KUPENDA kutendewa haki ni katika maumbile ya mwanadamu. Mwizi hapendi chake kiibwe japokuwa mweyewe ameota sugu katika kukwapua vya wenzake.
Vibaka, matapeli, huwa ni wenye kuchukua tahadhari ya hali ya juu ili vitu vyao visiibwe, hata kama wao wamevimiliki kwa taratibu zisizo halali watajitahidi kadri wawezavyo ili visirudi mikononi mwa wahusika.
Si mpenda haki yule anayetaka kutendewa haki hali ya kuwa hayuko tayari kuwa mfano wa kutendea wengine. Mpenda haki wa kweli daima hutenda kabla ya kutendewa! Na hii ndiyo tabia njema
Hakuna azaliwaye akiwa na tabia ya kudhulumu au kutenda haki, wala si mwenendo wa bahati nasibu. Hujengeka kwa kujifunza. Kujifunza kunakotokana na kufunzwa, kuiga, au kuzoeshwa.
Kujipamba kwa tabia ya kutenda haki kunahitaji jitihada za makusudi. Hii inatokana na kuwepo ushawishi mwingi uliozunguka unaomvuta mwanadamu.
Mwongozo wa Qur'an unatuelimisha kuwa ushawishi huo unafanywa na viumbe wa aina mbili. Yupo shetani asiyedirikika na binadamu wanaochukia kutenda haki.
Lengo kuu la ushawishi wa wasiotenda haki ni kupumbaza akili za watu ili waendelee kuzikiuka haki za wengine bila ya kupata pingamizi. Wanyonye na kugema ikibidi iwe milele kama uhai ungewaruhusu.
Sema najikinga katika ulinzi wa Mwenyezi Mungu, Bwana mwenye kulea. Mafalme wa watu. Mola wa watu. Najikinga na shari ya mwenye kutia wasiwasi mwenye kurudi nyuma. Anayetia wasiwasi nyoyoni mwa watu. Ambao ni katika majini na watu. (114:1-6)
Kumbe kuna watu wanaotia wasiwasi! Wanaokusudia kupumbaza na kujenga khofu nyoyoni ili kuwaogopesha wanaonyonywa wasigangamae katika kukataa dhuluma.
Upo ushawishi mkubwa sana unaofanywa kwa namna ya kupamba yanayodumaza akili za wana jamii. Kwa ulevi unavyosifiwa na kupewa majina mazuri, imewatia watu wasiwasi na kuhisi kuwa wanakosa kitu muhimu sana katika maisha.
Tahamaki watu wamenasika huko kwa maelfu! Kitanzi kipo shingoni , macho giza na kila siku akili zinachacha na kuchachishwa. Vijiweni kinacho tawala ni mazungumzo ya 'kuvumbua'.
Siku moja nilikikwaa kijiwe, niliwakuta vijana wako hoi hawajiwezi, harufu za midomo yao ni kama mapipa au kiwanda cha pombe. " Tanzania ni nchi ya amani sana ndio maana tunatesa" Ilikuwa ni katikati ya maombolezo, wiki alipofariki mwalimu Nyerere.
Lini akili itapata fursa ya kuyajadili matatizo ya kijamii. Ahoji mahala kodi inapotumika wakati wadogo zake wanasimamishwa masomo kwa kukosa ada, atafakari sababu za walimu kupungua na kutofundisha vyema mpaka watoto wa darasa la kwanza wanatakiwa kwenda tuisheni
Ni wakati upi akili itapata fursa ya kujiuliza kuwepo kwa ukata wa maji, madawa, na barabara kunatokana na nini. Na kwanini umaskini uzidi kupata kundi kubwa la wananchi kila kukicha hali ya kuwa upo uongozi unaokutana mwaka hadi mwaka kupitisha bajeti za maendeleo.
Wakati akili zinadumazwa katika bao, karata, draft, ushabiki wa mipira pamoja na majigambo ya kunywa sana ,waliokabidhiwa dhamana ya uongozi wanaonesha kulewa madaraka kiasi cha kutojuwa hali walioijenga kwa wananchi.
Kwa kuwa wao wanafunguo za hazina ya dola na uwezo wa kuwasomesha watoto wao popote wanapotaka,haiwapitii akilini kuwa wako wengi miongoni mwa wananchi wasiokuwa na uwezo wa hata wa kuwalipia ada .
Viongozi hao huamini kuwa wale wananchi wasioweza kuwalipia watoto michango ya UPE ni wavivu na wazembe. Ikiwa mwananchi anapimwa kwa mtazamo huu, yawezekana wale wanaokufa kwa njaa au kuishi kwa mlo mmoja kila siku wakadhaniwa kujipa unyoronyoro na kujizorotesha.
Waziri Mkuu, Bw Frederick Sumaye ameripotiwa na vyombo vya habari akisema kuwa mwanaume ambaye hawezi kumlipia mwanae mchango wa UPE wa shilingi elfu mbili kwa mwaka, hana sababu za kuoa wala kuzaa.
"Kama mwanaume mzima umemfuata mwanamke kwao, unashindwa kutoa sh 2,000 kwa ajili ya mwanao usingepaswa kuoa kabisa"
Wanyama kama kuku huongozwa kwa silka. Kwa silka zao huhakikisha kuwa watoto wao huwapa malezi na ulinzi mpaka wanapofikia kiwango cha kujitegemea. Hakatizi kipanga wala mwewe kwenye watoto zake bila ya kupambana nae.
Hatudhani kuwa kuna mzazi mwenye akili timamu asiyependa kumwandaa mwanae kielimu, aweze kuwa na sifa zitakazompa mazingira ya kuchaguliwa kwenye ubunge, uwaziri, au urais.
Mwanchi ambaye hana mifugo ya kumpa mwanae akachunge, ukimwona hampeleki shule mwanae atakuwa katika hali ngumu ya maisha kama si mwendawazimu.
Uongozi unaojali majukumu yake ya uwajibikaji, hautumii busara za kutoa ufumbuzi wa majibu ya papo kwa papo, kwamba "asioe", "asizae".
Kwa moyo wa kiutu ujitathimini wenyewe kuwa ni kwa kiwango gani umewajengea wananchi hali nzuri ya maisha itakayofanya wasishindwe kuchangia shilingi elfu mbili za UPE kwa mwaka.
Kuna ushawishi unaolenga kuisukumiza jamii kwenye kilele cha unyama. Wakishazama huko wasiweze kuvuta fikra za kujikwamua. "Tumia kondom" unafanywa kuwa wimbo wa taifa. Utadhani kuna uthibitisho wa kweli kuwa ni kinga ya ukimwi.
Cha kushangaza, hatujawasikia viongozi wanaoshikilia bango la kondom kueleza mafanikio halisi ya debe hilo. Pamoja na kondom kutawanywa kila kona, hutuba ya Rais imeonyesha kuongezeka maradufu uambukizwaji wa gonjwa la ukimwi.
Wimbo wa "mambo kwa soksi" ulionekana kuwa ni uchochezi wa zinaa, unafundisha uhuni na uasherati, hivyo ukapigwa marufuku. Leo viongozi wanauimba wimbo huu tena bila ya tafsiri, badala ya mambo kwa soksi inatajwa kondom. Inasikitisha!
Debe la "kondom ni kinga" ni ushawishi, badala ya kusisitiza ndoa na kuheshimu unyumba, eti "uwe na mpenzi mmoja". Hata washenzi wa jinsia moja pamoja na wazinifu waendelee na uchafu wao alimuradi hawaongezi mwingine.
"Kama ukiambiwa kuwa kuywa bia bila ya mrija utang'oka meno, utasema mrija ni ghali, na ninafikiri kondom matumizi yake ni hivyo hivyo"
Kauli ya Waziri Mkuu alitokana na maelezo ya mbunge wa Ngara (CCM) Bw Pius Ngeze aliyesema kuwa bei ya kondom vijijini inafika sh 200 na inafanya wananchi wajamiiane bila ya kutumia kinga (Majira, Juni 18).
Katika semina kuhusu uhai, ulinzi na maendeleo ya watoto, mbunge Pius Ngeze hakuwa na tatizo muhimu la waliovijijini isipokuwa kupanda kwa bei ya kondom. Kama kweli kuna wenye uchungu na maisha ya vijana kwa nini kusihamasishwe kuwahangia wasio na cha kuolea waoe na kupewa cha kuanzia maisha.
Zinajengwa hoja kuwa wakati umefika wazazi wasione haya kuwagawia kondom watoto na kuwaeleza mambo ya kujamiiana. Waziri Paul Kimiti anasema "Tuachane na dhana potofu kuwa mtu akipata UKIMWI kuwa ni malaya na muhuni".
Imekuwa ikitolewa mifano kuwa kwenye watu kumi walioambukizwa virusi, tisa huambukizwa kwa njia ya kujamiiana. Mume asiyemzinifu hawezi kumwambukiza mkewe, na mke siyemzinifu hawezi kumwambukiza mumewe na mtoto aliyetumboni.
Kusema haki kwa kauli na vitendo kunahitaji jitihada za makusudi. Ni rahisi sana kwa mtu kuona makosa ya wengine na kuweza kuonesha udhaifu wao, akashindwa kuona uzuri na wema walionao.
Urahisi hutokea pale mtu anapotaka kujikweza na kujiona bora kimaadili mema na uwajibikaji kuliko wengine. Hivyo huongea na kutenda dhidi ya wengine bila ya kutafakari kwa kina.
Tabia hii hujitokeza kwa mtu binafsi na kuwaambukiza wengine kwa njia ya kuiga, kufunzwa, au kuzoeshwa. Hivyo huweza kuona kikundi cha watu wanaodhihirisha tabia inayolingana utadhani ni urithi wa kijenetiki (genetic inheritance).
Viongozi wa chama tawala wamekuwa mstari wa mbele kunadi kwa tahadhari kuna vyama vya siasa vinavyohubiri chuki, udini, na fitna vyenye dhamira ya kumwaga damu na kuvuruga amani ya nchi.
Lakini kwa msingi wa dini viongozi hao hawakusita kushabikia uchochezi wa Paroko wa Kanisa Katoliki. Wakijua fika kuwa katiba wala sheria za nchi haziruhusu mauwaji, wakaruhusu polisi kuvamia msikiti na kuuwa Waislamu kwa kuwapiga risasi.
Wakati wao wamemwaga damu za wananchi kinyume cha sheria, wanahubiri kuwa wenye sera ya "jino kwa jino" watavuruga amani na utulivu ambao CCM wanadai kuwa ndio muhimili.
Kwa mujibu wa maana mojawapo ya "jino kwa jino" ni kwamba aliyeuwa pasipo haki na auwawe. Ni sababu ipi iliyoisukuma Serikali ya CCM iseme "jiwe kwa risasi". Kuna Muislamu aliyemlipua risasi polisi ikaipelekea kusema jiwe kwa risasi?
Likizingatiwa hili, ni watu na sera za chama gani zisizofaa zinazostahiki kuepukwa na wananchi. Wale wanaowataka raia wajibu mapigo kwa askari wanaopiga wananchi bila ya haki au wale wanaoshabikia kauli za Maaskofu na kuruhusu apigwe risasi mwenye kurusha jiwe?
Kwa upande mwingine ni vigumu sana kwa mtu kuona kosa. Inamwia uzito kugundua udhaifu wake alionao ambao wengine wanaushuhudia katika kauli na matendo yake.
Mithili ya ukimwi, tabia hii huambukizwa, hasa watu waliopamoja. Unaweza kushangaa kuona kundi la watu mia au zaidi wakasema na kutenda katika mkondo mmoja wa tabia.
Mara nyingi tunawasikia na kuwaona au kusoma nukuu za maneno ya viongozi waliopo madarakani wakitaka waaminiwe kuwa utendaji wa maamuzi yao unazingatia sheria na katiba.
Makeke ya kauli zilizofumwa kiufundi zinapingana na utendaji wao. Kuna kupwaya na udhaifu uliowazi zinaonyesha mfarakano baina ya dhamira nzuri za kimaneno na matendo.
Hebu jaribu kuvuta fikra! Ni kipengele kipi cha katiba au sheria walichotaja viongozi wa Serikali ya CCM kilichowakwamisha wasiwafanyie kweli waliohusika na mauwaji? Kuna sheria inayoruhusu kumwua mwananchi asiye na hatia? Au polisi akiuwa hapaswi kufikishwa mahakamani!
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |