Joka la Mdimu - 4
Na Dk. Abdallah J. Saffari
TINO
IDADI kubwa ya wakazi wa jiji la Mindule huishi Sega kiasi cha maili kumi nje. Huko wamejenga nyumba zao bila ya kupimiwa viwanja. Nyumba hizo zilizosongamana bila ya mpango zimejengwa vilimani, mabondeni na hata maporomokoni kwenye makonde ya mipunga. Hakuna barabara ya lami, mitaa rasmi, mitaro ya kupitishia maji machafu wala majalala maalum ya kutupia taka. Vichochoro na vijia mithili ya mistari ya ramani vimejinyonganyonga kukwepa vibanda na vijumba hivyo vilivyokabiliana pua na na mdomo.
Zamani za miaka kumi sifa kubwa ya Sega ilikuwa uchafu, ulevi, ufuska, na ujambazi. Ilisemwa: Hukatishi Sega usiku. Baadaye wafanyabiashara wakamaizi kuwa idadi kubwa ya wakazi wa Sega wangeweza kuwa washtiri wazuri. Naam, ghafla yakaanza mashindano ya kutafuta nyumba za kufanyia biashara. Kwa vile nyumba za hadhi kama hiyo zilikuwa chache, vibanda vilinunuliwa kwa mamilioni na kubomolewa. Maduka makubwa yakachipua mithili ya uyoga pamoja na majumba ya kulala. Hivi sasa katika barabara kubwa ipitayo katikati ya Sega kila nyumba ni duka, liwe la nguo, nyama, vyombo vya ujenzi na kadhalika. Vichochoro ndani kabisa kuliporomoshwa majumba ya fahari ya kulala, mashine za kupasulia mbao na kusagia nafaka. Viwanda vidogo vikachipuka na kustawi. Ukiachilia hayo, hali ya hapo ikaendelea kuwa duni zaidi ya miaka kumi iliyopita. Kama wenyewe walivyosema: Akheri ya zamani!
Jogoo aliwika na kupasua anga za alfajiri, wakapokezana mtaa hadi mtaa. Lakini nje, wingu kubwa lilitanda na kuondoa dalili zote za mapambazuko. Upepo ambao muda mfupi ulijikusuru kuyasukuma mawingu uliacha. Badala yake kukawa na mzizimo na unyevu wa mvua. Kimya kikahanikiza kote. Punde si punde kwa mbali kutokea kusini ya Sega, kukasikika sauti ya ngurumo. Sauti hiyo iliendelea na kukua mpaka ikazagaa kote. Mvua kubwa ya upepo ilianguka: Tone mzinga. Upepo huo ulivuma kwa kasi mno ukang'oa na kupeperusha baadhi ya mapaa ya nyumba. Ulipoacha kuvuma, kasi ya matone ya mvua, ambayo awali ilipunguzwa na upepo huo, ilishamiri maradufu. Mvua ikarindima kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu na nyasi zilizooza na kuwaadhiri wakazi waliojihifadhi chini yake.
Tino aliamshwa na mkikakika huo. Aligeuka na kulala chali. Tangu utoto wake alifurahia mvumo wa mvua ambao ulitumbuiza viwambo vya masikio na kuliwaza akili yake hivyo kumfanya alale vyema zaidi. Wale mbu ambao walikuwa wakiruka huko na huko kwa maelfu kutafuta karamu ya damu walijibana upenuni mwa kuta, mapaa na hata kwenye mivungu ya vitanda, meza na kila chombo kilichoweza kuwastiri. Harufu kali ya dawa ya mbu ya kuchoma ilitangaa mote chumbani mle.
Juu ya paa la mabati ya zamani maji yaliteremka kwa kasi ya kumwagika michirizini, vyooni, vidimbwini hadi kwenye vijimikondo vidogo vilivyomiminikia mitaro maarufu ya hapo. Katika moja ya bati la nyumba ya Tino kulikuwa na tundu. Taratibu yalipenya kwenye tundu hiyo yakatambaa kwenye pau la miti. Mwisho yalifika katika upande mmoja ambao ulifungwa kamba zamani. Yakashindwa tena kutiririka kama pale mwanzo. Badala yake yakarowanisha ile kamba hadi ilipokinai yakazama juu yake. Mwisho yakaanza kudondoka chini. Tone la kwanza lilitua juu ya jicho la Tino ambaye aligeuka shingo kujisogeza. Lakini kabla hajapima matokeo ya kitendo hicho matone mengi zaidi yalidondoka moja baada ya jingine na kufanya michirizi kamili. Upesi ulivundumka pale kitandani akakivutia katikati ya chumba. Kisha alitafuta ndoo tupu na kuiweka chini ya mchirizi ule wa maji. Sauti ya bati ya ndoo ikachanganyika na ile ya mvua nje.
Nyumba yenyewe ya Tino ilikuwa bondeni juu tu kidogo ya mtaro mkubwa uliokuwa ukipitisha maji machafu. Safari ya maji hayo ilianzia kwenye viwanda vya nguo, kupitia kwenye karakana za magari halafu ndipo yakaingia Sega penyewe ambapo yalikokota maji ya vyooni na makaroni na kadhalika. Hivyo rangi na grisi za viwandani. Harufu yake ilikuwa nzito ya mchanganyiko wa madawa hayo na mikojo pamoja na uchafu mwingine. Lakini leo harufu hiyo haikusikika kwa vile ilihanikizwa na wingi wa maji ya mvua ambayo yalikuwa yakipita kasi na kuvikumba vitakataka vyote vilivyokuwa sawa na njia yake. Sufuria, vyungu, sahani zikawa zinaelea. Mzaizai mkubwa mkubwa ukazuka, waume kwa wake, watoto kwa wazee wakajitoa kuvizuia vyombo vyao adimu visikokotwe na maji. Wengine walikuwa wakitoa vitanda vyao na madogoro kuvipeleka juu kidogo kwenye usalama. Visanduku vya mbao, mabati na makasha mengine yasiyo na thamani vilisambazwa huko na huko.
Tino alisikia ghasia hizo karibu na saa kumi na moja ya alfajiri. Akafungua mlango wa chumbani kwake na kutokea ukumbini. Nyumba yenyewe ilikuwa ndogo yenye vyumba vitatu vidogo. Chumba kimoja kilikuwa chake, cha pili cha watoto na wageni, na kingine alimpangisha Jinja Maloni. Kwa vile muda mrefu mkewe alikuwa akilima shambani kwao kijijini, na kwamba watoto wake walikuwa wanaishi na babu na bibi yao huko huko, chao kimoja kikawa kama sebule ya mazungumzo.
Kule nje Tino alijitoma ndani ya heka heka. Akaingia ndani ya nyumba ya ajuza mmoja, mgonjwa wa miguu, ambaye alikuwa akipiga kelele. Kibanda chake kilikuwa chini zaidi kimezungukwa na migomba hivyo maji yaliingia huko kwanza yakafika hadi kiunoni. Tino alimkuta bibi huyo alitangatanga huku na huko akijaribu kutafuta hiki na kile. "Hela zangu! Nguo zangu, Mungu wee! Masikini miye", aliomboleza. Alipomwona Tino alimtambua upesi na kuendelea. "Mwanangu nafa baba". Tino alimseta bibi huyo bila ya mazungumzo zaidi, kanzu yake na gauni vimetepeta maji machafu. Mbali na uzee wake alikuwa na tambo la kutosha. Lakini uzito huo ulikuwa si kitu si chochote katika misuli kamili ya Tino. Baada ya kumfikisha kwenye usalama alirejea tena kule kibandani kutoa vitu vyake vya thamani alivyoweza kuviona akaanzia na nguo. Muda si muda Minja Maloni alifika na kuanza kumsaidia Tino kutoa makasha, matendegu ya vitanda vya samadari na magodoro ambayo tayari yalikuwa yametota. Kote kulikuwa na kelele na vilio vitupu. Kwa wakati ule hakuna aliyeweza kukadiria kiasi cha maafa na hasara iliyopatikana.
Kufikia saa tatu ya asubuhi mvua kubwa ilikuwa imeacha yakabaki manyunyu tu. Tino alisimama pale nje kwa muda akiwaona watu waliokuwa wakipita wametota chepechepe wengine wamekamata majani ya migomba kama miamvuli. Kisha aliingia chumbani mwake akachukua springi ya kufanyia mazoezi. Aliinua mbele ya kifua chake mkono mmoja huku na mwingine kule akaanza kuivuta. Taratibu alitanuka pamoja na misuli ya kifua na mikono yake. Aliongeza nguvu za kuvuta. Aliuma midomo, uso ukakazana. Mbele ya paji lake la uso mshipa wa damu ukasimama. Kifuani na mikononi mishipa ya damu ilijitokeza kama ramani. Kila alipofika mwisho wa kuvuta ile springi, aliirejesha tena taratibu. Hivyo hivyo aliendelea kwa dakika kumi hadi pumzi zikaongezeka, akaacha kinywa wazi na kuhisi mvuke na mhemo wa pumzi zake. Kijasho chembamba kilianza kumvuja. Aliporidhika aliirejesha ile springi juu ya kabati. Kwa muda wa dakika tano nyingine alitumia kamba kufanya mazoezi ya kurukaruka. Kumalizika akachukua ndoo ya maji kwenda kuoga kwenye choo kilichozungushiwa kumbesa na milango ya gunia. Alirudi upesi akavaa suaruali nyeusi na fulana ya kata mikono, chini alivaa raba nyeupe. Sasa alizunguka tena uani mwa nyumba yake hadi pale alipoweka kwama akasimama kuliangalia. Miaka miwili sasa tangu alipoamua kuacha kazi ya kuajiriwa kwa ugumu wa maisha. Na tokea hapo alivithamini mno vitu hivyo: Kwama na afya yake. Kwama lilitengenezwa kila lilipoharibika na mwili wake haukuhiniwa bila kurutubishwa kwa kila aina ya mapochopocho aliyoweza kujichumia mwenyewe.
Kwama hilo lilikuwa kubwa la upana wa futi tatu na urefu takriban futi tano na kitu. Sehemu yake ya juu ilitengenezwa kwa vyuma vyembamba ili kupunguza uzito wake na kulipa nafasi zaidi ya kuhodhi mizigo. Fremu hiyo ilitua juu ya difu ya gari ndogo ambayo ilikuwa na matairi safi mawili, moja kila upande. Gari lote lilipakwa rangi nyeupe. Nyumba na pembeni liliandikwa ZINGATIA. Sasa Tino alipigapiga mipira hiyo kwa raba zake kupima upepo wake.
"Wa geto!" Sauti ya chini ya Jinja iliita kusalimu kama kawaida yake. Na bila ya kugeuka wala kuacha kadhia yake ya wakati ule Tino aliitika, "Sema Mzulu".
"Ni ndimi Gotagota, mwana wa Mfalme Chaka", Jinja alijigamba kwa sauti nzito. Tino aligeuka kumwangalia mpangaji rafiki yake akitabasamu.
Jinja Maloni, kama mwenyewe alivyostahabu kuitwa, Mzulu, alikuwa na umri usiopungua miaka hamsini. Mrefu wa futi sita, mwili wake ulianza kuchoka kutokana na kazi nyingi za sulubu alizozipitia kama kuli na kadhalika. Hata hivyo alikuwa na mshipa mzuri na wahuni wa Sega walihara kumwingia. Alitembea kokote na wakati wowote bila ya kuhofia chochote. Zama za ujana wake alikuwa bondia na kupata zawadi kem kem kutoka kwa mabaharia wa meli za nchi mbalimbali. Katika kipindi hicho alifanya starehe za kila aina, akabadilisha wanawake kama mashati. Ila wakati haukumkopesha. Hatimaye Jinja akastaafu hajadiriki mke wala mwana. Akaziponda pesa zake za kiinua mgongo kunywa pombe za fahari hadi zilipokwisha. Hana kibanda hana kitanda. Ndipo akatokea Tino na kumpangisha katika kibanda chake. Jinja hakuchagua kibarua, akachimba vyoo, kuvitapisha, kulima na chochote ambacho mikono yake iliangukia mradi tonge kinywani.
Akitokea uani Tino alikokota kwama lake taratibu, kunako kijia kidogo hadi njia kuu kidogo mpaka sehemu ambayo kwa utani paliitwa Hilton.
Lakini kinyume kabisa na ile hoteli ya Hilton katikati ya jiji la Mindule, hapo palikuwa ni mkusanyiko ya vijimikahawa vingi. Nje yake waliketi wanawake wa makamo, wasichana, vigori na hata wavulana wakiyaangalia masinia yaliyosheheni bidhaa mbalimbali kama vile vitumbua, maandazi, bajia, mikate ya kumimina, chapati, sambusa, mihogo ya kupwaza na kukaanga. Mandhari hayo yasingemtuma mpita njia kujitoma katika mashindano makali ya biashara. Bali mpaji Mungu. Hivi ssa vilima vya bidhaa zile vilipungua kadiri jua lilivyozama.
Tino akaegesha kwamba lake nje ya kijimkahawa kimoja. Kabla ya kuingia ndani alivinjari huku na kule kutafuta bidhaa ya kununua. Mtaaradhi wa kula, mteuzi mithili ya mbega, alipoteza muda katika harakati hiyo akizipuuza "karibu baba, karibu kaka, karibu mkwe" zote za kumchombeza kununua kutoka kwa wachuuzi wale. Hatimaye alimfikia mvulana wa miaka kumi. Mbele yake palikuwa na sinia kubwa sana iliyosalia vitumbua visivyozidi thelathini. Hana hili wale lile kichwani.
"Funga vinne", alishtushwa na sauti ya Tino. Mikono yake mepesi ilitekeleza amri hiyo kwanza ndipo akainua macho kumwangalia mshitiri wake. Kimya kimya alizipokea fedha zake, akaendelea kuhesabu fedha zake za kichele kama pale awali. Hatua chache mbele, Tino alinunua chapati nne kutoka kwa bi Mkubwa mmoja ndipo akarejea kunako mkahawa ambapo aliegesha kwama lake. "Eeee! wa geto", zilimlaki Tino ambaye alisimama kuwaangalia waliomsalimu. Kuwajibu aliinua mkono mmoja juu akaelekea kunako kona ya kulia na kuketi. Aliletewa supu bakuli mbili, akamaliza chapati na vitumbua vyote kabla ya kuvisafishia vizuri ndani kwa vikombe viwili ya chai ndipo aliinuka kumkabili mpokea fedha.
"Vipi, mbona leo saa hizi, waogopa mvua?" alitania yule mpokea fedha.
"Niogope mvua mimi? Wewe umekazana kupokea fedha hujui jirani zako wafa maji?"
"Kila mtu na lwake bwana".
"Sawa baba! Iko siku yako", Tino alilipa fedha akaelekea kutoka.
Akiwa amechangamka vilivyo alilivuta kwama lake kupitia kwenye ile barabara iliyokuwa na madimbwi ya maji, akajaribu kuyakwepa alivyoweza na kuyaingia aliyoyashindwa. Hivyo hivyo aliendelea hadi alipokaribia makaoni penyewe. Idadi ya watu iliongezeka na kuendelea kuwa kubwa kiasi cha kuogofya pale alipotokezea kunako barabara kuu yenyewe iendayo Mindule.
Huku na huku pembeni mwa barabara kuu kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu. Tino alipata taabu kuwapisha watu wale, lakini taratibu alifanikiwa hadi alipobaki kuvuka barabara. Ng'ambu ya barabara kulikuwa na kituo cha mabasi na teksi. Sio mbali na hapo paliegeshwa makwama yasiyopungua ishirini. Pote palikuwa na mzaizai watu wakishusha mizigo kutoka kwenye mabasi na malori machache yaliyoweza kusafiri kutoka Bara. Basi moja lilikuja na sehemu ya matenga ya nyanya. Kuna mwanaume mmja, kavaa kaptura, kifua chake wazi, kikubwa kimeviringana mithili ya pipa, miguu miembamba kuliko kawaida, alipanda juu ya ile basi. Alipofika juu ya ngazi wanaume wengine walimtwisha tenga moja juu ya kichwa chake. Uzito wa takriban kilo hamsini za tena ile uliuelemea mwili wake, misuli ikatutumka na miguu yake ikakaza mithili ya upinde uliotaka kufyatuka. Taratibu, tenga kichwani, yule bwana alishuka hadi chini ambako aliyapanga matenga kwa ustadi. Tenga moja shilingi mia mbili alinadi, kama waweza shusha mwenyewe. Tayari wenye makwama waliyazengea matenga hayo kutaka kuyapeleka yanakotakiwa. Katika mishemishe hiyo pakatokea msukumano.
"Wacha kunisukuma, mjinga wee!"
"Sasa unavimba?"
"Ndiyo, naweza kuvimba hata usoni kwako".
Walijibizana wavuta kwama wawili kabla ya hawajavamiana kupigania yale matenga. Watu walitaka kuwatenganisha lakini Tino aliwazuia akashabikia, "Wacheni wafanye mazoezi kidogo". Lakini hayakuwa mazoezi bali malau. Huyu alivuta ngumi, mwingine alikwepa. Akarusha kichwa, teke, ngumi tena, hivyo hivyo hadi pumzi zikawaishia. Maneno nayo yakawaishia wakabaki kuhema na kuanagliana kama majogoo.
Itaendelea Ijumaa.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |