Na Anaphy A. Said
AHLUL-KITAABI ni neno la Kiarabu lenye maana ya "watu wa kitabu". Katika istilahi ya Kiislamu, Ahulul-Kitabu ni watu waliopewa kitabu ambao ni Mayahudi (waliopewa Torati) na Manaswara (waliopewa Injili). Mayahudi na Manaswara pia hujulikana kwa jina la Banu Israel, yaani kizazi cha Israel. Israel ni jina la Nabii Yakub (a.s.). Huyu Nabii Yakub (Israel) ndiye aliyezaa watoto 12 ambao ndio chimbuko la makabila 12 ya Waisraeli.
TUKIANZA na Mayahudi, asili hasa ya neno "Yahudi" linatokana na neno "Tahawwud" lenye maana ya kutubia na kurejea kwenye haki. Na hii ndio kauli ya Ibn Abbas, Said bin Jubeir, Mujahid, Abul-Aaliyah, Dhwihaak, Ibrahim At-Taymiy, Assuday, Qutaadah na wengineo. Mayahudi walilipata jina hili kwa ajili ya kutubia kwao kwa Allah (s.w.) kutokana na kitendo chao walichokifanya cha kumwabudu ndama wakati Nabii Musa (a.s.) alipowaondokea kwenda kupokea kitabu cha Taurati katika mlima Sinai. Allah (s.w.) anatusimulia ndani ya Qur'an kuwa baada ya kitendo hicho cha dhambi, Musa na baadhi ya wafuasi wake waliomba dua hii kwa niaba ya wenzao:
"... Basi utusamehe na uturehemu. Nawe ndiye mbora wa kughufiria. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika akhera. Hakika sisi tumerejea kwako..." 7:155-156.
Kifungu hiki: Hakika sisi tumerejea kwako, kinasomeka hivi kwa Kiarabu: Innnaa hudnaa ilayka. Neno Hudnaa linatokana na neno Haada ambalo ni kitendo chenye maana ya alitubu/ametubu na kurejea kwenye haki. Na jina la mtendaji ni Yahuudiy lenye maana ya aliyetubu na kurejea kwenye haki. Pia tafsiri hii unaweza kuipata katika kamusi mbalimbali za Kiarabu. Kwa maana hiyo, neno Mayahudi maana yake ni waliotubu na kurejea kwenye haki. Na hawa Mayahudi ndio wafuasi wa Nabii Mussa (a.s.).
Baadaye alipopelekwa Nabii Issa (a.s.) kuwa Mtume kwa Bani Israeli, iliwapasa hawa Bani Israil kumfuata Nabii Issa (a.s.). Basi baadhi yao walimfuata na wengineo hawakumfuata (Qur'an 61:14 na 3:52). Wale waliomfuata ndio Manaswara.
Sasa tukija kwenye Manaswara, asili hasa ya neno "Naswara" linatokana na mji unaoitwa Naaswirah, yaani Nazareti, mji uliopo Falastin (Palestina) mashariki ya Kati. Wafasiri mbalimbali wa kutegemeka wa Qur'an kama vile Ibn Abbas na wafasiri wengineo kama vile Qatadah na Ibn Jurayiji, wameeleza kwamba neno "Naswarah" (ambalo hutumika kwa wafuasi wa Nabii Issa) limenasibishwa na mji wa Naaswirah (Nazareti). (Angalia tafsiri ya Qur'an ya Imam Ibn Khathyr kwenye maelezo ya aya ya 62 sura ya 2 na Fathul-Qadiyr ya Imam Muhammad Ali Shaukaniy).
Pia makamusi mbalimbali ya Kiarabu yametoa tafsiri hiyo hiyo. Katika makamusi ya Waislamu ni kamusi inayoitwa "Mukhtaarusw-Swihaah" ya Imam Muhammad bin Abi Bakri Ar-Razi (angalia ukurasa wa 583 wa kamusi hiyo), na katika makamusi ya wasiokuwa Waislamu ni "Al-Munjid" (angalia ukurasa wa 812 wa kamusi hiyo katika upande wa "Matini ya Al-Munjid katika lugha").
Na tafsiri ya Naaswirah kwamba ni Nazareti imetolewa pia katika kamusi hiyo hiyo ya Al-Munjid ukurasa wa 704 katika upande wa mufradat ambazo hazipo katika "matini ya Al-Munjid katika lugha".
Kwa hali hiyo basi, maana halisi ya Manaswara si Wakristo bali ni Wanazareti (au Wanazarayo), yaani wafuasi wa mtu wa Nazareti. Kwa maana Nabii Isa (s.a.) alizaliwa Bethelehemu na kukulia katika mji wa Nazareti (angalia Mathayo 2:1-23) pia kitabu Qiswaswul-Quraan ukurasa wa 221). Ndio sababu pia Nabii Issa alijulikana kama mtu wa Nazareti (Mathayo 21:11 na kadhalika).
Nabii Isa (a.s.) kama walivyo Manabii wengine, alikuwa Muislamu na aliwafundisha watu wake Uislamu. Wafuasi wake waliufuata vyema Uislamu (Qur'an 3:52 na 5:111). Allah (s.w.) anasema:
"Basi Isa alipoona ukafiri wao (umeshitadi) akasema: Nani watakuwa wasaidizi wangu kwendea (katika kuitangaza dini ya) Allah? Wanafunzi (wake) wakasema: Tumemwamini Allah na ushuhudie kwamba hakika sisi ni Waislamu". 3:52.
Baada ya kuondoka kwake Nabii Isa, watu wake walikuja kufarikiana na kuwa na imani tofauti juu yake (Qur'an 19:34-37 na 43:63-65). Waligawanyika katika makundi manne yafuatayo:
Kundi la kwanza liliamini kuwa Nabii Isa ni Mtume tu wa Allah, hili ndilo kundi sahihi na Nabii Isa lililoufuata Uislamu vyema (Qur'an 3:113-115). Ifahamike wazi kuwa Uislamu si dini aliyokuja nayo Mtume Muhammad (s.a.w.) kama wanavyofikiri watu wengi, lakini ni dini aliyokuja nayo Adamu (a.s.) aliyekuwa mtu, Nabii na Mtume wa awali kabisa.
Kundi la pili liliamini kuwa Nabii Issa ni Mungu (Qur'an 5:17 na 72). Kundi la tatu liliamini kuwa Nabii Isa ni mwana wa Mungu (Qur'an 9:30). Na kundi la nne liliamini Mungu mmoja katika nafsi tatu (Qur'an 5:73). (Pia angalia tafsiri ya Qur'an iitwayo Swaf-watut-Tafaasiyr ya Sheikh Muhammad Ali Swaabuuniy kwenye maelezo ya aya ya 17 ya sura ya 5, aya ya 65 sura ya 43).
Ukitoa kundi la kwanza, bila shaka makundi matatu yaliyobaki yalipoteza mwelekeo na kuingia katika ukafiri. Allah (s.w.) anasema:
"Na kwa wale waliosema: Hakika sisi ni Manaswara, tulichukulia ahadi kwao, lakini wakaacha sehemu ya yale yaliyokumbushwa (waliyoamrishwa katika Injili)..." 5:14.
Kutokana na tafsiri tuliyoiona juu ya makundi na Manaswara ni wazi kuwa hapo mwanzo majina haya hayakutumiwa kama majina ya wafuasi walio katika dini iliyo tofauti na Uislamu. Lakini baadaye katika kipindi ambacho hakukuwepo na Mitume, Mayahudi na Manasara waliacha mafundisho ya Mitume na kuingiza ushirikina na mambo mengine ya kikafiri katika dini ya Uislamu. Matokeo yake ni kuwa Uislamu ulifutika kwao, na Uyahudi na Unaswara zikaja kuchukua sura ya dini, na Ukristo ukachanganywa na Unaswara. Dini hizi zilianzishwa na watu wenyewe wakawazingizia Mitume wa Allah kuwa ndio waliozileta, hali ya kuwa Mitume wote walikuja na dini ya Uislamu ambayo ndiyo dini ya haki mbele ya Allah (s.w.). Rejea Qu'an 3:19 na 85.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |