Na John S.Zingi
NAOMBA nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu kauli ya Mheshimiwa Mangula, Katibu Mkuu wa CCM, kuhusu kauli za Profesa Lipumba. Profesa Lipumba alisema CCM haijafanya lolote la maendeleo tangu tulipopata uhuru. Tangu Tanganyika kupata uhuru wake mwaka 1961 hadi leo 2000 inakaribia miaka 40.
Ili kuchangia, nataka nimfahamishe Profesa Lipumba na wenzake kwa kuorodhesha baadhi ya mafanikio tuliyoyapata chini ya utawala wa TANU/CCM kama ifuatavyo:
Wakati tunapata uhuru kiwango cha elimu nchini petu kilikuwa sawa sawa na Kenya na vile vile Uganda. Hali ya shule zetu ingawa zilikuwa chache lakini zilikuwa na madawati na wanafunzi wakigawiwa mahitaji muhimu kama madaftari, uji, bulga, ugali, vitabu vya rejea, kalamu, vidau vya wino na kadhalika. Leo hii tumefanikiwa kuyaondoa yote.
Wakati tunapata uhuru, hospitali na vituo vya afya vichache vilivyokuwepo viliwahudumia wananchi na waliridhika. Elimu ya afya ilitolewa kwa umma na fadia yake ilionekana.
Mahospitalini, wagonjwa walitibiwa na kuhudumiwa kwa kuhurumiwa na kubembelezwa. Manesi na madaktari walikuwa kama wazazi kwa watoto wao. Hayo ndiyo mafunzo tuliyorithi kwa watawala wetu. Hivi leo huduma nafuu lazima inunuliwe kwa fedha.
Wakati tunapata uhuru miaka 40 iliyopita, nchi yetu ilikuwa na mashirika machache, mazuri yenye kutenda kazi kwa kuwajibika. Tulikuwa na Shirika la Reli, Shirika la Bandari na Shirika la Ndege, mazuri yaliyokuwa yakifanya kazi zake kwa moyo wa huduma. Watu wote waliridhika na huduma zake za uhakika.
Yalikuwepo mashirika mengine madogo madogo, viwanda na makampuni. Baada ya miaka kadhaa, utawala ukaanza kutafuna shirika moja baada ya jingine. Huduma zikaanza kudimimia hadi kufa. Mashirika, viwanda na makampuni yaliyokuwa ya umma yakadhoofika na kufa.
Idadi ya watu inaongezeka, ajira zinaondoka kwa kasi kubwa sana. Viwanda vinakufa ovyo ovyo tu. Tulikuwa na viwanda kama MWATEX, SUNGURATEX, MUTEX, Kiwanda cha Chuma Tanga, Kiwanda cha Mbolea na vingevyo. Leo havipo tena. Waliokuwa wafanyakazi katika viwanda hivyo leo ni wazururaji.
Vijana na wazee wao wote sasa wanaranda mitaani, hawana kazi. Hakuna shirika, hakuna kampuni ya umma. Hakuna ajira. Hiyo inahesabika ni hatua ya maendeleo baada ya miaka 40 tangu tujitawale!.
. Mfanyakazi anazeeka kazini, muda wake unakwisha anastaafu, anadhulumiwa haki zake.
Leo hii wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki fedha zao hawapati. Wenyewe wanakufa kwa njaa na matatizo mengine. Wastaafu viwandani na kila mahali wanalilia mafao yao lakini hawapati.
Huo ndio utawala wa wananchi. Hayo ndiyo matunda ya uhuru baada ya miaka 40. Profesa akisema kuwa nchi inarudi nyuma badala ya kwenda mbele, anaonekana hajui kupima maendeleo. Maendeleo yanapimwa kwa kuangalia viongozi wana nyumba ngapi, magari ya fahari mangapi na watoto wangapi wa vigogo wanaosomea nchi za nje za Ulaya na Marekani. Huko ndiko kupima maendeleo?
Maendeleo yapimwa kwa kuangalia shule za kusoma watoto wa walalahoi, zahanati za kutibiwa makabwela, ajira, milo ya wananchi na vitu vya namna hiyo.
Kuhusu suala la amani. Historia ya nchi ya Tanganyika hadi Tanzania ni ya amani. Hakuna ushahidi unaoonesha kuwa kuna kipindi kabla ya uhuru nchi yetu ilikosa amani.
Lakini kuna ushahidi wa wazi kabisa kuonesha namna serikali ya sasa inavyovunja misingi ya amani kwa makusudi. Kuwanyanyasa wananchi, kuwadhulumu, kukashifu dini za wananchi na kuwakashifu viongozi wao na hata kuwatupa gerezani bila makosa ya kisheria.
Kama yupo anayehitaji ushahidi zaidi wa maendeleo kwa kipindi cha utawala wa CCM au kujua mema yaliyoletwa na Azimio la Arusha aseme. Mimi niko tayari kumsaidia.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |