Tutumie kura zetu kuondoa dhulma
Ndugu Mhariri
HARAKATI za uchaguzi mkuu Tanzania ndiyo zimeanza, vyama mbalimbali umeshatangaza wagombea wake.
Wote tunapaswa kushiriki katika uchaguzi. Tujitokeze kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura. Tuchague viongozi ambao wataondoa dhulma katika jamii yetu.
Tunapaswa kutumia kura zetu kuondoa dhulma. Tumeshuhudia Waislamu wenzetu walivyouliwa Mwembechai. Na waliofanya hivyo hawakuchukuliwa hatua yoyote.
Mama Khairat,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi ili kupitia chombo hiki ambacho ndicho kilicho huru nitoe taarifa za Mheshimiwa mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba kutakiwa kwake Kigoma.
Tangu mwaka jana Prof. Lipumba alipoanza rasmi ujenzi wa demokrasia hapa nchini taarifa nyingi zimekuwa zikienda Kigoma zikieleza kwamba angeweza kufika muda si mrefu. Lakini kila mara wananchi wa mkoa huo wamekuwa wakibaki na shauku tu ya kumsikia kwenye vyombo vya habari.
Mfano mzuri, mimi mwenyewe mwaka jana mwezi Septemba nilikuwa Kigoma, zikaja taarifa kwamba Prof. Lipumba angeweza kuingia mkoani humo Oktoba 12. Kwa sababu wengi walifurahia taarifa hizo nilikuwa na kazi ya kujibu kwa kusadikisha au kukanusha taarifa zile, sikuwa na uhakika hivyo nilikuwa nikiwajibu tu kuwa inawezekana.
Uongozi wa chama wa kata ya Mtanga, Mwamgongo na Kagunga pamoja na vijiji vyake kama vile Kiziba, Bugamba, Zashe na Kalalangabo vilivyo mwambaoni mwa ziwa Tanganyika upande wa Kaskazini ni sehemu nilizobahatika kushuhudia jinsi watu walivyokuwa wamehamasika kwenda mjini kumpokea Profesa Lipumba kama angeweza kuingia mkoani humo.
Kutokana na mkoa huo kuachwa nyuma makusudi na serikali ya CCM, matumaini ya wana -Kigoma yamebaki kwako Profesa, fika Kigoma angalau watu wakuone ili siku ya kupiga kura waikumbuke sura yako wasifanye makosa mara mbili.
Unaombwa angalau ufanye mikutano minne tu mmoja ukiufanyia viwanja vya Mwanga Cummunity Centre wa pili kijiji cha Katinzi (Kigoma vijijini) wa tatu uufanyie Kasulu na baadae Kibondo itakuwa imetosha.
Maombi ya watu wa Kigoma kwako ndiyo hayo Mheshimiwa na wananchi kulinda kura kutokana na uzoefu walionao kutoka uchaguzi mdogo mwaka 1994 hadi leo.
Ramadhani A.L. Nkobokobo,
S.L.P. 90402,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
TAFADHALI naomba nafasi kidogo ili nitoe kero yangu.
Kumekuwa na mtindo wa baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini kutumiwa na chama tawala.
Vyombo hivyo huficha habari za vyama vya upinzani na hushirikiana na chama tawala kuzipotosha.
Sisi walalahoi tunaotaka mageuzi tuliliona hilo mapema na tukaacha kabisa kutegemea vyombo vya habari.
Tunapeana taarifa wenyewe kwa wenyewe, tunakodi magari kwa fedha zetu na sasa vyama vyetu vinapata wafuasi wengi siku hadi siku.
Baada ya mikutano mikubwa na maandamano makubwa ya Mwanza, Dar es Salaam, Unguja, Pemba na maelfu ya watu waliokutana katika ufunguzi wa matawi Kariakoo, vyombo vya habari wiki hii vimeanza tena propaganda ya "CUF chama cha Wapemba".
Kwa bahati mbaya wanaoendesha propaganda hii ni wamiliki wa vyombo vya habari, wengine wameanza kutuandikia eti nafasi ya wapinzani kushinda ni finyu.
Tunawaambieni wananchi tunazo akili zetu timamu, kiwe cha Wapemba, Wasukuma, Wanyamwezi, Wamakuwa, Wachagga, Wakristo au Waislamu tutakiunga mkono ilimradi sera yake ni haki sawa kwa wote.
Mwanaidi M. Athuman,
S.LP. 9240,
Dar es Salaam.
|
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook |