Matumizi sahihi ya Kiswahili

KATIKA hali ya kawaida ya maisha, wanaadamu ni lazima wawasiliane. Na chombo kikubwa cha mawasiliano ni lugha. Lugha hutumiwa na jamii kuweka mawasiliano katika shughuli mbalimbali.

Katika lugha ya Kiswahili yapo maneno mengi yanayotumiwa kimakosa na kufikia kuzoeleka na kuonekana ni sahihi pasi na watumiaji kujua kwamba ni makosa.

Katika hali hiyo, Rais wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Alli Hassan Mwinyi aliwahi kurekebisha baadhi ya maneno ya Kiswahili yanayotumika vibaya. Neno mojawapo lilikuwa "kuonyesha" likiwa na maana ya kuonekana kwa kitu na badala yake likawa "kuonesha" ambalo ni sahihi. Kwani "kuonyesha" linalotokana na na neno "kuonya" lenye maana ya kukataza. "Kuonesha" linatokana na neno "kuona" lenye maana kutazama.

Makala haya ni mwendelezo wa kuweka sawa matumizi ya lugha ya Kiswahili. Neno nitakaloanza nalo ni "kufundisha".

Watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili walitumia vibaya neno hili, kinyume na asili ya neno lenyewe. Kwa mfano "Mwalimu anafundisha hisabati". Hapa kosa la kawaida ni "kufundisha". Usahihi wake ni "Mwalimu anafunzisha hisabati". Kufunzisha ni kumpa mtu maarifa mapya. Na ndio maana anayepewa maarifa hayo huitwa mwanafunzi na haitwi mwanafundi.

Hili neno "kufundisha" asili yake ni "funda". Kwa mfano "Bibi anamfunda mjukuu wake". Hapa ukiangalia kwa undani wa sentensi hii utagundua kuwa maana ya sentensi hii ni kuwa bibi anampa mbinu mjukuu wake.

Vivyo hivyo hata neno "fundisha" ni kumpa mtu mbinu mbalimbali juu ya kitu fulani. Ndio maana watu wenye ujuzi wa kitu fulani wanaitwa "mafundi". Kwa hiyo yule fundi anayewaongoza watu kuwapa ujuzi fulani ndo sahihi kusema "anafundisha".

Kwa kutoa hitimisho juu ya neno hili si sahihi kusema "mwalimu anafundisha" bali ni sahihi kusema "mwalimu anafunzisha".

Neno lingine ni "Mgeni wa heshima".

Watumiaji wengi wa lugha ya Kiswahili wanalitumia vibaya neno hili. Kwa mfano katika hafla au sherehe mbalimbali zinapoandaliwa huwa anakaribishwa mtu maalum. Mtu huyo anaweza kuwa kiongozi wa ngazi fulani, hivyo anapewa heshima ya hali ya juu katika shughuli hiyo. Tuangalie mfano ufuatao:

Kuna hafla ya ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2000 iliyoandaliwa na Tume ya Uchaguzi na anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania afungue hafla hiyo. Tangazo linatolewa kwa wananchi kuwa "Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni wa heshima katika hafla ya ufunguzi wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2000".

Wananchi wataelewa kinachokusudiwa. Lakini katika matumizi ya lugha ya Kiswahili neno mgeni wa heshima si mahala pake kutumika hapo. Na lina maana nyingine ambayo ni kinyume na kusudio na maana yake ya msingi. "Mgeni wa heshima", maana yake ni kutokuwa na heshima. Kwa maana nyingine ni sawa na kusema ni kumtusi (kumtukana).

Kwa mfano mtu ni mara yake ya kwanza kwenda Arusha na anatokea Tabora. Ni sahihi kusema mtu huyu ni mgeni wa Arusha na ni mwenyeji wa Tabora. Maana yake ni kwamba mtu huyu mji wa Arusha haujui vizuri kama anayouvujua mji wa Tabora. Hivyo ukisema "mgeni wa heshima" maana yake heshima ni kitu kigeni kwake. Kwa maana nyingine hana heshima.

Neno sahihi linalotakiwa litumike badala ya "mgeni wa heshima" ni "mgeni muheshimiwa" yaani watu wa pale kwenye hafla hiyo wanamuheshimu na yeye pia anawaheshimu.

Nahitimisha kwa kusema kuwa si sahihi kumwita mtu "mgeni wa heshima" bali ni sahihi kumwita "mgeni muheshimiwa" au mgeni rasmi.

Haya ni maoni ya mwandishi. Wataalamu wa lugha ya Kiswahili mnasemaje?

Mhariri.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook