RIWAYA

Joka la Mdimu - 7

Omar Mahafudh alizikwa saa kumi na umati mkubwa mno akiwemo Jinja Maloni, Tino, Amani na Fundi wa kimataifa na wanachama wengi wa GV Club na timu maarufu ya mpira Sega Warriors ambayo marehemu alikuwa mmoja wa shabiki na kiongozi maarufu aliyejitoa kwa hali na mali kuisaidia.

Siku iliyofuata, Jinja Maloni aliamka kwenda kupakua choo katika nyumba moja. Alitia nguo za kazi ndani ya jumu lake pamoja na mafuta ya taa na kichupa kidogo cha manukato na sabuni kali ya marashi. Begani alipachika sururu na kureja, mkononi kashika ndoo iliyofungwa kamba ndefu.

Wenye nyumba walifahamu kazi iliyokuwa ifanywe siku ile. Hivyo kila mmoja alikwenda haja kubwa upesi upesi. Na hata pale Jinja alipowasili mwanamke mmoja ndiyo alifungua gunia la choo lililokuwa kama mlango. Alikuwa mnene, hivyo akashuka ngazi za chooni pole pole huku kopo tupu kalishika mkono wa kushoto.

"Haya pita babu," alisema huku akimtupia jicho Jinja Maloni.

"Isijekuwa nimekukatiza haja!" Jinja alitania huku kikundi cha wanawake waliosimama hapo kikaanguliwa cheko. "Oh! Cheba!"

"Cheba!" Jinja Maloni aliwaigiza huku akibana pua na kutishinga kiuno. Kikaanguliwa kicheko kingine na kibwagizo "Zulu oyee!"

"Oyee!" Jinja alijibu huku akiweka kapu lake chini karibu na choo ambapo palikuwa na kivuli cha mlimau. Baada ya kuweka zana zake chini aliichukua ile chupa ya mafuta ya taa akaingia nayo chooni na kuyamimina yote. Hakupoteza muda. Alitoka nje na kukizunguka choo chenyewe ambacho hakikuwa na kibanda bali kuta za matofali na mlango wa gunia la zamani. Kiliinuliwa kiasi cha urefu wa futi tatu kutoka usawa wa ardhi, na magogo yake yalitokezea pande mbili.

Kulikuwa na aina mbili za kupakua choo. Ya kwanza ilikuwa ni kukipakua kwa kuvunja sehemu ya juu ya choo na kutoa kinyesi chote na kukimwaga kwenye shimo lililochimbwa maalum pembeni karibu na choo chenyewe. Baadaye shimo hilo hufukiwa na choo kujengwa au kuzibwa vizuri kabla ya kutumiwa upya. Njia hii ilikuwa na sulubu zaidi kwa mtendaji na gharama kwa mwenye mali. Lakini iliepusha hatari.

Ya pili ilikuwa ni kutapisha. Shimo lilichimbwa sambamba na choo chenyewe hadi chini sawa na urefu wa choo hicho au kupita kidogo. Halafu, kutumia kwa sururu au kifaa chochote, ukuta wa choo hicho ulitobolewa kwa chini kabisa kukifanya kinyesi chenyewe kimiminikie na kuingia kwenye shimo jipya. Njia hii ilikuwa rahisi na ya gharama nafuu na safi zaidi. Mtendaji hakukizoa choo kama ilivyo katika ile njia ya kwanza. Lakini athari yake ilikuwa kuvunjika kwa kuta za vyoo vilivyooza. Aghalabu mvuke wa kinyesi uliziozesha kuta za vyoo ambazo zilibomoka na kuangukia wapakuaji mara walipozigusa na ncha za sururu. Wapakuaji waliangamia kwa sababu hiyo au kuumia vibaya.

Hivyo kabla ya shughuli ya upakuaji kufanywa mwenye mali aliamua njia ipi itimuke. Jinja alijiandaa kutumia ile njia ya kwanza. Kwanza alichimba kubwa kando ya choo chenyewe. Alifanya hivyo taratibu kusubiri mafuta, ama kama wenyewe walivyodai, dawa ya choo, ichanganyike na kinyesi. Mafuta yalikata harufu ya kinyesi na kuibadilisha kuwa mfano wa tope. Ilihitaji kiasi cha saa tatu au nne nzima kwa mabadiliko hayo kutokea.

Jua lilipanda taratibu hata likaanza kuwa kali. Kuku walizengea kutafuta mlo, wakacharuka huku na huko na kuondoka. Baadhi ya watoto na wanawake wa nyumba jirani waliokuwepo awali kumlaki Jinja Maloni waliondoka au kushika hamsini zao. Kazi yenyewe ilikuwa bado. Au kama walivyosema wenyewe kuwa ilikuwa trela tu, mchezo bado. Na taratibu Jinja aliendelea na trela yake.

Saa tano kasoro robo Jinja alimaliza awamu ya kwanza ya kazi yake. Alichomoa sigara na kuipachika mdomoni, akaanza kuivuta, taratibu akizunguka huku na kule.

"Babu Jinja leo hatuchapuki!, msichana mmoja chakaramu alitania. Alikuwa ameketi katika karo la nyumba hiyo akisugua sufuria kwa majivu, mchanga na brashi.

"Babu mzibe... kabisa" Jinja alirudishia dhihaka ile.

Kwa kawaida Jinja hakula chakula kizito mpaka amalize shughuli kama ile. Sana sana alikunywa chai tu. Na hata hivyo, ya nini kuwaudhi waungwana? Watoka kuchimba vyoo wakimbilia mikahawani?

Saa sita alianza kuvunja sehemu ya juu ya choo mpaka akapata upenyo wa kutumbukiza ndoo ndogo. Ndoo hiyo ilifungwa kwa kamba. Alitumbukiza ndani ya choo hadi ilipojaa, akaivuta juu na kumwaga mzigo ule kwenye shimo alilolichimba. Ukali wa mafuta ulikata harufu kali ya kinyesi, na nzi mmoja mmoja tu walizengea pale. Wanawake na watoto walirejea tena na kumsaidia Jinja kwa macho.

"Eee! Zulu!" Waliita kwa mas'hara. Mara moja moja Jinja aliguna tu. Lakini hakuinua macho kuwatazama. Mikono yake ilikuwa kama roda: kupandisha shehena ya kinyesi na kushusha ndoo tupu. Hivyo hivyo. Muda ukaenda hadi saa kumi kamili akawa amefikia kurega mkononi. Mvuke wa humo ulimkumba na kumtotesha jasho. Alikwangua kinyesi au tuseme tope tope zote zilizosalia chini na kutani. Halafu alizikusanya na kuzitoa tena kwa ndoo ile. Hata alipotoka alimwita mwenye nyumba, mzee wa miaka sitini.

"Bwana tayari! Angalia!" Jinja alimsemesha huku akielekea na kushuka chini ya ile ngazi hadi chini ya choo akachimba na kurega. Badala ya kinyesi alichimba mchanga mbichi.

"Nimeona", yule bwana aliridhika na Jinja akapanda ngazi taratibu kutoka nje. Alianza kufukia lile shimo la kinyesi lililojaa. Alitayarishiwa ndoo ya maji kwenye choo cha muda kilichozungushwa kumba (makuti) jirani na hapo. Huko alimimina yale manukato kutoka kwenye kile kichupa kidogo. Lilitoka povu kidogo. Ndipo alivua nguo zake na kuoga akitumia ile sabuni ya marashi. Vyote hivyo vilikuwa dawa ya kuua vidudu vya maradhi. Alioga taratibu huku akijisugua kwa dodoki, hadi saa kumi na moja kasorobo. Alijikausha na kuvaa nguo zake safi.

Saa kumi na moja alikabidhiwa shilingi alfu hamsini na kuondoka taratibu kurejea kwake.

*******

Saa tano na nusu usiku ule aliutipa Jinja Maloni mtindi wake ukamkubali. Alitembea na kupandisha kilima kurejea nyumbani kwake huku akiimba mwimbo maarufu Mama yake na Sofia. Lakini mwendo mfupi ghafla, akakatishwa na sauti ya mkoromo kutoka kando kidogo ya barabara. Ilikuwa ni sauti ya mtu aliyefanya jitihada ya kuita msaada akashindwa. Upesi Jinja alichomoa kurunzi yake ndogo kutoka mfuko wa nyuma wa suruali na kuiwasha.

"Nafa! Niacheni shenzi..." Sasa sauti ya kike ilimfikia Jinja Maloni. Upesi alielekea pale kwa hadhari huku kakaza mikono. Alipapasa ala ya kisu alichokichomeka kiunoni ndani ya shati lake, akaridhika.

Kwa ghadhabu kuu wale wanaume walimvamia Jinja ambaye alimtegea mmoja akaanguka wakati huo huo akampiga ngumi ya pua yule mwingine. Wote wakaanza kurudi nyuma, wakimwapiza kwa matusi.

"Mshenzi wee!

"Njooni basi", Jinja aliwadhihaki. Alimgeukia yule mwanamke ambaye alikuwa anasimama akitafuta vitu alivyopoteza. Kwa msaada wa kurunzi ya Jinja Maloni aliokota pochi yake ndogo na leso, akavipachika tena kwenye sidiria.

"Washenzi, wamekata mkufu wangu wa dhahabu na kuchukua hereni zangu", alifoka huku akipumua kwa nguvu.

"Bora uhai", Jinja alijibu kwa sauti ya chini.

Mara mwanamke aliitambua sauti ya Jinja, akasema, "Umeniokoa, nakushukuru Mzee Jinja".

"Wacha kutembea usiku! Dunia hii si ya wanyonge".

Yule mwanamke hakujibu na Jinja alimwuliza. "Sasa waenda wapi?"

"Nyumbani?"

"Basi nitakusindikiza, usiku mkubwa huu".

--
JuuRUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org


An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook