Mufti awajia juu wasemao CCM isipewe kura Okt.
MUFTI wa BAKWATA, Sheikh Hemed bin Jumaa ametahadharisha juu ya kauli kuwa CCM isipewe kura.

Ametoa tahadhari hiyo akizungumza na viongozi wa BAKWATA mkoani hapa katika ukumbi wa Rehema Hall, Bar & Guest House wiki iliyopita.

Amesema, mama mmoja huko Dodoma aliwahi kuwaambia Waislamu kura zote wasiipe CCM.

Sheikh Hemed amesema, kauli kama hiyo ni ya hatari.

"Woga wangu ni kuwa nao wataambizana katika faragha zao kwamba jamani ndugu Wakristo tufanyeni chini juu mpaka tuhakikishe kwamba Ikulu hakai tena Muislamu", ametahadharisha.

Aidha, Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed amesema, ni upotofu kutaka Wabunge au Rais Muislamu.

Amesema, ukimpa Muislamu Urais, atalazimika kusaidia maasi. Amesema Rais ataitwa kufungua kiwanda cha Bia, atakwenda amsimike Askofu wao. Na hivyo kusaidia uovu.

Hata hivyo, akasema, ni wajibu Waislamu kumtii Rais atakayechaguliwa. "Rais yeyote atakayekuja kwetu sisi Waislamu ni wajibu wetu kumtii. Mtume amesema, mtiini kiongozi wenu hata kama ni mtumwa wa Kihabeshi", alinukuu Hadith ya Mtume.

Sheikh Hemed ameyaeleza hayo akidai kuwa amewasikia baadhi ya watu wakihimizana wachague Muislamu.

Akitumia mfano huo amesema, Wabunge watakaochaguliwa watatunga sheria ambazo si za Kiislamu.

Katika kutoa tahadhari hiyo akasema kuwa jambo hilo laweza kuzaa balaa kama la Nigeria.

Hata hivyo Mufti alisema kuwa Waislamu hawajawa na uwezo wa kuongoza nchi.

Amesema, hospitali zote kubwa za Rufaa ni za Wakristo, na hata Muhimbili madaktari wote wakubwa Wakristo. Akawashutumu wafadhili wa Kiarabu kuwa hawajawajengea Waislamu hospitali.

Aidha, amesema, hakuna wataalamu Waislamu kiasi kwamba kesi zao hupelekwa kwa Majaji Wakristo

Kuhusu siasa, habari zinaeleza kuwa Mufti aliwataka mashehe wa Bakwata wasimruhusu mtu yeyote kuhubiri siasa misikitini.

Amesema, Msikiti ni mahala pa ibada tu na kwamba Mtume amesema: Maneno ya kidunia Msikitini yanakula mema kama moto unavyokula kuni.

Jambo jingine alilosisitiza Mufti ni kuwa Bakwata si la wana Bakwata pekee bali la waislamu wote wa Tanzania wapende wasipende maana pamoja na kuwepo vyombo vingine lakini serikali inaisikiza Bakwata pekee.

Amesema, tokea mwanzo Nyerere aliona taabu kuzungumza na vyombo 120 vya waislamu. Akavivunja vyoote na kuunda chombo kimoja tu. Kwa hiyo watu mashuhuri wakakusanyika mjini Iringa kuunda Baraza la waislamu wa Tanzania Bara.Amesema, walikuweko Mzee Karume, Sheikh Thabit Kombo, Mzee Kawawa na viongozi wengine waliokuwa na nyadhifa zao serikalini wakati huo. Basi ikaundwa Bakwata ili serikali iwe na chombo kimoja tu cha kuwasiliana nacho.

Katika mkutano wake wa ndani, sheikh Hemed alianza kwa kukanusha shutuma kuwa yeye yuko katika ziara ya kuipigia kampeni CCM."Mimi sikuja kupiga kampeni kama wanavyodai jamaa hawa. Kuna watu wana chuki tu na mimi", amesema

Katika mkutano wake na waumini nje ya Msikiti Mkuu, Sheikh Hemed alizungumzia hekaya ya vijogoo vidogo vinavyowika ovyo.

Hekaya hizo ziliwaelekeza wasikilizaji wayathamini na kuyaenzi majogoo makongwe na sio vijogoo vinavyoinukia sasa.

Kabla ya mkutano huo uliofanyika Juni 19, matangazo yalitolewa kupitia gari Na. TZN 3097 Pick-Up yakiwataka watu wote waende kumsikiliza Mufti.

Awali, Mufti alifika Shinyanga na kurejea Dar es Salam ghafla.

Taarifa za uchunguzi zinaeleza kuwa Mufti alipokuwa njiani kuja Shinyanga, Mkuu mmoja wa serikali Mkoani alifika ofisi za Precision Air na kutoa amri kuwa vyovyote itakavyokuwa aachiwe nafasi moja kwa ajili ya mtu wake.

Baadaye ilikuja kufahamika kuwa mtu huyo alikuwa Mufti. Haikuweza kufahamika ni kwanini alitakiwa arejee Dar es Salaam haraka.

Walipoanza ziara zao masheikh hawa walikuwa wanaongea kampeni za uchaguzi ndani ya Misikiti hata Sheikh mmoja kudiriki kuitaja CCM na Rais Mkapa wazi wazi msikitini.

Baada ya Sheikh Hemed kurejea Dar es Salaam, mwelekeo mpya umejitokeza.

Maelekezo juu ya uchaguzi hutolewa katika vikao vya ndani vya viongozi wa Bakwata ambao hupewa jukumu la kuwaendea waumini.

Kutoka Shinyanga, Mufti alikwenda Bukoba na Mwanza.


Kushangilia kwa kuitaja CCM kwapingwa Yanga

MTINDO wa baadhi ya wapenzi wa Yanga kushangilia timu yao inapokuwa uwanjani kwa kuitaja CCM huenda ukazusha mgawanyiko miongoni mwa wapenzi wa Klabu hiyo.

Imedaiwa na wapenzi wengi wa timu hiyo kuwa ushangiliaji huo umepitwa na wakati na hauna maana yoyote katika mazingira ya sasa.

Aidha, wapenzi hao wamesema, Yanga ilikuwa na mahusiano ya karibu na chama cha TANU sio CCM kama inavyodhaniwa na watu wengi.

Wapenzi hao wamedai kuanzishwa kwa timu hiyo na watani wao Simba miaka ya 30 ilikuwa ni katika harakati za watanganyika kutaka kujikomboa, harakati zilizokuja kufikia ukamilifu wake kwa kuanzishwa chama cha TANU miaka ya 50.

Timu ya Yanga na Klabu ya Taarabu ya Egyptian kwa upande mmoja, Simba na taarab ya Alwatwan kwa upande mwingine ni miavuli iliyotumiwa na Watanganyika kuasisi harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika kabla ya chama rasmi cha kisiasa.

Kufuatia kukasirishwa na wenzazo, tayari baadhi ya wapenzi wa Klabu hiyo walio wafuasi wa vyama vingine wameazimia kuanza kutumia 'slogan' za vyama vyao kushangilia timu yao itakapokuwa uwanjani.

Wapenzi wa Klabu hiyo waliozungumza na gazeti hili jana kufuatia pambano la timu yao na Klabu ya Simba, wamesema wamekasirishwa na wenzao waliokuwa wakishangilia kwa kuitaja CCM.

"Wengine sio wafuasi wa CCM, tuko vyama vingine na ni wengi kuliko wao, sasa na sisi tukianza kusema 'ngangari, ngangari' itakuwa matata kubwa", amedai Bwana Haji Ramadhani mkazi wa Ilala jijini.

Mzee Ali Abbas wa Kariakoo ambaye ni mmoja wa waasisi wa timu ya Pan iliyozaliwa kutokana mgogoro wa Yanga uliotokea mwaka 75, amesema wapenzi wengi wa vilabu vya Yanga, Simba na Pan African wako kambi ya upinzani wakihoji maendeleo ya nchi yao ikiwa ni pamoja na hali mbaya walizonazo wachezaji Star wa zamani walioiletea sifa nchi na kuporomoka kwa ujumla kwa soka ya Tanzania tofauti na ilivyokuwa miaka ya sabini.

"Wanaoshabikia Yanga kwa kuinasibisha na CCM hawajui historia ya Klabu hiyo na hawaelewi siasa ya nchi hivi sasa", amedai mzee huyo maarufu Kariakoo.

Aidha Kijana mmoja shabiki wa Simba amewakoga wapenzi wa Yanga kwa kudai kwamba kufungwa kwa timu yao kumetokana na mkosi wa kuitaja CCM.

Kijana huyo ambaye hakufahamika jina lake aliyatamka hayo nje ya msikiti wa Ubungo Darajani juzi jioni.

Hata hivyo, mkereketwa mmoja wa timu ya Yanga Bwana Omar Kambaya alidai katika mazungumzo hayo kuwa ni washabiki wa Simba waliokuwa wakitoa maneno ya kuwakejeli Yanga mojawapo likiwa ni kuwaita wao ni CCM.

Yanga ilipambana na Simba juzi katika mchuano wa ligi kuu Tanzania Bara, pambano lililokuwa na kila aina ya vijembe na kutambiana ambapo baadhi ya wapenzi walisikika wakishangilia CCM, CCM mchezaji mmoja machachari alipokuwa akiingia uwanjani kuchukua nafasi ya mchezaji mwingine.

Katika pambano hilo lililofanyika uwanja wa Taifa Jijini, Simba iliifunga Yanga mabao 2-1,Yanga ndio iliyotangulia kufunga katika pambano hilo na kulidumisha bao hilo hadi mapumziko.


Lipumba kufungua matawi kariakoo
MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba leo anatarajiwa kufungua matawi kadhaa katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi ofisi kwake, Katibu wa Jimbo la Ilala, Bw. Twahiri Abbas Sheshe amesema, jumla ya matawi 50 mapya yanatarajiwa kufunguliwa leo na Mwenyekiti wa chama hicho.

"Tulikuwa na matawi mengi sana ya kufunguliwa kama 50 katika jimbo letu hili katika Kata za Gerezani, Mchikichini, Kariakoo, Jangwani pamoja na Upanga Magharibi na Mashariki, kila kata ina matawi 15 lakini tutafungua matawi matatu matatu kila kata", amesema Sheshe.

Akieleza sababu za kutofungua matawi yote (50) amesema, ni kutokana na Profesa Lipumba kuwa na mkutano na akinamama siku hiyo hiyo (leo).

Aliyataja matawi yatakayofunguliwa na kata zake katika mabano kuwa ni Kibasila, Gerezani (Gerezani), Profesa Kighoma Malima, Mission Kota, Narung'ombe (Mchikichini), New Bosnia, Kariakoo mtaa wa Pemba, Amani na Utulivu ambalo ni Stawi la wazee lililopo Msimbazi polisi (Kariakoo).

Bw. Sheshe amesema, katika tawi hilo la wazee Profesa Lipumba atapumzika na kupata dua za wazee wa Kariakoo.

Aliendelea kuyataja matawi mengine yatakayofunguliwa kuwa ni Kariakoo, Mkunazini, Kingstone (Kata ya Jangwani). Katika kata ya Upanga Magharibi na Mashariki atafungua matawi ya Muhimbili, Tujitegemee, Kisutu pamoja na Kajiungeni.

Aidha, alieleza kuwa katika matawi hayo pia yalikuwemo ya chama tawala CCM ambayo yamegeuzwa kuwa matawi ya CUF baada ya wanachama wote wa matawi hayo kujiunga na CUF.

Amesema, shughuli hiyo itaanzia Gerezani saa sita.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook