Tahariri
Kura sio kipimo cha dhulma ya kuua

SUALA la mauaji ya Mwembechai ni agenda inayojitegemea. Ni suala zito la aina yake ambalo haliwezi kuunganishwa na uchaguzi mkuu. Uchaguzi mkuu pamoja na umuhimu wake, lakini ni suala la kawaida na moja tu ya taratibu za kistaarabu za kubadilisha uongozi katika jamii.

Lakini suala la mauaji ya Mwembechai ni uhai wa watu. Ni suala la uvunjaji wa haki ya msingi katika katiba ya nchi. Haki ya kuishi.

Haiwezekani ndugu yako akauliwa bila ya haki ukasema utalipiza kisasi kwa kutokumpigia kura aliyeua.

Itakuwa ni kosa kubwa iwapo watatokea watu waone hasira zao zote ziishie kwenye kura.

Kutoa au kutokutoa kura ni suala mbali na kudai haki na hatua zichukuliwe juu ya mauaji ya Waislamu ni jambo jingine.

Kwa maana kwamba hata kama CCM itaendelea kushinda chaguzi kumi zijazo, bado wadhulumiwa watasimama kupambana na dhulma na kudai haki ya damu iliyomwagika.

"Kisasi cha damu" hakitoisha kwa kuwa kura yako imeshindwa kumng'oa madarakani unayemtuhumu kwa udhalimu. Kutompa kura ni kielelezo tu cha kutokuridhika na tabia ya mtu au chama.

La muhimu hapa, lazima Waislamu waangalie mapana na marefu ya suala la kupigania haki zao.

Lengo ni kusimamisha haki na lengo hili huenda zaidi ya uchaguzi.

Kwamba kwa matokeo yoyote ya uchaguzi hayatakuwa jambo la kuwavunja nguvu watu waache kupambana na dhulma.

Kama watu watafikia hatua ya kutumia kura zao kama silaha hiyo ni hatua tu katika kukomaa kwao katika harakati za kudai haki.

Kwa hiyo silaha hiyo ifanikiwe au laa, watasonga mbele mpaka wafikie lengo. Wakitumia kila silaha watakayoona itawasongeza mbele.

Tunasema suala la kuuliwa Waislamu halitamalizwa na uchaguzi. Hata CCM na serikali yake iendelee kuwepo madarakani kwa mihula kumi ijayo haitakuwa sababu ya kuisahau dhulma hii.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook