Na Kivuruga Nguzo
MTAALA ni mjumuiko wa masomo, malengo ya kujifunza na kufundisha masomo na njia za ufundishaji, vifaa vya kufundishia na kujifunza mada za masomo na taratibu za upimaji na tathmini ya malengo ulioratibiwa.
Lengo kuu la kufundisha na kujifunza ni kumpatia mwanafunzi maarifa, stadi na mwelekeo sahihi wa maisha utakaomwezesha kuishi maisha bora yenye furaha na amani.
Wakati Mola wako alipowaambia malaika: "Mimi nitaweka mtawala (Khalifa) katika ardhi. Wakasema, utaweka humo watakaofanya uharibifu humo na kumwaga damu hali sisi tunakutukuza kwa sifa zako na kukutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika mimi nayajua msiyoyajua.
Na Mwenyezi Mungu akamfundisha Adamu majina ya vitu vyote kisha akaviweka mbele ya malaika na kusema. Niambieni majina ya hivi vitu ikiwa mnasema kweli.
"Wakasema utukufu ni wako! Hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha, bila shaka wewe ndiye mjuzi na ndiye mwenye hekima".
Akasema: Ewe Adamu! Waambie majina yake". Alipowaambia majina yake. Akasema: Sikuwaambieni kuwa mimi ninajua siri za mbinguni na ardhini tena najua munayadhihirisha na kuyaficha (2:30-33).
Kwa munasaba wa aya hizi ni wazi kuwa Mwenyezi Mungu ndiye mwalimu wa walimu na mtaalamu mkuu wa elimu. Hivyo hutufunza dhana ya mtaala. Alimfundisha Adamu masomo kwa lengo la kumpatia maarifa, stadi na mwelekeo utakomwezesha kuutawala ulimwengu ili kuishi kwa furaha na amani kinyume na hoja iliyotolewa na akina Darwin. Kwa kuwa kuna tendo la kufundisha na kujifunza ina maana kuwa alitumia mbinu na njia zilizomwezesha Adam kujifunza.
Mafunzo aliyopewa Adamu ni tofauti na yale waliyopewa malaika, hii ni kusema kwamba aina na viwango vya masomo yao vinatofautiana sana. Ndiyo maana malaika walipoambiwa kutaja majina ya vitu alivyofundishwa Adamu ikawa kwao ni usiku wa giza nene.
Baada ya kufundishwa Adamu alipimwa maarifa, stadi na mwelekeo aliopata. Akapewa mtihani wa kutaja majina, akafanya hivyo. Hivyo, akastahiki kupewa heshima ya kupongezwa na malaika kwa kumsujudia.
Na tulipowaambia malaika "msujudieni Adam" wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, akakataa na akajivuna na alikuwa katika makafiri (2:34).
Kijumla tunaweza kusema kwamba mtaala ni mkusanyiko wa mipango na uzoefu ulioratibiwa rasmi kwa ajili ya utoaji wa mafunzo ya aina fulani kwa watu wa kiwango fulani ili kufikia malengo maalum.
Kama msingi wa mtaala, mwanafunzi anatakiwa awezeshwe kuwa mtendaji mdadisi mwenye mwelekeo sahihi wa maisha. Awe mwenye kufikiri, kutafakari, kuchambua, kugundua, kutafsiri, kutoa maana aweze kuhusisha mambo na kujenga hoja zenye usahihi. Aweze kuwa mbunifu mwenye kutatua matatizo yake na ya jamii.
Mtaala umjengee mwanafunzi mtazamo sahihi wa kimaisha wenye kuinufaisha jamii. Mtazamo utakaomfanya aitumikie jamii bila ya kusukumwa. Awe mwajibikaji mwenye vigezo madhubuti vya kujikosoa, kukosolewa na kukubali kujirekebisha.
Hapana budi mtaala umwezeshe mwanafunzi kumtambua aliye Muumba, ajue haki za Muumba, haki zake binafsi, haki za wanadamu wenzie anazowajibika kuwatendea, na mwisho atambue haki za uwezo (powers) aliokuwa nao na matumizi ya rasilimali alizomilikishwa na Muumba wake.
Ajue na kukubali kuwa mamlaka ya mwisho ni ya Mwenyezi Mungu na ni yeye anayestahiki kutoa mwongozo wa maisha unaotakiwa kufuatwa na viumbe vyote. Mwongozo huo ndio kigezo cha sheria zote zitakazowekwa na dola au mamlaka yoyote.
Hujui ya kwamba ni wake Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi? Na hamna mlinzi wala msaidizi asiyekuwa Mwenyezi Mungu. (2:107)
Aidha, azijue na kuzikubali haki zake binafsi, ni haki za mwili kutoupa vyakula na vinywaji vyenye kuudhuru kama vile pombe, madawa ya kulevya. Aheshimu dhamana ya uhai wake na kwamba hana haki ya kujiua kwa namna na hali yoyote iwayo.
Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, vilivyo halali na vizuri. Na wala msifuate nyayo za shetani. Bila shaka yeye kwenu ni adui aliye dhahiri. (2:168).
Kadhalika ana haki ya kuzima kiu ya matashi ya ngono. Asijinyime wala kuvuka mipaka ya kiutu. Asiwe mtawa, asizini, bali aowe na kuyabeba majukumu ya kimalezi yanayoambatana na mahusiano ya ngono na matokeo yake.
Umwezeshe kufahamu haki ya mwili kuhifadhiwa, ikiwa maiti inasitiriwa kwa mavazi ya heshima, basi mwili wa binadamu aliye hai anastahiki heshima ya kusitiriwa zaidi. Iwepo tofauti kati ya mnyama, maiti ya yeye aliye hai.
Enyi wanadamu! Hakika tumekutemshieni nguo za kuhifadhi miili yenu, nguo za mapambo na nguo za heshima ni bora zaidi. Na wala usikaribie zinaa. Kwa hakika huo ni uchafu na ni njia mbaya kabisa. (7:26) (17:32)
Katika kumkuza kijamii, mtaala uimjenge mwanafunzi mwenendo utakaozithamini haki za wanajamii anaoishi nao. Akiwa katika harakati za kujitendea haki zake za kimwili asivunje na kuwakosesha wengine haki zao.
Ajuwe kwamba kila mtu amebeba haki za wengine anazowajibika kuwapa. Mathalan mtu asipooa au kukidhi matashi ya ngono kinyume cha maumbile, anawanyima jinsia nyingine haki ya mapenzi ya mume na kuisukumiza jamii kwenye uchafu wa zinaa na kuibua magonjwa yatakayogharimiwa matibabu kwa kodi za wanajamii, ambazo zingalitumika kwenye mambo mengine ya maendeleo. Zaidi ya hivyo kitaibuka kizazi kitakachokosa malezi bora ya wazazi hatimaye kuongeza idadi ya vibaka na machangudoa.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |