Nani kasema Biblia imetanganisha dini na siasa ?

Na Mwinjilisti Salvatory

LEO ninakuja na hoja nzito kidogo, juu ya wimbo wa sasa wa "tusichanganye dini na siasa". naiita nzito, kwa sababu, kama ingekuwa inaimbwa na watu wa kawaida nami ningeona ya kawaida lakini sasa badala yake inaimbwa hata wasomi, wanasiasa, hata viongozi wa dini. Tena cha ajabu eti wanaojiita Maaskofu nao wamo. Sijui kama wamo katika wimbo huo wakiuelewa au ni katika usemi ule "Mtukimikie kafiri upate mradi wako?"

NINACHOTAKA kusema hapa ni kwamba Biblia kama kitabu kitakatifu ninachokiamini mimi, hakijazuia wala kutenganisha dini na siasa. Kwa ushahidi kama ifuatavyo:

Tangu zamani Mungu alichukulia dini na siasa kuwa kitu kimoja kwa kuhakikisha viongozi wa ngazi zote anawateua yeye.Ninashangaa kuona makala moja kwenye gazeti moja litokalo kila Jumapili mtu mmoja ajiitaye Askofu akiisingizia Biblia eti imekataza kuchanganya dini na siasa. Tena kana kwamba hiyo haitoshi akawalaumu Mwinjilisti na Askofu mwenzie na kuwaona kama wanapotoka kuchanganya dini na siasa.

Pamoja na uchambuzi wa kina juu ya dini na siasa uliokwishatolewa na Mwinjilisti mwenzie aliyekosolewa, na mlolongo mrefu wa maneno uliotolewa na Askofu aliyeukosoa bado mimi pasipo maneno mengi ninasema kwa kifupi kuwa dini inahusika na mambo ya kiroho na siasa inahusika na mambo ya kimwili. Na kwa kuwa mwanadamu ni mwili na roho ndio kusema mwanadamu ni dini na siasa.

Hili halina ubishi maana hata viongozi wa kisiasa hapa Tanzania wanalijua ndio maana wanachaguliwa au kuteuliwa kisiasa lakini wanaapishwa kidini. Mungu alilijua hili ndio maana aliwateua Manabii, wafalme na makuhani kuongoza sawa sawa na mapenzi yake. Biblia inasema wazi kuwa Mungu aliwateua watu watatu kama Masihi na kutiwa mafuta kwa ajili ya uongozi (Kuhani - Kutoka 30:30, Mfalme - 1Sam: 9:16, Nabii - Isaya 61:1). Kama mmoja wa watu hawa alienda kinyume na maelekezo ya Mungu ilibidi aondolewe na kuwekwa mwingine 1 Sam 16:1.

Kwa mfano kama Mfalme ataongoza vibaya na kuwakosesha watu wake mbele za Mungu, Mungu alimweleza Nabii kupeleka maonyo kwa mfalme huyo kabla ya Mungu kupeleka adhabu. Mfalme akimsikia nabii na kukubali kutubu, kuhani alikuwa anaitwa ili kufanya mpatanisho kati ya mwenye dhambi na Mungu kulingana na Mungu atakavyoelekeza.

Katika utaratibu huu uliowekwa na Mungu mwanasiasa (mfalme) alitakiwa awe mtu mdogo sana na apokee maelekezo kutoka kwa Nabii au Kuhani. Hata kama mfalme angekuwa anatisha namna gani bado isingemzuia Nabii au Kuhani kufanya kazi yake. Iko mifano mingi ya Manabii waliowakemea wafalme hata kuuawa jambo ambalo viongozi wa kidini wa sasa hawawezi kulifanya, hawawezi kulifanya kwa sababu hawako katika utumishi wa kazi ya Mungu, wengi wao kama sio wote ni wafanyabiashara.

Ninawaita wafanyabiashara kwa sababu maovu yanapotendeka nchini kama rushwa na dhulma inayoelekea kukosekana kwa haki za msingi za raia hawasemi. Lakini serikali inapogusia kuhusu kufutwa kwa misamaha ya kodi ya makanisa yao wanainuka kwa kauli moja utadhani wameagana! "Serikali inakandamiza taasisi za kidini jambo ambalo siyo kweli. Na hata kama ingekuwa kweli Askofu au kiongozi yeyote wa kidini unapoenda uwanja wa taifa kuomba dua kwa kiongozi unayefahamu kuwa serikali yake haina dini, na wakati mwingine amemshirikisha Mungu katika kutafuta utawala kwa kwenda kwa miungu mingine kama matambiko, kafara na kadhalika mnategemea mfalme huyo atakapotawala atakulipa nini!

Kutokana na hali hiyo kama ya viongozi dhalimu inawaangukia viongozi wetu wa kidini kwa kwenda bila hekima. Matokeo yake viongozi wetu wa kidini wanapoitwa kuomba dua wakati wa kiangazi ili mvua inyeshe inakuja mvua ya kuzoa majumba na maafa mengine, wanapoitwa kuomba mvua zinapozidi, unakuja ukame, kwa hao kuomba dua au kutoomba ni sawa sawa tu. Viongozi wengi wa kidini tulionao hawaendi kuomba dua mbele ya viongozi wa serikali ili kumpa Mungu utukufu, kama ingekuwa hivyo basi dua zinazoombwa zingewabadilisha viongozi wetu.

Lakini badala yake wanaenda ili ama makanisa yao yasifutwe, Ministry (NGO's) zao zisajiliwe au tu waonekane kwenye vyombo vya habari. Wakiwa na mawazo haya hawawezi kukemea maovu, badala yake ni waimbaji wakubwa wa "usichanganye dini na siasa". Viongozi hawa Mungu anawaita "wachungaji mbwa waliobubu wasioweza kubweka" Isaya 56:10. Wachungaji wa mshahara Yoh 10:12.

Kukosekana kwa madawa mahospitalini, uchumi kuporomoka, elimu kudumaa na hali ngumu ya maisha vinapoongezeka viongozi wa kidini hamtakiwi kukaa kimya. Kemeeni, yamkini mtaliponya taifa.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook