Mufti Hemed eleza yako,
CCM watajitetea wenyewe
"SISI twaumwa siku zote. Lakini ndani ya Tanzania yetu, hospitali zote kubwa za rufaa, zote za Wakristo. Hata hiyo Muhimbili, waganga wakubwa wote Wakristo".
Hayo yalikuwa maneno ya Mufti wa BAKWATA, Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed akiongea na Masheikh wa BAKWATA huko Shinyanga.
Mufti aliyasema hayo akisherehesha kauli yake ya awali kuwa Waislamu hawajakuwa na uwezo wa kuongoza ulimwengu.
Mufti hakuishia hapo, bali akawalaumu aliowaita wakarimu wa Kiarabu kwamba hawajajenga hospitali.
Tunadhani Mufti angewasaidia zaidi Waislamu kama angejibu na kutoa maelezo juu ya maswali yafuatayo:
Ni kwanini Waislamu hawana hospitali za rufaa. Yeye akiwa kiongozi mkuu wa Baraza linalojiita la Waislamu na kama anavyojiita Mufti na Sheikh Mkuu kafanya nini juu ya tatizo hilo.
Mali za Waislamu zilizoporwa toka EAMWS wakakabidhiwa na serikali toka mwaka 1968 wamezifanyia nini.
Kwanini serikali iliifuta EAMWS ikataka iundwe BAKWATA ya Kiafrika yenye bendera nyeusi (mpaka leo) kuonesha uzalendo.
Je, Uislamu una uzalendo wa kitaifa na ukabila?
Je, Wakristo nao walifutiwa vyama vyao na kukatiwa mawasiliano yao na Wajerumani, Wataliano, Wadanish na wengineo!
Je, Mufti Hemed anajua ni hospitali ngapi, vyuo na miradi mingapi ya uzalishaji mali imeanzishwa na Benki ya Maendeleo ya Kiislamu (IDB) na OIC sehemu mbalimbali duniani?
Anaweza kueleza ni kwanini serikali ya CCM haitaki Tanzania ijiunge na OIC, lakini haioni dosari kuwepo ubalozi wa Vatican!
Katika maelezo yake, Sheikh Hemed alidai pia kuwa watu wanaoambizana wasiipe kura CCM, wanafanya hivyo kwa chuki za kidini.
Lakini nani kamwambia Sheikh Hemed CCM ni ya Wakristo.
Kwenye CCM yupo Dk. Omar Ali Juma, Yusuf Rajab Makamba, Ali Ameir Mohamed na wengineo.
Kama suala ni dini, basi Waislamu wasingempokea Nyerere, na Tanzania ya leo ingekuwa nyingine kabisa.
Sisi tunaamini CCM wenyewe wanajua, kwanini watu wamefikia hatua ya kutangaziana wasiipe kura.
Inajua serikali yake ilivyoshiriki mauaji ya Waislamu Mwembechai kwa shinikizo la Paroko Lwambano.
Inajua jinsi vyombo vya dola vya serikali yake vilivyowadhalilisha akinamama Waislamu baada ya kuwatoa ndani ya Msikiti.
Inajua pia jinsi Mzee Abdallah Chatta Kidagaa alivyoteswa na kufa baada ya kuachiwa.
CCM haina majibu juu ya dhulma hii. Ilitaka kuzitoa kafara baadhi ya Balozi za nje ikakwama. Ikataka kuwaparamia wafanyabiashara na yenyewe ikaona haya.
Lakini inajua pia jinsi waumini wanavyokamatwa na kunyanyaswa kila leo kwa visingizio mbalimbali.
Mufti kutolewa kafara kuleta propaganda kuwa watu wanaikataa CCM kwa sababu za chuki za dini ni salamu kutoka CCM kuwa haipo tayari kuondoa dhulma.
Sisi tunasema, propaganda haziondoi dhulma. Na penye dhulma hapawezi kuwa na salama na amani ya kudumu.
Alijisemea Mshairi, heri vijogoo vinavyoinukia vyenye hamu ya kuwika hata usiku wa manane, kuliko shari ya jogoo kongwe chimvi.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |