KWA kweli historia ni kitu muhimu sana, anasema Bw. Lus Farakan, kiongozi wa Nation of Islam kule Marekani, "Ukiikosa historia yako huna chako. Kwanza hutojiamini, hutojiheshimu na kuheshimiwa, hutozijua na kuzidai haki zako, na hutokuwa na msimamo katika maamuzi yako". Aidha, historia humuwezesha mtu au jamii kutathmini mtiririko mzima wa maisha yake, hutoa fursa kwa baadaye. Kwa kifupi historia ni kioo cha jamii.
TANZANIA tunayo historia yetu, lakini kwa bahati mbaya haijitegemei, imeshindwa kuwa kioo halisi cha jamii yetu, kwani imenyimwa haki yake ya kuwa historia, imechanganywa na mambo mengi ya uongo, na ukweli ukaachwa kwa makusudi maalum ya viongozi walioshika dola baada ya uhuru.
Hali inatupeleka tofauti na malengo ya umuhimu wa kitu historia, yaani hatutopata fursa ya kutathmini jamii yetu kama Watanzania, hatutopata muelekeo madhubuti na hatutoweza kurekebisha au kukosoa mienendo mibovu iliyojitokeza na hivyo kujenga mtazamo sawia wa jamii yetu.
Waislamu ni katika wana jamii ya Tanzania lakini wamekuwa ni waathirika wakubwa wa mifumo ya kijamii tangu uhuru. Hata hivyo kwa historia ya kweli wao ndio waliofanya juhudi kubwa kumtoa mkoloni na kuleta uhuru, japo kwa makusudi historia hii ilifichwa mpaka pale watu mahiri katika Waislamu walipofanikiwa kuichimbua na hilo sasa ni bayana kwa Waislamu wote pamoja na kuwa bado hatujaweza kuliingiza katika mitaala ya elimu.
Kwa kweli historia kwa upande wa jamii ya Waislamu wa Tanzania si nzuri, haipendezi na ni chungu. Waslamu wamefanywa wasiwe na maendeleo katika nyanja zote muhimu, wakinyimwa haki zao za kiibada na za kijamii, aidha, wamepewa uyatima usio mwangalizi. Kila mahali atasubiri huruma ya muhudumu na sio kama haki yake, si katika elimu, ajira, madaraka na huduma nyingine.
Historia kabla ya uhuru vile vile iliwanyanyasa Waislamu sana na ndiyo ikawa chachu na chemchem ya kupigania uhuru. Hata hivyo baada ya uhuru hali iliwekwa wazi juu ya madhila yale ya wakoloni na wakaahidiwa mambo mazuri na viongozi wa dola lakini hali ikawa kinyume, kila aliyehoji AHADI alidhibitiwa na kufumbwa mdomo kwa nguvu sambamba na vitisho vikubwa na unyanyasaji ukaendelea ndani ya uhuru.
Rais wa awamu ya tatu kama ilivyo kuwa kule nyuma naye alipelekewa waraka wa matatizo na malalamiko ya Waislamu, nalo tumelisajili katika historia, ilikuwa katika Baraza la Idd mwaka jana (1999) pale Diamond Jubilee, akaahidi kuyafanyia kazi, akakaa nayo mwaka mzima. Majibu yaliyokuja hayakutarajiwa na tafsiri yake haikuja moja kwa moja, yaweza kuwa kejeli au dharau, kibri au dhihaka, kwenye uungwana hayapokabisa na yalitawaliwa na jazba.
Waislamu wameumia kwa muda mrefu, wamenyanyaswa na wameuawa hadharani na kuvamiwa Misikitini kwa vipigo na mbomu ya machozi. Leo utafiti wa Rais unasema ni wahuni!
Aidha, Rais anasema hakuna mfumo rasmi wa kuwabagua, kuwanyanyasa na kuwabana Waislamu kwa sababu ya dini yao pamoja na kwamba anakubali hayo yapo. Hivyo basi hakuona haja wala sababu ya kuunda tume ya kuyashughulikia na kubwa zaidi ni matatizo ya kihistoria. Waislamu kweli wana matatizo Rais alikubali na ndiyo yanazidisha matatizo juu yao lakini yanatokana na sababu za kihistoria.
Hapa tunafikia kuitazama jamii kihistoria lakini Rais haeleweki na wala hajajibu ukweli. Hivi ni historia gani iliyopeleka Muislamu lazima afeli darasa la saba ila kama atajiita Julius, John au William ndio afaulu, ipo kweli historia iliyopelekea wakuu katika mashirika yote makubwa na madogo, ya umma na serikali lazima wasiwe Waislamu au ni historia gani iliyopelekea mashule ya Waislamu yaliyotaifishwa yasirudishwe ila ya Kanisa, ni ipi historia iliyopelekea Muislamu kupewa majina mabaya katika jamii ili aonekane kioja na haenei katika jamii, ni historia gani leo hii iliyowafanya wanawake Waislamu wasiruhusiwe kuvaa hijabu zao makazini au ni historia gani iliyopelekea Waislamu wawe rahisi na sawa kuuliwa kisha sharia isifuate mkondo wake.
Rais lazima atueleze kama tunayo pia historia iliyopelekea kila jambo baya avishwe Muislamu, mfano mabomu yalipolipuka katika balozi za Marekani kabla hata ya uchunguzi wametajwa Waislamu na mpaka leo serikali ya awamu ya tatu imewavalia njuga pamoja na kuonekana hawana hatia, au moto ulipowateketeza wanafunzi kule Shauritanga moja kwa moja walitajwa Waislamu bila uchunguzi wowote.
Matajiri Waislamu wamepandikiziwa makachero nao wamewaamini sana bila kuwajua kama wako kuchunguza kama wanasaidia Waislamu wenzao ili mambo yao yaharibiwe hatuoni historia iliyopelekea haya, au tunapata historia gani inayomzuia Rais kutoikubali OIC hali Vatican inazidi kung'aa.
Haya yote hatunayo majibu yake bali pia Rais amejigamba kufuata sheria na katiba, hatujui kama kuna historia iliyomfanya asikemee Bunge kwa kuruhusu katiba kuvunjwa bungeni pale walipomjia juu Waziri Muislamu alipotetea haki za kikatiba za Waislamu na kudai Alhaj (Muislamu) hawezi kuwa Waziri au na mpaka leo Masheikh wanakamatwa na wengine kufukuzwa nchini mwaka 1964 kwa jeshi kuasi, serikali haisemi kitu. Au ni historia gani iliyopelekea Bwana Said Tewa mwaka 1963 aachishwe Uwaziri kwa sababu anashirikiana na Waislamu wenzake au yaliyomkuta Sheikh Abubakar Mwlima kwa visingizio vya uongo ili tu awapishe wenyewe?
Yote hayo yanaashiria udhalimu, uonevu na unyanyasaji kwa Waislamu, aidha, Rais ili kufuta hili aliomba aletewe ushahidi wa kisayansi kuthibitisha madai hayo ya Waislamu. Kule Shinyanga watu walitakiwa kuleta ushahidi juu ya wachawi walio waadhibu kila siku na iliposhindikana kwa kuwa ni udhalimu wa siri za kichawi watu waliamua kuchukua sheria mkononi dhidi ya wachawi hao.
Rais haepukani na mfano huu, anajua kuwa ni siri kubwa ya hujuma zilizoratibiwa dhidi ya Waislamu na ina dhamana ya utekelezaji wake na mipango maalum yenye malengo (Rejea Dk. Sivalon).
Hivyo pengine ni katika mfumo huo huo usio rasmi ndio Rais aliposimamia ili kuhakikisha mambo yanaendelea shwari na asije kuwa yeye ndio sababu ya kuyavuruga.
Mwalimu Nyerere alikiri katika historia sahihi kuwa aliitwa katika harakati za uhuru na alikuwa Mkristo peke yake na wazee walimpenda sana wakimwita kijana wao, bila kujali dini yake kisha wakampa uongozi wa nchi. Hivi hii historia ya udini wa kihistoria dhidi ya Waisalmu imepatikana wapi? Kabla na baada ya uhuru mategemeo ya wananchi hususan Waislamu yalikuwa haki sawa kwa wote bila kujali rangi ya mtu, kabila au dini lakini hali ikawa kinyume. Sasa imekuwa lazima tuihoji historia ili itupe ukweli na muelekeo, ni lini historia ilibadilika na kutufikisha Waislamu hapa tulipo.
Hili somo, tunamuomba Muheshimiwa Rais alitoe na ni vizuri mwaka huu mapema 2000 na ni haki yetu kuhoji ili tujue mustakbali wetu. Tunahitaji kujua anakusudia historia kuanzia karne gani mpaka wapi, au ni wakati wa biashara ya utumwa, au ni kabla ya uhuru au baada ya uhuru kupatikana? Kulitokea ubaya upi mpaka tufikishwe hapa?
Sisi bado hatuoni majibu yenye hoja katika historia
ambayo ndio hivi tunazidi kuijenga, hatuoni kibaya tunachofanya zaidi ya
kulalamikia haki zetu.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |