,
Tushike dini halisi, bila ya kubaguana,
Kwa amani mahususi, tuishi kwa kupendana,
Maulidi bora sana, kumbukumbu ya Rasuli.
Rajabu Kirobo,
S.L.P. 100146,
Tandika Azimio,
Dar es Salaam.
Safina
Safina dau la Nuhu, limenenwa vitabuni,
Lilibeba masalihu, watii kwa Rrahamani,
Likaacha majurubu, marafiki wa shetani,
Safina nitie ndani, nifike ng’ambo salama.
Nifike ng’ambo salama, Safina nitie ndani,
Safina ni sawa mama, mtia mwana tumboni,
Akifanyiwa huduma, na wema usokifani,
Safina nitie ndani, nivushe ng’ambo salama.
Safina nakuneneza, naomba unimakini,
Kisa cha kukuchondeza, unondoshe khatiyani,
Naomba kunituliza, kwa kunitia chomboni,
Safina nitie ndani, nifike ng’ambo salama.
Safina ninakutaka, kwa sauti ya undani,
Naomba kuniitika, kwa itiko la hisani,
Kwako ninalolitaka, kuniingiza dauni,
Safina niingize ndani, nifike ng’a mbo salama.
Kwa ubeti namba tano, shairi litamatini,
Ninainua mikono, nikiwemo kisomoni,
Niombalo tangamano, twende vyema safarini,
Safina nitie ndani, nivushe ng’ambo salama.
(Mshairi - Bora)
Amiri A.S. Andanenga (Sauti ya Kiza)
S.L.P. 15430,
Kinondoni - Shamba,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |