Kesi ya uhaini Zanzibar: Haki au dhulma?

WAKATI viongozi 14 wa Chama Cha Wananchi (CUF) walipokamatwa mwezi Novemba mwaka 1997, mwanzo walishitakiwa kwa makosa ya uchochezi. Maombi ya dhamana yalipowasilishwa kwa wanachama hao kumi na nne, kosa likapandishwa na kuwa uhaini. Kosa ambalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kati ya Desemba 1997 na Mei 1998, wanachama wanne zaidi ya CUF akiwemo Juma Duni Haji, mshindi wa Kiti cha Mkunazini kwa tiketi ya CUF, alikamatwa na kuongezwa katika mashitaka ya uhaini.

Mwezi Mei, 1999 gazeti la The Guadian liliripoti kwamba Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Bwana Ali Mohamed Umar alitoa hati ya kukamatwa kwa wanachama kumi zaidi wa CUF akiwemo Seif Shariff Hamad na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho Bw. Khamis Mloo. Mwanasheria Mkuu alinukuliwa akisema: You can't arrest the lientnants and leave the generals. This is why ten other people need to be arrested and included in the trial.

Tafsiri: Huwezi kuwakamata Maluteni na kuwaacha Majenerali. Hiyo ndiyo sababu ya kuwakamata wengine na kuwaunganisha kwenye mashitaka.

Kufuatia shinikizo la kutoka ndani na nje ya nchi la kupinga kitendo hicho, polisi Zanzibar ilikataa kwamba ilikuwa na mpango wa kumkamata Hamad na viongozi wengine wa chama cha Wananchi CUF.

Misingi hasa ya kisheria na kikatiba ambayo watawala wa Zanzibar wameitumia katika kuwakamata na kuwafungulia mashitaka ya uhaini wanachama 18 wa CUF bado ni utata na kiza kitupu.

Hakuna maelezo ya kutosha mpaka leo yanayoonesha kwamba washitakiwa aidha kwa maneno au vitendo vyao wamejihusisha na njama za kuipindua serikali ya Dk. Salmin Amour. Tangu mwaka 1997 mamlaka ya Zanzibar imefanikiwa kuchelewesha kuanza kwa kesi hii ya uhaini kwa mbinu za kuichelewesha na kuiahirisha mara kwa mara.

Mwaka 1998 mzima kes hii imekuwa ikitajwa tu bila ya kusikilizwa. Upande wa mashitaka ulidai kwamba unahitaji muda zaidi wa uchunguzi, na wakati mmoja walidai kwamba watuhumiwa wengine wako nje ya nchi na bila ya wao kukamatwa kesi haiwezi kwanza majina ya watuhumiwa hao hayajawahi kutajwa mahali popote, wakati wowote mpaka leo.

Kufuatia madai rasmi kwamba mahakama za Zanzibar zimebanwa na mrundikano wa kesi na hakuna Majaji wazoefu, Majaji tisa waliletwa mwaka 1998 kutoka Nigeria na kesi akapewa Jaji mmojawapo.

Kitendo hiki kilisababisha upinzani kutoka kwa wanasheria wa visiwani na Tanzania Bara ambao walijenga hoja kwamba Majaji wa Tanzania wana uwezo wa kutosha kusikiliza kesi ya uhaini. Serikali ya Zanzibar ilidai kwamba haina fedha za kuendeshea kesi hiyo, hali iliyopelekea Chama Cha CUF kutaka kuisaidia kiasi cha fedha kinachohitajika ili mradi kesi isikilizwe.

Hatimaye SMZ ilitangaza mwezi Novemba mwaka 1999 kwamba imeshapata fedha kutoka katika mfuko wa dharura wa Hazina. Wakati wa mwezi Machi mwaka huo huo, upande wa mashitaka ulipotoa ushahidi wake na washitakiwa 18 walipelekwa mbele ya mahakama kuu ya Zanzibar, upande wa utetezi ulinyimwa nakala za faili la kesi kwa hoja za usalama wa Taifa.

Kama kawaida, baada ya kesi kuahirishwa mara nyingi washitakiwa 18 walitokea mahakamani tena Januari 19, 2000. Hata hivyo, kesi iliahirishwa tena kwa maombi ya upande wa mashitaka kwamba ulihitaji muda zaidi kurekebisha mashitaka na kuongeza watu 10 katika orodha ya washitakiwa.

Wanachama na wapenzi wa CUF walipinga kitendo hicho hali iliyopelekea polisi wawapige na kuwakamata. Watu sabini waliripotiwa kujeruhiwa vibaya na polisi waliojiandaa vyema na wengine arobaini kutiwa mbaroni. Aidha, msako wa polisi wa nyumba hadi nyumba ulifuata baadaye mpaka uvamizi wa nyumba za za viongozi na maafisa wa CUF. Mkutano wa hadhara wa CUF uliopangwa kufanyika siku ya pili ulipigwa marufuku.

Kesi iliahirishwa kutoka Januari 19 mpaka Januari 27 mwaka 2000. Ikaahirishwa tena mpaka Februari 28. Januari 26, Mwanasheria Mkuu mpya wa Zanzibar aliteuliwa. Yule wa mwanzo alifanya kosa gani?

Kwa mara ya kwanza ufa ukajitokezandani ya umoja wa CCM kuhusiana na suala hili. Wabunge 45 wa ngazi ya Muungano walisaini waraka maalumu wakiitaka serikali ya Zanzibar kuachana na mashitaka ya uhaini.

Halafu baadaye, baada ya kesi kutajwa siku ya Februari 28, ikaahirishwa tena mpaka Aprili 3, kufuatia ombi la upande wa mashitaka kurekebisha hati ya mashitaka iliyokuwa na makosa.

Tafsiri sahihi ya mwendo wa SMZ kuhusiana na kesi hii ya uhaini ni kudhoofisha chama cha upinzani CUF, katika uchaguzi mkuu ujao. Ushahidi wote uliopo unaonesha kwamba hii kesi ni ya kisiasa na haina mashiko ya kisheria wala katiba.

Tukumbuke Tanzania ikiwemo Zanzibar, imetia saini mkataba wa kimataifa unaoheshimu haki za kiraia na kisiasa (International Covenant on Civil and Polical Rights -ICCPR). Kwa hiyo inawajibika chini ya sheria ya kimataifa kuheshimu haki za washitakiwa kwa kuendesha mashauri yao katika mahakama huru na kwa uwazi.

Serikali ya Muungano ina wajibu wa kuhakikisha kwamba sheria za kimataifa za haki za binadamu zinatekelezwa Tanzania bila kujali uhuru na hadhi ya Zanzibar.

Kwa bahati mbaya, Rais wa Jamhuri ya Muungano hataki kabisa kutekeleza wajibu huu Zanzibar. Anatimiza zaidi wajibu wa Mwenyekiti wa CCM kuliko Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

-
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook