61 wasilimu Kigoma

WAKRISTO wapatao 61 wamerejea katika Uislamu huko Kigoma.

Arobaini na moja kati yao walikuwa wa dhehebu la Katoliki, kumi na moja Pentekoste na Assemblies of God wawili.

Anglikana walikuwa wawili, Wasabato wawili, Walutheri wawili na IAC mmoja.

Watu hao wamerejea katika Uislamu kufuatia mfululizo wa mihadhara ya kundi la Khidmat Dawah tawi la Mwanza iliyoanza Mei 19 hadi Juni 19.

Taarifa ya Khidmat imeeleza kuwa awali mihadhara hiyo ilikwama baada ya viongozi wa Makanisa kuingilia kati na Mkuu wa Wilaya Kibondo kutoa amri mihadhara isimame.

Mkuu huyo wa Wilaya alidai kuwa wahadhiri waliukashifu Ukristo kwa kusema Yesu si Mungu.

Sheikh wa wilaya Sheikh Eliasa alimweleza Mkuu huyo wa Wilaya kuwa inaonekana kuwa kuna dini tawala na dini tawaliwa.

Alisema, katiba imeweka wazi jambo la kutangaza dini liko nje ya mamlaka ya serikali, akahoji inakuwaje Waislamu wakisema Yesu sio Mungu tayari serikali hapo inagundua kuwa amani itavurugika, lakini wakati huo huo Wakristo wakitangaza Yesu ni Mungu na ni Mwana wa Mungu amani haivurugiki.

"Je, utakubaliana na mimi kuwa serikali imeamua kutubatiza kwa lazima? Pili Maaskofu wakileta malalamiko yanayohusu Waislamu basi serikali haifanyi uchunguzi kwanza ila ni kutekeleza tu matakwa ya viongozi wa Makanisa. Je, hii ni haki?" Alihoji.

Mkuu wa Wilaya alihoji kama kuna malalamiko ambayo Waislamu wameleta kuhusu Wakristo, serikali ikakaa kimya? Sheikh akatoa mkanda wa kaseti ambao ndani ya kanda hiyo kuna mahubiri ambayo yalitolewa na muhubiri wa Kikristo anayeitwa Francis Mgaluta ndani ya mahubiri yake amesema, yeye alikuwa Sheikh kule Mbozi Mbeya katika Msikiti wa Ijumaa lakini baada ya kumpokea Yesu ameokoka na sababu iliyomfanya aokoke ni kuwa Muhammad sio Mtume wa Mungu ila ni Mtume wa shetani tena aliwahi kumuoa mtoto wa dada yake.

Katika kanda hiyo Bw. Francis anadai Waislamu wanapoona maiti hukamua uchafu na kuuchanganya na uji siku ya arobaini.

Taarifa ya Khidmat imesema baada ya kanda hiyo kusikilizwa, Mkuu wa Wilaya alibaki kaduwaa kimya. Takriban dakika 3 hivi. Akauliza mliwaarifu polisi? Sheikh akasema alipokuwa akihubiri ni Kakonko karibu na kituo cha polisi hawakufanya lolote sisi tulipoleta suala hili halikuchukuliwa hatua yoyote.

Alipoulizwa O.C.D. akasema yeye wakati huo alikuwa hajaletwa hapo alikuwepo O.C.D. mwingine. Alipoulizwa Katibu Muhtasi wa wilaya alijibu kwa mkato tu kuwa hilo halina nafasi lilishapita, ndipo Mkuu wa wilaya alipowaambia Waislamu "kaendeleeni na mahubiri yenu na kibali chenu kinaendelea ila msivunje sheria".


Wajawazito walalamikia huduma duni za Afya

WAJAWAZITO wanaohudumiwa katika hospitali ya Magomeni mjini Dar es Salaam wamewalalamikia wauguzi wa hospitali hiyo kutokana na kutowahudumia vizuri.

Wakizungumza juzi na mwandishi wa habari hizi wamesema, huduma zinazotolewa haziridhishi na wakati mwingine hawapewi dawa.

"Ingawa serikali inatangaza wajawazito kuhudumiwa bure lakini sisi kwanza hatupewi hata dawa yoyote tukiuliza majibu tupewayo ni ya kunyanyaswa", amelalamika mama mmoja.

Aliongeza kuwa kuna wakati wanauliza swali pengine kwa ugeni wa hali zao hujibiwa kuwa wakaulize waume zao au kuambiwa wasiwadekee.

Alisema mjamzito huyo kuwa Juni 15, iliyokuwa siku yake ya kwenda Kliniki, walikalishwa katika foleni hadi saa sita mchana na kuja kuelezwa kuwa siku hiyo ilikuwa sikukuu ya Maulid na hawakuweza kuhudumiwa na kutakiwa kurudi Ijumaa bila kujali hali za wajawazito wengine ambao wanakakaribia kujifungua.

"Hivi kweli kwenye hospitali kuna sikukuu, na kama ipo yaani anayetaka kutibiwa au kujifungua itambidi sikukuu ipite ndio ahudumiwe?" Aliuliza dada huyo.

Nesi mmoja aliyeongea na mwandishi wa habari alikataa kusema lolote kwa madai kuwa msemaji ni Mganga Mkuu wa hospitali ya Manispaa ya Kinondoni ingawa alikiri kuwepo kwa malalamiko ya wajawazito juu ya wauguzi wenzake upande wa kliniki ya watoto na wajawazito.


Hatuachi

WAISLAMU nchini wamesema kuwa kamwe hawataacha kuendelea na mahubiri yao ya dini yanayodaiwa kuchanganywa na siasa kwa vile kufanya hivyo ni utekelezaji wa Sunna ya Mtume Muhammad (s.a.w.).

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Sheikh Ally Bassaleh wakati akiwahutubia waumini wa Kiislamu kwenye Msikiti wa Idrissa uliopo Kariakoo jijini mara baada ya swala ya Ijumaa.

Sheikh Basaleh alisema, Waislamu nchini kamwe hawataacha kuchanganya dini na siasa kwa kuhubiria Misikitini kwa vile hiyo ni Sunna na pia ni vigumu kwao kuiacha sunna kwa hofu ya watawala wa dunia.

"Kamwe hatutaweza kuacha maamrisho na mafundisho ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na ya Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa kuwaogopa watawala wa kidunia ilihali sisi ni wa kupita na pia tutakutana na Mola wetu siku ya siku", alisema na kuitikiwa na waumini hao kwa Takbir... Allah Akbar.

Aliongeza kuwa desturi ya kutumia Misikiti kuhubiria siasa na dini kwa Waislamu ilianzishwa na Mtume Muhammad kwa kujadiliana mambo yao yanayowakwaza na kuafikiana huko huko na hii kamwe haiwezi kuachwa na Waislamu eti kwa kufanya hivyo watahatarisha amani.

"Uislamu hujengwa kwa nguzo za imani sita ambapo mojawapo ni kumtii Mungu na Mitume wake sasa kuachana na mojawapo ni kwenda kinyume cha dini ", aliongeza Sheikh huyo.

"Tumechoka kuingiliwa kwenye imani zetu, tukifanya lolote sisi tunaonekana wakorofi lakini Kinisa aah... basi mtatukamata sana safari hii na tuko tayari kwa hilo kwani kufa mashahidi ni bora kuliko kuogopa kutekeleza imani ya dini yetu", amesema na kuitikiwa tena na Takbir.

Alisema, itikadi zao za vyama vya siasa haviwatofautishi Waislamu kiimani na kwamba jambo la dini yao ni la Waislamu wote na kuwataka Waislamu kutoogopa kujitokeza kutetea dini yao kwa hofu ya kunyimwa masilahi na viongozi wa vyama vyao.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook