PAMBA kwa wastani huliingizia taifa wastani wa asilimia 15 ya fedha zote za kigeni kulikuwa na ongezeko la uzalishaji.
Kutoka mwaka 1922 hadi 1966 asilimia 22. Serikali ilitia mkazo kilimo hicho kwa kufuata utaratibu wa kikoloni ulioanzishwa mwaka 1951, ambapo kulianzishwa mamlaka maalum za kusimamia tangu kwenda shamba, kupanda, kupalilia, kuvuna pamoja na soko.
Mamlaka hizo ikiwemo Halmashauri ya kuuza pamba zilifanya utafiti wa ardhi zenye rutuba na kufanikiwa kupanua kilimo cha zao hilo hususan katika mkoa wa Mwanza katika maeneo ya Geita, Biharamulo, Igunda pamoja na Sengerema. Serikali ilianza kuunda taasisi mbalimbali za kusimamia zao hilo vikiwemo vyama vya ushirika ambavyo baadaye vilichangia kwa kiasi kikubwa kuua zao hilo hasa pale zilipoanza kuwakopa na kutowalipa wakulima, kununua mazao ya wakulima kwa bei ndogo pamoja na kushindwa kuwatafutia pembejeo.
Mnamo mwaka 1951 serikali ilianzisha Halmashauri ya kuuza pamba nje ambayo ilikuwa mahususi kanda ya ziwa na kuanzisha vyama vingine vya ushirika ambavyo baadaye viliunda Victoria Federation of Cooperative Unions Ltd ambapo kwa kiasi fulani ilisaidia kukuza zao hilo nchini.
Mwaka 1973 kwa mara nyingine tena serikali ilianzisha sera ya mamlaka za mazao na kuanzishwa mamlaka ya pamba badala ya Halmashauri ya kuuza pamba.
Katika hatua nyingine mwaka 1976 serikali ilivunja vyama vya ushirika na mamlaka ya pamba ilitwaa majukumu yote ya kuhudumia zao hilo tangu kulima mpaka kuuzwa kwake. Vile vile mwaka 1985 serikali iliamua kurudisha tena vyama vya ushirika na bodi ya pamba kuundwa badala ya mamlaka ya pamba kwa mujibu wa sheria namba 19 ya mwaka 1984.
Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho katika sheria namba 5 mwaka 1990 na kuipa mamlaka pekee ya kuuza pamba nje ya nchi kwa niaba ya vyama vya ushirika na musuala yote yaliyohusu zao hilo. Mwaka 1993 bei ya pamba kwa mkulima ilikuwa ikipangwa na serikali kwa kuzingatia soko la dunia, gharama za uendeshaji na uzalishaji ambapo pamba yote ilikuwa ikinunuliwa na vyama vya ushirika na kuuzwa nje na bodi ya zao hilo.
Serikali mwaka 1993 ilianzisha sera mpya ya uchumi wa soko huria kwa madai ya kuondoa ukiritimba uliokuwa ukifanywa na bodi ya pamba na kuandaa bodi mpya ikiwa na jukumu la kuendeleza uzalishaji wa zao hilo.
Akiwasilisha taarifa ya kilimo cha zao la pamba mkoani Morogoro Mei 4, mwaka huu, katika kikao cha mkuu wa Mkoa huo, Mshauri wa kilimo Sekretari ya mkoa Bw. E. Shayo alisema, uzalishaji wa pamba likiwa ni zao la biashara mkoani humo miaka ya themanini ulipanda kufuatia kuwepo msukumo na kampeni kuhimiza zao hilo.
Bw. Shayo aliitaja mikakati iliyotumika kufanikisha kilimo cha pamba kuwa ni pamoja na kuwepo vyama vikuu na vya msingi vilivyoshughulikia upatikanaji na usambazaji wa pembejeo, mikopo kwa wakulima, ununuzi na usafirishaji pamoja na kuwepo kwa vituo vya ununuzi vilivyosimamiwa na vyama vya msingi.
Pia alisema, barabara zilizokuwa na zao hilo zilihudumiwa kikamilifu na "Cotton Fund" ili kuweza kurahisisha usambazaji wa pembejeo na mazao. Vile vile alisema, bei ya pamba wakati huo ilizingatia uzalishaji.
Kwa mujibu wa mshauri huyo wa mkoa wa Morogoro hali ya uzalishaji wa zao la pamba kwa tani katika kipindi cha mwaka 1992/93 na 1998/99 katika wilaya nne za mikoa huo zilikuwa kama ifuatavyo:
Morogoro vijijini 1992/93 tani 3,272, 1993/94 tani 1,116, 1994/95 tani 902, 1995/96 tani 757, 1996/97 tani 132, 1997/98 tani 375 na 1998/99 zilikuwa tani 356.
Katika wilaya ya Kilosa mwaka 1992/93 tani 1,205, 1993/94 tani 151, 1994/95 tani 335, 1995/96 tani 1,743, 1996/97 tani 574, 1997/98 tani 143 na 1998/999 tani 427.
Kwa upande wa wilaya ya Ulanga, mwaka 1992/93 tani 292, 1993/94 tani 275, 1994/95 tani 517, 1995/96 tani 387, 1996/97 tani 143, 1997/98 tani 59, 1998/99 tani 1026.
Wilaya ya Kilombero mwaka 1992/93 tani 2,556, 1993/94 tani 44, 1994/95 tani 3,865, 1995/96 tani 2,506, 1996/97 tani 1,850, 1997/98 tani 842 na mwaka 1998/99 kulikuwa hakuna kitu.
Aidha, Mshauri huyo katika taarifa yake hiyo alieleza sababu mbalimbali zinazochangia kushuka kwa uzalishaji wa zao la pamba ambapo alisema kuwa uzalishaji ulishuka kutoka hekta 15,654 zilizofikiwa mwaka 1987/88 hadi hekta 4,409 mwaka 1998/99.
Alisema kwamba mwaka 1992/93 bei iliyotangazwa ya shilingi 94 kwa kilo haikuzingatiwa na badala yake pamba ikauzwa kwa shilingi 60 tu kwa kilo. Aliongeza kusema hali hii ilisababisha kushuka sana kwa uzalishaji mwaka 1993/94.
Bw. Shayo aliendelea kusema katika taarifa yake hiyo kwamba uzalishaji umeendelea kushuka kuanzia mwaka 1993/94 hadi sasa ambapo bei ya pamba imeshuka kutoka shilingi 170 hadi shilingi 100 msimu huu wa 1999/2000.
WAISLAMU mjini Morogoro wametakiwa kutunza vizuri amana ya Uislamu waliyopewa na Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Mtume (s.a.w.).
Aidha, wameaswa kutoshughulishwa na mambo yasiyo ya msingi juu ya Uislamu wao zaidi ya kuwagawanya, agenda ambayo hailengi kabisa kuwanyooshea maisha yao hapa duniani wala kuweka vyema mustakabali wa maisha yao ya kesho Akhera.
Hayo yametamkwa na Ustadh Abdallah wa Atta-aun Girls Islamic High School alipokuwa akitoa waadh katika Maulid Nabii iliyofanyika Jumatano kuamkia Alhamisi ya wiki iliyopita katika Msikiti wa Boma Road mjini hapa.
Alisema, Waislamu wa mji huo hawana budi kuuendea Uislamu kama alivyo ufunza Mtume bila ya kuubagua katika matapo mawili, la dunia na la akhera.
Aliwataka waitumie hafla ya Maulid kutathmini hali zao toka kule watokako, walipo na hata wanapoelekea jambo ambalo litawahakikishia kulifikia lengo la kuubwa kwao.
"Tujiulize tumeufanyia nini Uislamu, na tuna mipango
gani kwa kuhuisha Uislamu katika maeneo yetu?" Aliuliza Ustadh Abdallah.
SIKU ya Jumatano Juni 12, 2000 mnamo saa mbili na robo usiku nilikuwa nimetulia nyumbani kwangu nikisikiliza redio inayoitwa ya Taifa (RTD). Ulikuwa ukitolewa ujumbe wa mwenge kwa mwaka huu na Rais wa sasa Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, ujumbe wake huo alikuwa akiwaasa vijana nchini kuhusiana na suala zima la kujikinga na ukimwi.
Ukweli kwa wakati tulio nao ukimwi umekuwa ni tishio kubwa kwa wananchi wa Tanzania na dunia nzima kwa ujumla wake. Na ilikuwa ni wakati muafaka kwa Rais wa nchi kuwatahadharisha vijana wake kuhusu janga hili la ukimwi ili waweze kujikinga nalo kwa faida binafsi na taifa kwa ujumla wake.
Katika ujumbe wake, Rais aliwasisitiza sana vijana kufanya mapenzi salama, sijui usemi huu alikuwa akimaanisha nini. Pia aliwataka kuzaa kwa kuamua na si kwa kutokea tu kwa bahati mbaya. Pia aliwataka mabinti wanaofanya ukahaba watafute njia nyingine bora za kujitafutia riziki badala ya kuuza miili yao kwani wanajitia kwenye maangamizi na vifo.
Pamoja na uzuri wake, ujumbe huo umekuwa na dosari nyingi, kwani amezungumzia tatizo na sio njia za kuondoa tatizo lenyewe ambazo ni za kijamii zaidi kuliko za mtu binafsi.
Tatizo linalopelekea hali hii ni sera mbovu za kuchochea na kufurahia maovu yafanyikayo nchini na hata kuyatolea fedha za kuyaendeleza na hata kuhamasisha ufanyikaji wake bila hata aibu yoyote ile.
Miongoni mwa sera hizo ni ile ya kufundisha elimu ya ngono mashuleni. Mbaya zaidi watoto wa shule za msingi nao wamekuwa wahanga wa tatizo hili. Hapa mjini Lindi ni wiki mbili tu zilizopita watoto wa shule za msingi wameoneshwa mikanda ya ukimwi ambayo imechupa mipaka kiasi cha kuonesha hata watu wakifanya jimai hadharani. Je, hii ndio njia ya kuwafanya watoto wajikinge au ndio njia ya kuwachochea nao wautafute ukimwi kwa hali na mali.
Ikumbukwe kuwa watoto ni rahisi kuiga upuuzi kuliko ujuzi, akili zao ni sawa na dodoki ndani ya maji hufyonza kila kitu utotoni kwa ajili ya matumizi ya ukubwani. Hivyo watoto wanajengewa msingi mbovu utotoni tusije baadaye kumtafuta mchawi na kumsakizia "siku hizi" watoto wote kuwa ndiye aliyewaharibu kumbe ni sisi wenyewe kwa kuwaonesha mikanda ya hovyo, tusiwapeleke katika maangamizi watoto wetu, tuwahurumie.
Pia televisheni zimekuwa zikionesha michezo ambayo ni kichocheo kikubwa sana cha zinaa hasa kwa vijana na watoto watazamao. Kama sababu kubwa ya kuenea ukimwi kama Rais alivyosema ni zinaa usitarajie vichocheo vya zinaa viwepo halafu zinaa isifanyike. Hivyo kwa mtu mwenye busara angeondoa kwanza njia zote zinazopelekea waache kufanya zinaa kuliko kuwahamasisha wakati milango yote ya kuendea ukimwi iko wazi hizo zitakuwa ni ndoto za Alinacha za kujenga ghorofa angani bila ya nguzo toka ardhini.
Dosari nyingine ni kukua kwa kasi kwa madanguro ambapo serikali ndio inayotoa vibali vya kujengwa kwa madanguro hayo. Na hakuna kifanyikacho humo ila ni zinaa tu, tusitegemee katika nchi yenye madanguro mengi kama Tanzania kisha ukimwi uweze kupigwa vita.
Pia pato la taifa la Tanzania linategemea zaidi ulevi na ulevi umekuwa ukihamasishwa, ukitangazwa sana na vyombo vya habari, kiasi Watanzania wengi wanaona ulevi ni kitu chenye thamani na ni stahiki yao. Mtu anapolewa anaweza kufanya lolote bila ya kujijua, ni ulevi huo h uo unaofanya watu wasifanye mapenzi salama, wabake hata watoto wadogo. Hivyo kama njia za ulevi hazitafungwa kujikinga na ongezeko la kasi ya ukimwi itakuwa ni kitu cha kufikirika tu na si cha kutekelezeka kama wafikiriavyo wao.
Hivyo hata kama Masheikh, wananchi, wazazi na
viongozi wa dini wakiwaelimisha watu wao kuhusu athari za ukimwi, athari
hizo hazitaonekana kama milango yote inayosababisha kuenea kwake haitafungwa.
Hivyo sera kwanza zibadilishwe kisha ndio wananchi waelimishwe hapo ndipo
tunaweza angalau kwa kiasi kidogo kupunguza kasi ya ongezeko la ugonjwa
huu hatari wa ukimwi.
Ufunguzi
wa Tawi la CUF Kariakoo:
Wazee wakumbuka enzi za kudai
uhuru
WAZEE wa kariakoo ambao hivi karibuni walikihama chama cha CCM na kujiunga chama cha CUF wamesema uwanja wa siasa wa awamu hii unawakumbusha harakati za kudai uhuru miaka ya hamsini.
Wazee hao wa Tawi la amani na utulivu lililopo eneo la kariakoo jijini wamesema historia imejirudia kama ilivyokuwa wakati wa kudai uhuru ambapo wiki iliyopita walishuhudia wanaCUF wakifanya kile kilichofanywa na wana TANU miaka hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wenziwe mzee Athumani Mwintanga (70) amesema zama zile wao wakiwa vijana walisukuma gari lililomchukua mwalimu Nyerere hadi nyumbani kwake Magomeni.
"Sisi wakati huo tulikuwa ngangari tulimsukuma Nyerere katika gari toka uwanja wa ndege mpaka magomeni nyumbani kwake huku tukiimba wimbo wa Baba kabwela UNO", Mzee Mwintanga amemueleza Mwandishi.
Naye Mzee Dafa ambaye ndiye katibu wa Tawi hilo ameliambia gazeti hili kuwa tangu waanzishe Tawi hilo wazee kutoka sehemu mbali mbali za jiji wamekuwa wakifika tawini hapo kuwapongeza.
Aidha amesema wazee wengi wa maeneo ya kariakoo wameonesha kuwaunga mkono, mpaka sasa idadi ya wazee wa tawi hilo imefikia 142 kutoka 132.
"Tulikuwa 132 sasa hadi leo (jana) imefikia 142 na bado itaongezeka zaidi", amedai Katibu huyo.
Amesema walipoamua kupandisha Bendera ya CUF mahali hapo walipata misuko suko kuanzia kwa mjumbe wa mtaa wa CCM.
"Tuliambiwa tuache kujenga Tawi na mjumbe wa mtaa Bwana Ali Chamshama lakini tuliamua lolote liwalo na liwe na tukapandisha bendera", amesema Katibu huyo.
Naye Mzee Salum Said (60) amesema, wamefungua tawi hilo kwa uchungu kutokana vitisho vya CCM.
"Imefikia hata Mwenyekiti wa mtaa ananyanyasa, kutuambia msifungue eneo la msimbazi polisi", amesema mzee Said.
Tawi hilo la wazee litafunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba mara tu atakaporejea Jijini Dar es Salaam, ufunguzi uanatazamiwa kuwa na shamra shamra kubwa.
Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa
maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye
Baraza
ya Wasomaji
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |