Kumbe kampeni bado!!

Ndugu Mhariri

TAFADHALI nipe nafasi ya kuhoji suala ambalo kwa siku mbili tatu hizi linanipa taabu sana kulifahamu.

Ni juzi tu nimebahatika kusikiliza Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kusikia moja ya taarifa zake za habari kikimnukuu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Lewis Makame akitoa taratibu za uchaguzi mkuu utakavyoendeshwa mwaka huu.

Nikashangaa kusikia kuwa amesema, kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza rasmi mwezi Agosti mwaka huu, jambo ambalo nimebaki mdomo wasi kwa kujiona ama mimi sijui maana ya kampeni au mtangazaji amemnukuu vibaya Mhe. Jaji Lewis Makame.

Kwanini nasema hivi, nimekuwa nikifuatilia mara kwa mara ziara za viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na mikutano ya hadhara wanayoifanya sehemu nyingi. Katika mikutano hiyo kuna maneno yanayoashiria kiongozi kunadi chama chake kichaguliwe .

Wananchi msidanganye na vyama vya upinzani, haviwezi kuleta maendeleo yenu, chama pekee ni CCM na maneno mengine mengi kama hayo.

Sasa je, hisi sizo kampeni au kampeni ni nini? Kingine ambacho kimenipa woga na wasiwasi ni kuwa Mhe. Makame hataruhusu viongozi wa serikali kutumia magari, ndege na hata nyumba za serikali katika kukampenia siasa.

Haya maneno ninayoyasema ya kuonesha viongozi kufanya kampeni yanasemwa wakati huo magari ya serikali ndiyo yanayotumika, ndege na vifaa vingi vya serikali vinatumika.

Mwisho ndugu Mhariri kupitia gazeti lako naomba nifahamishwe maana ya kampeni na ilinganishwe na msimamo wa Tume ya Uchaguzi juu ya kutotumia mali ya serikali katika kampeni.

Mwanaidi M. Athumani,
S.L.P. 9240,
Dar es Salaam.


Mwenye macho haambiwi tazama

Ndugu Mhariri

NIMESHUKURU, nimeona, kweli hizi zama za ngangari ngangari. Ikisemwa umati haitoshi, maelfu bado, labda haijawahi kutokea.

Ilikuwa ni 'mafuriko' ya watu mitaani kumlaki mgombea wa Urais Prof. Lipumba.

Lakini pamoja na mafuriko ya watu, hali ilikuwa shwari, salama salmini.

Mujue basi, fujo huletwa na vyombo vya dola vinapowachokoza watu au kuwanyima uhuru na haki zao. Hakuna sababu ya kuogopa jino kwa jino kama hugusi jino la mwenzako.

Ni ngangari ngangari kushikilia haki yako, ni ngangari ngangari kukataa kuonewa. Nyie kusanyeni watu kwa TOT, Remmy. Mambo iko huku... ngangari wanakuja wenyewe. hawahitaji kuhamasishwa wala kupewa nauli na posho .

Mramba Kimwaga,
Ilala,
Dar es Salaam.


Kampeni zashamiri Msikiti Raudhwa Lwamungo

Ndugu Mhariri

NAOMBA nafasi japo pembezoni mwa gazeti lako AN-NUUR niweze kutoa yangu machache yanikerayo.

Wakati chama tawala wakiimba wimbo wa siasa ndani ya nyumba za ibada ni kuchaganya dini na siasa namna wanavyotakidi wao. Ninasikitika wao wako mstari wa mbele.

Hapa Moshi wilaya ya Hai sehemu ninayoishi mimi kijiji cha Lwamungo Sinde Msikiti Raudhwa.

Sheikh wa Msikiti amekuwa akiwakaribisha wanataraji kugombea Ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuitisha mikutano ndani ya Msikiti huo.

Mwisho ninapenda kumuusia Sheikh wangu anapoamua kuongealea siasa ndani ya Msikiti siyo mbaya, lakini aelimishe waumini ukweli wa mambo. Wape ubaya au uzuri wa serikali iliyopo madarakani.

Hakuna haja ya kuficha maamuma wako. Hata kama wewe Sheikh ni mjumbe wa chama hicho katika kijiji, unahofu utakosa posho ya vikao, ni sawa na kuamini mwenye riziki yako ni Mwenyekiti wa kijiji na sio Allah.

Musa Issa,
Moshi.


Hawampati mtu

Ndugu Mhariri

MIMI nasema, hawa wanasiasa na waendelee kuimba tu... msichanganye dini na siasa, msilete udini, msivuruge amani...

Tunayajua sana yaliyovifuani mwao, wayasemayo na wanayoyatenda.

Kama ni kufanikiwa walifanikiwa miaka ya nyuma kutulaghai. Sasa wanajidanganya wenyewe. Hawampati mtu.

Wao nawaimbe ngonjera zao, sisi tunasonga mbele.

J. Muharram,
Mbagala,
Dar es Salaam.


Tuelimisheni zaidi

Ndugu Mhariri

NAOMBA sehemu ndogo tu nishukuru gazeti lako kwa kutufumbua macho na bongo zetu, na mimi nimshukuru mgombea Urais kupitia Chama cha CUF kwa kutuonesha kioo cha kujiona jinsi viongozi wa serikali na chama tawala wanavyotujali hasa afya zetu pale alipotufahamisha katika gazeti lako toleo Na. 258 Rabiul Awwal 1421 Ijumaa Juni 9-12, 2000 kuwa serikali kwa afya za wananchi imetenga kila mwananchi shilingi 160/- kwa mwaka.

Hilo hata asiyeenda shule hahitaji darasa la kuelewa. Wakati viongozi wanatibiwa nje ya nchi kwa mamilioni na wake zao mpaka kujiuzulu kwa kashfa hizo, sisi tumetengewa shilingi 160/- kwa mwaka.

Wakati ukienda hospitali unatakiwa uwe na daftari ambalo chini ni shilingi 100 likishaandikwa unalipa shilingi 500, bado hujaandikiwa dawa ambazo utaaambiwa uende ukanunue.

Hivyo naomba viongozi wa upinzani watuelimishe mengi waongeze kutufumbua macho na AN-NUUR mutufikishie.

K.J. Mziray,
S.L.P. 62,
Same,
Kilimanjaro.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook