Joka la Mdimu - 6
JINJA MALONI
JINJA MALONI alikuwa nyumbani kwake asubuhi wakati wanaume wawili mmoja chotara wa Kiafrika na Kiarabu, na mwingine Mwafrika walibisha hodi mlango wa nje. Jinja aliitikia na kuwaomba wamsubiri. Hakuwa na tabia ya kukaribisha wageni ndani wachilia chumbani kwake kwa kuchelea kuona uhaba na ukuukuu wa vifaa vilivyokuwepo mle ndani. Kwani kulizidi nini zaidi ya kitanda cha mwakisu na godoro la katani lililofanya vinundunundu na kunuka fondogoo?
"Nakuja sasa hivi!", alijibu akijitayarisha kutoka. Nje macho yake yalianguka juu ya yule chotara wa marika ya miaka ya arobaini, sura jamali. Nywele zake za mabotea zilianza kuota mvi za hapa na pale na kuongeza haiba yake. Mwenzake mwanamke alimzidi makamo, takriban miaka sitini hivi. Alivaa koti la samawati juu ya darzi safi nadhifu. Kichwani alivaa kofia ashrafu ya mkono.
"Ahaa! Maalim. Subalkheri", alisalimu Jinja huku akinyoosha mkono kumpa yule mzee halafu akamalizia na yule mwenzake. Alihisi mzizimo katika nyuso na mikono hakuwa na nguvu, akauliza, "Kulikoni maalim, mbona hivi?".
"Sahibu yako hayupo duniani". alijibu kwa sauti ya chini bila ya kumchanganya machoni Jinja Maloni.
"Yupi mmoja wapo?"
"Omar Mahafudh".
"Al hamdulillahi", alijibu Jinja Maloni macho kayachimbia ardhini. Kabla hajazinduka katika fazaa hiyo na kuuliza sababu ya kifo chake, yule mzee alisema udhuru uliowafikisha pale.
"Tunaomba ukatutayarishie malazi ya Al maruhum", alisema kwa sauti ya chini.
"Ni radhi maalim", Jinja aliitikia kwa sauti ya chini huku akiinua macho yake na kuuliza, "wapi sijui?"
"Kama uko tayari, bora tufuatane tukakuoneshe, sio mbali sana. Maana ajizi nuksai huzaa mwana kisirani". "Sadakta maalim. Bora twende".
Omar Mahafudh, mfanya biashara maarufu alikuwa masalia ya Waarabu kutoka Oman. Zama hizo alizofika aliuza majora ya nguo, ambayo aliyabeba na kuzunguka nayo mitaani. Huku na huko alipita, vichochoroni, mabarabarani hadi majikoni akiwakopesha washtiri wake. Biashara haikuwa rahisi. Alitembea kwa miguu mwendo mrefu akipiga kelele kutangaza biashara yake kila baada ya mwendo mfupi, guo! guo! guo! Wengine walimkopa wakahama nyumba na kutoweka na madeni yao. Au wanawake fisadi waliposikia sauti yake walikimbilia kusubiri katika mitaa au nyumba zisizokuwa zao ambako walimkopa wakisingizia wakazi wa nyumba hizo.
Mashindano makali ya kibiashara yaliongezwa wakati wauza mali kwa mali walibadilisha bidhaa zao kwa nguo kuukuu na vitu vingine vyovyote vile vya thamani. Badala ya kukatishwa tamaa na mashindano hayo Omar Mahafudh alizidisha adili yake, akajenga jina. Kuona hivyo alinunua baiskeli ya Raleigh akafunga mitumba yake katika kiti cha nyuma. Kwa msaada huo alifika sehemu nyingi zaidi kwa muda mfupi bila ya uchovu. Miaka si miaka akapata ustawi, akafungua duka mjini na kuoa mwanamke wa Kiafrika. Baadaye akahamishia duka lake Sega hadi faradhi ilipomkuta.
Mahafudh alizaa watoto wengi, wake kwa waume. Idadi yao kubwa walikwenda Mascut na miji mingine ya Oman kufanya kazi mbalimbali hasa baada ya hali mbaya ya uchumi kuikumba nchi hii. Katika miaka ya hivi karibuni biashara ya duka haikuwa nzuri hasa kwa uhaba wa vyakula na bidhaa nyingine. Zamani makasha ya vyakula yalijaa chungu za unga wa sembe, ngano, maharage, kunde, mbaazi na choroko. Sasa haikuwa hivyo tena. Vifaa hivyo vilipatikana kwa kuhonga na tijara ikawa haba. Uzee na ghasa hizo zote vikamtoa Mahafudh hamu ya kuendelea na biashara ya duka. Lakini ghafla serikali ikaruhusu watu ambao waliweza kuagiza vitu kutoka nje kwa fedha zao wenyewe wafanye hivyo na kupanga bei zao bila ya kuingiliwa. Mlango wa kheri ukafunguka upya. Miezi mitatu tu watoto wake walilijaza dula la baba yao kwa kila aina ya bidhaa. Duka likawavutia kila mtu na kuvuma Mindule yote. Watu waliingia na kutoka kununua saa, viatu, mashati, vitenge, khanga na kila aina ya urembo. Mwisho wa mwaka wakamletea mabasi matatu madogo ya aina ya Toyota Coaster ambayo yalimwingizia si chini ya shilingi laki mbili kwa siku kutokana na kusafirisha abiria sehemu mbalimbali jijini pale. Hivyo kila mtu, pamoja na majambazi, wakafahamu kuwa Mahafudh ni milionea.
Usiku uliopita majambazi walikusudia kuvunja dula la mzee Mahafudh kuiba. Mahafudh alikuwa hapungui miaka sabini na tano na alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya moyo. Inasemekana kutokana na ghasia za majambazi wale waliopiga risasi Mahafudh alianguka. Alikimbizwa hospitali ambako aliaga dunia bila ya kupata fahamu tena.
Wakati Jinja Maloni anajiandaa kuvaa nguo za kazi, kutafuta kureja, jembe na sururu, aliwaza namna walivyoshi na yule mzee wa Kiarabu. Waama hakuna usuhuba baina ya mwenye mali na fakiri lakini palikuwa na mlahaka kati ya Maloni na Mahafudh, ambao Maloni aliuthamini zaidi ya mahusiano ya kifedha ambayo aghalabu hupanda mbegu ya uhasama.
Kabla Sega hakujajengwa kulikuwa mashamba ya wakazi wa mjini. Lakini baadaye walihamia walinzi wa viunga vya minazi na mikorosho. Hatimaye wenye mali wenyewe walihamia huko. Walipokufa walizikana katika miazara yaliyozunguka au kuwa jirani na makao yao. Hata hivyo hivi leo maziara mengi yalikuwa ya koo maalum za Bwana huyu, na yule, Mwinyi kadhaa na jinsi kadhaa na kadhalika. Hata hivyo wageni nao walikuja na kuzikwa ama kwenye viunga vya koo hizo kwa ridhaa yao au walizikwa katika makaburi msafa.
Eneo la makaburi msafa lilikuwa limetengwa na nyumba, nyumba ya karibu ikiwa kiasi cha hatua ishirini kutoka hapo. Nayo ilikuwa nyumba ya zamani sana ya miti ya kupauliwa kwa viungo na mabati ya kuchomekachomeka. Kuta zake zilichakaa mno na kuporomosha madongo ovyo. Nyumba hiyo ilitumiwa na wagema pombe ya mnazi ambao waliweka mitungi ya "ndaza" humo ndani kabla ya kuipeleka kuuza vilabuni. Walevi maarufu walipata fursa ya kunywa katika chumba mahususi cha nyumba hiyo iliyoitwa "Baiti Sharab".
Na ukiachia utani au dhihaka ya jina hilo mazingira yote ya makaburi msafa yaliashiria dunia ya pili. Ni walevi tu waliomudu kukidhihaki kifo kilichozingira eneo hilo.
Baada ya mwendo mfupi Jinja Maloni na wenzake waliingia katika eneo hilo huku yule mzee aliyekuwa kiongozi akisema taratibu, "salaam aleikum mayitun". Jinja alishtuka kusikia maiti wanasalimiwa, lakini ya nini kuuliza kisa chake? Sururu, jembe begani na kureja mkononi, alipunguza hatua za kumwachia yule mzee aelekeze sehemu mahsusi ya kuchimba kaburi lenyewe la marehemu. Alivuka makaburi ya zamani hadi akafika kwenye makaburi mapya. Kulikuwa na msafa wa yale ya watoto na wakubwa. Ilionekana miti iliyoota juu ya makaburi. Ya zamani sana yalitambuliwa kwa uzee wa miti iliyopandwa juu yake: miwili kichwani, miwili miguuni.
Lakini sio yote iliyoota na kumea vilivyo. Mingi iliota nusu nusu, mitatu, miwili au mmoja, pengine hata kufa kabisa. Ilitegemea majira ambapo mtu alifariki na kuzikwa. Kama ni wakati wa masika dhahiri miti yake ilistawi na kufanya kivuli rasmi, na alama mahsusi. Wale waliozikwa msimu wa kiangazi aghalabu miti yao ilikuwa pamoja nao. Juu ya chaga zito walilofukiwa nalo ikaoza na kuwa mchanga kama wenyewe. Nani angepanda miti ya kaburi mara mbili kisha kuinyunyizia maji mithili ya bustani? Kuhofia kufa kwa miti ya makaburi wengine walichomeka chupa mbili mbili miguuni na kichwani mwa kaburi. Ila chupa hizo zilitumika zaidi katika maziara ya watoto hasa wale waliozikwa katika vibla vya Misikiti zama hizo kulipokuwa na nafasi katika vibla vya misikiti hiyo, sio siku hizi ambapo hata maziara yalifukuliwa na kujengwa vilabu na madanguro. Ukiachilia mbali miti na chupa, maziara mengine yalijengewa vikuta vya matofali au kuwekewa alama ya mawe yenye majina vichwani mwa makaburi.
"Hapa", Jinja Maloni alielekezwa huku akikabidhiwa kamba fupi ya futi tano na inchi nane. Hicho ndicho kilikuwa kipimo cha urefu wa marehemu. Jinja Maloni angeongeza urefu mwingine mdogo kiasi cha inchi mbili hivi kama tahadhari tu. Ni tahadhari tu, kwani uchimbaji makaburi ulikuwa na viroja vya kila aina: kutumbuka maji, kukutana na miamba, kutojaa mchanga baada ya mazishi na mifano kama hiyo. Mara tatu Jinja aliona makaburi hayakutosha kutokana na kuvimba ghafla kwa maiti na kusababisha kaburi kuongezwa ukubwa.
"Haya, shughulika Mwinyi", alisema yule mzee huku akimkabihi Jinja ijara yake na kuondoka, akifuatiwa na yule mwenzake ambaye tangu afike kwa Jinja hakutia neno lolote.
Walipoondoka Jinja Maloni alitia fedha zake mfukoni, akalaza kipimo kwa makini na kupigilia mambo kama ramani yake. Alilima kwa muda sehemu hiyo kisha, akatupa jembe pembeni na kuanza kutumia sururu. Alichimba hivyo kwa robo saa, akatupa sururu chini. Udongo ulikuwa bado mbichi na pote nyasi zilikuwa zimestawi vizuri. Aliokota kurega lake na kuanza kutupa mchanga nje ya kaburi.
Wachimba makaburi wengi walipenda kusaidiwa na wenzao. Na hakika zamani kazi hiyo ilifanywa na watani au ndugu wa karibu wa marehemu hasa vijana. Shughuli hiyo nzito ya sinamzi haikuhitaji upweke bila shirika. Bali ya kale ndiyo yamepita.
Jinja Maloni alichimba na kutoa mchanga bila ya kupumzika ila mara chache tu alipopachika sigara mdomoni, kuiwasha na kuivuta. Alisimama na kuwatazama watu wachache waliokatisha katika barabara ya miguu iliyopita maziarani hapo. Walitembea chapu chapu huku wamekazia macho chini au mbele. Hakuna aliyependa kujikumbusha kifo na wala kumtazama Jinja Maloni akitayarisha malazi ya marehemu.
Mazishi yalipangwa saa tisa alasiri. Saa saba kamili Jinja alianza kuchimba mwana ndani baada ya kwenda chini futi tano. Kazi hiyo aliifanya zaidi kwa kukisia umbo la marehemu hasa unene wake, maana urefu ulikuwa ni sawa na ule wa kaburi lenyewe. Alipomaliza shughuli hiyo alitupa kurega nje akajitoa kaburini. Alisimama akitweta kwa kasi ya kazi aliyoikamilisha. Aliangaza huku na kule akafikiria hatma ya mwanadamu. Aliinama kuokota shati lake, akalikung'uta na kulivaa pole pole. Halafu alichomoa kisu chake na kwenda kukata miti minne ya kupanda juu ya kaburi kutoka makaburi ya jirani. Alibeba zana zake na kuondoka huku fikra mbalimbali zikiendelea kupita akilini mwake.
Itaendelea Ijumaa
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |