Ufafanuzi juu misimamo ya CUF na kauli za Maalim Seif Sharif Hamad

Alikuwa ni Maalim Seif Shariff Hamad, aliyetoa kwa mara ya kwanza kwamba safari hii CUF itashiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba kwa kanuni ya jino kwa jino ili kuhakikisha haki inatendeka, kisha akaongeza kusema kamwe hatutakubali yale yaliyotokea 1995 yatokee tena 2000.

Je, ni mambo gani yalitokea 1995? CCM wanajua walichokifanya ndiyo maana hawakuuliza ni mambo gani hayo yanayowekewa msimamo mkali hivyo? Badala yake wakairukia kauli ya jino kwa jino na kuipigia kelele ili watu waichukie kama ni kauli ya hatari na dosari kuu na kwahiyo iwe ni kigezo cha kuinyima kura CUF siku ya uchaguzi.

Baya zaidi ni kwamba kwenye Televisheni ya TVT tayari kuna Mapadri wa Kikatoliki ambao wamepewa kipindi cha kuendesha misa lakini katika mahubiri yao wanalenga kukanusha misimamo ya baadhi ya vyama vya siasa (hasa CUF) kwa kutumia maandiko matakatifu ya Biblia.

Kwanza namshukuru Mungu kwamba sasa dosari ya udini ambayo CUF ilipakaziwa sasa inazidi kufifia siku hadi siku kiasi kwamba wenyewe CCM wamegundua kwamba haina nguvu tena ndiyo maana sasa wameishikia bango na kuishupalia kwa nguvu zote kauli ya jino kwa jino huku wakiitangaza kwa namna ya kupotosha kwamba ndiyo sera ya CUF wakati CUF ina sera ya UTAJIRISHO.

Umati uliojitokeza juzi kumpokea Profesa Lipumba haukuwa umati wa Waiaslamu bali ni umati wa wananchi na CCM haiwezi kukanusha kwamba wale hawakuwa wananchi bali walikuwa Waislamu. Kwa ufafanuzi zaidi juu ya kauli ya Maalim Seif, napenda kusema wazi kwamba Seif Sharif hakusema ifikapo Oktoba tutalipiza kisasi. Kwani hatuna kisasi na yeyote bali siku ya uchaguzi ni wajibu wetu kama chama kulinda kura zetu ili kuhakikisha yule aliyeshinda ameshinda kwa haki, na yule aliyeshindwa ameshindwa kwa haki.

Chini ya uchaguzi huru na wa haki tutayakubali matokeo bila kujali kama tumeshinda au tumeshindwa kwani ushindi ni wa wananchi wanaochagua na siyo yule anayepigiwa kura kwani yule anayepigiwa kura hana lolote la kufanya hadi ajigambe kwamba ameshinda.

Wala Maalim Seif hajasema kwamba tutashindana na CCM kwa uovu kiasi kwamba kama CCM imeua watu mamia basi sisi CUF tutaua maelfu sisi tutawadhulumu zaidi, ama kama CCM imewanyima wastaafu wa jumuiya ya Afrika Mashariki maelfu ya mafao yao basi sisi tutawanyima mamilioni yao ili kudhihirisha ubingwa katika mabaya. La hasha!

Kwahiyo kimsingi kauli ya Seif haiko kinyume na Injili ya Yesu anayeagiza kwamba msishindane kabisa na mtu mwovu. Wala hakuna kiongozi yeyote wa CUF aliyesema endapo tutafanikiwa kuingia madarakani basi tutawarudishia CCM kwa kila ovu walilotenda, sasa hisia za kulipa kisasi zinatoka wapi? Inavyoelekea ni wao wenyewe ndio wanaojishukuru hadi kuumba woga mioyoni mwao, sasa kama wamepatwa na homa ya kushindwa nini kitakachofuata endapo watang'olewa madarakani, hilo si jukumu waitibu homa hiyo, waende Afrika Kusini wakajifunze toka kwa makaburu waliishindaje hofu yao hadi wakakubali wakawaulize akina "Smith" walifanyaje kuishinda homa ya woga hadi wakakubali ushindi wa ZANU-PF mwaka 1980.

Namalizia kwa kuweka wazi kwamba kauli ya jino kwa jino wakati wa uchaguzi mkuu ina maana moja tu nayo ni kwamba tutadhibiti uhuni, wizi na udanganyifu kwa uwezo wetu wote. Ni mfano wa baadhi ya wakubwa waliojenga mahekalu huko Masaki, Mikocheni na Mbezi Beach wengi wao wamejenga ukuta au ngome za kuzunguka nyumba zao. Pamoja na kuta na grill, bado wengine wanafuga mbwa na kuweka nyaya za umeme au "Alarms". Je nia hasa ya kufanya hivyo ni nini?

Jibu ni kulinda usalama wa mali na watoto waishio ndani yake, kwahiyo kama atatokea jambazi na kulalamika kwamba kelele za mbwa wa Masaki zinakera au nyaya za umeme zinahatarisha maisha ya wengine au Alarms na kengele zao zinakera, na akataka mjadala wa kufikia mwafaka hakuna muungwana yeyote atakayeelewa wala atakayekuwa tayari kusikiliza kilio cha aina hiyo.

Kwa lugha nyingine hali hiyo ya ujenzi wa ukuta na vigingi vingine vyote vya kujihami tunaweza kuieleza kwamba mjenzi wa nyumba amechukua msimamo wa jino kwa jino dhidi ya ujambazi. Lakini hapo hakuna suala la kulipiza kisasi kwa jambazi ama kurudishia ubaya sawa na ule wa kumnyang'anya jambazi chochote kile isipokuwa ngome imekuwa mbaya kwa jambazi kwa sababu inapiku hatua zake. Sasa ngome ya chama na ukuta wa chama ni ni nini?

Ngome ya chama cha siasa ni misimamo. Chama cha siasa kisichokuwa na msimamo ni sawa tu na nyumba isiyo na ulinzi wowote. Kwa ajili hiyo wananchi wote wenye nia njema na mapenzi mema kwa nchi yetu watatuelewa vyema tunaposema kwamba msimamo wa CUF utabaki pale pale ni jino kwa jino na wezi wa kura na jicho kwa jicho na udanganyifu wote wakati wa uchaguzi.

Mwenye kulia alie tu, na mwenye kulaumu alaumu tu lakini sisi hatuachi msimamo wetu, kwa sababu jino kwa jino ni kanuni iliyotoka kwa Mungu. Hatuwezi kuacha kile alichokitoa Mungu na eti tukapokea kile wanachotoa matapeli kwa sababu tu ya kuwapendeza wanadamu. Hatuna sababu ya kujipendekeza!!
--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook