Mufti wa BAKWATA akacha kuhutubia waumini Mwanza
MUFTI wa Bakwata Hemed bin Juma bin Hemed ambaye yuko ziarani mikoa ya ziwa, alishindwa kuhutubia mkutano wa hadhara kama iliyoandaliwa na uongozi ya Bakwata mkoa wa Kagera. Badala yake Mufti alizungumza na Waumini wachache msikitini wakati wa swala ya Alfajiri.

Pamoja na kuombwa na waumini ahutubie ANNUUR imefahamishwa kuwa Mufti alikataa kwa madai kuwa alikuwa akiwahi Ndege ya kuelekea Mwanza.

Hata hivyo ilifahamika baadaye kuwa alielekea wilaya ya Karagwe ambako alifika Kayanga, Muleba, Kanazi kisha alirejea tena Bukoba kabla ya kuelekea Mwanza.

Katika mazungumzo yake sehemu zote alizotembelea Mufti na ujumbe wake aliwataka Waislamu kutojiingiza katika mambo ya siasa kwa kuwa kufanya hivyo ni kuchanganya Dini na siasa.

Akiwa mjini Mwanza, Mufti Hemed jumatatu wiki hii alionekana akiingia ofisi ya mkuu wa mkoa Mwanza ambapo baada ya kikao na mkuu huo alikwenda ukumbi wa shia Ithnashaaria uliopo mtaa wa uhuru ambako alikutana na watendaji wa mkoa huo.

Baada ya mkutano huo Mufti alihudhuria hafla ya chakula ambayo iliandaliwa na mfanyibiashara maarufu mjini hapa Bwana Mustafa Hassan Mohammed mtaa wa Liberty.

Hafla hiyo iliyowekewa ulinzi mkali wa polisi waliovalia sare rasmi za jeshi hilo na wale waliokuwa hawana sare pamoja maafisa wa idara ya usalama ilihudhuriwa pia na Mkuu wa wilaya ya Mwanza, katibu wa CCM mkoa wa Mwanza bwana Kayawana na Katibu wa vijana wa CCM wa mkoa Mwanza.

Baada ya hafla hiyo Mufti aliombwa kuhudhuria shughuli ya kuwaombea dua waliokuwa masheikh maarufu wa Mwanza ambayo hata hivyo hakuweza kuhudhuri badala yake aliwakilishwa na Sheikh Ali Kisiwa wa mkoa wa Arusha ambaye anaandamana naye katika safari yake.

Jioni ya siku iliyofuata Mufti aliandaliwa kukutana na waumini wa mkoa wa Mwanza ambao walifurika kwa wingi kumsikiliza huku wakiwa wamesambaza makaratasi yaliyokuwa na picha zinazomuonesha Katibu wa Bakwata mkoa wa Arusha akiwa na washindi wa mashindano ya Miss Arusha.

Makaratasi mengine yalikuwa yakieleza lengo la safari ya Mufti mikoani kuwa ni kufifisha nia ya Waislamu katika Uchaguzi mkuu ujao wakati jamii nyingine zikiwahimiza wafuasi wao kuhusu uchaguzi huo.

Makaratasi hayo yalionekana kuwahamasisha Waislamu kujiandaa kwa maswali ya kumuuliza Sheikh huyo mkuu wa Bakwata.

Hali hiyo ilizusha wasi wasi miongoni mwa viongozi wa Bakwata ambao baadaye Katibu wa baraza hilo alitoa taarifa kuwa Mufti angechelewa kidogo kufika mahali hapo na kisha alikemea usambazaji wa makaratasi hayo.

Haikupita muda Mzee Hemed aliwasili katika mkutano huo ambapo kabla ya hotuba yake Katibu wa Bakwata Bwana Mohammed Balla na Sheikh wa mkoa Mzee Salim Fereji waligombea kipaza sauti kuzuia Mufti asiulizwe maswali.

Kufuatia kutaharuki huko kwa viongozi hao, Mufti aliwageukia viongozi hao akiwauliza kuwa yeye asingeweza kuwahutubia watu wa Mwanza kwa kuwa anawajua.

"Sikuwakatalia kuwa mimi nahisi uzito... Mwanza naijua tangu nina umri wa miaka 17 sasa nina miaka 72.... nimekula vichwa vya sato zaidi ya miaka 40 ndio maana ya kurudi rudi hapa, lakini nahisi sasa simnaona hali ilivyo", alisema Mufti huyo wa Bakwata huku akiwakazia macho viongozi hao.

Aliongeza kusema kuwa "kama Mwanza dawa yenu ni mzizi wa Mwembe, basi Mwembe wa Mwanza sio wa Tanga, alisema Mufti akimaanisha kazi hiyo anawaachia Masheikh wa Bakwata wa Mwanza.

Habari ambazo ANNUUR imezipata kutoka kwa waandalizi wa ziara ya Mufti mjini Mwanza zinasema kulitokea mabishano kati ya Viongozi wa mkoa huo na Mufti Mwenyewe kuhusu utekelezaji wa ratiba katika mji wa Mwanza.


Wapuuzeni wasemao kupiga kura ukafiri

VIJANA mkoani Tanga wametakiwa kuwapuuza wale wanaodai kupiga kura ni ukafiri.

Wito huo umetolewa na mwenyekiti wa vijana wa chama cha TLP,Bw.Salum Sempoli akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni.

Bw.Sempoli amesema,wapo viongozi wa taasisi za dini wanaowakaza waumini kupiga kura kwa hoja kuwa serikali itakayochaguliwa si ya kidini.

"Viongozi hao msiwasikilize watawapotezea haki zenu vijana.",amesema na kuongeza,"itakuwaje haramu kuichagua serikali ya nchi yako wakati umo ndani ya utawala wake ukiwajibika kuitii na kulipa kodi."Jambo hili haliingii akilini,kama wanajua wanachokieleza wangeanza kuzuia watu wasilipe kodi halafu ndio wawakataze kupiga kura",amesema.

Bw.Sempoli amewataka vijana kujitokeza kwa wingi wakati wa uandikishaji wa kupiga kura ili waweze kuwapigia kura viongozi watakaowaletea maendeleo.

Amesema, vijana wengi hupuuza kujiandikisha kupiga kura wakidhani kuwa zoezi la upigaji kura linawahusu wazee tu.

"Kupiga kura ni haki ya kila mwananchi, sio wazee tu. Vijana mliotimiza umri wa kupiga kura mnayo haki ya kupiga kura", alisisitiza.


Rufani ya CCM Morogoro yatupwa

KAMATI ya malalamiko ya chaguzi ndogo serikali ya mtaa wa Boma mjini hapa imetupilia mbali malalamiko ya CCM kupinga ushindi wa Madadi Hassan Maringo wa CUF.

Akiongea na AN-NUUR ofisini kwake wiki iliyopita Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro Bw. Paul Baruti amesema, kamati husika imethibitisha kwamba matokeo ya uchaguzi wa Mwenyekiti wa mtaa huo ni halali na hayana dosari yoyote ile ya kisheria.

Amelieleza gazeti hili kuwa Bw. Madadi Hassan Maringo wa CUF ni mshindi halali wa kiti hicho kisheria.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amedokeza kuwa CCM wana nafasi ya kukata rufaa kwenye mamlaka husika katika kipindi kinachokubalika kisheria, endapo haikuridhika na maamuzi ya ofisi yake.

Uongozi husika wa CCM haukuweza kupatikana mara moja kuthibitisha kama watakata rufaa juu ya maamuzi ya kamati ya malalamiko au la.

Uchaguzi huo ulipofanyika mara ya kwanza CCM walidhindwa wakapinga matokeo.

Uchaguzi uliporudiwa mara ya pili CCM walishindwa tena.


Sera ya jino kwa jino ni tishio kwa CCM

MJUMBE wa Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF), Bw. Shekue Pashua amesema, viongozi wa CCM wanainadi vibaya sera ya "Jino kwa jino" kwa sababu sera hiyo ni tishio kwa chama hicho.

Amesema, baadhi ya viongozi hao wamekuwa wakidai kuwa sera hiyo iliyoandaliwa na chama chake imelenga kuleta machafuko nchini, madai ambayo hayana ukweli.

Amefafanua kuwa sera ya "jino kwa jino" ni utaratibu ulioandaliwa na chama hicho kulinda kura wakati wa uchaguzi baada ya kugundua kuwa katika uchaguzi wa mwaka 1995 kulikuwa na udanganyifu mwingi wa kura.

"Sera hii imeandaliwa ili kuhakikisha kuwa udanganyifu wa kura hautokei tena na sio kuleta machafuko kama baadhi ya viongozi wa CCM wanavyodai", alisisitiza Bw. Pashua.

Bw. Pashua ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho mjini hapa amewataka wananchi kupuuza matamshi ya viongozi hao na kukiunga mkono Chama Cha Wananchi (CUF) kwa vile kimelenga kuinua hali za wananchi.

"Sera ya chama chetu ni Utajirisho ambao umelenga kuinua h ali za wananchi. CCM wanapaswa waeleze walichofanya katika utawala wao na sio kuzungumzia vyama vingine", alisema Bw. Pashua.

Akielezea kuimarika kwa chama hicho, Bw. Pashua amesema kuwa chama kimejizatiti vya kutosha katika wilaya zote za mkoa huo.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook