Kigogo ni namba wani
1. Kwa ubabe namba wani, kwa ujanja namba wani,
Kwa uongo namba wani, kwa rushwa ni namba wani,
Kwa ngojera namba wani, kwa taarabu namba wani,
Wala hana mpinzani, kigogo ni namba wani.
2. Masikini namba wani, kwa kuuza namba wani,
Mbali na yote madini, Mwadui na Mererani,
Ushuru wa Bandarini, na ule wa mipakani,
Wala hana mpinzani, kigogo ni namba wani.
3. Enenda hospitalini, dawa hamna wodini,
Mia moja hamsini, milioni nabaini,
Kwa gari ya kampeni, TOT yende mikoani,
Wala hana mpinzania, kigogo ni namba wani.
4. Miaka arobaini, mekaa madarakani,
Hivi hamjabaini, raia wataka nini?
Nyimbo za TOT za nini? raia wamo shidani,
Wala hana mpinzani, kigogo ni namba wani.
5. Mashimo barabarani, hayazibwi asilani,
Ila aje namba wani, hapo ndipo ahueni,
Au ije kampeni, karibu uchaguzini,
Wala hana mpinzani, kigogo ni namba wani.
6. Mia nane hamsini, milioni shangaeni,
Kutumika msibani, kwenye nchi masikini,
Na raia wa jijini, maji ni ya visimani,
Wala hana mpinzani, kigogo ni namba wani.
7. Nawaombeni jamani, mijini na vijijini,
Wakija wazomeeni, TOT isiwazugeni,
Shere inawachezeni, kuwafanya punguani,
Wala hana mpinzania, kigogo ni namba wani.
8. Wakifika ondokeni, enendeni mashambani,
Na wengine viwandani, sokoni na magengeni,
Mazao kazalisheni, njaa itawauweni,
Wala hana mpinzani kigogo ni namba wani.
9. Vyuoni na mashuleni, elimu kimbilieni,
Kudanganywa kataeni, na nyimbo za namba wani,
Lakini jitokezeni, kwa wingi uchaguzini,
Wala hana mpinzania, kigogo ni namba wani.
10. Nasimama kituoni, beti kumi nasaini,
Chunguzeni gazetini, mengi tawaleteeni,
Hadi huyu namba wani, atoke madarakani,
Wala hana mpinzania, kidogo ni namba wani.
Bakari K.M.
Morogoro.
Ni Ngangali!
1. Haki sawa ni Ngangali, wengi tumeshuhudia,
Wameuacha ugali, uwanjani wamejaa.
Jua lilokuwa kali, sawa walijionea
Lipumba, Sharifu kweli, watikisa Tanzania.
2. Haki sawa ni Ngangali, hata kwenye kupokea,
Imegwaya Serikali, hili nawatobolea,
Wanakusanya faili, safari imewadia,
Lipumba, Sharifu kweli, si watu wa kuchezea.
3. Haki sawa ni Ngangali, mmeonyesha dunia,
Twaonewa kwelikweli, tumechoka Tanzania,
Mmedhamiria kweli; utawala kuung’oa,
Ndugu Lipumba Ngangali, mkombozi Tanzania.
4. Haki sawa ni Ngangali; mwito mmewatolea,
Mmechoka ufedhuli, mwataka kujikomboa,
Muilete afadhali, dhulma kuiondoa,
Sharifu yetu dalili, Visiwani kukomboa.
5. Haki sawa ni Ngangali, nani asojionea,
Yanayosemwa makali, nchi wanaichambua,
Hizi mbaya zetu hali ,CCM mekusudia,
Lipumba, Sharifu kweli, yafaa kuwachagua.
6. Haki sawa ni Ngangali, CCM wanajua,
CUF inastahili, kuongoza Tanzania,
Ule wao ukatili,kikomo umefikia,
Lipumba, Sharifu kweli, ni weupe waso doa.
7. Haki sawa ni Ngangali, wito ninawatolea,
Fitina msizijali, muongeze ushujaa,
Muwabane kweli mwili, washindwe pata pumua,
Lipumba wabane kweli, CCM tutang’oa.
8. Haki sawa ni Ngangali, shime mbele angalia,
Siku itapowasili, Ngangali ihamishia,
Kwa mistari miwili, shahada kuzichukua,
Lipumba uwe awali, nasi tunafuatia.
9. Haki sawa ni Ngangali, kura zenu jilindia,
Lije chatu janamwali, kosovo liangushia,
Hata mkipewa wali, sanduku ling’ang’ania
Sharifu wambie kweli, Ngangali yanichengua!!
10. Haki sawa ni Ngangali moto usiopoa,
Naomba hiyo Ngangali, nguvu kuiongezea,
Muishike Serikali, wanyonge kuwakomboa,
Lipumba, Sharifu kweli ,dua ninawaombea!
K. S. Luanda (Nolo)
Dar es Salaam.
Leo imefika mwaka
Assalamu alayka, ewe baba yetu mwema,
Leo imefika mwaka, wanao kuwa yatima,
Dunia kuiepuka, roho yako kuitema,
Leo imefika mwaka, baba yetu kututoka.
Tarehe tukihesabu, sasa imefika mwaka,
Tunamuomba Wahabu, Mwenyezi Mungu Rabuka,
Akuondolee tabu, adhabu na hekaheka,
Leo imefika mwaka, baba yetu kututoka.
Mtu akikumbuka, huwa akitwi Twalibu,
Jina limebadilika, Si Ally wala Yakubu,
Marehemu wasifika, kwa mabibi na mababu,
Leo imefika mwaka, baba yetu kututoka.
Kila ninapokumbuka, ninashindwa kuamini,
Lakini nafarijika, nisomapo Qur’ani,
Alishasema Rabuka, kwake ni marejeoni,
Leo imefika mwaka, baba yetu kututoka.
Daima nakukumbuka, kukusahau siwezi,
Moyo unasononeka, lakufanya hauwezi,
Nabaki nahuzunika, namkumbuka Mwenyezi,
Leo imefika mwaka, baba yetu kututoka.
Ewe Mwenyezi muweza, baba yetu mnusuru,
Umuondolee giza, nakumjalia nuru,
Iangaze mwangaza, iwe kinga na nusuru,
Leo imefika mwaka, baba yetu kututoka.
Muondolee adhabu, na madhila ya kaburi,
Yaliyomema majibu, kwa Munkar na Nakiri,
Kwa fasaha ayajibu, aweze kupata kheri,
Leo imefika mwaka, baba yetu kututoka.
Na Ukhii Fatmah Twalib Zahor
Jamiat Zahraa (a.s.)
Sare Salariya,
Box 37139,
Qum-Iran.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |