Tutumie 'jicho la fikra' kupima matukio

TUKIELEKEA uchaguzi mkuu wa pili wa vyama vingi hapa Tanzania, hao Oktoba, 2000, tayari yapo matukio yanayojitokeza yakiwa na taswira tofauti . Kimsingi matukio haya yanahitaji mtu atumie zaidi jicho la fikra, kuliko macho ya kawaida ili kupata tafsiri sahihi. Miongoni mwayo ni uchaguzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kutoka katika vyama, mikutano ya kuhuisha vyama husika katika ngazi mbalimbali, kuanzishwa miradi mbalimbali katika maeneo tofauti ya kupiga kura, zawadi na misaada ya wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali kwa wapiga kura na kikao cha Maaskofu wa CCT na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Jaji Lewis Makame.

JICHO la fikra lina sifa ya kuona mbali zaidi na linaambatana na maswali mengi ambayo pindi yakijibiwa kwa usahihi, tafsiri halisi ya matukio husika hupatikana. Kinyume chake macho haya ya kawaida, yana udhaifu mkubwa kiasi cha kutoa taswira/picha ya kitu tofauti na kinavyoonekana. Kwa hiyo wawe makini katika kuujua ukweli huo na wawe tayari kuufanyia kazi.

Mfano, kwa kutumia macho haya ya kawaida, utamuona mtu anacheka, na anazoishara zote za kucheka, lakini katika hali halisi mtu huyo amekasirika sana na ndani ya moyo wake anatokota kwa chuki, uadui na hasira kali dhidi ya wengine, na kinyume cha hali hiyo pia ni sawa sawa.

Kulithibitisha hili, waone wanasiasa wa Tanzania wanapokaribishwa katika hafla za Waislamu. Machoni hucheka sana, lakini hotuba na kile kinachoitwa nasaha zao kwa Waislamu hubeba picha nyingine kabisa tofauti na wanavyoonekana machoni. Huwakejeli, huwacheka, huwalaumu na hata kuwadhalilisha kisaikolojia, lengo likiwa ni kuwafanya waamini kuwa, wao ni raia wa daraja la pili katika jamii hii. Kutokana na ukweli huo ndio maana, tumeanza kwa anwani kuwa, jicho la fikra litumike ili tupate picha halisi ya mambo yanayojitokeza, lengo likiwa ni kuinusuru jamii na dhulma katika kipindi kijacho.

Tuchukulie mathalan, katika kikao cha Maaskofu na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imeelezwa kuwa wachunga kondoo hao walimpa wakati mgumu Mwenyekiti huyo kwa kumlaumu au kumshutumu juu ya utendaji wa Tume anayoiongoza. Katika kujibu lawama za Maaskofu yasemekana kuwa, Jaji huyo wa siku nyingi alitaka kulia mbele ya Maaskofu hao wa CCT, pengine kutokana na mguso wa yale aliyopashwa au vyenginevyo.

Picha inayochorwa hapa ni kwamba, madai yaliyotolewa yalikuwa makali mno na kwa bahati mbaya si ya kweli. Ndio maana, katika kuwajibu Maaskofu hao, Jaji alijipa ushupavu wa kutoa mifano ya utendaji wa Tume yake dhidi ya CCM ambayo inaonesha kuwa, hakuna upendeleo kwa chama hicho.

Kimsingi, hiyo ni tafsiri ya kwanza inayopatikana kutokana na macho ya kawaida na kila mmoja anaweza akaridhika nayo.

Hata hivyo, tukio hilo likitazamwa kwa jicho la fikra, lenye sifa ya kuona mbali na vizuri zaidi, picha nyingine tofauti na ya mwanzo inapatikana na hii ni halisi zaidi kwa wale wenye kujua hadhi yao stahiki katika jami hii. Kuiona picha hiyo ni vyema mtiririko wa maswali ufuatao ukatumika.

Je, Maaskofu wa CCT nao ni wanasiasa? Jibu likiwa ndiyo, swali jingine litakuwa, ni vyama gani vya siasa wanavyoviwakilisha Maaskofu hao?

Jibu la swali la kwanza likiwa ni hapana, swali lingine litakuwa, kwanini askari hawakuwakamata Maaskofu hao waliotaka kumliza Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi? Ikumbukwe kuwa, Maaskofu ni viongozi wa kidini, ambao kwa Tanzaina hawaruhusiwi kuzungumzia siasa, kwani kufanya hivyo, watakuwa wamechanganya dini na siasa na stahiki yake ni kuswekwa lupango na kufunguliwa kesi za uchochezi, kama inavyotokea kwa Masheikh wa Waislamu.

Labda itasemwa kuwa, wakulaumia ni huyo Jaji Lewis Makame aliye Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, kwa sababu ndiye aliyewafuata katika midhibahu yao. Kwa hiyo kuwakamata Maaskofu si sahihi. Kama tutakuja na mtazamo huu, tuwe tayari kujibu swali lifuatalo, kule kutaka kulia kwa Mwenyekiti wa Tume mbele ya ya Maaskofu kunaashiria nini? Jibu la swali hili lisiukimbie ukweli wa jicho la fikra kuwa, mtu anaweza akalia kumbe anacheka na akawa anacheka kumbe analia, kama tulivyoonesha mwanzo. Pia mtoa jibu asisahau ukweli kuwa, tayari tume ya uchaguzi ya Taifa imeshatoa orodha ndefu ya wasimamizi wakuu na wasaidizi wao katika uchaguzi mkuu ujao, ambao kwa asilimia kubwa ni wafuasi wa Maaskofu (Wakristo). Kwa kuzingatia hali hizo, tunaamini kuwa jicho la fikra litafanya kazi sawa sawa na utoa majibu sahihi.

Swali lingine, je, Jaji atakuwa na ushupavu wa kukutana na Shura ya Maimamu? Je, ikitokea Jaji akalia kabisa, baada ya kupashwa na Shura ya Maimamu ni kitu gani kitakachofuata, kwa Maimamu watakuwa wamemliza kabisa Jaji, kinyume na Maaskofu ambao walitaka kumliza?

Kwa kuzingatia mtitiriko usiokoma wa aina hiyo ya maswali ni wazi kuwa ipo haja kwa Watanzania wenye kulijua lengo na hadhi yao stahiki , kutumia zaidi macho ya fikra katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu ili kuyapa tafsiri matukio yanayojiri na kuitahadharisha jamii isije ikajuta baadaye. Tusijefanywa 'kuku' wa kienyeji ambaye hutafuta chakula mwenyewe lakini wakija wageni yeye hufanywa kitoweo.

Pia izingatiwe kuwa, hotuba za viongozi zinazotolewa sasa, vitabu na hata magazeti kwa ujumla wake, ni sehemu ya mambo inayohitaji jicho la fikra la kupata tafsiri halisi. Tusije tukasahau kadhia ya Mwembechai na jinsi vyombo hivyo vilivyoshughulikia kadhia hiyo. Watu wameuliwa na damu yao ikafukiwa kwa mchanga, kinamama wamedhalilishwa na wengine wametiwa vilema vya maisha.

Katika yote haya na yanayofanana na haya, yaliyojiri katika jamii hii, vyombo husika pamoja na mamlaka zilizopo vilitoa misimamo yao. Kwa hiyo, ili jicho la fikra lifanye kazi yake vizuri, ni busara matukio hayo pamoja na misimamo iliyotolewa mwanzo, vikahusianishwa na maneno matamu yatolewayo sasa katika kuomba kura.

Dhulma ni kosa bila ya kujali ni nani anaifanya dhulma hiyo. Kuiondoa dhulma, ni kazi ya wanaodhulumiwa kuunganisha nguvu zao na ufahamu wao. Jambo hilo linawezekana, ikiwa kila mmoja atatumia jicho la fikra kupata tafsiri sahihi ya mambo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook