RIWAYA

Joka la Mdimu - 3

FUNDI wa kimataifa wala hakuwa wa kimataifa kamwe. Alikuwa ni kijana aliyemiliki gereji moja maarufu hapo Sega. Gereji yake ilikuwa na sehemu mbili. Moja ni uwanja mkubwa chini ya mikorosho ambapo matengenezo madogo ya magari yalifanyika. Sehemu nyingine ilikuwa ni banda madhubuti lililozungushiwa ua wa mabati ya mabaki ya magari ya zamani. Zana za ufundi zote zilihifadhiwa mle ndani ya banda. Na matenengezo yote makubwa kama kushusha injini yalifanyiwa humo.

Zamani fundi wa kimataifa alikuwa jambazi la kutupa. Na hata hivi sasa, isipokuwa alibadilisha nyendo tu. Hakujihusisha tena na uvunjaji wa vijumba na wala kutia watu kabali. Kama alivyodai mwenyewe, yeye alikuwa wa kimataifa hata katika wizi wake.

Fundi huyo aliajiri vijana wengi, wengine stadi hasa katika fani za ufundi wa magari ingawa hawakuwa na vyeti maalum kutoka taasisi rasmi za ufundi. Alinadi fundi vitendo, sio vyeti.

Amani alifika pale gereji saa dhaifu kidogo kama saa nane na kitu. Chini ya mikorosho palikuwa na gari ndogo tatu, lori moja na Landrove mbili za serikali zikifanyiwa matengenezo.

"Fundi yupo?" Amani alimuuliza kijana mmoja aliyekuwa akitengeneza ile Landrover.

"Bahati yako ndiyo ameingia punde tu".

"Vizuri, yuko wapi?"

"Ndani", yule kijana alionesha kwenye lile lango la gereji kwa spana yake na kuendelea tena na shughuli zake.

Milio mbalimbali ya mikwaruzo ya vyuma ilisikika mle ndani wakati Amani alipokaribia lango ambalo lilikuwa limefungwa nusu. Ndani aliona magari madogo kadhaa ya mashirika ya serikali, mengine yakichomewa kwa gesi, mengine yakipulizwa rangi, na mengine yamefunguliwa injini. Fundi mwenyewe alikuwa anaangalia Rangerover moja ya shirika la serikali. Alitabasamu alipomuona Amani, akavuta miwani yake myeusi ya jua na kuipachika juu ya nywele zake.

Akapanua miguu na kuweka mikono yake kiunoni kama afanyavyo mpiganaji mieleka kabla ya pambano. Fundi alivaa dengrizi ya codorai ya kahawia na fulana ya njano ya kubana iliyotunisha zaidi misuli yake ya mikono na kifua.

"Sema boss", alinyoosha mkono kumsalimu Amani. Wepesi wa Amani ulidhihiri katika ganja kubwa la Fundi.

"Shida tu", alijibu.

"Basi poa".

"Habari ya tangu majuzi?" Amani aliuliza, alichomoa sigara kutoka ndani ya paketi na kuipachika mdomoni.

"Fresh tu. Karibu ofisini", Fundi alisema na kumshika mkono Amani.

Waliingia ndani ya chumba kidogo ambacho kilionekana kama stoo ya spea zaidi kuliko ofisi ya mkuu wa gereji. Baada ya mazungumzo mafupi, Amani akasema shida yake.

"John?", Fundi aliita kwa nguvu. Kijana mmoja aliyekuwa akimsaidia pulizia rangi pale nje alifika akapewa funguo za stoo na kuamriwa, "lete plagi na piston ring".

"Aina gani na ngapi"? aliuliza yule kijana kwa unyenyekevu.

"Champion fanya sita", Amani alijibu.

"Na ring piston kumi".

Punde si punde yule kijana alirejea na vifaa vile na kumkabidhi Amani.

"Vipi una akiba ya mipira?" Amani alimuuliza Fundi.

"Ya nje?"

"Yote yote".

"Sasa sina, lakini sema idadi yake nitakupa siku uje uchukue".

"Miwili ya nje, minne ya ndani".

"Vizuri, pita kieshokutwa utaikuta".

Amani alilipia vifaa alivyonunua. Fundi alizitia fedha zile mfukoni. Wakaongozana hadi mlangoni, wakaagana.

Hakuna spea ambayo Fundi alishindwa kuipata. Kwa oda maalum aliuza hata injini mpya za gari. Jinsi alivyopata vitu hivyo ilikuwa siri yake. Kutoka pale Amani alikuwa karidhika kidogo. Alipitia katika kimkahawa kula chakula kisha akelekea nyumbani kujipumzisha.

Kwa muda Amani alikiangalia chumba chake ambamo daima alijiona mgeni. Maana alidamka alfajiri, akarejea mchana na kutoka, kama muda huo alipatikana. Vinginevyo alitoka usiku hadi usiku. Baada ya kuridhika na usalama, na wala sio mandhari ya mle ndani (chambilecho mlikuwa na nini?) alichomoa jozi ya viatu vyake akajitupa kitandani. Alinyosha mkono kufungua feni iliyokuwa si mbali na hapo na kuacha impepee. Usingizi mzito uliyawinda macho yake ambayo pole pole yalizidiwa na uzito na kusalimu amri yake.

Naam, usingizi dawa, kwa wandwele na wakamavu pia. Kwani saa moja baadaye aliamka akajiona kama kapitia kwenye josho la uzima. Ona basi, sasa ndipo alivua nguo zake, akavaa taulo, mswaki kinywani na kutoka moja kwa moja kwenda kuoga.

Punde si punde alirejea ndani, akachana nywele na kuvaa suruali ile ile ila alibadilisha shati, akavaa jekundu. Upesi alichoropoka chumbani kama afukuzwaye. Moja kwa moja hadi ndani ya gari lake akapiga moto upesi na kuondoka. Mwendo wa kasi wa robo saa ulimpitisha kwenye mitaa michafu ya jiji hilo lenye barabara ya lami iliyochimbika na nyumba zisizo na ghorofa, akaingia kwenye mitaa afadhali ambayo ilikuwa na lami nzuri kiasi nyumba za ghorofa hadhi tano zilionekana. Sehemu hii walikaa zaidi wafanyabiashara ya Kiasia. Halafu alitokea kwenye barabara safi zaidi, pana na nadhifu. Na idadi ya ghorofa za nyumba za sehemu hii iliongezeka hadi kufikia ishirini na tano na kuendelea. Kwa usahihi kabisa aliendesha gari lake hadi katika bustani moja ambapo kuliegeshwa gari ndogo nyingi. Kikundi cha vijana sita kilimvamia, mikononi wameshika makopo ya plastiki na masponji.

"Mimi bradha, mimi", kila mmoja aliita vyake na kwake.

"Ngojeni nitoke basi, Amani alitokeza uso nje akijaribu kufungua mlango uliozongwa na vijana hao wanaohaha. Kwa bahati mara kuliwasili gari mbili za Wazungu. Do! wote walikimbilia kule wakiminyana kufa na kupona kama kaa wanaogombea haja kubwa ya mvuvi. "Bora", Amani alisema, huku akimweleza kijana mmoja aliyestahamili kubakia pale. "Endelea bwana".

Kwa mikono myepesi yule kijana alitoa mabusati ndani ya gari ile akayakung'uta, akafyagia kwa kifyagio kidogo halafu ndipo akaanza kulisafisha gari kwa maji na sabuni, kuanzia ndani hadi nje. Baada ya muda wa robo saa alikuwa amemaliza awamu ya kwanza. Sasa akachukua kitambaa kikavu na kuanza kulifuta gari kwa unadhifu. "Nipige polish?" aliuliza yule kijana.

"Naam, Amani alijibu ambaye punde aliingalia, "Ngoja kwanza jumla itakuwa kiasi gani?" "Shilingi alfu moja".

Baada ya maelewano Amani aliridhia kazi hiyo ikamilishwe. Kutoka hapo gari lilikuwa lameremeta. Mizunguko mingine michache alifika kwenye viwanja vya Hoteli maarufu ya Hilton na kuegesha gari lake.

Sifa za hoteli ya Hilton ilivuka mipaka ya nchi hii. Kwa mkopo wa nchi moja ya magharibi hoteli hiyo yenye ghorofa thelathini na ukumbi wa mikutano mzuri, ilijengwa mara baada ya uhuru wa nchi hii ili kupanua biashara ya utalii. Kwa nje hoteli ilionekana kama msonge ulioinukia kutoka kwenye viwanja vipana taratibu ukakwea juu huku ukipunguza mapana yake kwa mduara hadi kileleni kabisa.

Tangu ijengwe hoteli hiyo ilipitia migogoro mingi mno ambayo Amani aliisikia na kusoma magazetini kama habari zisizo muhusu. Yeye na utalii wapi na wapi? Alilojua ni kumtumikia kafiri kupata muradi. Na chombo chake ndicho lile Zepher 6 ambalo sasa aliketi ndani yake akisikiliza kanda ya nyimbo za Lionel Richie aliyoitia kwenye chombo cha kupigia muziki, wakati akisubiri abiria.

Saa nne ya usiku iliwadia. Pale kituoni katika viwanja vya hoteli ya Hilton ambapo Amani alikuwa ameegesha gari lake aliweza kukiona vizuri kivuli cha jengo la Hazina. Ingawa lilikuwa la kale bado lisimama na haiba ya aina yake. Lilikuwa na kuta nene zilizohimili ghorofa tano na vyumba visivyopungua hamsini na ushei. Huku na huko lilizungukwa na uwanja uliopandwa maua na miti mirefu ya kuvutia. Kiza cha miti hiyo kilionekana kwenda juu sambamba na ghorofa zile tano. Kuvizunguka viwanja vile kulikuwa na ua madhubuti wa vyuma vilivyochongoka juu. Kila baada ya hatua ishirini kulikuwa na taa za duara kulizunguka jengo lote. Usiku taa hizo ziliwaka kuwaasa wapitaji wasivuke zaidi ya mipaka yake. Kwenye malango makuu ya au huo walikaa askari wasiopungua kumi, ala kamili.

Ndani ya jengo hakukuwa hata taa moja. Ila vioo vya madirisha yake vilijibu miali ya taa za ukutani na kutoka katika hoteli ya Hilton. Mara moja moja askari wa zamu walionekana wakitembea taratibu huku na huku wakipita katika vivuli na kutokea tena kunako taa, bunduki mikononi. Kila mtu ana kazi yake, Amani aliwaza, akiangalia mandhari yale. Ukiachilia miendo hiyo ya askari, kote kulikuwa kimya hata ikiwa vigumu kuamini patachangamka tena.

Binafsi Amani, kama ilivyokuwa kwa ile Hoteli Hilton, hakuwa na muamana na Hazina Kuu. Alielewa vituko vya humo kwa wale waliotafuta dola za Kimarekani, paundi za Kiingereza na fedha nyingine za kigeni pamoja na vibali au leseni za kufanya biashara nje. Jina tu "fedha za kigeni" lilitosha kumtapisha. Lakini kilio cha mmoja, kipato cha mwingine.

Wakati mawazo haya na yale yakipita akilini mwake alishtushwa na miguu ya watu. Ghafla aligeuka kushoto akaona Mzungu mmoja mwanaume na msichana wa Kiafrika wanaelekea gari lake. Mwendo wao ulikuwa wa kusepetuka kidogo huku yule mzungu kauzungushia mkono wake kwenye makalio ya yule msichana. Aliketi vizuri pale kitini kuwasubiri. Alipapasa kisu chake cha kufyatua alichokichomeka ndani ya mfuko wa suruali yake kwa kutumia mnyororo uliofungiwa kwenye kanda nene pale kiunoni. Chini ya kiti alipoketi palikuwa na sime kali mno. Mwanaume silaha, alijipa moyo.

"Mission to Seamen please" alisema yule Mzungu, kipande cha haja. Amani alihisi ni Baharia, akajibu, "Oka", wote waliketi nyuma. Amani nywele zilimsimama. Daima alihisi hivyo wakati wa usiku alipowapakia nyuma watu asiowafahamu. Ila ile sura ya yule msichana haikuwa ngeni kwake. Alipiga moto gari lake, akawasha taa za mbele na kuondoka kwa mwendo wa kawaida. Mitaani taa ndefu ziliangaza kote hata kuzifanya taa za gari la Amani zisionekane. Katika mazingira haya, aliwasha taa za karibu yaani dim.

Baada ya mwendo wa dakika kumi Amani alihisi kitu kinatokea kule nyuma. Bila ya kugeuka alitumia kioo cha kuonea nyuma cha gari lake akaona wale wamelaliana nusu uchi. Moyo ulimwenda kasi lakini hakusimama. Aliendelea taratibu kana kwamba hakuona kitu. Fikra mbalimbali za kukirihi nafsi zilimtafiri hasa ile mihemo yao. Vipi, awashushe? Hapana. Lakini akasema kwa sauti kali, "Hey Man, you will pay extra dollars".

"Sure", yule Mzungu alijibu akihema katikati ya mishughuliko ile. Mission to Seaman ilikuwa ni klabu mahsusi ya mabaharia kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Walikutana hapo wakashiriki ulevi na zinaa ambavyo aghalabu vilizuka katika malau na vipigo. Kwa makusudi klabu hiyo ilijengwa si mbali sana na Bandari ya Mindule. Kutoka pale ilipo taa za milingoti ya meli zilionekana wazi wazi.

Amani, ambaye katu hakuwa mgeni na klabu hiyo, aliingiza gari yake katika uwanja wake akageuka kuwakazi macho abiria wake ambao tamaa chafu ya kumaliza haja zao iliwavua utu wote. Lakini muhitaji mjinga, lau kana mwerevu. Amani alitoka nje ya gari kuwapa wasaa mzuri abiria wale wakidhi haja yao. Upepo wa kuzizima ulimpata na kumfariji. Aliangalia kwenye klabu akaona kuwa idadi ya mabaharia ilikuwa ndogo sana. Kwa kweli klabu yote ilipwaya.

Ilipita tena robo saa ndipo abiria wake wakachomoza, akianzia yule mzungu huku akifuatia yule msichana, macho kayakazia chini. Mzungu alitimiza ahadi yake. Akatoa noti moja ya dola mia za kimarekani kumkabidhi Amani. Aliiangalia vizuri kisha akaichomeka kwenye mfuko wa ndani wa suruali yake, moyo ukimwenda mbio. Kesho asubuhi angebadilisha dola hizo kwa fedha za nyumbani. Dola moja shilingi mia nane, yuko karibu? Aliwaangalia tena wale abiria wake wakielekea kunako ile klabu bado wamekumbatiana, wakisimama na kubusiana kila baada ya hatua chache. Alichushwa na unyama ule, akaingia ndani ya gari na kuondoka.

Kupakia mabaharia ilikuwa ngekewa kwa dereva wa teksi kwa vile waliwatoza na pengine wenyewe tu walitoa kiasi kikubwa cha fedha. Isitoshe waliuwa washitiri wa miamala mbalimbali ya fedha za kigeni. Wengi wao walinunua bangi, msokoto mmoja hadi shilingi mia tano. Siku moja Amani alimuuzia baharia mmoja kilo moja ya bangi kwa dola mia tano za Kimerakani.

Na haikuishia hapo tu.

Pia ulikuwa na ukuwadi. Walioridhi kuwatafutia mabaharia wanawake au mashoga walilipwa bakshishi sio haba.

Amani aliyafanya yote hayo ila ukuwadi. Kwa hilo nadhari yake ilimkatalia katakata. Na kila wakati alipowapakia wasichana wa Kiafrika kuja kule kutafuta muradi wao aliingiwa na hofu za aina mbili. Kwanza, utu na usalama wa wasichana wale, pili, hali ile ingeendelea hadi lini?

Kutoka hapo Amani aliendesha gari na kuliingiza kunako kituo kimoja cha petroli ambako kilikuwa kitupu isipokuwa kwa gari mbili zilizoegeshwa na mlinzi mmoja aliyekuwepo.

"Hapana mafuta", yule mlinzi alimwendea na kumweleza Amani ambaye alijibu, "Nataka kujaza maji ndani ya rejeta".

Yule mlinzi aliondoka na Amani akafungua mlango wa nyuma wa gari. Mdomo ulimjaa mate kwa kile alichokiona. Ilibidi asafishe uchafu ule uliokuwepo kwa maji na sabuni hata aliporidhika. Akapangusa kiti chake kile vizuri na kuondoka.

Itaendelea toleo la Ijumaa
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook