Rais wa Bosnia kujiuzulu

"LENGO letu ni: kuwafanya Waislamu waufuate Uislamu wao kwa vitendo. Mbinu yetu: Kuamini na kujitahidi kadri ya uwezo wetu. Hii ni kauli ya Alija Izetbegovic katika nyaraka aliyoiita "Islamic Declaration", iliyotolewa mnamo mwaka 1970.

"Ewe Elija, Ewe Mheshimiwa! Unaiendesha mbio Amerika!" Hii ni moja ya beti toka katika shairi la Kiarabu lililoandikwa na Mujahadeen wakati wa vita vya Bosnia.

Wiki iliyopita, Alija Izetbegovic alitangaza uamuzi wake wa kujiuzulu kama Rais wa Bosnia. Mtu huyu ambaye wa-Bosnia kwa mapenzi makubwa humuita "Deedo" au babu, ataachia rasmi kazi ya Urais mwezi Oktoba mwaka huu.

Katika hotuba yake ya kutangazaa kujiuzulu, Izetbegovic alitaja matatizo ya afya kuwa ndiyo sababu kubwa ya uamuzi wake, lakini pia aliongeza maneno haya: "Jumuiya ya Kimataifa inalazimisha mambo fulani hapa Bosnia... lakini inafanya hivyo kwa gharama na mhanga wa umma wa Kiislamu. Nahisi hii si haki", alisema. "Haya ni mambo ambayo siwezi kuishi".

Kujiuzulu kwa Izetbegovic ni tukio ambalo Waislamu ulimwengu mzima ni lazima walitafakari. Yeye ni mmoja wa viongozi wa kisiasa wa Kiislamu wachache wa wakati huu ambaye amethibitisha kwa kauli na vitendo vyake jinsi alivyo na mapenzi na Uislamu, na historia ya harakati zake inatoa mafundisho ya jinsi nchi za Magharibi zinavyowatazama Waislamu wa Ulaya na jinsi zinavyokabiliana na wanaharakati wa Kiislamu waliopo madarakani.

"Je, tunataka ummah wa Kiislamu uepukane na utengano wao, kujitegemea kwao, kuwa kwao nyuma kimaendeleo na umaskini?", alipata kuandika Izetbegovic. "Basi sisi tunaonesha wazi njia ipi itakayotufikisha katika lengo hilo, nayo ni kuusimamisha Uislamu katika kila nyanja ya maisha, kuanzia kwenye maisha ya mtu binafsi, katika familia na jamii nzima... na kuweka ummah wa kipekee wa Uislamu toka Morocco hadi Indonesia".

Kwa Izetbegovic haya hayakuwa maneno matupu, ulikuwa ni mpango kamili wa vitendo ambao alijaribu kuutekeleza katika maisha yake yote.

Mwaka 1940, akiwa na umri wa miaka 19, yeye na wenzake walianzisha jumuiya waliyoiita "Vijana wa Kiislamu", ambayo ilikuwa ni ya kisiasa na kidini pia wakifuata mfano wa Ikhwan Al-Muslimin ya Misri. Miaka 6 baadaye yeye na rafiki yake Nedzib Sacirbey walifungwa na serikali ya Kikomunisti ya Yugoslavia kwa kusaidia kuchapisha jarida lililoitwa "Mujahid".

Baada ya kuachiwa, Wakomunisti walipitisha msako mwingine dhidi ya vijana wa Kiislamu na mnamo mwaka 1949 waliwahukumu wafuasi wanne adhabu ya kifo na kuwafunga wengine wengi kutokana na harakati zao za Kiislamu. Mwaka 1983 Izetbegovic alikamatwa tena kwa kueneza kile kilichoitwa propaganda ya Kiislamu na kuhukumiwa kifungo cha miaka 14 jela hadi alipoachiwa mwaka 1988.

Haiyumkiniki kwamba mtu huyu angepata kuwa Rais wa nchi ya Ulaya siku moja. Lakini mnamo mwaka 1990, Izetbegovic alichaguliwa kuwa Rais wa Bosnia na Herzegovina kufuatia kumalizika vita vya nchi yake vinavyotolewa mfano wa Daudi na Goliath, dhidi ya Yuguslavia na Croatia.

Badala ya kufunga virago vya yeye na familia yake kuikimbia nchi baada ya kuvamiwa na kuzidiwa kivita, kama walivyofanya viongozi wa nchi moja ya ghuba hivi karibuni, yeye alibaki kuwaongoza watu wake katika vita vyote akiwa katika ofisi yake iliyozungushiwa magunia ya mchanga. Kwa kufanya hivyo, akaondokea kujulikana duniani kama alama ya mapambano ya kujinusuru kwa watu wa Bosnia dhidi ya mauaji ya maangamizi dhidi yao.

Izetbegovic aliongoza jeshi ambalo liliweza kulirudisha nyuma kwa kipigo kikali jeshi kubwa mara kadhaa lililoundwa na askari kutoka Croatia na Serbia. Lakini ameacha urithi mwingine mkubwa. Kwa wa-Bosnia alifanikiwa kuwafanya wasione aibu kuwa Waislamu. Katika Yugoslavia, kwenda Msikitini mara kwa amra kulimaanisha kwamba mtu angepoteza kazi katika nchi hiyo ambayo uchumi wake ulitawaliwa na chama cha Kikomunisti. Uislamu uliandikwa vibaya katika vitabu ya historia, na wanafunzi wa Kiislamu waliojitahidi kutimiza maamrisho ya dini yao waliambulia kupata maksi ya chini darasani bila kujali wangesoma na kujitahidi kwa namna yoyote ile.

Hata maneno ya Kiarabu na Kituruki ambayo hupatikana kwa wingi katika lugha ya Ki-Bosnia , makusudi yaliondolewa kwa hoja kwamba "Si ya kistaarabu'.

Lakini "Alija Izetbegovic alifanikiwa kuwaunganisha Waislamu wa Bosnia kama taifa moja", amesema Dk. Zundija Adilovic ambaye ni profesa wa Chuo Kikuu cha Kiislamu kilichopo Zenica kumueleza mwandishi wa makala hii. "Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Waislamu kupata fursa ya kutawala katika Bosnia".

Kwa kutumia fursa hiyo, Rais alitia mkazo sera ya kufufua utamaduni wa Bosnia. Leo hii watoto wanajifunza dini yao katika shule za serikali, wafanyakazi wa serikali, wafanyabiashara, askari na wanafunzi wa vyuo vikuu wanaweza kutekeleza Uislamu wao waziwazi. Muumini ndani ya Msikiti uliojaa wa Sarajevo anaweza kusali bega kwa bega na meya wa jiji.

Izetbegovic na msimamo wake thabiti wa kuitetea dini yake na kwa kutumia nguvu yake ya kisiasa bila kuyumba, alizifanya nchi za magharibi zikose raha. Huku kukiwepo hofu ya kile kilichoitwa, kuwepo kwa taifa la itikadi kali ya Kiislamu ndani ya Ulaya, Marekani na Jumuiya ya Ulaya zilisimama pembeni na kuruhusu mauaji ya halaiki ya Waislamu wa Bosnia kwa kipindi cha miaka mitatu. Mwaka 1995 wakati vikosi vya jeshi la Bosnia vilipoanzisha kampeni kali ya kijeshi iliyopeleka kukombolewa asilimia 30 ya eneo lililotekwa na Waserbia tena kwa muda wa siku chache tu, ikaonekana kwa nchi za magharibi kwamba wasije Waislamu kushinda vita hivyo haraka haraka Marekani na nchi za Ulaya zikatoa wito wa kusitishwa mapigano.

"Mpango wa amani" ulioundwa na kusimamiwa na Marekani na kulazimishwa utekelezaji wake kwa kuingizwa majeshi ya NATO Bosnia, ulipelekea kuifanya Serbia izawadiwe taifa lao wenyewe lenye ukubwa upatao nusu ya eneo la Bosnia, wakati ambapo Wacroatia waliambuliwa robo ya eneo hilo.

Mpango huo wa Marekani uliwaacha Waislamu, ambao ni nusu ya idadi ya wakazi wa Bosnia, kufungiwa ndani ya robo iliyobakia katika eneo la nchi yao.

Mpango wa amani wa Marekani uliunda mfumo wa serikali katika Bosnia ambao kwa hakika ulilenga kufifiza maendeleo ya Waislamu kiuchumi na kisiasa na pia kuwadhoofisha katika maamuzi yao ya kisiasa.

Waserbia, Waislamu na Wacroatia kila moja katika makundi haya ana sauti sawa katika "Urais" wa Bosnia unaoundwa na watu watatu, licha ya kwamba Waislamu ndio wengi zaidi. Kama kweli nchi hiyo ingekuwa ya "kidemokrasia" halisi kwa kila raia kuwa na "sauti" sawa basi kwa hakika Waislamu walistahki kuongoza kwa minajili ya wingi wao. Na katika mfumo uliopo, serikali inatoa maamuzi kwa njia ya "muafaka" wa "marais" wote watatu. Na kwa jinsi ambavyo Waserbia na Wacroat walivyopania kuwagandamiza Waislamu katika kila namna, muafaka mara zote haupatikani, na kwa hali halisi, utawala halisi wa Bosnia, unafanywa na jumuiya ya Ulaya.

Mwandishi wa makala hii alimuuliza Nedzib Sacirbey, balozi anayeiwakilisha Bosnia kimataifa na ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Izetbegovic toka walipokuwa vijana, kwamba Izetbegovic alikuwa akimaanisha nini aliposema, "Jumuiya ya kimataifa inalazimisha mambo fulani hapa Bosnia ... kwa gharama na mhanga wa ummah wa Kiislamu".

" Pingamizi namba wani ni kuwa jumuiya ya Kimataifa haikutumia uwezo wake kuwarudisha wakimbizi katika maeneo yao ili kujenga jumuiya ya watu wa asili zote", alijibu Sacirbey. "Kwa mfano, huko Banja Luke, Waserbia waliharibu Misikiti yote lakini sasa ni miaka mitano baada ya vita, na bado hakuna ruhusa kujenga hata msikiti mmoja. Hali ndivyo ilivyo pia kwa upande wa Croatia".

Kushindwa kwa jumuiya ya Ulaya kuwarudisha wakimbizi wa Kiislamu katika maeneo ya Bosnia, ni sawa na kusaidia lengo la vita hivyo ambalo lilikuwa kuwangamiza Waislamu. Wakati huo huo Waserbia na Wacrotia wako huru kusafiri na kuishi maeneo ya Waislamu kwa uhuru.

Katika safari ya mwandishi wa habari hii aliyoifanya kwenda Mostar, jiji lililogawanywa nusu kwa Waislamu na Wacroatia alipata fursa ya kuongea na wakazi wa maeneo ya mawili, mama mmoja alipoulizwa iwapo anapata woga kusafiri kwenda upande wa Waislamu alijibu kwamba, "Hapana, nakwenda huko mara nyingi kununua bidhaa na kumtembelea binti yangu".

Kwa upande mwingine, Wacrotia kadhaa walisema kwamba hawataki Waislamu kuja maeneo yao, na Waislamu wengi walisema kwamba wamebughudhiwa na kupewa vitisho vya kudhuriwa kila mara wanapovuka mto unaoutenganisha jamii ya hizo mbili.

Marekani na jumuiya ya Ulaya, hata hivyo wanatumia uwezo wao kukidhi kwa makusudi chama kinachoongozwa na Izetbegovic cha Party for Democratic Action (SDA) na kukipigia debe chama cha zamani cha kikomunisti cha Bosnia ambacho kilipewa jina la Social Democrat Party (SDP). Wakiwa wamechoshwa na ukosefu na maendeleo ya uchumi, kundi kubwa la wapiga kura Waislamu wa Bosnia waliamua kukiunga mkono chama cha Kikomunisti cha SDP katika uchaguzi mdogo wa hivi karibuni. Hata baada ya kubainika kwa ukweli kwamba Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa msaada wa hali na mali kwa kampeni za SDP lakini hii haikuonekana chochote.

Na wakati huo huo, Wolfgang Petritsch, kiongozi wa jumuiya ya Ulaya anayeshughulikia mamlaka ya uraia ndani ya Bosnia, alitoa wito kwa wapiga kura kutowachagua "viongozi waliotokana na vita", ambapo Izetbegovic ndiye pekee aliyebakia.

Na jumuiya ya Ulaya ilitoa matangazo ya televisheni katika kituo wanachokiendesha kuwahimiza watazamaji wake kupiga kura ya "mabadiliko" au kwa maneno mengine "wabadilishe uongozi unaopingana na chama cha Kikomunisti".

Kwa kutumia kauli za kinafiki, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inasimulia matokeo ya juhudi yake hii kuwa ni ushindi wa "mfumo wa vyama vingi... kwa gharama ya vyama vya kitaifa viliopo madarakani". Sacribey kama mtu yeyote asiyependelea upande wowote, anasema kwamba hii ni kuingilia taratibu za demokrasia. "Tunawategemea wao waseme, "tumia haki yako ya kupiga kura, chagua kiongozi bora", na sio, "mpigie kura huyu na usimpigie kura huyu", alisema Sacirbey.

Waislamu wanasababu nyingi kukiogopa chama cha SDP. Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tuzla miezi miwili iliyopita, wanachama wa SDP walifanya karamu ya nyama ya nguruwe ili kuonesha kwa vitendo 'usekula' wao. Na wametangaza azma yao ya kubadili jina la barabara kuu katika eneo lenye kudhibitiwa na Waislamu la Zenica na kuipa jina la dikteta wa zamani wa kikomunisti wa Yugoslavia hayati Tito. Vile vile inaripotiwa kwamba kundi la wakereketwa wa chama hicho juzi waliupopoa kwa mawe Msikiti.

Mengi katika matatizo tunayopata katika ulimwengu wa Kiislamu, ambayo huwa tunatoa lawama kwa wengine, kimsingi wa kulaumiwa huwa ni Waislamu wenyewe lakini hali ni tofauti Bosnia. Katika njama hizi za kimataifa zinazolenga kuwadhoofisha na kufifiza maendeleo ya Waislamu Bosnia, Alija Izetbegovic ameamua kwamba yeye hana tena nguvu ya kuendelea. "Lazima aje mtu mwingine atakayekabiliana na matatizo haya", alisema.

Maafa ya Bosnia siyo tu yalihusu vifo vya wanaume, wanawake na watoto wapatao 350,000 pekee ambao walikufa kwa sababu tu majirani zao waliwachukia sana kwa kuwa ni wa dini tofauti na yao au kwa kuwa wanawake kwa maelfu walibakwa wakati wa vita. Je maafa haya yanasema nini kuhusu ustaarabu wetu, kwamba wanasiasa wa Marekani na Ulaya walikuwa na uwezo wa kuzuia mauaji ya Waislamu lakini wakachagua kutokufanya lolote?

Vile vile maafa haya siyo tu yanatoa ujumbe kwamba maisha ya Waislamu hana thamani kwao. Kushindwa kusimamisha mauaji ya kuangamiza dhidi ya Waislamu pamoja na tabia inayooneshwa na nchi za magharibi baada ya vita vya Bosnia, vinatoa ushahidi kwamba mauaji ya kuwangamiza yanaweza kuvumiliwa ili kufikia lengo la kisiasa, na lengo hili ni kuzuia kuibuka taifa la Kiislamu katika Ulaya. Fundisho kwa Waislamu hapa ni kwamba zama hizi ambapo demokrasia inatajwa kwa maneno matamu, ifahamike kuwa Marekani na Ulaya, propaganda yao ya "kujenga demokrasia" mara zote inazidiwa na hofu yao kubwa dhidi ya Uislamu.

Lakini licha ya maafa ya mauaji ya maangamizi na usaliti wa nchi za magharibi, Izetbegovic amepata ushindi. Aliiongoza Bosnia kupata uhuru toka Yugoslavia na kuwa taifa linalojitawala. Alijenga jeshi kuwalinda watu wake. Aliongoza harakati za kuujenga upya Uislamu katika Bosnia, huku akilinda haki za Wakristo katika maeneo yaliyokuwa chini ya mamlaka yake. Kwa jambo hili tunamshukuru na kumtakia kila la kheri.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook