Umaskini katika jamii

UMASKINI ni tatizo linalozikabili jamii nyingi duniani hasa nchi za ulimwengu wa tatu. Tatizo hili huwafanya watu kuishi maisha ya tabu na dhiki.

Umaskini huweza kusababishwa na sababu mbalimbali ikiwemo sababu kubwa ya kushindwa kuendesha uchumi wa nchi inavyotakiwa kwa kuzingatia rasilimali za nchi.

Tatizo hili la umaskini husababisha matatizo mbalimbali kama wizi, maradhi, ujinga, uasherati, mauaji na kadhalika.

Kutokana na hali ngumu ya maisha watu wengi huamua kujiingiza katika matendo maovu ili angalau kuweza kujinusuru kwenye hali hiyo.

Umaskini umesababisha huduma za jamii, afya, elimu, umeme na maji kuwa duni. Wananchi wamekuwa wakitumia maji yasiyo salama matokeo yake kumekuwa na ongezeko la magonjwa ya matumbo, kipindupindu na kuharisha.

Pia baadhi ya wanawake wameamua kujiingiza kwenye shughuli za kuuza miili yao ili kuweza kujipatia chochote na hivyo kupelekea kuongezeka magonjwa ya zinaa hasa ukimwi.

Vijana wamekuwa mstari wa mbele katika kufanya uhalifu wa ukabaji au uvunjaji ili wapate chochote cha kujikimu katika maisha yao.

Matokeo ya vitendo vyote hivi viovu huwapelekea wahusika kuwekwa chini ya mikono ya dola na kupata mateso na adhabu mbalimbali kwa makosa waliyoyafanya.

Lakini je, ni kweli kuwa wao ndio wanaopaswa kulaumiwa kwanza? Je wanafanya haya kwa hiyari yao? Kama wangekuwa na hali nzuri ya maisha wangefanya haya?

Kimsingi hawafanyi haya kwa hiyari yao bali ni kutokana na shinikizo la hali mbaya ya maisha ambayo inasababishwa na uchumi mbovu. Je, ni nani anayesababisha hali mbaya hii ya uchumi?

Tanzania ni moja katika nchi zenye rasilimali nyingi. Ina ardhi nzuri na kubwa, ina madini ya kutosha, mabonde yenye rutuba, milima, maziwa, bahari, mito na kadhalika.

Uchunguzi unaonesha kuwa kama bonde la mto Rufiji lingetumika ipasavyo lingekuwa na uwezo wa kulisha Tanzania nzima bila matatizo. Kama vyanzo vya maji vingetumika ipasavyo kusingekuwa na tatizo la maji safi na salama.

Lakini zimekuwa zikitolewa sababu zisizo na msingi za kuhalalisha kutotumika kwa rasilimali hizi na matokeo yake nchi inazidi kuwa masikini kwa kuagiza bidhaa zinazotumia rasilimali kutoka nje.

Kama migodi mbalimbali iliyopo nchini ingetumika na kudhibitiwa ipasavyo katika kuendeleza uchumi ni wazi kuwa hali ya maisha kwa wananchi ingeboreshwa.

Kwa ujumla nchi ina vivutio vingi vya utalii, kama wanyama na milima, lakini havitoi mchango mkubwa katika kuinua maisha ya Watanzania na kuondokana na hali mbaya ya umaskini.

Inaelekea kuna sera na mikakati mibovu ya usimamiaji na utekelezaji wa kuzitumia rasilimali hizi ipasavyo ili ziweze kuleta hali nzuri kwa wananchi.

Tuna mifano mingi ya mashirika, viwanda na makampuni mbalimbali ambayo yamekufa kutokana na kuwa na uongozi mbaya usiotaka kusimamia maslahi ya umma bali kujinufaisha wenyewe binafsi.

Na kimsingi wananchi wa kawaida ndio wamekuwa waathirika wakuu wa tatizo hili. Tumeshuhudia dada zetu, mama zetu, kaka zetu na hata baba zetu wakiingia matatizoni kutokana na janga hili.

Idadi ya vifo hivi sasa imeongezeka sana kutokana na wananchi kushindwa kumudu gharama za matibabu pindi waumwapo kwa sababu ya umaskini.

Kutokana na umaskini, wananchi wengi wamekuwa ombaomba tatizo ambalo limekuwa ni kero kwa muda mrefu pamoja na mikakati mbalimbali ya kuwarudisha makwao lakini hilo si suluhisho.

Rushwa pia imekuwa kubwa ambalo husababishwa na umaskini. Pamoja na madai na ahadi ya kulimaliza tatizo hili inayotolewa kila leo bado tatizo hili limeendelea kuwa kero kubwa.

Wimbi la matukio ya unyang'anyi, ukabaji na mauaji limekuwa likiongezeka siku hadi siku kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili watu.

Kuna mifano mbalimbali ya mauaji ya watu kwa minajili ya kujipatia ngozi kwa ajili ya kuuza, mzizi wa yote haya ni umaskini.

Wapo baadhi ya vijana ambao wameamua kukabiliana na tatizo hili la umaskini kwa kujiajiri kwenye shughuli mbalimbali kama vile kufanya biashara ndogo ndogo.

Cha ajabu ni kuwa miongoni mwa wafanyabiashara hao ndogo ndogo wamekuwa wakipata upinzani na vikwazo mbalimbali kutoka serikalini kama vile kuvunjiwa biashara zao na kukamatwa.

Matukio haya yanaonesha kuwa kuna walakini katika uongozi. Haiwezekani watu wafanye jitihada ya kujikwamua kiuchumi halafu wapate vikwazo tena kutoka serikalini!

Hivi sasa tuna nafasi nzuri ya kuweza kuchuja na kuchagua viongozi ambao tunahisi utatusaidia katika hali hii, kila mtu ana akili, hivyo ni suala la kuzitumia ili kuboresha hali zetu.

Mara nyingi tumekuwa tukipewa sababu kuwa fedha zinatumika kulipa madeni ya nje ambayo hata hayaeleweki yalikopwa kwa minajili ipi na yametumikaje.

Tufikie mahali nasi tujiulize, hili tatizo la umaskini litakwisha lini? Ni nani wahusika wa kuliondoa tatizo hili? Kuna faida gani basi ya kuwa na wachumi wetu hali ya kuwa na uchumi mbovu?

Ni kweli kuwa kuna suala la teknolojia ambalo linapelekea nchi hizo kutuzidi kimaendeleo lakini bado si kwa kiwango hiki. Ni wazi kuna uzembe na ubadhirifu unaofanyika kwenye hizo raslimali.

Kwa kweli kuna haja kubwa ya wananchi kutafuta ufumbuzi dhidi ya tatizo hili badala ya kusubiri serikali.

Hali za maisha ya watu na maendeleo ya jamii husika hutegemea uongozi uliopo madarakani, kama uongozi utakuwa mbovu basi hali za watu na maendeleo yatakuwa duni pia.

Na kama uongozi utakuwa mzuri na unaojali maslahi ya wengi, ukaanzisha na kusimamia miradi mbalimbali ipasavyo kwa manufaa ya wengi basi ni wazi kuwa watu watakuwa na hali nzuri na pia kutakuwa na maendeleo katika jamii husika.

Wananchi wafahamu kuwa kuna tatizo kubwa la umaskini ambalo husababisha matatizo mengine mbalimbali. Na umaskini huu huletwa na hali mbaya ya uchumi, hivyo adui yetu ni yule anayeudunisha uchumi.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook