Unafiki wa Kotwe
Ndugu Mhariri
NAOMBA nitoe maoni yangu juu ya kipindi maarufu cha propaganda cha Radio ya Taifa (RTD) kiitwacho "Maneno Hayo" cha Alhamisi Juni 23, mwaka huu.
Kipindi hiki kimeeleza mengi juu ya tabia ya bata maarufu kama Kotwe. Tabia ambazo umbile lake la nje ni tofauti na undani halisi.
Mtangazaji wa kipindi hiki alinigusa hasa alipofananisha tabia za Kotwe na upinzani wa Tanzania na kwamba viongozi wetu wa upinzani wana kauli njema za kuleta haki, usawa, amani, umoja, mshikamano na utengamano wa taifa lakini kauli zao kama jino kwa jino au jicho kwa jicho ni sawa na Kotwe.
Kama ni Kotwe basi mahali pake ni CCM.
Utakumbuka kuwa pamoja na CUF kutamka jino kwa jino, CCM wametoa yao ya shavu kwa shavu. Je, katiba ya CCM inao msemo huo wa shavu kwa shavu?
Kama kutokuwepo kauli ya jino kwa jino katika katiba ya CUF, ni ukotwe je, kutokuwepo kauli ya kofi moja kwa mawili si ukotwe?
Katiba inatoa uhuru wa vyombo vya habari na inatamka vyombo vya taifa visifungamane na chama chochote cha siasa. Je, matumizi ya RTD, TVT na TVZ kwa kutangaza habari za CCM pekee na kupotosha na kutoa propaganda dhidi ya upinzani haya yapo katika katiba?Huu si ukotwe?.
Tena sio katiba ya CCM ni katiba ya nchi inayotoa haki za maoni, habari na mawasiliano mbona inavunjwa? Je huo sio ukotwe?
Je, watangazaji wa RTD ni wasemaji wa CCM? Au RTD ni chombo cha CCM? Huo sio ukotwe? Je, sheria sasa inaruhusu kupendelea chama fulani? Rais Mkapa katamka na kuahidi kutumia nguvu zote ili yeye na mgombea wa Zanzibar washinde, je, hili halipingani na katiba na haki za binadamu. Je, nani Kotwe hasa?
Kauli za Nchimbi, Kapinga, Mhe. Mangula na Mhe. Malecela sio ukotwe?
Ayub Juma,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
SISI Waislamu tumekuwa hatuna thamani hata kidogo japo ni wazawa wa hapa nchini.
Tupo daraja la chini. Tukiwa misikitini tunafuatwa na polisi kila siku. Tukijiunga na vyama tunaambiwa tunachanganya dini na siasa. Tukiwa katika mihadhara utasikia tunakashifu dini nyingine.
Ili nasi tuwe kama watu wengine tufanye nini? Waislamu umefika wakati wa kujikomboa. Kwani hii CCM na serikali yake haitutakii mema.
Sasa tuangalie maandiko ya Mwenyezi Mungu pale aliposema katika Qur'an 2:83 na sisi lazima tuikatae CCM na serikali yake.
Mosi Abdallah Lioche,
S.L.P. 261, Nachingwea
Lindi.
Ndugu Mhariri
NIMEKUWA nikiwasikia kwa muda mrefu viongozi mbalimbali wa Chama tawala CCM wakitueleza juu ya kukua kwa uchumi wa Tanzania. Hongera kwa hilo.
Ingawa mimi si mwanauchumi ila ninachofahamu kukuwa kwa uchumi ni kukuwa kwa pato la mwananchi. Huenda basi pato la mwananchi limekuwa. Sasa tuseme vipi pato la wananchi ama uchumi wa nchi umekuwa wakati hata idadi ya wananchi wako ni ya kubahatisha?
Sasa hilo pato mmeligawa kwa idadi ipi ya wananchi hata mkaona pato la uchumi limekuwa? Ama bado mnatumia sensa ya karne ya 20 ya watu milioni ishirini na tano
Mimi mshahara wangu shilingi 60,000, nikijalipwa 100,000 itakuwa pato langu limekuwa (itategemea na wakati uliopo). Lakini wakati napata 100,000. Ninachotakiwa kujua ni kuwa bado nipo peke yangu? Kama nitakuwa nina mke na watoto tisa basi pato la nchi linaendeana na idadi ya watu. Nchi ipi duniani isiyojua idadi hata ya raia wake? Utapanga vipi maendeleo yao?
Nune Costa Figo,
S.L.P. 21396,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi niseme machache. Waswahili wanasema siku ya nyani kufa miti yote huteleza.
Katika gazeti moja litokalo kila siku kwa lugha ya Kiswahili katika toleo lake la hivi karibuni, Balozi wa Msumbiji Bw. Pedro Davane amewataka Watanzania kuipa kura CCM.
Balozi huyo amevishambulia vyama vya upinzani kwa kutoa ahadi za uongo. Mwisho akasema toka azaliwe hajawahi kuona chama kama CCM.
Sisi Watanzania tunaungana na Balozi, kweli hatujawahi kuona chama kama CCM.
Katika bajeti ya mwaka huu serikali ya CCM imemtengea kila Mtanzania shilingi 160. Pesa hiyo ndiyo gharama ya matibabu kwa mwaka. Ni kweli balozi hajaona chama kama CCM.
Katika nchi za wenzetu, serikali huuza madini wanayochimba migodini na bidhaa wanazozalisha viwandani. Lakini serikali ya CCM inauza viwanda na migodi, badala ya bidhaa na madini. Ni kweli balozi hajaona chama kama CCM.
Hivi karibuni muswada umepitishwa unaompa msimamizi uwezo wa kuhamisha sanduku la kura na kulipeleka anakotaka. Ni kweli balozi hajaona chama kama CCM.
Lakini kubwa zaidi balozi anajua sumu waliyomwaga CCM mpaka leo RENAMO na FRELIMO wakawa paka na chui.
Bado mwaipenda CCM?
Shwaibu Swai,
Dodoma.
--
![]()
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |