Nishani za heshima za nchi yetu

MAGAZETI kadhaa yameandika juu ya heshima ya Watanzania kumpa Mwalimu Julius K. Nyerere ambaye sasa ametunukiwa nishani kubwa na nchi kwa ujasiri wake baada ya kuondoka duniani.

Nukta yangu ni kwamba serikali imeamua Mama Maria Nyerere awe Mama wa Taifa kuwa ni mrithi wa Cheo cha Baba wa Taifa. Lakini tumesahau haraka mno kwamba Mwalimu Nyerere asingeweza kufikia alipofikia bila ya wenzake waliomkaribisha na kumfikisha kupata hadhi hizo alizozipata. Kwa muhtasari, wenyeji wenye heshima hapa Dar es Salaam ndio waliomfikisha hapo, bila ya hivyo asingejulikana hata kidogo.

Tukisoma historia za Tanganyika, ni wazee wetu ndio waliotufikisha hapa na watoto wao walichukua uzito wa kutafuta uhuru - na sio mtu mmoja, kama Mwalimu Nyerere ni Baba wa Taifa na Mama Maria Nyerere ni mama, kila ukoo lazima kuna ndugu, wajomba, mashangazi na babu katika familia hiyo, kwa hivyo Baba wa Taifa nduguze ni wale waliomkweza na kufikia alipofika.

Inakera sana, tumewasahau kuwatunukia heshima za nishani na kuwakumbuka walioondoka na walio hai ambao wametufikisha hapa.

Je, tumewasahau marehemu AbdulWahid Sykes aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa TAA iliyounda TANU na ndie aliyempisha nafasi hiyo Nyerere.

Marehemu Dossa Aziz- aliyekuwa mmoja wa waasisi wa mwanzo wa Kamati Kuu na kutumia gari lake kwa kazi zote za chama kutoka mfukoni kwake. Ameondoka duniani bila kupewa heshima ya kitaifa kama alivyostahili.

Hayati John Rupia - Mweka Hazina wa kwanza na aliyetumia pesa zake katika kuanzisha TANU na pia alikuwa mmoja wa TAA.

Marehemu Mzee Said Chamwenyewe, mmoja wa wazee aliyekuwa muasisi kutoka Rufiji ambaye alikuwa anakuja Dar es Salaam siku za masika kwa kuchukua kadi za chama, kuandikisha wanachama na kuimarisha chama, siku za masika katika miaka hiyo hakuna magari ya kwenda Rufiji, na kuhatarisha maisha yake kusafiri kwa baiskeli.

Hayati Dennis Phombea, mmoja wa waasisi mwenye asili ya Malawi aliyekuwa akifanya kazi ya Umeneja Arnautoglu Centre, alisaidia sana kutoa pikipiki yake kwenda kumfuata Mwalimu Nyerere Pugu St. Francis College kila Ijumaa kuja naye Dar es Salaam na siku zingine alikuwa Bw. Ally Sykes, akifanya kazi hiyo - Phombea alifariki Uingereza na hakuna jina lake katika kumbukumbu za chama.

Bw. Ally Sykes, aliyekuwa Katibu Mkuu siku za mwisho wa TAA, na wa kwanza wa TANU, na kuwa karibu mno na Mwalimu Nyerere mpaka kupigania uhuru, sio kweli hayati O. Kambona alikuwa Katibu Mkuu - kuweka historia kwa uwazi na safi - hayati Kambona alikuwa Katibu wa kulipwa yaani mfanyakazi wa TANU. Alikuja kutoka Dodoma alikokuwa anafanya kazi ya ualimu na marehemu AbdulWahid na Dossa ndio waliomuazima baiskeli kumuona Mwalimu Nyerere Pugu.

Hayati Stephen Muhando alikuwa katika Kamati na alishughulikia sana mambo ya nchi za nje.

Dome Okochi - Mjaluo aliyekuwa akifanyakazi Shankardas Music Store, alikuwa mmoja wa mstari wa mbele TANU ilivyoanzishwa na alitimuliwa nchini kwa kisingizio cha serikali ya Waingereza eti alikuwa mmoja wa Mau mau na kutimuliwa Wakenya wengi kwa kisingizio hicho.

Je, hawa wachache waliotajwa hapo juu, mnawadhalilisha kuwanyima heshima wanazostahili. Basi hata nishani ya kufutia machozi hamna. Badala yake amepewa Kostebol wa Trafiki nishani ya ushujaa kwa kucheza chindimba kwenye makutano ya barabara zenye taa za kuruhusu gari kupita (Traffic Light) akiona gari la Rais limepita.

Au kuna sababu za serikali kufanya hivyo?

Athumani Kibwana,
Kiwalani,
S.L.P. 18353,
Dar es Salaam.
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook