Ufafanuzi kuhusu jino kwa jino

"MMESIKIA kwamba imenenwa, jicho kwa jicho na jino kwa jino, lakini mimi nawaambia kabisa msishindane kabisa na mtu mwovu". Kinachokatazwa hapo ni mashindano ya uovu na udhalimu. Kwamba nani awe zaidi ama bingwa wa mabaya kwani Yesu alijua fika kwamba bingwa wa uovu ni shetani na kwahiyo wanafunzi wake wakiingia kwenye kinyang'anyiro cha kushindana na waovu kamwe hawatafikia lengo, wala hawatafikia kikomo.

Yesu hasemi kwamba, amini nawaambia msiijali tena sheria ya jino kwa jino ila salimuni amri kwa udhalimu badala yake Yesu anasema: "Yale mnayotaka kutendewa na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo kwa maana hilo ndilo hitimisho la torati yote na maneno yote ya Manabii".

Yesu aliwasisitizia wamuaminio kwamba, "bali mimi nawaambia kila amwonaye ndugu yake hasira itampasa hukumu, na mtu akimfyolea ndugu yake itampasa baraza, na mtu akimwapiza ndugu yake itampasa jehanamu ya moto. Kumpasa mtu hukumu, au baraza au jehanamu ya moto siyo kulipiza kisasi bali ndio kuitimiza torati vinginevyo kama lengo la torati ni kudhibiti uovu kisha mtu mwingine kwa ujanja au utapeli wake akalegeza sheria (torati) na uovu ukastawi basi hata kuweko kwa sheria kunakosa maana. Sasa Yesu hakuja kulegeza sheria wala kuagiza kulipiza kisasi bali alichokifanya ni kuondoa au kuhamisha majukumu toka vitabuni (zilikoandikwa sheria) hadi mioyoni mwa wanafunzi wake.

Kwa maneno rahisi ni sawa na kusema kwamba jukumu la kudhibiti uovu ni la mtu binafsi. Badala ya mwanafunzi wa Yesu kutegemea torati (au sheria) idhibiti uovu, sasa achukue kwamba jukumu la kudhibiti uovu ni lake kama mtu binafsi ili asiwe mzigo au kero kwa wanadamu wengine. Wala Yesu hakuagiza kwamba wale wamwaminio wakiuona uovu unawajia, wasijihami wala eti wasifanye lolote bali waachie tu uovu uwadhuru hadi kiwango cha mwisho kabisa cha madhara ili iwe ishara ya kuuthibitisha utakatifu wao.

Wapotoshaji kwa makusudi na kwa muda mrefu wamediriki kuitumia Injili ya Yesu kuhami udhalimu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wao wanaamini kuna watu wenye haki ya kufanya uovu, na kwa haki hiyo basi waovu pia wanayo haki ya kusamehewa daima na wengine wanayohaki ya kufanyiwa mabaya na kwa hiyo kutokana na maagizo ya Yesu hao wanao wajibu wa kusamehe daima.

Huu sio Ukristo ni Ushetani. Kwa ajili hiyo mtu yeyote anayesimama kidete kutetea uovu wa dola kutokana tu na dhana hiyo ya kwamba wale walioko madarakani wanayo haki ya kuwafanyia mabaya walio chini ya mamlaka yao, huyo ieleweke wazi kwamba ni mtumishi wa Ibilisi japokuwa anaweza kujitambulisha kama Nabii, au Askofu au Mchungaji au Malaika au Sheikh.

Watu wa jinsi hiyo ni sawa kabisa na Mafarisayo (waliokuwa viongozi wa dini ya Kiyahudi) ambao Yesu anasema "ninyi siyo wa Ibrahimu bali ninyi ni wa Baba yenu Ibilisi, na tamaa zake ndizo mzitendazo kwa maana Yeye ni muuaji tangu mwanzo hakusimama na kweli kwakuwa hiyo kweli haimo ndani yake".

Kwa hiyo dola yoyote iliyoweka mbele uuaji, dhulma na ukandamizaji ni dola ya kishetani na inastahili kupingwa kwa nguvu zote hasa na wale wanaomwamini Mungu kwasababu kuupiga udhalimu bila woga ni wajibu na agizo kutoka kwa Mungu.

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook