Kijiji chakosa maji muda mrefu

WANANCHI wa kijiji cha Changarawe, tarafa ya Mlali wilaya ya Morogoro Vijijini wameitaka serikali iwatatuliwe tatizo la maji linalowasumbua kwa muda mrefu.

Wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti hivi karibuni kijijini hapo, wananchi hao walisema kwamba tangu mwaka 1968 eneo hilo halikukosa maji hadi walipokuja kukatiwa miaka miwili iliyopita kwa sababu zisizotambuliwa.

"Kwa zaidi ya miezi 24 sasa kijiji kizima hakina maji licha ya mabomba kuwepo", alisema mzee Said Ramadhani mkazi wa muda mrefu kijijini hapo.

"Ukitaka maji labda uende kwa Padri Kigunga (shuleni) au sekondari ya Askofu Adrian Mkoba hapo kanisani na Mzumbe Chuoni. Sasa huku si kutesana? Wakati kodi ya maendeleo na nyinginezo tunalipa, zinakwenda wapi?" Alihoji Mzee Saidi.

Naye Bibi Fitina Zakaria Mdugutu ameliambia AN-NUUR kwamba taarifa za tatizo hilo zilikwisha fika kwa Mbunge wao Bw. Suleiman Sadiq Murad (CCM) -Morogoro Kaskazini) hata hivyo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

"Tunateseka. Viongozi hawatujali kabisa, ingawa wako pale kwa kura zetu", alisema mama huyo huku akimlipa mkodisha baiskeli pesa na maplastiki yake mawili machakavu akamchukulie maji shuleni Adrian Mkoba.

Wakati huo huo wananchi wametakiwa kuwa makini katika uchaguzi ujao ili kupata viongozi wanaofaa.

Wito huo umetolewa Ijumaa iliyopita na Ustadh Jumanne wa Jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu chuo cha uongozi wa maendeleo Mzumbe.

Akizungumza na Waislamu wa Msikiti Mkuu wa kijiji cha Changarawe, tarafa ya Mlali wilaya ya Morogoro vijijini, Ustadh huyo alisema kura ikitumiwa vyema huondoa viongozi wabovu.

Ameonya kuwa endapo watakuja madalali kuwarubuni wasiwakubali.

Aidha, amesema wakati huu wa hafla za Maulidi Waislamu wawe macho na sherehe zao kutumiwa kama ngazi ya kupatia kura watu wasiofaa. Badala yake Waislamu wayatumie vizuri majukwaa hayo kama fursa ya kujikomboa.

Aidha, Imamu wa Msikiti huo uliojengwa na marehemu Taj Muihammad miaka 11 iliyopita, Sheikh Said Ramadhani (62) ametoa wito kwa wanakijiji Waislamu wa hapo, taasisi za Kiislamu na Waislamu kwa ujumla kuisaidia madrasa ya Changarawe iliyokamilika kujengwa hivi karibuni.

Ameliambia gazeti hili kuwa madrasa hiyo yenye umri wa miaka mitano, ina tatizo la mwalimu, vitabu, madawati na mitalaa inayooana na wakati pamoja na mazingira yaliyopo.

Pia alitoa changamoto kwa taasisi za Kiislamu zilizopo mkoani kujenga shule, chuo au hospitali ya Kiislamu kwenye Msikiti huo wenye kiwanja cha kutosha.

Sambamba na hayo, kinamama wa Kiislamu wa Changarawe wamefungua Darsa msikitini hapo na kubuni mradi wa kilimo, ambapo mwaka huu wamelima mpunga.


Tanga wajiandaa kumpokea Lipumba

WANACHAMA na wapenzi wa Chama Cha Wananchi (CUF) mkoani hapa wanandaa mapokezi makubwa kwa mgombea Urais wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba anayetarajiwa kuwasili mjini hapa Julai 6 mwaka huu kwa ziara ya kichama.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho mjini hapa, Shekue Pashua, katika ziara hiyo Prof. Lipumba atafuatana na uongozi wa juu wa chama hicho.

Baadhi ya viongozi watakaokuwa katika msafara huo ni pamoja na mgombea mwenza wa kiti cha Urais wa Muungano Mhe. Nassoro Khamis, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Mhe. Shabani Mloo na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Mhe. Seif Sharif Hamad ambaye atatangulia kuwasili mjini hapa.

Maalim Seif pia ni mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha CUF.

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo iliyotolewa na chama hicho Julai 6, Prof. Lipumba atafanya mkutano wa hadhara katika uwanja wa Tangamano.

Julai 7, Prof. Lipumba atafungua kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kitakachofanyika wilaya ya Muheza.

Miongoni mwa shughuli atakazofanya akiwa mjini hapa, Prof. Lipumba atafungua matawi 17 ya chama hicho katika Manispaa ya Tanga.


Malecela awaonya CCM kuhusu CUF

MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe. John Malecela ameitahadharisha CCM kutowadharau wapinzani wake hasa Chama Cha Wananchi (CUF) na kuwafananisha na mwiba mdogo ambao ulimuua tembo.

Mhe. Malecela aliyasema hayo hivi karibuni katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM ya wilaya ya Tanga uliofanyika kwenye ukumbi wa Majestic Cinema mjini hapa.

"CCM isibweteke na kuwadharau wapinzani, maana kamwiba kadogo kalimuua tembo. Wapinzani hasa CUF tuwaone sawa na moto wa porini", alisema.

Akionesha kuwa upinzani hasa wa CUF kwa hivi sasa ni tishio kwa CCM alisema: "Adui mbovu ni yule uliyemkanyaga chini sio yule unayetizamana naye macho kwa macho.

"...Mtu unaposema CCM itashinda umaanishe hivyo vinginevyo tukishindwa ugomvi wetu utakuwa mkubwa kuliko wapinzani", Malecela aliwaonya wana CCM hao.

Kuhusu Chama cha Wananchi (CUF) alidai anamhurumia mgombea Urais wa chama hicho Prof. Lipumba kwa kuwa amedanganywa na wana CUF wa Zanzibar.

Akiishutumu sera ya jino kwa jino Malecela alisema sera hiyo haitamwezesha Lipumba kuingia Ikulu kwa vile iliandaliwa kwa ajili ya Zanzibar.

"Lipumba ameponzwa na madevu, sera hii imeandaliwa kwa ajili ya Zanzibar, huku bara wanafuata mkumbo tu", alisema Malecela.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook