Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo wamedai awali walifika katika ofisi hiyo askari waliodai kuwa wafuasi hao wa CUF hawaruhusiwi kuangalia mikanda ya video bila kibali.
Imedaiwa kuwa baada ya wanaCUF kuhoji na kudai waoneshwe kifungu cha sheria kinachozuia kufanyika shughuli hiyo ndani ya tawi lao, askari hao walianzisha tafrani ambayo hata hivyo haikufanikiwa kuzuia onesho hilo.
Bwana Mohamed mmoja wa watu wanaosemekana kushuhudia sakata hiyo ameliambia gazeti hili kuwa baada ya askari kushindwa kuwasambaratisha wananchi hao, waliamua kurudi kituoni na haikupita muda kundi la askari 17 waliokuwa na silaha liliwasili mahali hapo na kuanza kupiga virungu watu waliokusanyika mahali hapo.
Katika kujitetea imedaiwa wananchi hao waliwarushia mchanga polisi ambao imeelezwa walikuwa wamejiandaa kikamilifu kimapambano.
Dakika chache baadae askari hao imedaiwa walianza kufyatua risasi hewani na kusababisha wakazi wa eneo hilo kukimbia hovyo.
Katika piga piga hiyo polisi inasemekana ilimkamata kijana anayemiliki mitambo iliyotumika kuoneshea kanda hizo na kuondoka naye.
Imedaiwa Kijana huyo baada ya kupigwa sana aliburuzwa bara barani akiwa na nguo ya ndani tu hadi kituo cha polisi.
Taarifa hizo zimedai kuwa siku iliyofuata polisi iliendesha msako mkali kuwasaka na kufanikiwa kuwatia mbaroni watu wanane.
Waliokamatwa ni pamoja na Athumani Kimbindu mmiliki wa runinga, Selemani Kinja na Mohammed Hamza.
Wengine ni Hussein Chaole, Said Chaurembo(Beho), Bakari Tegeege, Salum Myowela na Habibu Mbwana.
Watuhumiwa hao kwa pamoja walifikishwa mahakamani Alhamisi iliyopita ambako walisomewa mashtaka mawili ya kuonesha kanda ya video tawini bila kibali na kuwazuia polisi kufanya kazi yao.
Watuhumiwa hao wamenyimwa dhamana na wako ndani hadi kesi yao itakapotajwa.
Kutokana na tatizo ya mawasiliano ANNUUR haikufanikiwa
kumpata kamanda wa polisi mkoani Lindi kupata kauli yake kuhusiana na sakata
hiyo ya aina yake.
NAIBU waziri wa viwanda mama Shamim Khan amejikuta akiwa katika hali ngumu baada ya kurushiwa shutuma kali na akinamama Waislamu Moro.
Mama Khan alifikwa na mtihani huo jumamosi iliyopita katika sherehe za Maulid ya wanawake wa kiislamu iliyofanyika Jabal hira.
Mashambulizi ya kinamama dhidi ya waziri huyo yalifuatia kauli yake kuwa akinamama waislamu wajiepushe na kuchanganya dini na siasa,badala yake aliwataka wachukue fomu kugombea uongozi katika uchaguzi mkuu ujao.
Waziri huyo pia aliwalaumu akina mama waislamu kuwa wako nyuma kimaendeleo hivyo aliwataka wajiunge pamoja ili wakapewe mikopo na jumuiya moja isiyo ya kiserikali iliyoko mkoani humo.
Aidha waziri Khan ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hiyo alidai kuwa kutokana na uchache wa Waislamu na hasa akina mama wa kiislamu bungeni wabunge Waislamu hushindwa kutetea mambo yanayowahusu Waislamu.
Kauli hizo ziliibua minong'ono ya chini chini ambayo hatimaye mama mmoja aliyefahamika kwa jina la mama Fatma alimkabili Mbunge huyo na kumwambia yeye kama mwanasiasa amefuata nini katika sherehe ile ya kidini.
Aidha alimwambia kama Waislamu hawatakiwi kuchangamya siasa na dini iweje yeye awatake akina mama wa kiislamu wachukue fomu kwa ajili ya kugombea uongozi.
"Waiziri unatuchanganya unapotukataza tusichanganye dini na siasa wakati huo huo unatuhimiza tuchukue fomu za kugombea uongozi CCM", alisema kwa ukali mama huyo.
Aidha mama huyo alimtaka waziri Khan aeleze yeye kama waziri Muislamu ameufanyia nini Uislamu tangu alipoanza kushika nyadhifa nzito za serikali miaka kumi iliyopita na kwa nini aamue kuzungumza hayo hivi sasa.
Kadhalika mama Khan alitakiwa aeleze kwa nini serikali yake iliua Waislamu Mwembechai.
Kusikia hivyo Waziri Khan alikusanya makabrasha yake kutaka kuondoka, hata hivyo baadhi ya waandazi wa shughuli hiyo walimsihi awe mvumilivu.
Akinamama waliohudhuria sherehe hiyo walimlaumu
waziri huyo kwa kutaka kutumia kikao cha kidini kufanya kampeni za kisiasa.
Kano, Nigeria.
Likiwa na wakazi milioni nane kati yao asilimia 90 ni Waislamu, Kano jumatano iliyopita imetangaza rasmi kuanza kutumia sheria ya Kiislamu katika jimbo hilo.
Gavana wa Kano, Rabiu Kwankwaso akitoa tangazo hilo kwa njia ya radio amesema Serikali yake imetangaza matumizi ya sheria hiyo kuitikia matakwa ya muda mrefu ya wakazi wa jimbo hilo lililoko kaskazini ya Nigeria.
Awali kuliwepo tetesi kuwa iwapo sheria ya kiislamu ingelitangaza kutumika rasmi kungelizuka vurugu kutoka kwa wakazi wakristo wasiozidi asilimia 10 kama ilivyotokea jimbo la Kaduna lililo umbali wa kilometa 140 kutoka Kano, hata hivyo hali imeendelea kuwa shwari na watu wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
"Maduka, mabenki na biashara katika mji wa Kano ambazo zilifungwa kufuatia kutangazwa sharia ya Kiislamu Jumatano iliyopita, zimefunguliwa na hali imeendelea kuwa ya kawaida", ripoti kutoka Kano zinaeleza.
"Tusio Waislamu tumeondokwa na hofu tuliyokuwa nayo nyuma kabla ya kutangazwa sharia, kama unavyoona watu wakiendelea na shughuli zao bila ya kuwekewa vikwazo vyovyote vile, anaeleza makazi wa Kano Bwana Emeka Okoro ambaye ni hujishughulisha na uuzaji wa vifaa vya Elektroniki jijini hapo.
Taarifa kutoka Kano zinafahamisha kuwa mamilioni ya watu yalikusanyika katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Gavana wa jimbo hilo kusikiliza tamko rasmi la kuanza kwa sharia.
Kano ni jimbo la nne la Nigeria kutangaza kutumia sheria ya kiislamu kijamii.
Majimbo yaliyotangulia ni Zamfara, Sokoto na Kaduna ambako Wakristo walizusha ghasia wakidai sheria hiyo ingewakandamiza wasio Waislamu.
Hata hivyo dai hilo lilikanushwa na wakazi wasio Waislamu wa jimbo la Zamfara ambao walisema sheria hiyo haimkandamizi mtu bali imesaidia kurejesha maadili mema katika jamii.
Miongoni mwa mambo ambayo wamesema yamesaidia kurekebisha mwenendo wa jamii yao ni pamoja na mahimizo ya mavazi ya heshima kwa watu wote na serikali kuwasaidia wasiojiweza na wasio na ajira, waweze kujikimu kimaisha.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |