Wazee hao wameweka tawi lao katika makutano ya barabara ya Tandamti na Msimbazi jirani na Msikiti wa Idrisa.
Mmoja wa wazee hao, Mzee Ali Mustafa Sigareti amesema ilikuwa tawi lao lifunguliwe rasmi na Prof. Lipumba Juni 17.
Hata hivyo, akasema zoezi hilo lilikwama kutokana na Prof. Lipumba kuchelewa kuwasili toka Mwanza.
Mzee Ali Mustafa (67) amesema, wanaandaa mnanda, mdunduko na ngoma nyingine ili kulifungua tawi lao rasmi mara Prof. Lipumba akirejea kutoka Zanzibar.
Amesema, wanataraji tawi hilo la wazee wa Kariakoo litakuwa lishakuwa na wazee 300 hadi siku hiyo ya ufunguzi.
Mzee Ali ameeleza kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na unyanyasaji, upendeleo wa wazi na kupuuzwa haki za binadamu chini ya uongozi wa CCM.
Mzee Athumani Mwintanga (70) yeye amesema, wamekaa wakaona serikali ya CCM inawadanganya.
Amesema, serikali inadai kuwaondolea kero wananchi pamoja na kuwapa huduma za afya bure kwa wazee, lakini hakuna kitu. "Sasa tumechoshwa na serikali hii ya CCM", amesema Mzee Mwintanga.
Wazee hao wamesema, hali katika elimu, uchumi na huduma za jamii ilianza kwenda kombo miaka michache baada ya uhuru. Wamesema badala ya kwenda mbele nchi ilikuwa ikirejea nyuma kimaendeleo.
Wamesema siasa ya ujamaa iliwapora wananchi mali zao na kufanya zidhibitiwe na viongozi wachache.
"Tuligundua kumbe siasa ya ujamaa ni kuchukua mali za wanyonge", amesema Mzee Athumani.
"Tuliambiwa kulima kwa ushirika maduka ya ushirika... ikafika kilimo kinaongozwa kisiasa, biashara inafanywa kisiasa, elimu nayo siasa tupu... uchumi ukaanguka na kila kitu", amesema Mzee Sigareti.
Wakielezea awamu hii ya sasa wamedai, awamu hii imewarudisha watu miaka ya "47". "Ni viongozi wa CCM tu ndio wanaoneemeka. Imefikia hali ambayo watu wameshakata tamaa ya maisha. Mzunguko wa pesa umedumaa, hali imekuwa ngumu", amesema Mzee Ali Mustafa.
Wameeleza kuwa ili kurudisha hadhi ya nchi hii
wameamua kuingia CUF ili kuleta mabadiliko katika uongozi wa nchi.
MAPOKEZI ya aina yake yamefanyika jumamosi na jumapili wiki hii jijini Dar ea Salaam na Zanzibar kufuatia kuwasili katika miji hiyo kwa wagombea wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Sharrif Hamad.
Mapokezi hayo yamekuja siku chache baada ya yale ya wagombea wa chama tawala, Rais Benjami Mkapa ambaye aliandaliwa sherehe maalum mjini Dodoma na bwana Aman Karume aliyepokelewa kwa shangwe Zanzibar.
Uteuzi wa wagombea wa chama cha CUF ulifanyika mjini Mwanza ambapo mkutano maalum wa chama hicho ulimteua Profesa Ibrahim Lipumba kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano na bwana Seif Shariff Hamad Urais wa Zanzibar.
Umati mkubwa wa wafuasi wa chama hicho ambao umeelezwa kuwa haujawahi kutokea kwa chama chochote nchini ulifurika katika viwanja vya ndege na barabara za Dar es Salaam na Zanzibar.
Jijini Dar es Salaam maelfu ya wananchi walimiminika uwanja wa ndege kuwalaki wagombea hao ambao waliwasili mnamo saa saba za mchana wa jumamosi.
Nderemo na vifijo vilizizima eneo la uwanja wa ndege Jijini mara baada ya kuwasili kwa Profesa Ibrahim Lipumba na mgombea wake mwenza bwana Nassoro Khamis.
Wafuasi wa chama hicho waliojipanga kando kando ya barabara kuanzia mlango wa kutokea wageni air port hadi barabara ya Nyerere(Pugu Road) ambako msururu mwingine watu na magari uliunga hadi maeneo ya kipawa.
Msafara wa wagombea hao ulitembea mwendo wa taratibu ukisindikizwa na maelfu ya watu waliosongamana na kuijaza barabara yote ya Nyerere hali iliyosababisha askari wa usalama barabarani kuyasimamisha magari mengine.
Msafara huo ulipita barabara za Nyerere, Mandela, uhuru hadi uwanja wa kidongo chekundu Gerezani Jijini ambako wagombea hao walitambulishwa kwa wananchi na baadaye Mwenyekiti wa chama Prof. Lipumba kuhutubia wananchi.
Katika hotuba yake Profesa Lipumba alielezea tishio la njaa linaloikabili mikoa ya kanda ya ziwa.
Alilaumu Bajeti iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita kuwa haikugusia chochote kuhusu hali hiyo ya njaa inayoyakabili maeneo hayo na mikoa ya kati.
Aidha Profesa Lipumba alizungumzia kukosekana kwa sera makini juu ya viwanda hali iliyosababisha viwanda vingi kufungwa.
Alitolea mfano wa Kiwanda cha nguo cha Musoma ambacho alisema kutoka na hali ngumu inayokikabili wafanyakazi wake wamefikia kulipwa khanga na shuka kama mshahara wao mwezi.
Amesema uchumi wa nchi umedidimia na hali za wananchi kimaisha zimekuwa ngumu mno.
"Wananchi kanda ya ziwa wamechoshwa na hali hiyo, hawako tayari kuendelea kuwapa uongozi watu waliowafikisha hapo", Prof. Lipumba aliwaambia wakazi wa Jiji.
Mwandishi mjini Zanzibar anaripoti kwamba uma mkubwa wa wazanzibari ulijitokeza jumapili kuwalaki wagombea hao waliowasili mjini humo kwa ndege wakitokea Dar es Salaam.
Mvua kubwa iliyonyesha kisiwani humo haikuathiri mapokezi hayo yaliyoanzia uwanja wa ndege ulioko kilometa kadhaa kutoka mjini, kupitia barabara kadhaa hadi viwanja vya Malindi ambako Mgombea wa Urais Zanzibar kupitia chama hicho aliwahutubia wananchi waliofurika mahali hapo.
Katika hotuba yake, Bwana Hamad aliahidi kurudisha umoja na mshikamano wa Wazanzibari iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo.
Alisema suala hilo la umoja litakuwa katika programu ya Rais, kwa hiyo litakuwa na usimamizi wa moja kwa moja kutoka ofisi ya Rais.
Alisema mgawanyiko ulioko Zanzibar hivi sasa utawafikisha mahali pabaya Wazanzibari.
"Maradhi ya kugawanyika ni Kansa na Kansa lazima ikatwe mapema kabisa, kwa hiyo serikali itakayoongozwa na mimi itahakikisha inarejesha umoja wa wazanzibari wote", alisema Maalim huku wananchi wakimshangilia.
Aidha Maalim Seif alisema serikali atakayounda iwapo atachaguliwa kuwa Rais itazingatia haki za binaadamu na kupiga vita unyanyasaji wa raia.
Kadhalika alizungumzia hali ngumu ya maisha inayowakabili wazanzibari wengi ambapo alisema serikali atakayounda atahakikisha inaboresha maisha ya wananchi hao.
Alisema maisha ya wazanzibari wengi ni mbaya sana, ajira hakuna vijana wengi hawana ajira hivyo umasikini umezikumba familia nyingi.
Aidha, Maalim Seif aliwaambia wananchi hao kuwa
serikali atakayounda itahakikisha kurejeshwa hadhi ya Zanzibar katika ulimwengu
wa biashara.
Waliokamatwa na kuwekwa ndani ni Ustadh Nuhu Juma (Imamu wa muda), Ustadh Mwinyikambi Ahmad (Mwenyekiti) na Ustadh Amrani.
Hadi jana saa 2:00 usiku viongozi hao walikuwa bado wameshikiliwa na polisi Magomeni. Taarifa nyingine zilieleza kuwa wangehamishiwa Oysterbay.
Polisi Magomeni ilikuwa imewaandikia barua viongozi hao wafike kituoni kuonana na OCD. Viongozi hao walipofika waliwekwa ndani.
Tukio hili limefuatia uchaguzi uliofanyika hivi karibuni ambapo Sheikh Omar Bashir alichaguliwa Imamu.
Uchaguzi huo ulifanyika Juni 16 Msikitini hapo ukisimamiwa na Shura ya Maimamu na Baraza Kuu la Taasisi na Jumuiya za Kiislamu.
Habari kutoka kwa waumini wa Msikiti huo zimedai chokochoko zinaletwa na wazee wa CCM wanaotaka Msikiti huo uendeshwe kama tawi la CCM.
Wamedai wazee hao wa CCM wanakitumia kiwanda cha Urafiki na polisi kuingilia uongozi wa Msikiti.
Wamesema, kutokana na shinikizo hilo la CCM, kiwanda cha Urafiki kimetoa barua inayoeleza kuwa wanaotakiwa kuswali Msikitini hapo ni wafanyakazi tu wa Urafiki wanaoishi katika nyumba za kiwanda.
Waumini hao wamewaomba Waislamu jijini Dar es Salaam kuswali swala ya Adhuhur leo Msikitini kwao ili kujua wenzao waliowekwa ndani.
"Kila atakayejaaliwa leo aswali Urafiki tutafakari la kufanya juu ya dhulma hii", amesema muumini mmoja.
Hadi tukienda mitamboni, juhudi za gazeti hili
kupata maelezo ya polisi Magomeni juu ya tukio hili, hazikuweza kufanikiwa.
--
![]()
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |