Zanzibar inahitaji chama bora

Na Abu Aysha


 


SIKU chache zilizopita, chama tawala (CCM) kilimtangaza mgombea wake visiwani Zanzibar Bw. Amani Abeid Karume. Jambo la ajabu mgombea huyu amefanywa kama mkombozi na jawabu la mgogoro wa kisiasa unaofukuta visiwani humo. Lakini ni ukweli Karume ndiye atakayeleta hali ya amani na utulivu Tanzania visiwani?

KWANZA kabisa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla wanapaswa waelewe sababu za mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar. Tatizo la Zanzibar siyo mtu gani anafaa kuwa Rais bali ni sera za chama gani zinakidhi haja na matarajio ya Zanzibar ya leo. Sera zenye uwezo wa kuwaunganisha Wazanzibari kama taifa na kuwakomboa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Zanzibar hakuna tatizo la ubaguzi wa rangi, kikabila wala dini kama inavyoelezwa na makada wa chama tawala. Pamoja na kwamba Zanzibar ni jamii mchanganyiko (multi-racial society) wananchi wote wa visiwa hivyo wanaunganishwa na mila, itikadi na desturi moja.

Wazanzibari wanaunganishwa zaidi na udugu wa damu na ndoa kuliko wanavyotenganishwa na sera za vyama. Kiini macho cha kuilaumu historia ya Zanzibar kuwa ndiyo msingi wa mgogoro wa sasa ni mbinu tu ya watawala kuwapumbaza wananchi wasijuwe ukweli ulivyo.

Sera za chama tawala hazifai tena Zanzibar kwa kipindi hiki. Wazanzibari wamechoshwa na sera za maamgizo zenye lengo la kuwafuta katika ramani ya dunia kama taifa. Ndiyo maana katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 dunia nzima ilishuhudia Wazanzibari wanataka nini na wanapinga kitu gani.

Labda jambo la kujiuliza ni kwanini wananchi wa visiwa hivyo wameweka nguvu zao za kisiasa nyuma ya CUF, kwa kipindi kifupi hata kufikia mahali pa kuwatia wazimu watawala wa visiwa hivyo na Tanzania Bara?

Nguvu za kisiasa walinazo CUF Tanzania visiwani ni taswira ya matakwa ya Wazanzibari. Chama cha CUF kina itikadi na sera zinazohitajika kuleta maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii visiwani Zanzibar.

Sera za uchumi kutumikia siasa zimeshakwama duniani kote na mataifa yote hivi sasa wanazungumza lugha ya kuinua uchumi ili kuboresha maisha ya wananchi wake. Wazanzibari wameliona hilo na ndiyo sababu mojawapo kubwa ya kuiunga mkono CUF.

CCM imeshindwa kabisa kuboresha maisha ya Wazanzibari walio wengi hususan katika visiwa vya Pemba. Imebaki tu ikitafuta 'kikaragosi' cha kutupia lawama kwa kushindwa kwao kuinua uchumi na maisha ya Wazanzibari.

Hiyo ndiyo kawaida ya watawala wote wanaongamiza uchumi wa nchi kwa ajili ya kulinda maslahi yao ya kisiasa. Tangu mwaka 1995 serikali ya Mapinduzi Zanzibar haijfanya lolote la maana katika uchumi wa visiwa hivyo zaidi ya kupambana na wapinzani ili wabaki madarakani milele. Wazanzibari hawahitaji hilo.

Dunia ilishuhudia wanachama wa upinzani wakitupwa gerezani bila kosa na serikali ya SMZ, waandishi wa habari wakitishwa wasiseme ukweli ulivyo, na raia wakipigwa virungu na polisi kwa lengo la kuwatia hofu wasidai na kutetea haki zao za msingi.

Na watendaji wote wa udhalimu huu wanaongozwa na sera za CCM. Rais wa Jamhuri ya Muungano hafanyi lolote kunusuru maisha na uhuru wa Wazanzibari wa kawaida. Yeye ndiyo kwanza 'anabariki' hali hiyo kwa kuwapongeza watendaji wake katika hotuba zake.

Watu hao leo wanatuletea mgombea wao waliyempamba kwa sifa nyingi na waandae mapokezi yake ya kumpongeza kama tukio la kitaifa, nasi tukubali kuhama kwenye ajenda zetu kwa kutekwa nyara tu!

Hapana! Sababu zinazowafanya Wazanzibari watake kuing'oa madarakani CCM ziko pale pale. Na kiongozi yeyote hata akiwa mzuri namna gani, hataweza kuleta mabadiliko Zanzibari kwa kutumia sera za CCM. Kwa sababu kinacholeta mabadiliko ni sera na siyo mtu. Uzuri wa mtu uko katika kutekeleza sera za chama chake kikamilifu. Sera za CCM zimeshindwa hata kuleta matumaini wachilia mbali kuleta mabadiliko kwa wananchi wa Zanzibar.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinafanya kila namna kuwasahaulisha Wazanzibari kwa kutumia vyombo vya habari yaliyotokea katika visiwa hivyo tangu mwaka 1995. Wanatangaza Zanzibar anatakiwa kiongozi mwenye siasa za wastani kama Amani Karume! Nani kasema tatizo la Zanzibar ni siasa za wastani? Siasa za wastani maana yake nini?

Tatizo la Zanzibar ni utawala utakaosimamia haki, demokrasia, na kuinua uchumi wa Wazanzibari.

Jambo moja lenye kutia matumaini ni kwamba Wazanzibari wamezaliwa ndani ya siasa. Kama taifa wanajua nini wanataka na namna ya kupata wanachotaka. Tofauti na sehemu nyingine nchini, Wazanzibari hawadanganyiki kwa propaganda.

Hatua ya chama tawala kumnadi Bw. Karume kwa gharama kubwa na mapokezi mazito yanayoashiria ushindi kabla hata ya uchaguzi ni kielelezo tosha kwamba chama hicho kinajaribu kuingia katika nyoyo za watu kwa kutumia propaganda zaidi kuliko siasa.

Wazanzibari wanatakiwa waandae maswali ya kuwauliza wagombea wa CCM katika kampeni za uchaguzi yanayohusu sera za chama hicho katika kuboresha maisha ya wananchi na kwanini hali zao mpaka leo ni duni.

Maswali mengine ni kama haya: Nini lengo na hatma ya sera ya Muungano wa serikali mbili kwa wakati huu?

Nini faida ya kuwa na muundo huu wa Muungano kwa Wazanzibari wakati haki za binadamu zinavunjwa na Rais wa serikali ya Muungano anashindwa kuwasaidia wanyonge kwa kisingizio cha Zanzibar ina mamlaka na katiba yake?

Kama Zanzibar ina mamlaka na katiba yake, kwanini Salmin Amour alipotaka kubadilisha katiba ya Zanzibar ili aendelee kugombea, CCM iliingilia na kuua agenda hiyo?

Mamlaka ya Zanzibar inaanzia wapi na inaishia wapi katika muundo wa Muungano wa serikali mbili?

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji


   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook