Jino kwa jino imetoka kwa Mungu

Na.Mwinjilisti Kamara Kusupa

NI jino kwa jino, jicho kwa jicho, waweza kuiita sera kama ukiamua kuiitwa hivyo. Waweza kuiita sheria, ukiamua kuiita hivyo. Waweza kuiita kanuni, ukiamua kuifanya hivyo. Waweza kuita msimamo na kadhalika. Lakini ukweli ni kwamba jino kwa jino ni "falsafa" ya Mungu iliyoletwa duniani kwa mkono wa Musa, na hatimaye ikaja kueleweka kwamba ni sheria ya Musa, ama "torati" ya Musa kwa lugha nyingine.

Nia kuu na makusudi halisi ya falsafa hiyo ni kulinda haki kwa wote pasipo kujali tofauti za kibinaadamu zinazojitokeza katika maisha ya ulimwengu huu kama vile tofauti za rangi, jinsia, maskini na tajiri, mtawala na mtawaliwa, Bwana na Mtumwa, msomi na mbumbumbu au mnyonge na mwenye nguvu.

Mwenyezi Mungu kama Muumba wa binaadamu, ndiye anayeijua vema thamani halisi ya kiumbe aitwaye binaadamu. Kulingana na mafundisho ya YESU, mali za Mungu siyo dhahabu na almasi na vito vya thamani au vitu vinginevyo vyenye kushikika ambavyo sisi wanaadamu tukiwa navyo basi tunajihesabu kuwa matajiri.Bali utajiri wa Mungu na mali za Mwenyezi Mungu ni watu. Hapa duniani Mungu hana rasilimali nyingine wala utajiri mwingine wowote zaidi ya watu wanaoishi duniani, ndiyo maana YESU alisema "Kama hamtakuwa waaminifu wa kutunza mali ya mtu mwingine ni nani anayeweza kuwaamini na kuwapa ninyi amana ya mali za kweli?"

Tafsiri halisi ya kauli hiyo ni kwamba mtu, awe mtawala, au awe tajiri, au awe yeyote yule, kama hatakuwa mwaminifu katika kuwatunza binadamu wengine, badala yake akawatenda jeuri yaani kwa kipindi hiki kifupi cha miaka isiyozidi mia moja aliyoishi nao katika dunia hii, mtu huyo atawezaje kujiaminisha kwa Mungu kwamba atawatendea vyema hao binadamu au malaika pamoja na Mungu mwenyewe hapo atakapokuwa anaishi nao mielele na milele?

Kwa hakika kutunza mali za Mungu ni kutunza wanadamu na kuthamini mali za Mungu ni kuthamini wanadamu wala si vinginevyo. Upo usemi kwamba "Cheza na tajiri lakini usicheze na utajiri wake, au cheza na mwenye mali lakini usicheze na mali yake". Laiti kama watu wangejua kwamba Mungu ni mkali sana na mali zake basi wasingewachezea wanadamu (wenzao) wengne.

Ni ukali huo wa Mungu ndio ambao ulidhihirishwa ndani ya Torati au Sheria ya Musa ya jino kwa jino na jicho kwa jicho. Lakini maana halisi ya jino kwa jino ni nini?

Wapotoshaji na hasa wapiga debe wa chama tawala wanasema jino kwa jino kuleta shari.Lakini hapo hakuna suala la shari bali kulinda haki. Tuangalie ufafanuzi wa Bwana Yesu kuhusu jino kwa jino, katika hotuba yake ambayo wengi walioelemewa na maisha na kukata tamaa, kama ambavyo wengi wamezoea kuiita hoyuba ya Mlimani.Kwanza Yesu anasema "Msidhani ya kwamba nalikuja kuitangua Torati (kuibadili au kuirekebisha) bali kuitimiliza. Maana Amin, Amin nawaambia mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka hata yote yatimie".

Kwa habari za watu, pamoja na ulalahoi wao, umaskini wao, na kupuuzwa kwao bado YESU aliwaambia" Amin, amin nawaambia hata nywele za vichwa vyenu vimehesabiwa". Tafsiri yake ni kwamba hata nywele ambazo sisi wanadamu tumezihesabu kama vitu kisichokuwa na thamani kiasi kwamba twaweza kwenda kwa kinyozi na kuzinyoa ama kuzikata na kuziacha kwenye chombo cha takataka na mwisho kuzisahau kabisa au kuzihesabu kuwa sawa na takataka zingine, bado mbele ya Mungu nywele hizo zimehesabiwa kuwa na thamani.

Hivyo mtu yoyote mwenye mtazamo sahihi au mtizamo wa kimungu kuelekea binadamu wenzake anaweza kuona ni kwa jinsi gani binadamu alivyo na thamani isiyoweza kulinganishwa wala kufananishwa na chochote chenye thamani ambayo haiwezi kupimwa kwa mizania ya fedha, na dhahabu au mengineyo yote yaliyohesabiwa kama ni yenye thamani sana na walimwengu. Wala kiungo cha binadamu hakiwezi kufidiwa kwa fidia halisi endapo kitaharibiwa.

Kwa ajili hiyo ili kusisitizia thamani hiyo, Mungu akasema jino kwa jino, jicho kwa jicho. Maana yake ni kwamba thamani ya jicho la mtawala, ndiyo thamani hiyo hiyo ya jicho la mtawaliwa. Thamani ya jicho la tajiri ni sawa kabisa na thamani ya jicho la maskini, hivyo isije ikatokea mtu mmoja kwa uzembe tu au ulevi wa mali zake, na utajiri wake, ama ulevi wa madaraka yake, akathubutu kutwaa msumari na kumtoboa mwenzake jicho kisha akasema basi acha nikulipe kiasi fulani na mambo yaishe, naye huyo muathiriwa kwa sababu ya umaskini wake akasema sawa nilipe kiasi fulani kama fidia basi mambo yakaisiha hapo. La!! Mungu akaagiza kwamba ni jicho kwa jicho. Yule anayetoboa jicho la mwenzake kwa makusudi na lake litoboke. Yule anayevunja jino la mwenzake kwa makusudi na lake livunjwe.

Wakati jicho la mshenzi huyo litakapokuwa linatobolewa, jino lake litakapokuwa lnavunjwa ndipo utaijua thamani halisi ya jicho na jino la binadamu. Kwa kifupi ni kwamba wewe mtu kama unaona jino lako ni la thamani na ni muhimu kwa maisha yako ya hapa duniani basi hesabu kwamba hata jino la mwenzako lina thamani na umuhimu ule ule na kwa ajili hiyo ulithamini bila kujali kama unamzidi huyo binadamu mwenzako utajiri, elimu, au ubora wowote ule wa kidunia.

Kama wewe mtawala unaona kuwa mguu wako una thamani basi hesabu ya kwamba na mguu wa yule unayemtawala una thamani ile ile na umuhimu ule ule. Kwahiyo haitazamiwi itokee kwamba wewe unayejua umuhimu wa viungo vya binadamu uwe mwepesi wa kutuma FFU kwenda kuvunja watu miguu au kwenda kuwamininia risasi za moto, waue na kujeruhi kisha ukategemea watu hao waseme asante sana. Umetumia nguvu za dola kulinda amani.

Mtizamo wa Ibilisi

Tatizo kuu la wote wanaoipigia kelele falsafa ya jino kwa jino ni ule mtazamo wao wa kishetani kuwaelekea wanadamu wengine. Wao wanaukiri usawa wa binadamu kwa midomo yao tu lakini katika mioyo yao wanakiri tofauti za binadamu. Wao (wapiga debe wa chama tawala) wanaona kwamba kuna watu wanaostahili kuitwa watu na kutendewa kila neno jema awezalo kutendewa binadamu. Kundi jingine ni watu ambao ni sawa na si kitu. Hawa wana mtizamo wa kama wa Ibilisi wa kuwaona watu kama "Subjects" ndiyo maana hata wakiua na kujeruhi, hakuna kelele nyingi za kulaani umwagaji wa damu, lakini mara zinapotolewa kauli zinazoelekea kuhatarisha maslahi ya tabaka la watawala basi zinakuwepo kelele nyingi za kulaani kauli za umwagaji damu. Je, hao ambao tayari wamemwaga damu, na hao wanaotishia kumwaga damu nani aliye mwovu zaidi?

Itaendelea Ijumaa.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook