CCM yadaiwa kuhusika kukamatwa waumini
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimedaiwa kuhusika na zoezi la kuwakamata baadhi ya waumini linaloendelea jijini.

Aidha, imedaiwa kuwa zoezi hilo linafanyika ili kuhakikisha Misikiti inaongozwa na watu wanaodaiwa kuwa watiifu kwa CCM.

Madai hayo yametolewa na mamia ya waumini waliokusanyika Masjid Ihsani(Urafiki) Ijumaa Juni 23.

Waumini hao wameilaumu polisi kwa kile walichodai kutumika kuwanyanyasa Waislamu kwa visingizio kadhaa.

Aidha, wametuhumu kuwa huenda kamata kamata hiyo inaendeshwa ili kuwakoseha Waislamu kujiandaa na uchaguzi.

"Hawa matendo yao Mwembechai yanawasuta. Wanaona kura hawana. Wanawataabisha mkate tamaa kuwang'oa", alisema muumini moja.

Muumini huyo Bw. Abdul amesema, "kamata kama hii itakuwa ni fursa nyingine ya kuwafikisha waumini Oktoba wakiwa na makovu mabichi ya dhulma mbali ya yale ya mauaji ya Mwembechai",

Amewataka waumini wasisikilize ahadi wala ilani ya uchaguzi. Bali kigezo chao cha kutoa kura kiwe mauaji ya Mwembechai, kukamatwa waumini wenzao na dhulma nyingine.

Imamu wa Msikiti huo Sheikh Omar Bashir aliwataka waumini kuwa na subra, na msimamo na kuwa tayari kuondoa dhulma.

Kauli hiyo iliungwa mkono na nasaha za Ustadh Salum aliyesema, iwapo waumini hawatakuwa tayari kujihami na kuilinda dini yao, wataendelea kukamatwa.

Mzee mmoja aliye katika wazee wa CCM alipohojiwa kuwa wanatumiwa na CCM kukataa uongozi uliowekwa na waumini, alifoka na kusema, "Sisi hatutaki watu wanaoleta siasa Misikitini hata kama watatuita vibaraka wa CCM", mzee huyo ambaye alikataa kutajwa jina lake gazetini amesema kuwa yeye ataendelea kutetea msimamo wa chama (CCM) wa kutochanganya dini na siasa.

Mamia ya waumini walifurika katika Msikiti wa Ihsan(Soko la ndizi) ijumaa iliyopita ili kujua hatma ya wenzao waliokamatwa na polisi.

Waumini wengine wamekamatwa katika Misikiti ya Tegeta na Manzese Uzuri.

Wote wanatuhumiwa kufanya fujo, kuharibu mali na kutishia kuua.


Wenye upeo mdogo wasipewe uongozi

WASOMI wa Kiislamu nchini wametakiwa kutowaachia watu wenye upeo mdogo na fikra finyu nafasi za uongozi katika jamii.

Aidha, wamepewa changamoto kutumia akili kuikomboa nchi toka katika dimbi la umaskini, maradhi na ujinga.Hali ambayo imeelezwa kuifanya jamii iishi chini ya nidhamu ya woga ikigubikwa na dhulma iliyopea mipaka.

Nasaha hizo zimetolewa na Mwalimu Ally Issa Ijumaa iliyopita wakati akihutubia kwenye Msikiti wa Chuo Kikuu (SUA) mjini hapa. Ustadh huyo aliwatanabaisha Waislamu kuwa macho na vita vya kiakili vinavyoendeshwa na maadui wa dini yao. Vita hivyo vimeelezwa kuwa uwanja wake wa mapigano ni bongo na silaha yake kubwa ikiwa vyombo vya habari.

"Vyombo hivi vimeacha kuzungumzia uhalisia wa mwenendo mbovu wa jamii chini ya utawala wa serikali ya CCM, ambapo rushwa imeota mizizi katika maeneo yote badala yake vinaelekeza nguvu zake kwenye mambo kama mashindano ya uzuri, rusha roho (mipasho) na mengineyo ya kupumbaza jamii", amesema.

Akisisitiza hilo, Ustadh Issa amesema, vyombo vya habari vimesahau kabisa kuzungumzia mzigo wa kodi unaowaumiza wanyonge, huku wachache wakifaidi jasho la wengi.

"Hebu tuangalie uwiano uliopo baina ya maendeleo ya kiuchumi na maendeleo ya kijamii. Ni aibu tupu. Lakini vyombo vya habari vinafumba macho", amesema na kuongeza "Ongezeko la kodi na pato la taifa vinavyoimbwa kila siku na watawala wa nchi hii haviendani kabisa na hali halisi ya maisha ya wanyonge; nani kaandika jambo hili? Tazama viwanda na wawekezaji wanaosamehewa kodi kila uchao, je, wanaongeza ajira ya kweli au vibarua wenyemalipo duni wasiolindwa na sheria za kazi? Nani kathubutu kuandika jambo hili? Angalia jinsi bidhaa zilivyojaa madukani na viongozi wa serikali ya CCM wanavyojivunia nazo, je, kuna uwezo wa kuzinunua? Nani kaandika hili?" Alihoji mwalimu huyo.

Aidha, amewahimiza kinamama na vijana waangalie hali zao na wasikubali kufanywa daraja la kupitisha watawala badala ya viongozi bora kwenye uchaguzi mkuu ujao.

"Uwezo wa mtu kujua alipo na kutazama aendako, unategemea uweza wake wa kuangalia atokako. Je, kinamama na vijana wa Kiislamu mnajua mtokako"? alihoji kwa msisitizo.

Wakati huo huo waumini wa Msikiti wa Kiwanja cha Ndege mjini hapa wametakiwa kuzingatia kwa makini kile alichoacha Mtume (s.a.w.) katika kipindi hiki cha kusherehekea kuzaliwa kwake.

Akitoa nasaha zake mwishoni mwa wiki Msikitini hapo, Khatibu wa Msikiti huo Ustadh Umar Sungura aliwahimiza Waislamu wakiangalie kwa makini kipindi cha maisha ya Mtume (s.a.w.) Makkah na kuoanisha na hali yao hivi leo nchini.

"Ni kipindi cha kupigiwa mfano. Hivyo tumieni historia kusimamisha haki, kumbukeni pasipo haki na uadilifu basi amani iko mashakani. Njia nyepesi kwenu ni kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura wakati ukifika",amesema.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook